Oljoro JKT |
Ashanti United |
Timu hizo zinazofuata toka mkiani zikiwa juu ya Rhino Rangers inayoburuza mkia na pointi zake 13 zitaumana kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Ni ushindi pekee kwa kila timu utafufua matumaini ya kuendelea kucheza ligi ya msimu ujao, vinginevyo huenda wakajiweka pabaya zaidi kushuka daraja kama walivyo wenzao wa Rhino ambao watashuka dimbani Jumapili dhidi ya JKT Ruvu.
Ashanti inayonolewa na kocha Abdallah Kibadeni ina pointi 18 ikiwa nafasi ya 12, huku wapinzani wao wakiwa chini yao na pointi 16 kila moja ikiwa imecheza mechi 22.
Kila timu inahitaji ushindi ikizingatiwa zimetoka kuchezea vichapo katika mechi zao zilizopita, Ashanti ikizamishwa mabao 2-0 na Ruvu Shooting na Oljoro ikizabuliwa na Azam.
Timu hizo zilizobadilisha makocha baada ya kuyumba kwenye duru la kwanza, zimekuwa kama homa ya vipindi kwa viwango vyao kupanda na kushuka kulingana na aina ya mechi.
Kivumbi zaidi cha ligi hiyo kitakuwa Jumapili ambapo viwanja sita vitawaka moto kwa kuzikutanisha timu 12 zikiwamo tatu zinazowania taji la ubingwa wa ligi hiyo linaloshikiliwa kwa sasa na Yanga.
Azam watakuwa kwenye uwanja wa Taifa kuivaa Simba, ikihitaji ushindi ili kuujongelea ubingwa huo na pia kuiombea mabaya Yanga watakaokuwa ugenini mjini Tanga kupepetana na Mgambo JKT iteleze katika mechi yake hiyo itakayopigwa uwanja wa Mkwakwani.
Azam ina pointi 50, nne na ilizonazo Yanga licha ya kuwa mbele kwa mchezo mmoja na timu yoyote ikiteleza itatoa nafasi kwa mwenzake kuubeba ubingwa huo kwa msimu wa 2013-2014.
Mbeya City waliopo nafasi ya tatu na pointi 42 wakiwa nao wanauota ubingwa watakuwa uwanjwa wa Sokoine kuumana na ndugu zao Prisons wanmaougulia kipigo cha mabao 5-0 walichopewa na Yanga juzi.
Ushindi wowote kwa Mbeya utamaanisha unaiweka pabaya Simba katika mbio zake kutaka kuambulia angalau nafasi ya tatu kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Simba wana pointi 36 na wamesaliwa na mechi nne, ambazo kama watashinda zote itafikisha pointi 48 zilizopitwa na Azam tayari.
Simba itavaana na Azam ikiwa inauguza kipigo cha bao 1-0 ilichopewa na Coastal Union mwishoni mwa wiki iliyopita kqwenye uwanja wa Taifa.
Mabingwa hao wa soka wa 1988 wenyewe watawafuata Mtibwa Sugar kuumana nao katika mchezo utakaochezwa uwanja wa Manungu, huku timu zote zikiwa hazina nafasi ya ubingwa wala hofu ya kushuka daraja.
Michezo nyingine ya Jumapili ni pamoja na Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting katika pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa mjini Bukoba, ambapo Msemaji wa Ruvu Masau Bwire ametamba kwamba wanaenda Kaitaba kuvuna pointi tatu.
Hata hivyo Bwire anatamba akitambua wazi kuwa Kagera Sugar huwa wagumu kwene uwanja wao wa nyumbani.
Timu hizo mbili zinafukuzana kwenye nafasi ya tano na sita zikitofautishwa na pointi moja, Kagera wakiwa na pointi 32 na Ruvu wenyewe wana pinti 31.