STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, December 16, 2014

Dirisha dogo lafungwa, 15 waombewa ITC

http://www.rockersports.co.tz/wp-content/uploads/2014/11/meshak.jpg
Meshack Abel alipokuwa Bandari Fc
http://shaffihdauda.co.tz/wp-content/uploads/2014/11/wawa-2.jpg
Wawa
 
 USAJILI wa dirisha dogo msimu wa 2014/2015 umefungwa rasmi jana (Desemba 15 mwaka huu) huku wachezaji 15 kutoka nje wakiombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kutoka nchi mbalimbali.
Wachezaji walioombewa ITC kwa timu za Ligi Kuu ni Abdulhalim Humoud kutoka Sofapaka ya Kenya kwenda Coastal Union, Brian Majwega kutoka KCC (Uganda) kwenda Azam na Castory Mumbara kutoka Three Star Club (Nepal) kwenda Polisi Mara.
Wengine ni  Charles Misheto kutoka SP Selbitiz (Ujerumani) kwenda Stand United na Chinedu Michael Nwankwoeze kutoka Nigeria kwenda Stand United.
Pia wamo Dan Serunkuma kutoka Gor Mahia (Kenya) kwenda Simba, Emerson De Oliveira Neves Roque kutoka Emerson De Oliveira Neves Roque kutoka Bonsucesso FC (Brasil) kwenda Yanga, Halidi Suleiman kutoka Flambeau (Burundi) kwenda Stand United na Juuko Murushid kutoka SC Victoria University (Uganda) kwenda Simba.
Wachezaji wengine ni Kpah Sean Sherman kutoka Aries FC (Liberia) kwenda Yanga, Meshack Abel kutoka KCB (Kenya) kwenda Polisi Morogoro na Moussa Omar kutoka Flambeau (Burundi) kwenda Stand United.
Pia wamo Nduwimana Michel kutoka Flambeau (Burundi) kwenda Stand United, Serge Pascal Wawa kutoka El Merreikh (Sudan) kwenda Azam na Simon Serunkuma kutoka Express FC (Uganda) kwenda Simba.
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF inatarajia kukutana hivi karibuni kwa ajili ya kupitia usajili wa wachezaji wote walioombewa katika dirisha dogo wakiwemo wale wa mkopo.

Breaking News! Jaji Werema aachia ngazi

http://2.bp.blogspot.com/-HfIVzV9HEPE/Uq2Qh28re9I/AAAAAAAALfk/iZ76iAX0yLA/s640/1.png
jaji Werema aliyetangaza kuachia ngazi mwenyewe

HABARI zilizotufikia hivi punde zinasema kuwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema ametangaza kujiuzulu nafasi yake hiyo.
Habari hizo zinasema Jaji Werema mmoja wa vigogo wanaotuhumiwa kuhusika na sakata la uchotwaji wa fedha za Akaunti za Tegeta Escrow zipatazo zaidi ya Sh Mil 300.
Kwa mujibu wa taarifa hizo zinasema kuwa Jaji Werema ameamua kujiuzulu mwenyewe kwa hiari yake na kwamba Rais Jakaya Kikwete ameafikiana na maamuzi hayo na kumshukuru kwa ujtendaji wake na kumtakia kila la heri katika maisha yake mapya.
Hata hivyo taarifa hizo zinasema kuwa, maamuzi hayo yamekuja baada ya shinikizo kubwa ambalo limekuwa likitolewa kila pembe ya nchi kwa Rais JK kuwawajibisha wote waliotajwa kwenye mapendekezo nane ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhusiana na sakata hilo ambalo limeitia doa Tanzania mbele ya nchi wahisani.
MICHARAZO itazidi kuwaletea habari zaidi.

Gwiji Shem Karenga afariki, kuzikwa leo Kisutu

Shem Ibrahim Karenga enzi za uhai wake.
MWANAMUZIKI mkongwe nchini aliyekuwa amejaliwa kipaji cha kuimba na kucharaza gitaa kiongozi la Solo, Shem Ibrahim Karenga amefariki dunia jana akiwa katika Hospitali ya Amana  jijini Dar es Salaam alipokuwa akitibiwa na anatarajiwa kuzikwa leo.
Marehemu Kalenga anayekumbukwa kupitia tungo zake mbalimbali zilizochangia kumpa umarufu, alizozifyatua akiwa na bendi mbalimbali kama vile ‘Tucheze Segere’, ‘Muna’, ‘Kila jambo’ na ‘Mbelaombe’, alifariki asubuhi ya jana wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEg4wpGMAyOuYjuumKhAvBULpmmVN7j8iYWt3pn5pydekJm6qKAiT67ntH80ZpBjtDt7c9s5ewZsTIyWO4J9KC5B1o4Ysw0YVAM2VwbCPtbXVXaa8jSxvRwJfjtiRK2dkhGi_ETYZuaP9pM/s1600/DSCN9027.JPG
Mzee Shem Karenga akiwa jukwaani enzi za uhai wake
Kwa mujibu wa Kiongozi wa bendi ya African Minofu, Joseph Matei, marehemu aliugua siku chache zilizopita kabla ya kukumbwa na mauti na kwamba anatarajiwa kuzikwa leo kwenye Makaburi ya Kisutu jijini Dar. 
Gwiji hilo Shem Karenga alizaliwa mwaka 1950, Bangwe, Kigoma na kupata elimu ya msingi katika shule ya kimishionari ya Kihezya kuanzia mwaka 1957 hadi mwaka 1964.  
Mwaka 1964 alijiunga na bendi ya Lake Tanganyika Jazz ambayo maskani yake yalikuwa mjini Kigoma. Mwaka 1972, aliitwa kwenye bendi ya Tabora Jazz kama mwanamuziki mwenye kipaji cha utunzi, mwimbaji na mpigaji wa gitaa la Solo. 
Mwaka 1983 alijiengua kutoka Tabora Jazz na kusimama kabisa kujihusisha na muziki, ambako kilichofuatia ilikuwa ni kifo cha bendi hiyo. 
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEivfVcUbJ3EtZF8fu2-MOehiBeFARjSF0W4Bund8Mk9Yk8pE7YiR7QXlX-T5zL8HBGKVAWTiHGmYR_8WHcw-M_xFKwTjYZTAtr96hyO37PwP9VLqzVfNV2QuAe7U-QsKxqGDtsRQHvaCdA/s1600/PICTURE+07.jpg
Shem Karenga akicharaza gitaa na kuimba kiasi cha kumkuna Mayaula Mayoni (kulia)
Mwaka 1990 aliondoka Tabora na kutua jijini Dar es Salaam. Mwaka 1990 alijiunga na MK Beats. 
Mwaka 1995, MK Beats ilisambaratika, ambako mwaka uliofuata, yaani 1996 alianzisha bendi ya Tabora Jazz Star kwa kushirikiana na Ibrahim Didi. Mpaka mauti yanamfika, Shem Karenga Mkurugenzi Msaidizi katika Bendi ya Tabora Jazz Star ambapo Mkurugenzi Mkuu ni Ibrahim Didi. Moja ya vibao vyake viliwahi kunyakuliwa na kurejewa na kundi la Sokousou Stars kuonyesha alivyokuwa mkali.
MICHARAZO inatoa pole kwa ndugu, jamaa na familia ya marehemu pamoja na wanamuziki na wadau wote wa fani ya muziki nchini kwa msiba huo.
MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU Mahali PEMA PEPONI.

Jennifer Mgendi 'aifumua' Shelina

Muimbaji na muigizaji filamu, Jennifer Mgendi
MUIMBAJI nyota wa muziki wa Injili nchini ambaye pia ni mtayarishaji na muigizaji wa filamu, Jennifer Mgendi amesema anaifanyia marekebisho filamu yake mpya ya 'Shelina' kuwa filamu fupi ya mfumo wa wimbo ili kuzidi kuwapa raha mashabiki wake.
Akizungumza na MICHARAZO, Jennifer alisema ameona ni vema kuibadilisha 'Shelina' kuwa katika mfumo mwingine ili kuwapa ladha tofauti mashabiki wake ambao wamemzoea katika kazi nyingine alizowahi kuzitoa nyuma.
Jennifer alisema atautumia wimbo wake uitwao 'Kaa Chonjo'.
"Nimeamua kufanyia marekebisho filamu yangu ya 'Shelina' na sasa naitengeneza kama filamu fupi ya mfumo wa wimbo, nikiutumia wimbo wa 'Kaa Chonjo," alisema Jennifer anayejiandaa kuachia albamu yake ya nane iitwayo 'Wema ni Akiba'.
Filamu hiyo ya 'Shelina' inakuja wakati akitamba na kazi yake iitwayo 'Mama Mkwe' ambayo inaendelea kusumbua sokoni.
Mbali na 'Mama Mkwe', Jennifer pia amewahi kutamba na filamu nyingine kama  'Chai ya Moto', 'Joto la Roho', 'Teke la Mama', na 'Pigo la Faraja'.

Salha wa Hammer avunja ukimya na Kishtobe cha Mtaa

MUIMBAJI nyota wa muziki wa taarab, Salha Abdallah amevunja ukimya baada ya kutoka kwenye likizo ya uzazi kwa kuibuka na wimbo uitwao 'Kishtobe cha Mtaa' uliopo kwenye albamu mpya ya kundi la Five Star Modern.
Akizungumza na MICHARAZO, Salha maarufu kama 'Salha wa Hammer' alisema wimbo huo ni miongoni mwa nyimbo tano zitakazokuwa katika albamu yao itakayozinduliwa Ijumaa wiki hii.
Salha alisema wimbo huo ni wa kwanza kwake tangu alipoenda likizo ya uzazi na kuwataka mashabiki wajitokeze kwa wingi kwenye uzinduzi huo ili kupata uhondo toka kwake na wanamuziki wote wa Five Star.
"Baada ya likizo ya uzazi, hatimaye natarajia kuanza kazi na wimbo wa 'Kishtobe cha Mtaa' ambao nimekiimba mwanzo mwisho nikisaidiana na akina Mwape Kibwana na wengine kitakuwa kwenye albamu itakayozinduliwa Ijumaa," alisema Salha.
Mbali na wimbo huo wa Salha, albamu hiyo ya 'Kichambo Kinakuhusu' ina nyimbo za 'Big Up Dear', 'Ubaya Hauna Soko', 'Sina Gubu Nina Sababu' na 'Kichambo Kinakuhusu' wenyewe.

Everton yaiangamiza QPR, Redknapp maji ya shingo!

QPR striker Bobby Zamora scores against Everton
Bobby Zamora akimtungia Howard
Everton midfielder Ross Barkley
Barkley akifunga bao la kuongoza la Everton kwa shuti kali
KLABU ya Everton usiku wa kuamkia leo wamepata ushindi mwepesi nyumbani baada ya kuifumua QPr mabao 3-1 na kuzidi kukwea katika Ligi Kuu ya England inayozidi kushika kasi.
Ross Barkley alifunga kwa shuti kabla la mita 20 katika dakika ya 33, kabla ya Kevin Mirallas kufungwa kwa mpira wa adhabu ndogo katika dakika ya 43 na mpira wa kichwa wa Steven Naismith kwenye dakika ya 53 yalitosha kuwaangamiza QPR inayonolewa na kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur, Harry Redknapp.
QPR ambao kipigo hicho kilikuwa cha nane ugenini katika ligi ya msimu huu, ilipata bao la kufutia machozi katika dakika ya 80 kupitia Bobby Zamora aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Tim Howard.
Ushindi huo umeifanya Everton kuitambuka wapinzani wao wa jadi Liverpool wsanaolingana nao pointi 21 na kukaa nafasi ya 10 huku Reds wakiporomoka hadi nafasi ya 11. wakati QPR wamesalia katika nafasi ya tatu toka mkiani wakiwa na pointi 14, nne zaidi ya timu inayoshilikia mkia ya Leicester City.

Manchester Utd yatabiriwa kutwaa ubingwa wa England

http://i.huffpost.com/gen/1226648/thumbs/o-PHIL-NEVILLE-570.jpg?6
Phil Neville enzi akiichezea Manchester United kabla ya kutimkia Everton
USHINDI wa mara sita mfululizo katika mechi zake za Ligi Kuu ya England iliyopata klabu ya Manchester United kumetajwa ni dalili za kurejea kwenye 'fomu' yake na kutabiriwa kutwaa ubingwa wa msimu huu.
Nyota na kocha msaidizi wa zamani wa klabu hiyo, Phil Neville, amenukuliwa akisema kwamba klabu hiyo ina nafasi kubwa ya kuwa mabingwa wa England baada ya kutulia kutoka kwenye misukosuko ya msimu msimu uliopita.
"Ndiyo wanaweza'' alisema Neville aliyenyakua mataji sita ya Ligi Kuu ya England akiwa kama mchezaji kabla ya kuangukia kuwa miongoni mwa makocha msaidizi chini ya David Moyes aliyetimuliwa.
 "Wachezaji wanaamini wanaweza kutwaa taji na hilo Louis Van Gaal anaweza kulifanya," alisema Neville.
Kauli ya Neville imekuja baada ya Manchester United kupata ushindi wa sita mfululizo kwa kuifumua Liverpool kwa mabao 3-0 katika pambano lililochezwa siku ya Jumapili.
Kabla ya hapo klabu hiyo ilionekana kuyumba kiasi cha mashabiki kuanza kupoteza imani kwa Van Gaal kabla ya kocha huyo kuwatuliza na kuanza kuwapa raha kwa kushinda mfululizo.
Mechi hizo sita za Manchester United iliyoshinda mfululizo ni hizo hapo chini:

8 November:  Crystal Palace 1-0 (nyumbani)
22 November: Arsenal 2-1 (ugenini)
29 November: Hull 3-0 (nyumbani)
2 December: Stoke 2-1 (nyumbani)
8 December: Southampton 2-1 (ugenini)
14 December: Liverpool 3-0 (nyumbani)

Nyota Manchester Utd katika 'kashfa' ya rushwa Hispania

http://www4.pictures.zimbio.com/gi/Manchester+United+v+Valencia+ODBuEmnisftx.jpg
Ander Herrera anayetuhumiwa kwa upangaji matokeo ya mechi ya La Liga 2011
http://www4.pictures.zimbio.com/gi/Jefferson+Montero+Exeter+City+v+Swansea+City+Rttkn623zmEl.jpg
Montero naye yumo katika mkumbo huo
http://static.goal.com/187500/187540_heroa.jpg
Nahodha Gabi,  naye anatuhumiwa
http://static.weltsport.net/picmon/e9/dVK_baa3z_l.jpg
Kocha Aguirre

KIUNGO nyota wa Manchester United, Ander Herrera na nahodha wa Atletico Madrid, Gabi ni miongoni mwa wachezaji wanaochunguzwa kwa kujihusisha na tuhuma za upangaji wa matokeo ya mechi ya kufungia msimu wa 2010-2011 wa Ligi Kuu ya Hispania.
Wengine waliohusishwa na kadhia hiyo ni Kocha wa zamani wa Real Zaragoza anayefundisha timu ya taifa ya Japan Javier Aguirre na mchezaji wa Swansea City, Jefferson Montero.
Kwa mujibu wa BBC, Mwendesha Mashtaka wa Idara ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Hispania Alejandro Luzon, ameiagiza Mahakama kumchunguza kocha wa zamani wa klabu ya Real Zaragoza na baadhi ya wachezaji kutokana na tuhuma za kudaiwa kuuza mchezo dhidi ya Levante.
Katika pambano hilo la kufungia msimu Zaragoza ilishinda mchezo huo kwa mabao 2-1 na kuepuka kushuka daraja, lakini sasa imebainika kuwa matokeo hayo yalipangwa baada ya kutembezwa mlungula.
Upande wa mashitaka uliowasilisha mashtaka yake katika Mahakama mjini Valencia jana Jumatatu, unadai kuwa watuhumiwa wanahusishwa na rushwa ya dola million mbili. 
Baadhi ya wachezaji wanaotuhumiwa katika kashfa hiyo ni Kiungo wa Manchester United aliyewahi kukipiga Zaragoza wakati wa mchezo huo kabla ya kuhamia Athletico Bilbao, Ander Herrera, anayeichezea Manchester United, nahodha wa Atletico Madrid, Gabi, Montero na Javier Aguirre.
Inadaiwa kuwa wachezaji wa Lavante walishikishwa fedha ili kupoteza pambano hilo na kuinusuru Zaragoza isishuke daraja katika pambano la Mei 21, 2011.
Jumla ya watu 41 wakiwamo wachezaji, makocha na wakurugezi wa timu hizo mbili wamehusishwa katika upangwaji huo wa matokeo ya pambano hilo.

Kumekucha! Maximo atupiwa virago kama Brandts, Pluijm arejeshwa

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEirHsHAOLesgeko6449ITJAGxd3GFzvxJ4YBsnuG54Z_IHmqZpPn0Rcn5HtpJ20BHmV_Xmm3ra1JRpa1YBgtVVw-KSoIGH0WZJvcJpteX_m9EYMWT_OK1dT-MVqydunhScqSyS6RsOndkH5/s1600/DSC_0306.JPG
Marcio Maximo na msaidizi wake Leonardo Neiva wakati wakiinoa Yanga

KAMA ilivyokuwa kwa kocha Ernie Brandts aliyetimuliwa baada ya Yanga kufungwa na Simba kwenye mchezo wa 'bonanza' wa Nani Mtani Jembe, hali hiyo imemkuta Marcio Maximo.
Kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars kutoka Brazil ametimuliwa Yanga baada ya kipigo cha mabao 2-0 katika pambano la Nani Mtani Jembe-2.
Taarifa ambazo ni za uhakika toka ndani ya Yanga zinasema kuwa, kocha Maximo amepewa mkono wa kwaheri na nafasi yake inarudi kwa aliyekuwa kocgha wa timu hiyo  Hans Van Der Pluijm.
Mmoja wa viongozi wa kamati ya utendaji ya klabu ya Yanga amesema, Maximo ataondoka nchini ndani ya siku tatu baada ya kukubaliana na uongozi.  
"Si kwamba amefukuzwa, lakini ni makubaliano kwamba anaondoka.  
"Ni kweli, lakini msitake kulikuza hili jambo ionekane kama tumemfukuza," aliuliza na alipotakiwa kujua mrithi ni nani, alikataa kusema.  
Hata hivyo ni kwamba Maximo amepewa mkono wa KWAHERI sambamba na kiungo aliyekuja naye toka kwao, Emerson Oliveira ambaye inaelezwa amekosa ITC japo ukweli ni kwamba ameonekana ni bomu.
Yanga ilimfurusha Brandt na wasaidizi wake, Fred Felix Minziro na Razack Ssiwa baada ya timu yao kulala mabao 3-1 na safari hii Maximo anaondoka na wasaidizi wake akiwamo Mbrazil mwenzake Leonardo Neiva ambaye alimleta baada ya kusaini mkataba.