STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 12, 2017

SIMBA, AZAM NI ZAIDI YA VITA KOMBE LA MAPINDUZI 2017

Kikosi cha Simba
Wababe wa Chamazi, Azam FC
Na Rahma White
HABARI ndio hiyo. Leo Alhamisi ndio kilele cha sherehe za Mapinduzi, ukiwa ni mwaka wa 53, lakini kazi bwana ipo kesho kwenye Uwanja wa Amaan.
Unajua nini? Wekundu wa Msimbazi, Simba kesho itavaana na Matajiri wa Azam kwenye pambano la fainali za michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017.
Sasa kama ulikuwa haujui ni kwamba Simba ndio klabu iliyotwaa Kombe la Mapinduzi mara nyingi, ikifanya hivyo mara tatu tangu lianze kuchezwa kwa mfumo wa sasa. Pia Simba ndio klabu iliyotinga mara nyingi kwenye fainali  ambapo pambano lao la kesho dhidi ya Azam litakuwa ni la sita sita ikiiacha Mtibwa Sugar waliokuwa wakilingana nao ambayo msimu haikualikwa.
Vinara hao wa Ligi Kuu Bara kesho itavaana na Azam klabu inayofuata kwa kulibeba taji hilo mara nyingi nyuma ya Simba, ikilitwaa mara mbili tena ikiwa klabu pekee kuwahi kulitetea ikifanya hivyo mwaka 2012 na 2013.
Simba imefika hatua hiyo ya fainali za mwaka huu kwa kuitambia Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-2 baada ya kumaliza dakika 90 la pambano lao bila milango ya timu hiyo kuguswa, huku Azam ikifika hatua hiyo kwa kuing'oa Taifa Jang'ombe kwa bao 1-0.
Azam ndio klabu ambayo mpaka inafika fainali wavu wake haujaguswa ikiweka rekodi, huku Simba ikifuata ikiruhusu bao moja tu.
Kwa mnasaba huo fainali ya kesho itakuwa tamu ile mbaya kwani, licha ya kila timu kusaka heshima ya kulibeba taji hilo, lakini pia zinataka kuonyesha nani mkali zaidi katika suala zima la kulinda lango lao.
Mchezo huo wa kesho una uhondo zaidi kwenye eneo la kiungo ambako klabu zote zinatambia mafundi walionao ambao wamezifanya kuwa kali katika kuzuia na kushambulia.
Makocha wa pande zote wamekuwa wakijinasibu timu zao kuibuka na ushindi, lakini kwa kulinganisha na rekodi zilizopo ni lazima Simba iwe makini mbele ya Azam ambao waliistaajabisha Yanga kwa kuipiga mabao 4-0.
Ingawa mpaka sasa kwenye michuano hiyo ya Mapinduzi, Azam imekuwa wanyonge wa Simba, lakini kwa namna walivyoizima Yanga ni wazi Simba isiende kichwa kichwa Uwanja wa Amaan kama wanataka kurejesha taji lao hilo walilolipoteza mwaka jana na kuliacha likibebwa na URA ya Uganda.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja amekiri pambano litakuwa gumu, lakini kubwa wanachotaka ni kurudi jijini Dar es Salaam na taji hilo, huku Idd Nassor 'Cheche' akiamini hakuna cha kuwazuia kubeba Kombe la mwaka huu.
Vikosi vya timu hizo vinatarajiwa kuwa hivi;
AZAM: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Yakub Mohammed, Aggrey Morris, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Frank Domayo, John Bocco, Yahya Mohammed na Joseph Mahundi.
SIMBA:
Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein, Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mzamiru Yasin, Juma Liuzio, Mohammed Ibrahim na James Kotei.

Mabingwa wa Mapinduzi

2007-Yanga
2008-Simba
2009-Miembeni
2010-Mtibwa Sugar
2011-Simba
2012-Azam
2013-Azam
2014-KCCA
2015-Simba
2016-URA
2017-  ''

Utamu wa Ligi Kuu Bara umerudi tena

JKT Ruvu
Toto Africans
Ruvu Shooting
Na Rahim, Junior
ACHANA na pambano la kesho la fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi,
itakayozikutanisha Simba na Azam kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, unaambiwa utamu wa Ligi Kuu Bara nao unarudi rasmi wikiendi hii.
Ligi hiyo iliyokuwa mapumziko ya wiki kama mbili hivi, inarudi kwa michezo itakayochezwa mfululizo kuanzia leo mpaka Jumatano.
Wapinzani wa jadi, maafande wa JKT Ruvu na Ruvu Shooting zinatarajiwa kumaliza ubishi katika pambano linalosubiriwa kwa hamu kwenye Uwanja wa Mabatini, ulioko Mlandizi mkoani Pwani.
Pambano hilo la kisasi linafanyika huku kila timu ikiwa katika hali tofauti, JKT Ruvu wakiwa hoi mkiani, huku wapinzani wao angalau wakipumua maeneo ya juu na wanatambia ushindi wa bao 1-0 iliyopata katika mechi yao ya kwanza.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ligi hiyo itaendelea Jumamosi kwa pambano jingine la 'derby' ya Mkoa wa Shinyanga kati ya Stand United na Mwadui  zitakazovaana kwenye Uwanja wa Kambarage mjini humo, huku kukiwa hakuna mbabe wa mechi ya awali.
Jumamosi pia kutakuwa na mtanange mwingine mkali wa Kagera Sugar itakayokuwa mwenyeji wa Ndanda ya Mtwara kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Utamu utaendelea tena Jumapili kwa mchezo mmoja tu ambapo Mbao itaialika African Lyon ya Dar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kivumbi cha ligi hiyo inayoingoa raundi ya nne ya duru la pili, itaendelea tena Jumatatu kwa mchezo mmoja tu kati ya Prisons Mbeya itakayokuwa mgeni wa Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Michezo mitatu ambayo ilikuwa haijapangiwa tarehe hapo awali kwa alama ya TBA ikiwa na maana ya kutajwa baadaye (To Be Announced), tayari Bodi ya Ligi, chombo cha TFF, kinachosimamia na kuendesha ligi, imepanga tarehe.
Jumanne ya Januari 17, 2017, Yanga itakuwa ugenini mjini Songea kuvaana na Majimaji kwenye Uwanja wa Majimaji na siku inayofuata yaani Jumatano, Mtibwa Sugar itakayocheza na Simba kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakati Azam itakuwa mwenyeji wa Mbeya City Uwanja wa Azam Complex.
Mchezo huu wa Azam na Mbeya City umepangwa kuanza saa 1.00 usiku wakati michezo yote tajwa hapo juu itaanza saa 10.00 jioni lengo likiwa ni kutoa nafasi kwa mashabiki kushuhudia mechi nyingi kupitia Kituo cha runinga cha Azam.

Ratiba ya VPL imekaa hivi;
 
Jan 13, 2017   
JKT Ruvu v Ruvu Shooting

Jan 14, 2017Stand United v Mwadui
Kagera Sugar v Ndanda

Jan 15, 2017Mbao v African Lyon

Jan 16, 2017
Toto Africans v Prisons

Jan 17, 2017Majimaji v Yanga

Jan 18, 2017Mtibwa Sugar v Simba
Azam v Mbeya City
 

Zaha aanza mambo Ivory Coast ikiilipua Uganda x3

Straika Serge Aurier akishangilia bao la tatu la Tembo ya Afrika dhidi ya Uganda The Cranes
STRAIKA Wilfried Zaha akiichezea Ivory Coast kwa mara ya pili tangu alipoikana England, ameanza kuonyesha cheche zake baada ya kufunga bao lake la kwanza kwa Tembo hao wa Afrika wakiichapa Uganda kwa mabao 3-0.
Pambano hilo lilikuwa la kirafiki la kimataifa kujiandaa na michuano ya Afcon 2017 inayoanza wikiendi hii na lilichezwa nchini Ivory Coast na kushuhudia mpaka mapumziko hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.
Zaha anayeichezea Crystal Palace wa England,  alifunga hilo katika dakika ya 58, ikiwa ni la pili kwa timu yake kwani dakika saba nyuma yake Jonathan Kodjia kuifungia Ivory Coast bao la kwanza.
Bao jingine la Serge Aurier katika dakika ya 72 na kuwazamisha wawakilishi wa ukanda wa Cecafa, Uganda ambayo inaends Gabon ikiwa ni mara ya kwanza tangu miaka 38 iliyopita waliposhiriki fainali hizo za Afrika.
Katika mechi nyingine ya kimataifa za kirafiki kwa maandalizi ya Afcon 2017 itakayochezwa Gabon kuanzia wikiendi hii, Senegal iliitambia Congo kwa mabao 2-0.

Liverpool majanga, yapigwa kidude na Southampton

Nathan Redmond akishangilia bao lake alililowatungua Liverpool usiku wa jana kwenyer Uwanja wa St Mary's katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Ligi (EFL)
LIVERPOOL imekwama aisee, baada ya usiku wa kuamkia leo kuchapwa bao 1-0 na Southampton katika mechi ya Nusu Fainali ya kwazna Kombe la Ligi.
Kwa ushindi huo, Southampton imejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kama itafanya kweli kwenye mechi ya marudiano ugenini Januari 25.
Bao lililowazamisha vijana wa Jurgen Klopp liliekwa kimiani na Nathan Redmond katika dakika ya 20 katika mchezo huo mkali uliopigwa kwenye Uwanja wa St. Mary's mjini Southampton.
Kipigo hicho cha Liverpool kimekuja siku chache tangu walipong;anganiwa na timu ya daraja la chini ya Plymouth katika mechi tya raundi ya tatu ya Kombe la FA ambao watarudiana nao Januari 18.
Wikiendi hii Liverpool itakuwa na kibarua kigumu mbele ya Man United ambayo juzi iklipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Hull City katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Ligi na kujiweka pazuri kutinga fainali.
Vijana wa Klopp watakuwa na wiki ngumu kwa kutakiwa kucheza mfululizo mara baada ya kuumana na Man United Jumapili hii.

Wenger kumbe hata huyu naye ulimkosa?

KOCHA Arsene Wenger amekuwa akihusishwa na kushindwa kunyakua nyota mbalimbali kutokana na kuwa mgumu kutoa fedha zinazohitajiwa na klabu husika. Orodha hiyo kwa sasa imeangukia kwa beki wa AS Roma. Wakala wa beki huyo Kostas Manolas amedai kuwa AS Roma ilikataa kitita cha euro milioni 40 kutoka Arsenal ili kumnasa nyota huyo msimu huu.
Arsenal walikuwa wakihusishwa na usajili wa beki huyo katika kipindi cha usajili wa kiangazi mwaka jana, lakini suala lake halikufanikiwa baada ya kumchukua Shkodran Mustafi kutoka Valencia badala yake. Wakala wa beki huyo amesisitiza kuwa kiasi cha fedha walichokitaka Roma ndio kilikuwa chanzo kikubwa cha kuvurugika kwa dili hilo. Hata hivyo wakala huyo aliendelea kudai kuwa Kostas anaweza kuondoka Juni mwaka huu ingawa ameondoa uwezekano wa kwenda China.

Schneiderlin huyooo Everton, Man United yakubali kumuuza

HAKUNA namna tena. Klabu ya Manchester United imekubali kumuuza kiungo wake Morgan Schneiderlin kwenda Everton kwa kitita cha pauni milioni 22. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa mwenye umri wa maiak 27, alisajiliwa United na Louis van Gaal kwa kitita cha pauni milioni 25 akitokea Southampton Julai mwaka 2015. Toka atue United amecheza mechi 47, lakini msimu huu amefanikiwa kucheza mechi nane pekee chini ya Kocha Jose Mourinho zikiwemo mechi tatu za Ligi Kuu.
Kwa upande mwingine Everton imekubali kumpeleka kwa mkopo mshambuliaji Oumar Niasse mwenye umri wa miaka 26 kwenda Hull City. Nyota huyo wa kimataifa wa Senegal alisajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 13.5 kutoka Lokomotiv Moscow Februari mwaka jana, lakini hajafanikiwa kung’ara baada ya kucheza mechi saba pekee.

Ronaldo tisha mbaya, ateuliwa tuzo nyingine

Pichja tofauti zikimuonyesha Ronaldo na tuzo zake za hivi karibuni ikiwamo wa Ballon d'Or anayoibusu
WAMBILI kweli havai moja. Straika wa kimataifa wa Ureno na klabu ya Real Madrid, Cristiano Ronaldo ametajwa katika orodha nyingine ya watakaogombea tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Mwaka ya Laureus. Nyota huyo amekuwa na miezi 12 yenye mafanikio baada ya kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na Euro 2016. Kiwango kikubwa alichoonyesha kimemfanya kutwaa tuzo za Ballon d’Or na tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa FIFA. Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa mwaka hupigiwa kura na wanahabari na Ronaldo atakuwa akishindana na nyota wengine wakiwemo nyota wa mpira wa kikapu Marekani Steph Curry na Lebrone. Pia watakuwepo mwanariadha nyota wa mbio fupi wa Jamaica Usain Bolt, mwanaridha nyota wa Uingereza Sir Mo Farah na kinara wa mchezo wa tenisi duniani Sir Andy Murray. Kama akitwaa tuzo hiyo Ronaldo atakuwa mwanasoka wa kwanza kufanya hivyo toka kuanzishwa kwa tuzo hizo mwaka 2000. Mshindi wa tuzo hiyo anatarajiwa kutangazwa Februari 14 mwaka huu jijini Monaco.

Azam FC yapata mrithi wa Guardiola wao, anatokea Ronania

Na Rahma Junior
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, mchana huu imemtangaza, Aristica Cioaba, kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho.
Cioaba, 45, anakuja Azam FC kurithi mikoba ya Mhispania Zeben Hernandez, aliyesitishiwa mkataba pamoja na benchi lake zima la ufundi.
Kocha huyo atasaidiana na makocha wazawa, Idd Nassor Cheche na Kocha wa Makipa Idd Abubakar, walioiongoza timu hiyo kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo saa 10.15 jioni ya leo itasaka fainali kwa kukipiga na Taifa ya Jang’ombe.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Saad Kawemba, tayari wamefanikiwa kumpata kocha huyo na wameingia naye mkataba wa muda wa miezi sita wenye kipengele cha kuongezwa.
Alisema Cioaba ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika na ataiongoza Azam FC kwa kipindi hiki hadi mwishoni mwa mwa msimu, ambapo baada ya kuisha watakaa tena mezani kufanya tathimini ya mafanikio yake na wapi wanaweza kuendelea kutokana na kazi iliyofanyika.
“Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC inapenda wadau wote wa mpira na wapenzi na mashabiki wa Azam kwamba klabu imempata mwalimu, ambaye ndiye ataiongoza klabu kwa kipindi hiki hadi mwishoni mwa msimu.
“Kwa hiyo kwa mashabiki wetu maana yake ni kwamba tukiingia kwenye mechi inayofuata ya ligi, kocha atakuwa ameanza kazi na Cheche (Idd Nassor) atakuwa msaidizi wake na benchi lake zima alilokuwa nalo hivi sasa litaendelea,” alisema.
Kawemba aliongeza kuwa hivi sasa kocha huyo atakuwa na kikosi visiwani Zanzibar kufuatilia mwenendo wa timu ulivyo na ataendelea kutoa ushauri panapohitajika na ataanza rasmi kukaa kwenye benchi mpaka pale vibali vyake vya kufanya kazi nchini vitakapokamilika.
“Taratibu hizo zitakwenda kwa mujibu wa sheria za nchi, ambapo tutaziheshimu na kuona ya kwamba tutazifanya kwa haraka zaidi ili mwalimu aweze kupata kibali cha kufanya kazi hapa nchini, kwa hayo machache tunawaomba mashabiki wetu wawe watulivu wampe sapoti kocha na wadau wote wa mpira waone ya kwamba tumefanya jambo la kheri,” alisema.
Kauli ya kwanza ya Cioaba
Kwa upande wake Cioaba, alisema kuwa anafuraha kubwa leo hii kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo huku akiahidi kazi nzuri na kuifanya timu hiyo kuwa bora.
“Najua Azam FC hapa Tanzania ni moja ya timu kubwa yenye historia huko nyuma, napenda kuushukuru uongozi kwa kuniamini na kunipa nafasi kuja kufundisha soka kwenye nchi hii, kwa mashabiki napenda kuwaambia kuwa nalijua soka la Afrika, nimewahi kufundisha Ghana na kupata matokeo mazuri.
“Kuhusu wakati ujao, nina furaha sana kuhusu uongozi walipoongea na mimi wakati tunaweka mipango ya timu ya hapo baadaye na hili ni jambo zuri kwa kocha, kitaaluma nawaahidi mashabiki na watu wote wanaoipenda Azam FC, niko hapa kuwapa mambo mazuri katika kazi yangu kwenye klabu,” alisema.
Msimu uliopita, Cioaba aliiongoza Aduana Stars ya Ghana kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Ghana, ambapo anafahamiana kwa ukaribu na nyota wawili wa Azam FC, Yakubu Mohammed na Yahaya Mohammed, waliosajiliwa kutoka timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo.
Mbali na kufundisha soka nchini Ghana pia amewahi kufanya kazi kwenye miamba ya Morocco, Raja Casablanca, Al Masry ya Misri na katika nchi za Romania, Kuwait, Oman na Jordan.