STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 15, 2013

Miss Tanzania 2007 ataka watanzania kuwapenda wenye shida



Miss Tanzania wa zamani Richa Adhia (kati) wakati wa Siku ya Wapendanao

DAR ES SALAAM
MREMBO aliyewahi kuwa Miss Tanzania 2007 Richa Adhia amewataka watanzania kujenga utamaduni wa kuwakupenda na kuwajali watu wengine wakiwemo wenye mahitaji maalum kama watoto na wazee kwa kuwa wanahitaji faraja toka kwa jamii nzima nyakati zote badala ya kusubiri maadhimisho ya sikukuu mbalimbali.
Akizungumza wakati wa kilele cha msimu wa siku ya wapenda nao ulioandalia na Kampuni ya bia ya Serengeti kupitia kinywaji cha Baileys katika viwanja vya shoppers jijini Dar es Salaam.
“Siku ya wapendanao ikitumika kuongeza ari ya kuwasaidia watu wenye mahitaji inakuwa na maana zaidi kuliko kuitumia siku hiyo kwa mapenzi zaidi na sio vibaya kutumia siku ya wapendanao kuanzisha mapenzi mapya au kuboresha mapenzi yaliyokuwepo lakini pia itumike kuwakumbuka wahitaji ambao ni wazee na watoto”. Richa alisema
Kwa upande wake meneja masoko wa vinywaji vikali kutoka Kampuni ya bia ya Serengeti Emilian Rwejuna amesema wameamua kufanya kampeni hii ili kuamsha ari ya kuwajali na kuwapenda wengine ikiwemo kujenga utamaduni wa kuwanunulia zawadi kwani Baileys inatambua kuwa zawadi zina mchango mkubwa katika maisha ya mahusiano.
“Hivyo mtoto anayempa zawadi mzazi wake hujiweka katika mazingira mazuri kimahusiano kuliko asiyefanya hivyo”. Richa alisema
Pia alielezea kuwa Kampuni ya bia ya Serengeti imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuhamasisha na kutoa chachu na kuahidi itaendelea kuhamasisha mahusiano mema miongoni mwa jamii.
Kampeni ya msimu wa sikuu ya wapendao ulioandaliwa na Kampuni ya bia ya Serengeti kupitia kinywaji chake cha Baileys ulinza tarehe mosi mwenzi wa Februari kwa kupita katika maeneo mbalimbali ya manunuzi ili kuwahamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kuwanunulia wenzi wao zawadi na kukamalika siku ya wapendanao Februari 14 ambapo Baileys pia ilitoa zawadi kwa watu mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Liverpool kuvuna nini kwa Swansea City EPL


Kocha wa Liverpool, Brandin Rodgers
 BAADA ya wiki iliyopita kunyukwa nyumbani na West Bromwich na kisha kulala ugenini mbele ya Zenith katika michuano ya Ligi ndogo ya Ulaya (UEFA), klabu ya Liverpool Jumapili inatarajiwa kujaribu bahati yake tena kwa kushuka dimbani uwanja wa Anfiled kuivaa Swansea City.
Mechi hiyo pekee ya Ligi Kuu ya England kwa wikiendi hii inatarajiwa kuwa kipimo kingine cha kocha Brendan Rodgers ambaye alikuwa akiinoa Swansea kabla ya kutimkia Anfield kutokana na mwenendo mbaya wa kikosi chake kwa msimu huu.
Vijana hao wa Rodgers mpaka sasa wapo nafasi ya tisa wakijikusanyia jumla ya pointi  36 moja nyuma ya Swansea ambao wanakamata nafasi ya sasa kwa sasa wakitenganishwa na West Bromwich wanaolingana nao kwa pointi 37.
Walipokutana katika pambano la la kwanza msimu huu kwenye uwanja wa Liberty timu hizo zilishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu ya kutofungana, ilihali wakati kikosi cha Swansea kikiwa chini ya Rodgers  msimu uliopita waliitambia Liverpool mechi zote mbili, wakishinda mechi ya ligi bao 1-0 na Kombe la Ligi bao 3-1 kabla ya kuhamia Liverpool.
Kocha huyo amewataka wachezaji wake kuwa makini uwanjani, ili kuweza kufunga mabao baada ya usiku wa jana vijana wake kukosa mabao mengi ya wazi na kuishia kulazwa mabao 2-0 na Zenith.
Kwa mujibu wa rekodi baina ya timu hizo mbili tangu mwaka 1982 walishakutana mara nane ambapo Swansea wamewatambia Liverpool mara tatu dhidi ya vipigo viwili ilivyuopewa na wapinzani wao hao na mechi tatu zilizosalia walishindwa kutambiana kwa kutoka sare.
Je, vijana wa Rodgers watathibitisha kuwa kocha wao ni mahiri hata akiwa Liverpool ama ni Swansea watakaoendelea kutoa dozi kwa vijana wa Anfield ambao katika mechi yao iliopita ya ligi hiyo iliifumua QPR kwa kuikandika mabao 4-1.

Vijana wa Liverpool na Swansea walipoumana katika mechi yao ya awali iliyoisha kwa 0-0 msimu huu
Michael Essien alipokuwa akitambulishwa Real Madrid
KIUNGO mkabaji wa timu ya Real Madrid, Michael Essien amelisifia soka la Hispania na ligi yake kwa ujumla akidai ni lenye ufundi na kuvutia  kulinganisha na lile la England linalotumia zaidi nguvu.
Essien mwenye umri wa miaka 30 na aliyejiunga na Real Madrid msimu huu kwa mkopo akitokea Chalsea ya England Augost mwaka jana na kuichezea jumla ya mechi 23 katika miezi sita ya mwanzo ya kucheza La Liga, alisema kwa uzoefu wake Ligi ya England inatumia zaidi maguvu wakati ile ya Hispania imejaa ufundi wa kupasia mpira kadri iwezekanavyo.
"Ligi ya England imejaa maguvu mengi," alisema Essien kiungo wa kimataifa wa Ghana aliyeongeza kusema; "kitu nilichokiona katika la Liga ni timu kucheza kwa kufungua njia ya mpira kwa kupasiana mwanzo mwisho," alisema.
"Nimeona vitu tofauti hapa kulinganisha na England na inapendeza," alisema Essien aliyeungana na makocha wake wa zamani waliowahi kumnoa Chelsea.
Kiungo alikuwa mmoja wa wachezaji waliokuwa benchi Jumatano iliyopita wakishuhudia timu yake ikilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Manchester United katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, anadai ana matumaini makubwa ya timu yake kutwaa ubingwa.
Alisema ana matumaini makubwa kwa timu yake kufanya vema katika michuano hiyo baada ya kulikosa taji hilo mwaka 2008 alipokosa penati alipokuwa Chelsea katika mechi ya fainali dhidi ya Mashetani Wekundu watakaorudiana nao katika mechi ya mkondo wa pili kuwania kufuzu robo fainali.
"Kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa ni jambo kubwa na muhimu kwangu na klabu yangu" alisema
"Kama mchezaji ndoto yangu ni kutwaa taji hili. Wote tutajitolea ili kuona tunafanikisha hilo," aliongeza.
CAF YASITISHA UKAMISHNA WA HAFIDH ALI




Na Boniface Wambura

SHIRIKISHO la Kabumbu Barani Afrika (CAF) limesitisha ukamishna wa Hafidh Ali. Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyokutana Januari 17 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.



Kwa mujibu wa barua ya Katibu Mkuu wa CAF, Hicham El Amrani kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ukamishna huo umesitishwa kwa vile hadi sasa Shirikisho hilo halijapata ripoti ya mechi namba 78 kati ya Comoro na Libya ambayo Ali aliteuliwa kuisimamia.



Hivyo, ukamishna wa Ali umesitishwa hadi hapo CAF itakapopokea ripoti kuhusiana na mechi hiyo ambayo ilikuwa ni kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za AFCON zilizofanyika mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Kila la heri, Simba Azam na Jamhuri Afrika

Kikosi cha Jamhuri ya Pemba
kikosi cha Simba

Wachezaji wa Azam wakishangilia goli katika baadhi ya mechi zake nchini

Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezitakia kila la kheri wawakilishi wa nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.

TFF imezitakiwa mafanikio mema timu hizo, Azam, Jamhuri na Simba ambazo mwishoni mwa wiki zinatarajiwa kutupa karata zake katika mechi zao za awali nyumbani dhidi ya wapinzani wao katika michuano hiyo.

Azam wenyewe watashuka dimba la Taifa Dar es Salaam kesho kuvaana na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini katika michuano ya Kombe la Shirikisho, huku Jamhuri nao watakuwa uwanja wa Gombani kupepetana na St Georges ya Ethiopia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa.

Simba wenyewe watavaana na Recreativo do Libolo ya Angola siku ya Jumapili kwenye uwanja wa Taifa katika pambano la Ligi ya Mabingwa ambapo Simba inatarajiwa kutumia uzi mpya toka Sunderland uliotambuliwa leo jijini Dar es Salaam.

TFF YAUPONGEZA UONGOZI MPYA WA TASMA


Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeupongeza uongozi mpya wa Chama cha Wataalamu wa Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Februari 10 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TASMA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia tiba ya wanasoka nchini.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TASMA chini ya uenyekiti wa Dk. Mwanandi Mwankemwa aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo kwa kura 18 dhidi ya 7 za aliyekuwa Mwenyekiti Biyondho Ngome

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya TASMA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TASMA chini ya Dk. Paul Marealle na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Safu nzima ya uongozi wa TASMA iliyochaguliwa inaundwa na Dk. Mwanandi Mwankemwa (Mwenyekiti), Dk. Nassoro Matuzya (Katibu Mkuu), Sheky Mngazija (Katibu Msaidizi), Dk. Juma Mzimbiri (Mhazini), Joakim Mshanga (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF) na Dk. Hemed Mziray (mjumbe wa Kamati ya Utendaji).

Ukiondoa nafasi ya Mwenyekiti, wagombea wengine wote hawakuwa na wapinzani. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti haikupata mgombea, hivyo itajazwa katika uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye mwaka huu.

YANGA, AFRICAN LYON ZAINGIZA MIL 68/-









Na Boniface Wambura

PAMBANO namba 119 ya Ligi Kuu ya Vodacom lililochezwa juzi (Februari 13 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Yanga kushinda 4-0 imeingiza sh. 68,438,000.

Watazamaji 12,147 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 16,170,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,439,694.92.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo 10,982 walikata tiketi hizo na kuingiza sh. 54,910,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 8,222,162.26, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 4,933,297.36, Kamati ya Ligi sh. 4,933,297.36, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,466,648.68 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,918,504.53.

AZAM YAALIKA WATANZANIA TAIFA WAKIWAKABILI WASUDAN


UONGOZI wa klabu ya Azam umewaomba mashabiki wa soka jijini Dar es Salaam na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kwenye dimba la Taifa kesho katika pambano lao dhidi ya wapinzani wao kutoka Sudan Kusini, Al Nasir Juba katika mechi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Azam inayoshiriki kwa mara ya kwamba michuano ya Afrika, ina matarajio makubwa ya kufanya vema katika mechi hiyo ya kesho ikitambia nyota wake wa kimataifa wa ndani na nje ya nchi waliosajiliwa katika kikosi chao kinachonolewa na kocha John Stewart  Hall.
Afisa Habari wa Azam, Jaffer Idd Maganda, aliwataka mashabiki kuwaunga mkono kesho ili kuwapa raha Watanzania ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakishindwa kuburudika wawakilishi wao wakishiriki katika michuano mikubwa ya kimataifa.
"Njooni muone soka, njooni muone Azam ikifanya kweli, tumepania kupata ushindi katika mechi ya kesho ili iwe rahisi katika pambano la marudiano wiki mbili baadaye," alisema Jaffer.
Jaffer alisema kikosi chao chote kipo imara na wachezaji wana ari kubwa ya pambano hilo ambalo litachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda.
Azam inatambia wakali wake wakiwamowachezaji wa kigeni Humphrey Ochieng Mieno na Jockins Atudo kutoka Kenya, Mganda Brian Umony, Wa ivory Coast mapacha Kipre Balou Tchetche na Kipre Herman Tchetche mbali na nyota wa Tanzania walioifanya timu hiyo izitetemeshe Simba na Yanga kwa sasa.
Viingilio katika mechi hiyo ya kesho bei ya chini kabisa ni 'buku 2' yaani 2000, kwa wale watakaokaa viti vya Kijani na Bluu, wale watakaokaa viti vya rangiu ya machungwa (Orange) watalipa Sh 5,000 na watakaokaa VIP C na B watatoa 10,000 tu na VIP A watajinafasi kwa Sh 20,000.
Mechi hiyo ilitangazwa ingechezwa kwenye uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam lakini yakafanyika marekebisho na kuhamishiwa uwanja huo wa Taifa unaochukua watazamaji 60,000.

Liverpool chali, Chelsea, Tottenham zapeta UEFA

gareth Bale akifunga moja ya mabao yake katika mec hi yao ya jana usiku

JAHAZI la timu ya Liverpool ya Uingereza limezidi kuzama baada ya usiku wa jana kukandikwa mabao 2-0 na Zenith, wakati timu zinazofukuzana kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, Chelsea na Tottenham Hotspurs zikitakata kwa kushinda mechi zao za Ligi ya UEFA.
Liverpool inayochechemea kwenye ligi ya nyumbani ilipata kipigo hicho ugenini kwa magoli ya Hulk na Semak, huku nyota wake kutoka Uruguay, Luis Suarez akikosa mabao kadhaa ya wazi.
Katika mechi nyingine za michuano hiyo maarufu kama Europa ndogo, Chelsea ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sparta Praha likitumbukizwa wavuni na Alex, huku Tottenham wakiwa nyumbani waliishinda Olympicque Lyonn ya Ufaransa mabao 2-1 yote yakifungwa na Garetht Bale.
Nao Newcastle United ilijikuta ikipata sare ya bila kufungana dhidi ya Metalist ya Ukraine huku ikinyimwa mabao mawili yaliyotumbukizwa wavuni na Msenegal, Bemba Cisse na kumfanya kocha Allan Pardew.
Matokeo mengine ya mechi hizo timu ya Samuel Et'oo, Anzhi Makhachkala ya Russia iliishindilia Hannover ya Ujerumani mabao 3-1, Et'oo akitupia moja,  Bate na Fenerbahce (0-0), Levante v Olympiiakos Piraeus (3-0), Dynamo Kyiv v Bordeaux (1-1), Bayer Leverkusen v Benfica (0-1), Ajax v Steaua Bucuresti (2-0), Napoli v Viktoria Plzen (0-3), Atletico Madrid v Rubin Kazan (0-2), Inter Milan v CFR Clui (2-0), Stuttgart v Genk (1-1), Dnipro Dnipropetrovsk v Basel (0-2) na Borrusia M'gladbach v Lazio (3-3).
Mechi za marudiano za michuano hiyo zinatarajiwa kuchezwa wiki ijayo kwenye viwanja tofauti kwa zile zilizokuwa ugenini kuhamia nyumbani na kinyume chake kwa zile zilizokuwa nyumbani kusafiri ugenini.