MAZITO yameibuka kufuatia kupigwa risasi kwa Mtangazaji wa
Independent Television (ITV), Ufoo Saro na mtu anayedaiwa ni mzazi
mwenzake, Ateri Mushi, Risasi Mchanganyiko lina mkanda mzima.
Ufoo Saro akitolewa chumba cha upasuaji.
Ufoo alipigwa risasi na mwanaume huyo na kujeruhiwa tumboni na mguuni
katika tukio lililotokea Oktoba 13, mwaka huu nyumbani kwa mama yake
mzazi, Anastazia Saro, Kibamba, Dar es Salaam kufuatia kutoelewana kati
ya wawili hao.
Katika tukio hilo la kutisha, Ateri pia alimuua kwa risasi mama wa Ufoo na kujiua mwenyewe na maiti zao kupelekwa Muhimbili.
MAZITO YALIYOIBUKA
Juzi, Shekilango, Ubungo jijini Dar, Risasi Mchanganyiko lilizungumza
na rafiki mmoja wa marehemu Ateri aliyejitambulisha kwa jina moja la
Urassa ambaye aliweka wazi mambo anayoyajua kuhusu marehemu kabla ya
kujiua kwa risasi.
Alisema tangu mwaka huu (2013) uanze, marehemu Ateri alikuwa akilalamika kwamba, anampenda sana Ufoo lakini hamuelewielewi.
“Tangu mwaka huu ulipoanza nimekuwa
nikiwasiliana na Ateri. Alikuwa akisema anampenda sana Ufoo lakini kama
hamuelewielewi katika mambo fulani ya uhusiano.
“Alisema kukaa kwake
mbali (Sudan) na mchumba wake huyo anahisi kama mambo yanakwenda
kufikia mwisho wa uchumba wao. Kwa jumla Ateri alishajua nini atakifanya
mwaka huu kuhusu uhusiano wake na yule mtangazaji maana maneno yake
mengi yalikuwa ni malalamiko tu,” alisema Urassa.
MAREHEMU ALISEMA AMECHOKA KUISHI
Akienda mbele zaidi, Urassa alisema Septemba, mwaka huu marehemu
alimpigia simu na kumwambia anahisi amechoka kuishi kwenye dunia hii
yenye maumivu ya mapenzi kila kukicha.
“Nilimuuliza amechoka kuishi
kivipi? Akanijibu anaona kuna mambo hayaendi sawa kama anavyotaka yeye
kwa huyo mchumba wake. Lakini kwenye simu hakuniambia kama hayo mambo ni
yapi? Ila nahisi ni mapenzi yao,” Urassa alizidi kutoboa.
Ufoo Saro.
ALIIBUA TABIA YA KUPENDA KUSALI
Katika mazungumzo na Urassa, pia
alimgusia marehemu kwamba kwa siku za karibuni aliibua tabia ya kusali
kila wakati kuliko siku za nyuma.
“Siku moja akiwa Sudan alinipigia
simu, akasema anapenda kama mahali anapoishi kule pangekuwa na kanisa
karibu ili awe anasali alfajiri, mchana na jioni lakini akaniambia kule
hakuna makanisa.
“Nilimuuliza mbona amepanga kusali mara tatu zote
hizo kwa siku, akanijibu binadamu tunatakiwa kujiandaa kwani saa yoyote
roho inaweza kutoka,” alisema Urassa.
Baadhi ya wananchi na wanahabari wakiwa hospitalini kujua hali ya Ufoo.
MAREHEMU ALIKUWA AKILIA WIVU
Risasi Mchanganyiko: Kwa hiyo
unawaza nini kuhusu marehemu kumuua mama mkwe wake na kumjeruhi mchumba
wake kisha na yeye kujimaliza?
Urassa: Kwa kweli ninavyojua mimi ni
wivu tu. Unajua yule alikuwa yuko kikazi Sudan, mchumba wake yupo Dar.
Mfano siku moja aliniambia anatamani apate mtu wa kumfuatilia Ufoo
kwenye nyendo zake za kila siku kwani anahisi anaibiwa japo hakuniambia
kama ana uhakika.
DALILI ZA MAUAJI ZILIONEKANA MAPEMA
Kwa mujibu
wa ndugu, licha ya kwamba hawakujua litakalotokea mbele, lakini baada
ya kutokea ndiyo wamebaini kwamba marehemu Mushi alishabadilika roho
muda mrefu.
Walisema uchangamfu na utani aliokuwa nao siku za nyuma
alipokuwa akienda kuwatambelea viliisha ghafla kwani hivi karibuni
alikuwa akienda, baada ya salamu hakuwa akiongeza neno.
LENGO LA MAREHEMU
Kwa mujibu wa watu waliofika nyumbani kwa mama Ufoo mapema, marehemu alionesha dalili za kuteketeza familia hiyo.
“Huyu bwana (marehemu) nahisi alitaka kutekeza familia, maana kabla ya
kujiua yeye, alipiga risasi mtungi wa gesi ukiwa na nguo, ukalipuka.
Sasa hapo unadhani lengo lake lilikuwa nini kama si kuiangamiza familia
yote ya mzee Peter Saro?” alisema jirani mmoja kwa mtindo wa kuhoji.
UFOO ALILIJUA HILO
Habari zinasema baada ya Ufoo kupigwa risasi, akiwa anatambaa na damu
zake tumboni aliwataka ndugu zake kutotoka kwani shemeji yao alikusudia
kuwaua wote. Kauli ya Ufoo inakwenda sambamba na madai ya mzee aliyesema
dhamira ilikuwa kuiangamiza familia hiyo.
ALIKUWA HAELEWANI NA BABA WA UFOO
Godluck Saro ni mdogo wa Ufoo, yeye akizungumza na gazeti hili juzi,
nyumbani kwao, Kibamba, Dar alisema marehemu shemeji yake alikuwa
haelewani kabisa na baba wa Ufoo, marehemu mzee Peter Saro aliyefariki
dunia Julai 16, 2011 kwa shinikizo la damu.
“Kwanza shemeji alianza
kufika hapa nyumbani baada ya baba kufariki, kabla ya hapo alikuwa
hafiki maana walikuwa hawaelewani kabisa. Baba alikuwa anasema shemeji
ni mkorofi, hawezi kuwa mume wa dada,” alisema kijana huyo.
MAJIRANI WA KWA UFOO
Juzi, Risasi Mchanganyiko lilipata bahati ya kuzungumza na baadhi ya
majirani wa kwa Ufoo, Mbezi jijini Dar es Salaam ambapo karibu wote
walidai kusikia majibizano ya muda mrefu usiku wa kuamkia siku ya tukio.
“Tulisikia majibizano kwa muda mrefu ule usiku, lakini si ya wazi sana
kiasi cha kumfanya mtu ajue nini kilikuwa kinaongelewa,” alisema jirani
mmoja.
“Mimi alfajiri wakati wanaondoka niliwasikia, lakini sikujua
wanakwenda wapi na nilijua wapo na amani tu kwani hakukuwa na mazungumzo
ya ugomvi,” alisema jirani mwingine.
UFOO NA MAREHEMU
Ufoo
yeye bado amelazwa Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu. Yeye na
marehemu walibahatika kupata mtoto mmoja wa kiume, Alvin Ateri Mushi.
MAZISHI YA WOTE
Juzi, ndugu wa marehemu Mushi walikutana katika kikao cha ratiba ya
mazishi pale 92 Hotel, Shekilango - Ubungo, Dar ambapo walisema mwili wa
marehemu utasafirishwa kabla ya Ijumaa kwenda kijijini kwao Uru, Moshi
kwa mazishi.
Mwili wa marehemu Anastazia ulisafirishwa
jana kwenda Machame, Moshi ambapo mazishi yake yalipangwa kufanyika leo
katika eneo hilo.
Mwenyezi Mungu aziweke pema peponi roho za marehemu. Amina.
GPL