STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, January 7, 2013

SIMBA YATINGA NUSU FAINALI MAPINDUZI CUP, 'YAJITOA'

Kikosi cha Simba kilichotinga Nusu Fainali jana

Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
PAMOJA na kufuzu hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi jana, Simba SC italazimika kuiachia timu yao ya pili, maarufu kama Simba B iendelee na michuano hiyo hata kama ikiingia fainali, ili kikosi cha kwanza kiende Oman keshokutwa.
Kocha Mkuu wa Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, anataka kwenda Oman na kikosi kamili ili aweze kuwajua wachezaji wote na kuweza kuipanga vyema timu yake.
Kuhusu wachezaji wa timu ya taifa, ambayo Januari 11 itacheza mchezo wa kirafiki na Ethiopia, Liewig alisema suala hilo linashughulikiwa na viongozi wa klabu hiyo. “Najua viongozi walikuwa wana kikao na viongozi wa shirikisho (TFF).
Sijui wamekubaliana vipi, lakini naweza kuwavumilia wachezaji hao wajiunge na timu Oman baada ya mechi na Ethiopia,”alisema.
Simba jana ilifuzu Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi, licha ya kutoka sare ya 1-1 na Bandari ya hapa katika mchezo wa mwisho wa Kundi A, kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimekwishafungana bao 1-1, Bandari wakitangulia kupata bao kwa penalti, mfungaji Haitham Juma dakika ya sita kabla ya Kiggi Makassy kuisawazishia Simba SC dakika ya 16.
Refa aliwapa penalti Bandari baada ya Haruna Shamte kumchezea rafu Fauzi Ally katika eneo la hatari na Haitham akaenda kupiga penalti, ambayo ilipanguliwa na kipa Dhaira na mpira kumkuta tena mpigaji, aliyeukwamisha nyavuni.
Kiggi alifunga kwa mpira wa adhabu kutoka upande wa kulia wa Uwanja, umbali wa mita 20, baada ya Abdallah Seseme kuangushwa.    
Kipindi cha pili, Simba walianza kwa kuimarisha kwa kikosi chao wakiwaingiza kwa mpigo, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo na Jonas Mkude kuchukua nafasi za Mussa Mude, Salim Kinje na Ramadhani Singano ‘Messi’, wakati Bandari walimtoa kipa wao Hassan Hajji na kumuingiza Ahmad Suleiman.
Kwa matokeo hayo, Simba SC imeungana na Tusker ya Kenya kufuzu Nusu Fainali ya michuano hiyo. Tusker ni kinara wa kundi kwa pointi zake saba na Simba imeingia kama mshindi wa pili kwa pointi zake tano.
Wachezaji wa Simba SC walioitwa Stars ni kipa Juma Kaseja, mabeki Amir Maftah na Shomari Kapombe, viungo Amri Kiemba na Mwinyi Kazimoto na mshambuliaji Mrisho Ngasa.
Katika wachezaji wote hao walioitwa Stars, walio kwenye kikosi cha Simba kinachocheza Kombe la Mapinduzi ni Kapombe na Mwinyi Kazimoto pekee. Kaseja, Ngassa, Kiemba ni majeruhi, wakati Amir Maftah imeelezwa ana madai yake anayosubiri alipwe ndipo ajiunge na timu.  

Imehamishwa Bin Zubeiry

Sepp Blatter apinga kitendo kilichofanywa na Boateng, AC Milan

Rais wa FIFA, Sepp Blatter

RAIS wa Shirikisho wa Soka Duniani, FIFA, Sepp Blatter ameponda kitendo cha nyota wa AC Milan, Kevin Prince Boateng kuamua kususa pambano lao la kirafiki la wiki iliyopita dhidi ya timu ya daraja la chini ya Pro Patria, akidai haiwezi kuvumiliwa.
Blatter alinukuliwa jana akiwa Dubai kwenye zira ndefu ya Mashariki na Kati, akisema kuwa kilichofanywa na Boateng na timu yake ya Milan haiwezi kusaidia kumaliza ubaguzi zaidi ya kuongeza tatizo, iwapo kila timu au kila mchezaji watakuwa wakiamua kususa mechi kwa kufanyiwa vitendo kama hivyo.
"Sidhani kama kuondoka uwanjani ndio suluhisho la tatizo, inaweza kutumiwa vibaya na timu nyingine hasa kama timu imefungwa katika pambano hilo," alinukuliwa Bletter.
Alisema wanasubiri taarifa toka Shirikisho la Soka la Italia kujua kitu gani kilichotokea, ingawa alisisitiza kuwa pamoja na kwamba FIFA inapinga vitendo vya ubaguzi, lakini pia haiungi mkono tabia ya kususia mechi vinapotokea vitendo kama hivyo wakati wa mechi.
Kevin Prince Boateng kiungo wa AC Milan

Boateng nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana, Black Stars, aliamua kutoka uwanjani baada ya kufanyiwa vitendo vya kibaguzi na mashabiki wa Pro Patria katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Alhamis iliyopita ambapo licha ya kubembelezwa aligoma kufuta msimamo wake na kusababisha mechi hiyo kuvunjika.
Jana Jumapili wachezaaji wa timu hiyo ya Milan, walitinga uwanjani katika pambano lao la Seria A wakiwa na jezi zenye maandishi ya kupinga ubaguzi wa rangi ambapo timu hiyo ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Siena.
Vitendo vya kibaguzi dhidi ya wachezaji wenye asili ya Afrika kwa mataifa ya Ulaya vimekuwa vikizidi kushamiri kwa siku za karibuni, baadhi vikifanywa na wachezaji wenyewe kwa wenyewe na wakati mwingine vikifanywa na mashabiki kama ilivyotokea kwa Boateng.


Wachezaji wa AC Milan wakiwa wamevaa jezi zinazopinga ubaguzi wa rangi kabla ya mechi yao ya Seria A dhidi ya Siena jana
Hata hivyo pamoja na FIFA na FA za nchi mbalimbali kuvipinga vitendo hivyo na kutoa adhabu kwa wahusika bado havijaleta tija hasa kutokana na adhabu zake kuonekana nyepesi kuliko ukubwa wa jambo hilo.

TAFF YAWAONYA WASANII WALIOHARIBU MSIBA WA SAJUKI


Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba


SHIRIKISHO la Filamu Tanzania (TAFF) limekemea baadhi ya wasanii walioonyesha utovu wa nidhamu katika msiba wa  aliyekuwa msanii wa filamu nchini, Juma Kilowoko ‘Sajuki’.

Pia limesisitiza kuwa msanii atakaeripotiwa katika vyombo vya habari kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu atafungiwa kuigiza.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba alisema amesikitishwa na kitendo cha wasanii kuacha msiba na kwenda kunywa pombe wakati msiba huo ni wa dini.

Alisema baadhi ya wasanii kuonyesha utovu wa nidhamu katika msiba wa marehemu Kanumba na wengine katika msiba wa Sajuki.

“Nasikitika kuona msanii hajitambui hata kidogo, yani anaacha msiba anakwenda kunywa pombe tena jirani na mahala pa msiba, jamani huu msiba ni wa dini, hivyo atakayeripotiwa vibaya katika misiba TAFF tutamfungia” alisema Mwakifwamba.

Katika hatua nyingine alisema msiba huo ulitawaliwa na utani hali ya kwamba umewakutanisha watani wa makabila.

Msiba huo ulitawaliwa na utani baada ya kuwepo kwa wasanii wachekeshaji kama vile, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’ ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya fedha, Lucas  Mhuvile ‘Joti’ na wengineo wengi.

Tuzo za wakali wa filamu 2012 kutolewa Februari



MBIVU na mbichi ya nani mkali katika fani ya filamu kwa mwaka 2012 zinatarajiwa kufahamika mwezi ujao wakati wa hafla ya kutangaza washindi itakapofanyika jijini Dar es Salaam.
Tuzo hizo za Wasanii Bora wa Filamu 2012 zilizoandaliwa na Mtandao wa filamucentral zinatarajiwa kutolewa kwa washindi mwezi Februari katika tarehe na ukumbi utakaotajwa na waratibu wake.
Mratibu wa tuzo hizo, Myovela Mfaiswa, aliiambia MICHARAZO kuwa maandalizi kwa ujumla ya hafla hiyo inaendelea vema huku wadau wa filamu wakiendelea kuwapigia kura washiriki wanaochuana katika kinyang'anyiro hicho.
Mfaiswa alisema vipengele vinavyowaniwa katika tuzo hizo zinazofanyika kwa mara ya pili baada ya kufanyika mara ya mwisho mapema mwaka jana kwa wasanii bora wa 2010 ni pamoja na cha Muigizaji Bora wa Kike inayowaniwa na Yvonne Cherry 'Monalisa', Jacklyne Wolper, Wema Sepetu, Jennifer Kyaka 'Odama' na Elizabeth Michael 'Lulu'.
Tuzo nyingine ni ya Mchekeshaji Bora inayowaniwa na wasanii Haji Salum 'Mboto', King Majuto, Sharo Milionea, Kitale na Kinyapi, huku Muigizaji Bora Chipukizi ikiwaniwa na Mariam Ismail 'Mammy', Abdallah Ambua 'Dulla', Slim Omary 'Mdudu Kiu', Jose Mteme 'Baga' na Halima Ali.
Tuzo ya Muigizaji Bora wa Kiume inawaniwa na Jacob Stephen 'JB', Vincent Kigosi 'Ray', Steven Kanumba, Hisani Muya 'Tino' na Single Mtambalike 'Richie', wakati tuzo za Mwandishi Bora wa Mswada inawaniwa na Octavian Natalis, Ali Yakuti, F Kanuti, Elizabeth Chijumba na Kimela Bila.
------

KUMEKUCHA MISS UTALII TANZANIA


KAMBI ya warembo watakaoshiriki fainali za shindano la urembo la Utalii, Miss Utalii Tanzania, inatarajiwa kuanza rasmi Jumamosi ijayo ikishirikisha warembo walioshika nafasi mbili za juu ya mashindano ya ngazi ya mkoa.
Rais wa Miss Utalii Tanzania, Gideon Chipungahelo 'Chipps' aliiambia MICHARAZO kambi hiyo itakuwa ya siku 21 kabla ya kufanyika kwa kinyang'anyiro hicho mwishoni mwa mwezi huu jijini Dar es Salaam.
Chipps aliwataja warembo watakaoingia kambini tayari kuwania taji hilo la Tanzania na tuzo nyingine 28 zitakazowaniwa kuwa ni pamoja na Rose Godwin (Arusha), Irene Thomas, Sophia Yusuph na Ivon Stephen wote wa Dar.
Wengine ni Erica Elibariki (Dodoma), Jamia Abdul (Geita), Debora J. Mwansepeta (Iringa), Anna Pogaly (Kilimanjaro), Zena Sultan (Kigoma), Asha Ramadhani (Katavi), Joan John (Lindi), Doreen Bukoli (Mara), Dayana Joachim (Mbeya) na Jessica Rugalabamu wa Mwanza.
Warembo wengine ni Halima Suleman (Mtwara), Hadija Saidi (Morogoro), Mary Rutta (Manyara), Paulina Mgeni (Njombe), Anganile Rogers (Rukwa), Furaha Kinyunyu (Ruvuma), Neema Julius (Singida), Flora Msangi (Simiyu), Lightness Kitua (Shinyanga), Magreth Malale (Tabora) na Sarafina Jackson wa Tanga.
Wawakilishi wa vyuo wakaoshiriki kinyang'anyiro hicho ni Irene Richard Makoye na Hawa Nyange.
Tuzo zitakazowaniwa na warembo hao mbali na taji litakalompa mshindi uwakilishi wa nchi katika shindano la kimataifa ni pamoja na tuzo za heshima za Jamii, Elimu ya Jamii, Afya ya Jamii, Utalii, Utamaduni, Uchumi, Miundo Mbinu ya Utalii, Uwekezaji, Madini na maliasili mbalimbali za taifa.

Suarez afunga bao la utata na kuivusha Liverpool Kombe la FA

HATUA KWA HATUA YA BAO LA UTATA LA SUAREZ JANA
Suarez akijitengenezea vizuri mzuri kwa mkono
Amefanikiwa na sasa anaelekea kufunga bao

Akimtoka kipa aliyejaribu kumzuia
Kazi imekuwa nyepesi anafunga kilainii..huku Mansfield wakiinua mikono wakilalamikia bao hilo

Anashangilia na wenzake

Anaubusu mkono wake kwa kazi nzuri uliofanya

 

NYOTA wa timu ya Liverpool, Luis Suarez, jana akitokea benchi alitengeneza bao kwa mkono kisha kufunga na kuivusha timu yake kwenye michuano ya Kombe la FA nchini England.

Bao hilo ambalo tukio la kutengenezwa na mkono halikuonwa na mwamuzi wa pambano hilo la raundi ya tatu ya michuano hiyo iliisaidia kuipa Liverpool ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya

Mansfield Town.
Raia huyo wa Uruguay ambaye anakumbukwa na Waafrika kwa kulizuia bao la Ghana katika Fainali za Kombe la Dunia 2010, alifunga bao hilo katika dakika ya 59 dakika tano tangu aingie dimbani kuchukua nafasi ya Daniel Sturridge, aliyetangulia kufunga bao la mapema.
Wenyeji Mansfield waliolalamikia tukio hilo, walipata bao la kufutia machozi dakika ya 80 kupitia Matt Green, ambalo halikuwasaidia kutong'oka kwenye michuano hiyo ambayo pia jana ilishuhudiwa Arsenal wakilazimishwa sare ya 2-2 ugenini na Swansea City.
Arsenal ilielekea kushinda pambano hilo baada ya kutoka nyuma ya bao 1-0 mara kipindi cha pili kilipoanza baada ya dakika 45 za kwanza kwenda mapumziko bila kufungana na kufunga mabao mawili dakika 10 za mwisho wa mchezo huo kabla ya kujisahau na Swansea kusawazisha zikiwa zimesalia dakika tatu.
Michu alianza kuiandikia Swansea bao dakika ya 51 kabla ya Lucas Podolski kusawazisha dakika ya 81 na Kieran Gibbs kufunga bao la pili dakika mbili baadae na wakati wengi wakiamini Arsenal imepita kwa raundi ya nne,  Danny Graham kusawazisha bao hilo na kuzifanya timu zao sasa kurudiana tena ili kufuzu hatua ijayo itakayoanza Januria 26.

Amefanikiwa na sasa anaelekea kufunga bao

TUZO BALLON D'OR LEO, AGUERO ATAKA MESSI APEWE

Aguero  akiwa na Lionel Messi

NYOTA wa timu ya Mamchester City ya England ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Argentina, Sergio 'kun' Aguero, amesema kwamba tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia ya Ballon d'Or inapaswa kwenda kwa Lionel Messi. 
Sherehe za kumtangaza mwanasoka bora wa dunia wa mwaka 2012 zitafanyika leo kwenye Ukumbi wa Zurich Convention Centre nchini Uswisi.

Aguero akihojiwa na gazeti la Argentina la 'Ole', alisema Muargentina mwenzake huyo anayeichezea Barcelona ya Hispania anastahili kupewa tuzo hiyo.
"Anastahili tuzo hiyo kwa yote aliyoyafanya akiwa na Barcelona na timu ya taifa ya Argentina," alisema Muargentina huyo, ambaye pia ana ndoto za kuja kuwa mchezaji bora wa dunia siku moja.
 "Si jambo rahisi, lakini kama utafanya mambo yako vizuri huwezi kujua (unaweza kushinda tuzo). Unajua daima unapaswa kuota kuwa mchezaji bora duniani," aliongeza.
Aguero pia alizungumzia kiwango cha timu yake cha sasa. "Hatujacheza kama ambavyo tulikuwa tukicheza msimu uliopita, lakini tuko katika nafasi nzuri. Tunaongezeka ubora na katika mechi mbili zilizopita tulicheza vizuri sana. Tuna kikosi kizuri na tuna uwezo wa kurejea katika kiwango kama cha msimu uliopita. Kutolewa kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ilikuwa pigo kubwa kwa sababu tulikuwa na matumaini makubwa katika michuno ile. Tulikuwa katika kundi gumu. Taji la Ligi ya Klabu Bingwa ni jambo tunaloliota pia. Tutafanya vyema siku zijazo," alisema.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina pia alijumuisha mwaka wake 2012 akisema: "Ulikuwa ni mwaka mzuri katika maisha yangu ya soka. Ulikuwa muhimu katika kujijenga kwenye klabu ya Man City na kutwaa ubingwa wa England. Na kikubwa ni kufunga goli lile lililoamua bingwa katika dakika za lala salama. Ilikuwa ni ndoto iliyogeuka kwa kweli," aliongeza Aguero.
Mshambuliaji huyo pia alizungumzia timu ya taifa ya Argentina, akisema: "Jambo muhimu zaidi ni kwamba tufuzu kwa Kombe la Dunia 2014 mapema iwezekanavyo. Kama ukipoteza mechi mbili katika michuano hii migumu ya kuwania kufuzu timu nyingine zinakufikia. Ulikuwa ni mwaka mzuri kwa timu ya taifa. Tumeanza kuzoeana na kufanya mambo sahihi uwanjani," alisema.