Hii ndiyo kazi ya Mombeki kuwaokotesha mipira mabeki na kipa |
Mombeki alitajwa yupo katika hatihati ya kulikosa pambano hilo la watani wa jadi litakalochezwa kwenue uwanja wa Taifa siku ya Jumapili baada ya kujiumiza mazoezi katika kambi ya timu hiyo iliyopo Bagamoyo.
Hata hivyo habari njema kwa wanachama na mashabiki wa Simba ni kwamba mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na Simba akitokea Pamba ya Mwanza, amerejea tena uwanjani na kuna uwezekano mkubwa Jumapili atashirikiana na mfumani nyavu mahiri, Amissi Tambwe kuichachafya ngome ya Yanga.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliiambia MICHARAZO kuwa, Mombeki amerejea tena uwanjani baada ya hali yake kutengemaa na kuwapa matumaini makubwa ya kushuka dimbani Jumapili kuiangamiza Yanga.
Kamwaga alisema hata hivyo kikosi chao bado kitaendelea kukosa huduma za wachezaji wao nyota kama Henry Joseph, Issa Rashid 'Baba Ubaya' na Miraj Adam.
"Tunashukuru hofu ya kumkosa Mombeki imeondoka baada ya mshambuliaji huyo kurejea tena dimbani, japo Simba itawakosa Henry Joseph ambaye hayupo kambini, Baba Ubaya, Miraj Adam na Abdallah Seseme ambao ni majeruhi," alisema Kamwaga.
Kamwaga alisema kikosi chao kina morali na ari kubwa ya kushinda mechi ya Jumapili, licha ya kudai litakuwa pambano gumu.
Pia alisema katika kuwatia motisha wachezaji ili kuigaragaza Yanga kwenye uwanja wa Taifa, viongozi na 'matajiri' wa Simba wanatarajia kuteta na wachezaji siku ya Jumamosi kwa lengo la kuwaweka sawa kisaikolojia pamoja na kuwatia morali zaidi ili kuwashinda Yanga.
"Viongozi na matajiri wa Simba wataitembelea kambi na kuzungumza na wachezaji kati ya Ijumaa na Jumamosi ili kuwaweka sawa na kuhakikisha Yanga anakufa Jumapili Taifa," alisema Kamwaga.
Simba na Yanga zitakutana katika mchezo huo, huku Simba ikiwa na deni la kulipa kisasi cha kipigo walichopewa katika mechi yao ya mwisho ya ligi iliyopita iliyochezwa Mei mwaka huu ambapo Yanga ilishinda mabao 2-0.