STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, March 19, 2013


JOSE MOURINHO NDIYE ANAYEVUTA MKWANJA MNENE 

Jose Mourinho -- Anaongoza kwa mpunga wa mwaka baada ya kuingiza Sh. bilioni 29.
Marcelo Lippi - Sh. bilioni 25/-
Wenger -- Sh. bilioni 19.5

Ferguson -  Sh. bilioni 12.6
Kocha wa Real Madrid, Mreno José Mourinho ndiye aliyelipwa fedha nyingi zaidi kwa mwaka uliopita kwa mujibu wa jarida la soka la 'France Football', ambalo limemuweka kocha huyo wa Ureno kileleni kwa mara ya nane mfululizo tangu mwaka 2004 lilipoanza utararibu wa kutaja orodha ya makocha wanaolipwa fedha nyingi zaidi kwa mwaka.

Katika orodha hiyo mpya ya 'France Football', Mourinho yuko kileleni baada ya kuvuna euro milioni 14 (Sh. bilioni 29); euro milioni 12 (Sh. bilioni 25) zikitokana na mshahara na nyingine zikitokana na mikataba yake ya matangazo ya biashara.

Kama ilivyokuwa mwaka jana, kocha huyo wa Real Madrid amempiku Muitalia Carlo Ancelotti, aliyekamata nafasi ya pili kwa mara nyingine ingawa kipato chake kimeshuka kwa euro milioni 1.5 (Sh. bilioni 3) na sasa kuwa euro milioni 12 (Sh. bilioni 25) kulinganisha na mwaka uliopita.

Kocha wa klabu ya China ya Guangzhou Evergrande, Muitalia Marcelo Lippi anakamilisha orodha ya vinara akiwa na euro milioni 11 (bilioni 23), nafasi iliyotwaliwa mwaka uliopita na aliyekuwa kocha wa Barcelona, Mhispania Pep Guardiola, ambao hivi sasa yuko katika mapumziko yake ya mwaka mmoja kabla ya kuanza kuiongoza Bayern Munich msimu ujao.

Mholanzi Guus Hiddink, anayeiongoza klabu ya Ligi Kuu ya Urusi ya Anzhi Makhachkala, anakamata nafasi ya nne katika orodha hiyo akiwa na euro milioni 10.8 (Sh. bilioni 22), wakati raia wa Scotland, Kenny Dalglish anafuatia baada ya kuvuna euro milioni 10 (Sh. bilioni 21) alipokuwa Liverpool kabla ya kutimuliwa mwezi Juni.

Wanaokamilisha orodha ya makocha wanaolipwa pesa nyingi zaidi ni kocha wa Arsenal, Mfaransa Arsène Wenger (euro milioni 9.4 -- Sh. bilioni 19.5), kocha wa timu ya taifa ya Urusi, Fabio Capello (euro milioni 9.2 -- Sh. bilioni 19), Roberto Mancini wa Manchester City,  Alex Ferguson wa Man U na kocha wa timu ya taifa ya China, José Antonio Camacho (euro milioni 6.1 --  Sh. bilioni 12.6).

Kiingilio mechi ya Stars, Morocco buku 5 tu!

Stars na Morocco zilipokutana mara ya mwisho jijini Dar es Salaam

Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la soka nchini, TFF limetangaza viingilio vya mechi ya pambano la kimataifa la kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kati ya timu ya taifa, Taifa Stars na Lions of the Altas ya Morocco, ambapo kiingilio cha chini kabisa kikiwa ni Shilingi 5000 maarufu kama Buku 5.
Kiingilio hicho cha chini katika mechi hiyo itakayochezwa kwenye uwanja wa Taifa siku ya Jumapili kitahusisha viti vya rangi ya kijani.
Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.

Viingilio vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.

Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku mbili ya mchezo (Ijumaa na Jumamosi) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni na Dar Live Mbagala.

Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi. Vilevile tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.

Samatta, Ulimwengu watua, kambi ya Stars yanoga


 
Na Boniface Wambura
WASHAUMBULIAJI nyota wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wamewasili nchini jana usiku na kwenda moja kwa moja kambini.

Ujio wa washambuliaji hao unafanya idadi ya wachezaji walioripoti kambini kufikia 20 kati ya 23 walioitwaa baada ya mshambuliaji Khamis Mcha aliyekuwa na kikosi cha timu yake ya Azam nchini Liberia naye kuripoti kambini leo asubuhi.

Wachezaji John Bocco na makipa Mwadini Ally na Aishi Manula ambao pia nao walikuwa Liberia na timu yao ya Azam wataripoti kambini leo alasiri. Wachezaji hao ni sehemu ya msafara wa timu ya Azam ambao utakuja na ndege ya mchana kutokea Nairobi kwa vile ile ya asubuhi waliyotangulia nayo wenzao kuwa imejaa.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ikiwa chini ya Kocha Kim Poulsen leo inaendelea na mazoezi Uwanja wa Taifa. Mazoezi hayo yataanza saa 9 alasiri.

Moro United yazidi kuporomoka, Morani nao mh!


 

Na Boniface Wambura
WAKALI wa zamani wa kandanda nchini Moro United imezidi kuporomoka baada ya kushuka Ligi Daraja la Pili sambamba na timu nyingine mbili zilizoteremka baada ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Daraja la Kwanza 2012-2013.
Moro Utd iliyowahi kuiwakilisha Tanzania katika michuano yua Kombe la Shirikisho imetemka daraja na sasa itacheza Ligi ya Mkoa msimu ujao wa 2013/2014 baada ya kushika nafasi za mwisho katika ligi daraja la kwanza iliyomalizika wikiendi iliyopita.
Timu nyingine zilizoungana na Moro United ni Small Kids ya Rukwa na Morani ya Manyara zilizoshindwa kufuruka katika makundi yao ya FDL.

Small Kids ya Rukwa imeporomoka kutoka kundi A baada ya kuondolewa kwenye michuano hiyo mapema kwa kushindwa kufika uwanjani kwenye moja ya mechi zake. Kwa mujibu wa kanuni matokeo yote ya mechi ilizocheza yalifutwa.

Moro United ya Dar es Salaam ndiyo iliyoaga FDL kutoka kundi B baada ya kumaliza mechi zake ikiwa na pointi tatu. Wakati kutoka kundi C timu iliyoshuka ni Morani ya Manyara iliyomaliza ligi ikiwa na pointi kumi na moja.

Timu zilizopanda daraja kucheza Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2013/2014 ni Mbeya City ya Mbeya iliyoongoza kundi A ikiwa na pointi 31, vinara wa kundi B timu ya Ashanti United ya Dar es Salaam yenye pointi 29 wakati Rhino Rangers ya Tabora imepanda kutoka kundi C ikiwa na pointi 32.

FIFA yampa ulaji Liunda Kombe la Dunia



Na Boniface Wambura
Mwamuzi Msaidizi wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Leslie Liunda ameteuliwa kuwa mtathimini wa waamuzi (referee assessor) kwenye moja ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia.

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Liunda kutathimini waamuzi kwenye mechi kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Libya itakayochezwa Jumapili (Machi 24 mwaka huu).

Mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Martyrs jijini Kinshasa kuanzia saa 9.30 alasiri kwa saa za Afrika ya Kati (CAT).

Waamuzi watakaochezea mechi hiyo William Selorm Agbovi atakayekuwa mwamuzi wa kati, Malik Alidu Salifu (mwamuzi msaidizi namba moja), David Laryea (mwamuzi msaidizi namba mbili) na mwamuzi wa mezani (fourth official) Cecil Amatey Fleischer. Waamuzi wote hao wanatoka Ghana.

Mohammed Banka akiri Ligi Kuu ya Kenya kiboko

Mohammed Banka (kushoto) akiwa na wachezaji wenzake wa Bandari Kenya

Mohammed Banka (kati) akijifua gym ya klabu yake
KIUNGO mahiri wa zamani wa Simba na Yanga anayecheza soka la kulipwa Bandari Kenya, Mohammed Banka amekiri Ligi Kuu nchini humo ni ngumu yenye ushindani  na ufundi mwingi kulinganisha na Ligi Kuu ya Tanzania.
Akizungumza na MICHARAZO kutoka Kenya, Banka anayeicheza Ligi Kuu ya Kenya kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kuipandisha Bandari toka Ligi Daraja la Kwanza alisema kwa muda fupi tangu waanze kucheza ligi hiyo ameona tofauti kubwa inayomshangaza.
Banka alisema moja ya tofauti ni namna wachezaji wanavyojitambua, wakijituma uwanjani na asilimia kubwa wakiwa na viwango sawia na kutumia nguvu kubwa, kiasi kila timu huwa na gym kuwaweka fiti nyota wake.
"Huku bana ki ukweli wametuzidi wapo vizuri hata uchezaji wao watu wanajua Ligi ya Kenya ni nguvu tu,  hapa licha ya viwango nguvu ni sehemu ya mchezo ndiyo maana hata sisi tuna gym na mwalimu ana siku zake na wachezaji kuingia gym, " alisema Banka.
Tofauti ya pili alisema ni namna klabu zinavyowathamini wachezaji wao na kuwapa kila wanachokihitaji kwa ajili ya kuzipa mafanikio timu zao.
Juu ya timu yake, Banka alisema mpaka sasa imecheza mechi nne ikishinda moja, kufungwa moja na Ulinzi na kutoka sare mbili.
"Sisi tunaendelea vyema tumecheza mechi nne, tukishinda na kupoteza moja na kupata sare mbili na Jumapili tunatarajia kuvaana na Sony Sugar kabla ya kuivaa mabingwa watetezi, Tusker wiki ijayo," alisema Banka.
Alisema mechi yao ya kwanza ilikuwa dhidi ya Ulinzi Stars na kunyukwa bao 1-0 kabla ya kupata sare mbili mfululizo dhidi ya Western Stima (1-1) na City Stars (2-2) na Jumapili walifanikiwa kuilaza Homeboyz kwa mabao 3-2 na kushika nafasi ya tano.

Simba yawananga wanaoikejeli haina fedha

Msemaji wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga
KLABU ya soka ya Simba imetoa ufafanuzi juu ya tuhuma zilizotolewa na baadhi ya wanachama kwamba Simba haina fedha ndiyo maana wameamua kuzunguka mikoani kucheza wakati wakielekea Kagera kuuamana na wenyeji wao, Kagera Sugar.
Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliandika katika wall yake ya Facebook, akifafanua tuhuma hizo na kueleza namna uongozi wa Simba unavyowahudumia wachezaji wao tofauti na kejeli zinazotolewa.
Kamwaga alianza kwa kuandika; Nauli ya bei nafuu kabisa kutoka Dar-Luanda-Dar ni dola 1000 kwa kichwa. Simba imekwenda Angola pasipo kutembeza bakuli kwa mtu. 
Na wote waliosafiri wakalipwa posho kwa USD (si kwa fedha za madafu). Fedha hizo ni mara kumi ya zile ambazo wachezaji walikuwa wakilipwa miaka minne hadi sita iliyopita wakiwa safarini na Simba.... Leo inazushwa kwamba eti Simba haina fedha za kwenda Kagera ndiyo maana inapita Dodoma, Tabora, Shinyanga kucheza ndondo!!!!!! Inachekesha. 
Gharama ya mafuta, kwa sababu Simba ina basi lake, haifikii hata nauli ya mtu mmoja kwenda Angola... Sasa vije leo isemwe eti Simba haina fedha za kwenda Mwanza? Yaani za kwenda Angola zipo ila za Mwanza hakuna? Kuna sababu kubwa mbili kwanini timu inakwenda Kagera TARATIBU. 
Mosi, zaidi ya nusu ya wachezaji waliosafiri wanatoka TIMU B na wengine hawajawahi kufundishwa na Patrick Liewig. Benchi la ufundi liliona ni vema hawa wapate nafasi ya kujaribiwa katika mechi ya kirafiki ili wajue kocha anahitaji nini na kocha awafahamu zaidi wachezaji wake. 
Ikumbukwe pia, kiufundi, Simba haikutakiwa kuwa na mechi kwa wiki zaidi ya mbili kutokana na ratiba iliyozingatia ushiriki wake kwenye Ligi ya MABINGWA. Hiyo ni sababu ya kiufundi. Kuna sababu ya 2 ambayo ni ya kimantiki. Kwamba Simba ni klabu ya Watanzania wote na si wale walioko Dar es Salaam na mikoa yenye timu za Ligi Kuu. 
Kuna mikoa kama Tabora ambayo Simba haijacheza kwa takribani miaka 10 lakini wapo Wana Simba ambao wangependa kuiona. Vivyo hivyo kwa Shinyanga ambapo tulipata sapoti kubwa sana tulipokwenda mwaka jana. Tunahitaji kuwafurahisha wapenzi wetu wa kona zote. 
Tunahitaji pia kutengeneza fan base kubwa zaidi hata kwa watoto ambao wataiona Simba ikicheza Tabora.... Mwaka jana tulipeleka Kombe letu katika baadhi ya mikoa. Mara baada ya kumalizika kwa ligi msimu huu, tuna mpango wa kwenda kwenye mikoa ambayo Simba haijakwenda kwa miaka mingi... 
Mikoa kama vile Rukwa, Kigoma, Singida, Mara, Iringa n.k... Jamani huko kote kuna washabiki wa Simba na watafurahi kuiona ikicheza mbele ya macho yao. TUNASUBIRI KWA HAMU pia tuambiwe tunaenda kucheza ndondo wakati huo ! 
Watu wanafikiri Man United inakwenda China kufanya mazoezi pekee!!!! Hapana, inakwenda kutangaza brand yake ili wapate pa kuuza merchandise yao... Tutakwenda kote itakakowezekana, INSHALLAH... 
Ili mradi Simba ikianza kufanya biashara huko tuendako, na wakati huo utafika tu, tusianze kuulizana tulimtumia MGANGA gani kufanya biashara ya merchandise yetu vizuri.... Hiki ndicho kile rafiki yangu John Shibuda huwa anakiita kwa maneno mawili tu; FIKRA MCHAKATO....