Mtoto Honrina akionyesha kinyama kilichoota kwenye ulimi wake na kumfanya awe na ndimi mbili |
Muonekano wake unatisha na kuogofya mbali na kutia simanzi na kuonyesha namna gani mtoto Honorina Christian (11) anavyoumia na kuishi katika hali ya MATESO na MAUMIVU.
Kwa kinywa chake mwenyewe mtoto huyo kwa sauti ya upole anasema kuwa AMECHOKA kuishi kwa MATESO na anahitaji asaidiwe ili naye aishi kwa furaha kama watoto wengine.
Anasema maumivu anayoyapata kupitia vidonda alivyonavyo yanayotafuna ngozi yake yanamnyima raha na kumpa mateso makubwa na kwamba hana analoweza kukiokoa katika hali hiyo kama siyo serikali, watu wenye uwezo na wasamaria wema ambao wataguswa na hali yake.
"Naumia...Nateseka na sijui niseme nini. Nawaomba Watanzania kuanzia Rais, Wabunge, Mawaziri na watu waliojaliwa uwezo wanisaidie niweze kupata matibabu, nimeteseka vya kutosha, ninateseka sana na ugonjwa huu..." Honorina alisema huku akianza kulia kwa simanzi.
Anasema anapenda kurudi darasani kusoma baada ya kukwama akiwa darasa la pili baada ya kushindwa kuona kufuatia kupasuliwa jicho lake la kushoto.
"Nataka kusoma....Naomba nisaidieni...naumia sana ...."Honorina anaomboleza huku akiwa amejifunika kofia pana inayokinga kichwa chake ambacho kimetafunwa na kuacha madonda ya kuogofya.
Mama yake mzazi aliyebeba jukumu la kuhangaika na Honorina baada ya mzazi mwenzie Christian kufariki kwa ajali ya gari mwaka 2007, Grace John anasema hali ya mwanaye inamsikitisha na kumliza kila mara kwani anaamini inapa mateso makubwa mtoto wake huyo wa kwanza kati ya watatu aliyezaa na mzazi mwenzake.
Grace anasema tangu kuzaliwa kwa mwanaye kulikuwa na mambo ya kushangaza, lakini hakujua kama yangefikia hapo walipo sasa.
Akisimulia kwa simanzi, Grace anasema Honorina alizaliwa Juni 12 mwaka 2002 katika Hospitali ya Morogoro akiwa na afya njema, isipokuwa mwili wake mzima ukiwa umekaa nywele kama mwili wa mnyama.
"Hali hii ilinitisha mno kwa namna mwili mzima wa mtoto kujaa nywele, lakini nilielezwa hiyo haina tatizo na hivyo kuruhusiwa kurudi na mwanangu nyumbani nikiwa na furaha na mwenzangu (mwanaume aliyezaa naye),
Grace anasema na kuongeza kuwa, baada ya mwezi mmoja nywele hizo zote zilipukutika na kuiacha ngozi ya mtoto wake ikiwa na madoa madoa kama ngozi ya Chui jambo lililowatisha na kulazimika kurejea tena hospitali ya Morogoro na kupewa mafuta ya kumpaka kusaidia kurekebisha tatizo hilo.
"Kingine cha ajabu ni kwamba kadri alivyokuwa akikuwa ndivyo mtoto wake alivyokuwa akizidi kubadilika ikiwemo kugundua ana ndimi saba na pia kuna vitu vigumu vilivyojitokeza pembeni ya kichwa chake kama pembe za mbuzi," anasema.
Anasema hali hiyo iliwatisha na kuhangaika kutafurta matibabu, lakini wakati wakitafuta namna ya kumsaidia baba wa mtoto huyo aliyekuwa amezaa naye mtoto mwingine wa pili aitwaye Dickson ambaye kwa sasa ana miaka 9 na kumuachia mimba ya miezi saba alipata ajali na kufa mwaka 2007.
Anadai baada ya kujifungua mwanae wa tatu akiwa anaishi katika nyumba aliyojenga na mwenzake, alienda hiospitali kumtibia mwanae baada ya jicho lake la kushoto kupoteza kiini cheusi na kushauriwa kwenda CCBRT waliomfanyia upasuaji katika jicho hilo mwaka 2008 wakati Honorina akiwa darasa la pili.
"Bahati mbaya upasuaji huo ulisababisha mwanangu kupoteza uwezo wa kuona na hivyo kurudi nyumbani na kuanza kumlea kama asiyeona kwani jicho lake jingine pia halikuwa na uwezo mzuri wa kuona mpaka sasa," anasema na kuongeza hata hivyo mwaka mmoja na ushei mwanae alianza kuota pembe.
Anadai alimpeleka hospitali ya KCMC ambapo alifanyiwa upasuaji, lakini ikamuacha mwanaye akiwa matundu wazi katika mifupa iliyokatwa na kuwalazimisha madaktari kukata nyama za paja kuziba eneo hilo na puani kulikokuwa kukimomonyoka kila uchao.
"Yaani sijui mpaka sasa mwanangu amekuwa na kitu gani kwani nyama za pua zilikuwa pia zikimomonyoka na kumdondoka na pia kuota ndimi za ziada na kufukia saba, ambazo hata hivyo zilikatwa na kubakishwa moja ambayo hata hivyo kwa sasa imeongezeka nyingine," anasema Grace kwa huzuni.
Anasema baada ya kuwauliza madaktari kwa kuwabembeleza sana juu ya ugonjwa wa mwanae walimueleza kuwa alizaliwa kama mlemavu wa ngozi (Albino Mweusi).
"Walinieleza mwanangu ni Albino Mweusi na kwamba hawana cha kumsaidia ila kumpa dawa za kupaka kabla ya kushauriwa nije Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi Hospitali ya Muhimbili ambapo hata hivyo hakuna cha maana alichofanyiwa mwanangu zaidi ya kuambiwa nirudi naye nyumbani," anasema.
Anasema kwa kifupi amesumbuka na mwanaye na kukata tamaa asijue nini hatima ya Honolina, ambaye kwa hali yake imemfanya asiweze kufanya kazi yoyote ili kuhangaika naye kumtafutia matibabu, huku wanawe wengine wakiishi kwa mateso Mgeta-Morogoro kwani yeye mwenyewe (mama) hana ndugu wa kumsaidia.
"Sina mtu wa kunisaidia, baada ya nyumba niliyojenga na mzazi mwenzangu kuuzwa na mama mkwe kwa madai ni mali ya mtoto wao, nimekuwa natangatanga nimepanga mara mbili nyumba ya kwanza nilifukuzwa kwa kukosa kodi ya kuendelea kuishi kabla y kujipigapiga na kupata hapo Mgeta nilipowaacha watoto," anasema.
Anasema kwa jijini Dar es Salaam amekuwa akiishi kama ombaomba eneo la Ubungo ili kukidhi mahitaji yake na ya mwanaye na kudai hali hiyo imemchosha na kuungana na mwanae kuililia serikali na watu wengine wenye uwezo kumsaidia fedha za matibabu ili mwanaye atibiwe na kupona naye apumue.
"Kama mtoto anavyokueleza, nawaomba wasamaria wema, serikali na watu wenye uwezo watusaidie.. wanichangie nimuokoe mwanangu...miaka 11 ya mateso nadhani inatosha, sitaki kumpoteza mwanangu nampenda katika hali aliyonayo," anasema Grace akilengwalengwa na machozi.
Anasema hajui mwanaye alipatwaje na matatizo hayo ilihali wanae wengine waliomfuata wapo vyema kiafya bila tatizo lolote.
"Huyu ni mtoto wangu wa kwanza kuzaa na Christian niliyezaa naye watoto watatu, wengine ni Dickson (9) na mwisho aliniacha nikiwa mjamzito wa mimba yake ni Francis (6), ambao wote hawana tatizo kama dada yao, hili ndilo linalonishangaza na kuendelea kuwalilia wasamaria wema wanisaidie kumuokoa mwanangu," anasema.
Grace anayedai wapo baadhi ya watu wamekuwa wakimnyanyapaa kwa hali ya mwanae ambaye amejaa vidonda ambavyo vinatoa harufu kali, lakini akawakumbusha kuwa hayo ni matatizo ambayo hakuna aliyeyaomba pia akirejea usemi kwamba 'Hujafa Hujaumbika'.
Anamalizia kwa kumuomba yeyote atakayeguswa na tatizo la mwanae anaweza kumsaidia kwa kuwasilisha michango yao kupitia MICHARAZO MITUPU ama simu za mkononi za mama huyo za 0719-749542, 0687-402694 na 0762-425973. kwa huduma za Tigo-Pesa, M-Pesa au Airtel Money.