Yanga |
Simba |
HATMA ya Simba kuendelea kulifukuzia taji lake la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara inalolishikilia inatarajiwa kufahamika Jumamosi wakati itakapovaana na Toto African jijini Mwanza katikia mfululizo wa ligi hiyo iliyobakisha mechi tano kabla ya kufunga msimu.
Simba iliyojeruhiwa jana kwa kulambwa bao 1-0 na wenyeji wao Kagera Sugar, mjikni Bukoba itaikabilia Toto kwenye uwanja wa CCM Kirumba na matokeo yoyote mabaya kwao yatawafanya waliteme rasmi taji lao na kuliacha bila mwenyewe.
Kwa sasa mabingwa hao wana pointi 34, pointi 14 nyuma ya vinara wanaoongoza ligi hiyo Yanga ambayo nayo itakuwa dimbani wikiendi hii mjini Morogoro kuvaana na maafande wa Polisi Moro na ushindi wowote utamaanisha utawavua Simba ubingwa.
Hata hivyo Simba itavuliwa rasmi ubingwa Jumamosi iwapo Yanga itashinda kisha wao wapate sare au kipigo toka kwa Toto kwani haiataweza kufikisha pointi ambazo itakuwa imezikusanya Yanga yaani 51. Kwa sasa Yanga ina pointi 48.
Tayari Simba kupitia kocha wake msaidizi Jamhuri Kihwelu 'Julio' wameapa kupigana kiume CCM Kirumba ili kuhakikisha wanazoa pointi tatu toka Kanda ya Ziwa.
Wakati Simba ikiwa katika kitimtim hicho jini Mwanza, Yanga timu pekee ambayo haijapoteza mechi yoyote ndani ya mwaka huu wa 2013, itakabiliana na timu isiyotabirika ya Polisi ambayo tangu ifanye mabadiliko ya benchi la ufundi imekuwa tishio.
Kocha wa Yanga Ernst Brands amenukuliwa akisema kuwa vijana wake tayari kuendeleza rekodi ya ushindi ili kutangaza ubingwa mapema, licha ya kukiri Polisi sio timu ya kubeza.
Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo mbali na mechi hizo za watani wa jadi zinazochezwa viwanja tofauti, michezo mingine ya wikiendi hii inatarajiwa kuzikutanisha timu ndugu za Kagera Sugar itakayoialika Mtibwa Sugar mjini Bukoba, huku Azam wenyewe watakuwa Mlandizi kuvaana na Ruvu Shooting iliyotamba kuwashikisha adamu Jumamosi.
Mechi nyingine kwa wikiendi hii itazikutanisha timu zaJKT Oljoro watakaovaana na maafande wenzao JKT Ruvu mjini Arusha ambayo haitakuwa na nyota wake, Zahoro Pazi aliye majeruhi wa goti, huku African Lyon itaikaribisha Coastal Union uwanja wa Chamazi ikiwa inapigana kujinasua mkiani ilipokung'ang'ania kwa muda sasa.