|
Jaja hakufua dafu kwa vijana wa Mtibwa kwani alikosa penati |
|
Watetezi Azam walioanza kwa kishindo kwa kuilaza Polisi Moro |
|
Yanga iliyokufa Morogoro na Jaja wao |
|
JKT Ruvu walioanza kwa suluhu dhidi ya Mbeya City |
|
Prisons walioanza kwa ushindi wa mabao 2-0 ugenini mbele ya Ruvu Shooting |
|
Mbeya City |
MSHAMBULIAJI Didier Kavumbagu ameifungia Azam mabao mawili na kuwasaidia mabingwa watetezi hao kuanza vyema Ligi Kuu Tanzania Bara, huku timu yake ya zamani, Yanga ikifa Morogoro kwa mabao 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar.
Kavumbagu aliyekuwa mfungaji tegemeo wa Yanga kwa misimu miwili akiwa na kikosi hicho alifunga mabao yake katika dakika ya 14 na 90 wakati Azam wakiizamisha Polisi Morogoro kwa mabao 3-1 katika mechi iliyochezwa uwanja wa Chamazi.
Bao jingine la watetezi hao waliotoka kunyukwa mabao 3-0 na Yanga kwenye mechi ya Nago ya Jamii liliwekwa kimiani na nahodha wa zamani wa Azam, Aggrey Morris dakika ya 23 wakati Polisi walipata bao lao la kufutia machozi dakika ya 60.
Katika mechi nyingine iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa nchini iliyochezwa uwanja wa jamhuri, Morogoro, Yanga ilishindwa kutamba mbele ya Mtibwa Sugar kwa kukandikwa mabao 2-0, huku nyota wake mpya, Jaja akikosa penati na mabo mawili ya Yanga yakikataliwa na mwamuzi kwa madai wafungaji Simon Msuva na Mrisho Ngassa wameotea.
Mussa Hassan Mgosi alianza kuitia aibu Yanga kwa kufunga bao la kuongoza dakika ya 16 kabla ya Ame Ali kuongeza bao la pili dakika ya 82 na kuifanya Yanga kushindwa kuamini kama kwa miaka minne mfululizo wameshindwa kupata ushindi kwenye dimba la Jamhuri mbele ya Mtibwa inayonolewa na nahodha wa zamani wa Stars Mecky Mexime.
Mwamuzi Dominick Nyamisana wa Dodoma, alitoa adhabu ya penati kwa Yanga dakika ya 46, lakini Genilson Santana Jaja alikosa baada ya mkwaju wake kupanguliwa na kipa wa zamani wa Yanga, Said Mohammed.
Mwamuzi huyo aliyakataa mabao mawili ya Yanga katika dakika ya 47 na 49 kwa madai washambuliaji wa Yanga Simon Msuva aliyetokea benchi na Ngassa kuotea.
Katika mechi nyingine Mbeya City na JKT Ruvu zimetoshana nguvu kwa kutoka suluhu, huku maafande wa Ruvu Shooting wakifa nyumbani kwao Mlandizi kwa mabao 2-0, huku Ndanda Fc ikianza ligi kwa kishindo kwa kuilaza wageni wenzao Stand United kwa mabao 4-1 mjini Shinyanga.
Nayo Mgambo ilianza vema ligi hiyo kwa kupata ushindi mwembamba nyumbani dhidi ya Kagera Sugar baada ya kuwazamisha wakata miwa hao bao 1-0. Bao pekee la mchezo huo lilifungwa na ramadhani Pela na kuifanya Mgambo kuanza tofauti iliyovyokuwa msimu uliopita ilipopigana kuepuka kushuka daraja.