KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokutana hivi karibuni imekubali mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ya kurejesha michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL).
Lengo la kurejesha ligi hiyo ni kuongeza wigo wa mashindano kitaifa ambapo itasaidia kushirikisha kundi kubwa zaidi la wachezaji kwenye mashindano makini yanayozingatia viwango na vigezo ili kuwapa wachezaji maendeleo ya kiuchezaji ikiwemo kuendelezwa vipaji vyao kitaalamu.
Ligi hiyo yenye timu 24 itachezwa katika hatua ya makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini ambapo mshindi wa kila kundi atapanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL). Timu ya mwisho kila kundi itarudi kwenye ligi ya mkoa wake.
Hatua ya pili ni kutafuta bingwa wa SDL ambapo timu zilizoongoza makundi (nne) zitacheza kwa mtoano nyumbani na ugenini. Utakuwepo mchezo wa fainali ambapo mshindi atkuwa bingwa wa SDL msimu wa 2014/2015.
Timu zitakazocheza SDL kwa msimu huu ni zile zilizoshika nafasi ya pili hadi ya nane katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) katika makundi yao msimu uliopita, na tatu zilizoshuka kutoka FDL msimu uliopita.
Kundi A litakuwa na timu za Milambo FC (Tabora), Mji Mkuu FC (Dodoma), Mpanda United (Mpanda), Mvuvumwa FC (Kigoma), Singida United (Singida) na Ujenzi (Rukwa). Kundi B ni Arusha FC (Arusha), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Eleven Stars (Kagera), Mbao FC (Mwanza), Pamba FC (Mwanza) na Rwamukoma JKT (Mara).
Timu za kundi C ni Abajalo (Dar es Salaam), Kiluvya United (Pwani), Kariakoo FC (Lindi), Mshikamano FC (Dar es Salaam), Navy FC (Dar es Salaam) na Transit Camp (Dar es Salaam). Kundi D ni Magereza FC (Iringa), Mkamba Rangers (Morogoro), Njombe Mji (Njombe), Town Small Boys (Ruvuma), Volcano FC (Morogoro) na Wenda FC (Mbeya). Ligi itachezwa kuanzia Novemba mwaka huu.
Wakati huo huo; Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2014/2015 itachezwa katika makundi mawili kwa mtindo wa nyumbani na ugenini kuanzia Oktoba 11 mwaka huu.
Kundi A lina timu za African Lyon, African Sports, Ashanti United, Friends Rangers, Kimondo SC, Kurugenzi Mafinga, Lipuli, Majimaji, Mlale JKT, Polisi Dar es Salaam, Tessema FC na Villa Squad.
Wakati kundi B lina timu za Burkina Faso, Geita Veterans SC, Green Warriors, Kanembwa JKT, Mwadui SC, Oljoro JKT, Panone FC, Polisi Dodoma, Polisi Mara, Polisi Tabora, Rhino Rangers na Toto Africans. Ratiba ya Ligi hiyo itatolewa hivi punde.