Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu' |
MAKAMU Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’
na katibu mkuu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala ni miongoni mwa watu waliohojiwa
na Jeshi la Polisi jana kusaidia uchunguzi mkali kuhusiana na ujambazi
uliosababaisha kuporwa kwa Sh. milioni 10.59 za klabu hiyo zilizotokana na
mgawo walioupata katika mechi yao ya kirafiki dhidi ya Tusker ya Kenya kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.
Akizungumza na jana jijini Dar es Salaam,
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela, alisema kuwa
wameshawahoji Kaburu, Mtawala na watu wengine kadhaa ili kupata maelezo muhimu
yatakayosaidia kupatikana kwa ukweli kuhusiana na kilichotokea.
"Tumewahoji viongozi hao wawili wa Simba (Kaburu
na Mtawala) ili kujua taratibu za uhifadhi na utunzwaji wa fedha na mali za
klabu yao... maana inastusha kusikia mtu mmoja anakwenda nyumbani kwake na mali
ya klabu, tena buila ulinzi wowote ule," alisema Kenyela.
"Tumeamua pia kuwahoji ili kujua hasa ni nini
kilichotokea kuanzia Uwanja wa Taifa maana tulibaini kuwa wao (Kaburu na
Mtawala) ndiyo waliosaini na kupokea mgawo wa Simba kule uwanjani
(Taifa)," aliongeza.
Kataka hatua nyingine, Kenyela alisema kuwa Mhasibu
wa Klabu hiyo, Erick Sekiete na watu wengine wawili, Said Pamba na Stanley
Phillipo (23) waliokuwa wakishikiliwa na Polisi kuhusiana na tukio hilo
waliachiwa kwa dhamana jana.
Sekiete na wenzake hao, walivamiwa wakati wakiwa katika
eneo la Sinza kwa Remmy baada ya kuteremka katika gari aina ya Toyota Premio
yenye namba za usajili T869 BKS iliyokuwa ikiendeshwa na Pamba.
Katika tukio hilo, ilidaiwa kuwa Sh. milioni 7.59 na
dola za Marekani 2,000 (Sh. milioni tatu) zilizotokana na mgawo wa klabu hiyo
katika mechi yao dhidi ya Tusker FC ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam ziliporwa baada ya Sekiete (28) kuvamiwa na majambazi sita katika
eneo la Sinza kwa Remmy jijini Dar es
Salaam ambapo risasi kadhaa zilipigwa hewani. Tukio hilo lilitokea saa 3:20
usiku.
Kamanda Kenyela alieleza kuwa Afisa Habari wa Simba,
Ezekiel Kamwaga alimdhamini Sekiete huku Phillipo akidhaminiwa na ndugu yake
aitwaye Julius Kiwale.
Kamanda Kenyela alisema kuwa Pamba, ambaye alikuwa
dereva wa gari lililowabeba Sekiete na Phillipo, alidhaminiwa na Kasim Pamba.
“Wanatakiwa waripoti katika Kituo cha Polisi Magomeni
Jumatano (kesho),” aliongeza Kenyela.
Chanzo;NIPASHE
----------