STRIKA
USILIKOSE
Friday, July 23, 2010
Mtoto wa Balozi Chokala ajitosa kumrithi Kimbisa
MTOTO wa Balozi Mstaafu Patrick Chokala, Simon Mashiku Chokala (28), amejitokeza kuchukua fomu za udiwani katika Kata ya Kivukoni kwa lengo la kumrithi Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa aliyekuwa diwani wa kata hiyo aliyeamua kujiweka kando.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi mara baada ya kurejesha fomu ofisi ya CCM kata ya Kivukoni, Chokala alisema lengo la kutaka kuongoza kata hiyo yenye ofisi ya Rais (Ikulu), ni kutaka kubadilisha mazingira ya kata hiyo.
"Kama kijana nimeamua kuchukua fomu ya udiwani ili niweze kuiweka kata hii katika mazingira ya kisasa zaidi...Ikulu ipo katika kata hii hata wageni wengi wa nchi lazima waje hapa, hivyo nimejipanga kuiweka sawa," alisema Chokala.
Alisema pamoja na Meya Kimbisa kuifanyia makubwa kata hiyo, bado anahitaji kuifikisha mbali zaidi kwa sasa.
Chokala ambaye baba yake akiwa Balozi nchini Urusi mwaka 2005, alijitokeza kuwania urais kupitia CCM, lakini alijitoa katika kura za maoni.
Akizungumzia taaluma yake, Chokala alisema alimaliza elimu ya msingi katika Bunge jijini Dar na kisha kupata elimu ya sekondari nchini Kenya kabla ya kuchukua digrii ya biashara nchini Urusi.
Aidha, alichukua mafunzo ya kompyuta nchini Urusi wakati baba yake, Balozi Chokala akiiwakilisha nchi huko.
Chokala anachuana na wagombea wengine waliojitokeza kuwania kiti hicho akiwemo Mbunge wa Afrika Mashariki, Didas Masaburi.
Meya Kimbisa ameamua kuwaachia vijana kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo kwa madai anakwenda katika jimbo moja mkoani Dodoma kuwania Ubunge kupitia chama tawala.
Mwisho
Subscribe to:
Posts (Atom)