Danny Welbeck (kulia) akiruka juu kuifungia Manchester United bao la kuongoza katika mechi ya usiku wa jana. |
VINARA wa Ligi Kuu ya England, Manchester United usiku wa kuamkia leo imelazimisha sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya wenyeji wao Real Madrid katika pambano la awali la mechi za mtoano za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika pambano hilo lililochezwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu, mjini Madrid, Hispania Manchester ilianza kutangulia kupata bao lililofungwa nyota wake, Danny Welbeck katika dakika ya 20.
Wenyeji walicharuka baada ya kufungwa bao hilo na kufanikiwa kusawazisha dakika kumi baadae kupitia mshambuliaji wake nyota, Cristiano Ronaldo.
Katika pambano jingine lililochezwa pia jana ilishuhudiwa wenyeji Shakhtar Donetsk ilishindwa kutamba kwa kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na wageni wao Borrusia Dotmund ya Ujerumani.
Wenyeji ndiyo waliotangulia kupata bao kupitia Darijo Srna dakika ya 31 kabla ya wageni kusawazisha kwa goli la Robert Lewandowski dakika ya 41 na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 1-1.
Kipindi cha pili wenyeji waliendelea kutakata kwa kujipatia bao la pili lililofungwa na Douglas Coast dakika ya 68 kabla ya Wajerumani hao kuchomoa kipigo dakika mbioli kabla ya kumalizika kwa pambano hilo kwa bao la Mats Hummels.
Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Machi 5 mechi itakayoamua timu ipo itinge riobo fainali za michuano hiyo ya Ligi ya Ulaya.