Kijogoo katika pozi tofauti |
Muigizaji huyo wa kundi la Jakaya Arts linalotamba na michezo yake kupitia kituo cha runinga cha ITV, anasema alikuwa 'kichaa wa soka' akishiriki michezo ya Shule za Msingi na Sekondari na kucheza Ligi Daraja la Nne katika timu ya Burudani kabla ya Frank aliyekuwa Kaole Sanaa kumhamisha na kuwa muigizaji.
"Kipaji cha uigizaji ni cha kuzaliwa nacho, ila Frank ndiye aliyenifanya nibadili mawazo yangu katika sanaa, ninashukuru ndoto nilizokuwa nazo tangu nijitose kwenye fani hiyo zimeanza kuonekana japo sijaridhika," anasema Kijogoo.
Msanii huyo anasema enzi akicheza soka alimudu nafasi za ushambuliaji kuanza namba 7, 8, 9 na 10 na baadhi ya rafiki zake wanashangaa kukuona kwenye sanaa kwa umahiri aliokuwa nao katika mchezo huo, japo anaendelea ila siyo kama zamani.
Kijogoo anasema aliingia jumla katika uigizaji mwaka 2010 kupitia kundi la Jakaya Arts, igizo lake la kwanza likiwa ni 'Riziki' kabla ya kufuatiwa na 'Barafu la Moto', 'Mapito', 'Donda la Kichwa', 'Ulimbo' na igizo lililoisha hivi karibuni la 'Chekecheo anaoutaja kama mchezo bomba kwake.
Mbali na tamthilia, Kijogoo ambaye ni kocha wa timu ya soka ya kikundi hicho cha Jakaya, anaigiza pia filamu baadhi ya kazi alizocheza ni 'Mahaba Niue', 'Like Father Like Son', 'XXL', 'Best Player' na nyingine.
"Kwa kweli nashukuru sanaa imesaidia kunitambulisha mbele ya jamii, naingiza kipato kinachonisaidia kuendesha maisha yangu pia na mengine ambayo sikutegemea," anasema na kuongeza;
"Hata hivyo sijaridhika hadi nije kutamba kimataifa na kumiliki kampuni yangu binafsi ya kuzalisha filamu na kuwasaidia chipukizi, ambao wamekuwa wakipuuzwa pale wanapohitaji msaada," anasema.
UHASIBU
Kijogoo shabiki mkubwa wa Yanga na Arsenal akiwazimia nyota wa timu hizo, Haruna Niyonzima na Mesut Ozil, mbali na usanii na uanasoka kitaaluma ni Mhasibu aliyesomea fani hiyo Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).
Mkali huyo anayependa kula pilau na kunywa vinywaji mchanganyiko, anasema anafurahi kuhitimu masomo yake hayo akitarajia kutunikiwa shahada yake hivi karibuni na kudai ametimiza ndoto zake za utotoni za kuwa mhasibu.
"Nilikuwa na ndoto za kuja kuwa Mhasibu na ninashukuru ndoto hizo zimetimia baada ya kuhitimu masomo yangu na ninamshukuru kaka yangu Rabson Gilliard aliyenisomesha na kunikazania masomo kwani wazazi wetu wote walishafariki na yeye kubeba jukumu la kutusaidia wadogo zake," anasema.
Msanii huyo anakiri hakuna tukio linalomtoa machozi mpaka leo kama hilo la kuwapoteza wazazi wake wote japo kwa nyakati tofauti kutokana na ukweli wazazi ni kila kitu na nguzo ya maisha ya binadamu yeyote, japo anamshukuru Mungu kwani ni yeye aliyeumba na ni yeye anayetwaa.
Kijogoo anayemzimia kwa sasa Jacob Stephen kwa umahiri wake wa kuigiza nchini, anasema sanaa ya Tanzania imepiga hatua kubwa lakini imekuwa haina manufaa kwa wasanii kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwemo wizi na unyonyaji.
Pia anasema fani hiyo ni ngumu tofauti na wengi wanavyoichukulia na hasa msanii anapokuwa mchanga kwa kushindwa kupewa sapoti kwa waliomtangulia.
Kuhusu skendo zinazofanywa na wasanii wachache, Kijogoo anasema hiyo inatokana na ushamba na ujinga walionao baadhi yao kwa kudhani kujihusisha na skendo kutawasaidia kupata umaarufu wa haraka ilihali wanajiharibia mbele ya jamii na kusababisha sanaa nzima kuonekana kama ya wahuni, kitu ambacho sicho.
"Mimi nawaona ni kama wajinga kwa sababu mtu mwenye akili zake hawezi kukubali kila siku kuandikwa kwa mambo ya upuuzi, umaarufu unakuja kwa mtu kuchapa kazi kwa ufanisi, hivyo wasanii wajitambue wao ni kioo cha jamii na kubadilika kwani wanajiharibia pengine tunakosa hata matangazo kwa matendo maovu yanayofanywa na wachache wetu," anasema.
ALIPOTOKA
Boniface Gilliard alizaliwa Machi 16, 1985 jijini Dar es Salaam akiwa ni mtoto wa nane kati ya 9 wa famili yao na alisoma Shule ya Msingi Mwananyamala Kisiwani kabla ya kujiunga na masomo ya Sekondari katika Shule ya Kambangwa jijini Dar es Salaam na kumalizia Ifunda-Iringa kabla ya kujiunga Chuo cha IFM.
Msanii huyo anayechizishwa na nguo za rangi ya maziwa (cream), anasema wakati akisoma alishiriki kwenye sanaa na michezo akiigiza, kuimba na kucheza soka akishiriki michuano ya UMISHUMTA na ile ya UMISSETA huku akicheza pia Ligi Daraja la Nne wilayani Kinondoni.
Alikuja kuachana na soka alipotua Jakaya Arts na kuhamishia akili zake katika sanaa akishiriki michezo na filamu mbalimbali.
Kijogoo anayefurahishwa na tukio la kuzaliwa kwa mwanae wa pekee aliyenaye sasa Nabri anaiomba serikali iwasaidie wasanii kuondokana na wizi wanaofanyiwa katika jasho lao pamoja na kuwathamini kama inavyowathamini wanapokuwa wakiwatumia katika shughuli zao ikiwamo kampeni na uhamasishaji wa mambo mbalimbali.
"Wasanii unajua tumegeuzwa kama karai la kujengea, hatuthamini mpaka nyumba inapohitaji kukarabatiwa, tuthaminike na kusaidiwa vipindi vyote na siyo wakati wa shughuli maalum tu za kiserikali au kisiasa," anasema.
Msanii huyo anayemshukuru kaka yake na ndugu zake kwa ujumla, kundi zima la Jakaya Arts na rafiki zake wote ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakimpa sapoti.
Kijogoo anasema anapenda kutumia muda wake wa ziada kuangalia soka, muvi na kubadilishana mawazo na watu wengine sambamba na kufanya mazoezi.