STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 13, 2013

Maskini Cape Verde, FIFA yaing'oa WC yaipa nafasi Tunisia


KIKOSI cha Cape Verde hakitashiriki mchuano wa kombe la dunia mwaka 2014 baada ya kubanduliwa nje ya kinyanganyiro cha kufuzu kwa dimba la dunia Mwakani kwa nchi za Afrika.
Kwa mujibu wa tovuti ya shirikisho la soka duniani FIFA, Cape Verde ilikosea kwakumshirikisha mchezaji aliyekuwa amepigwa marufuku katika mechi yao dhidi ya Tunisia Jumamosi iliyopita
Kwa mujibu wa FIFA Fernando Verela hakufaa kucheza katika mechi hiyo waliyoshinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Tunisia . FIFA sasa imebadilisha matokeo hayo na kuipa Tunisia ushindi mkubwa wa mabao 3-0.



Kauli hiyo imeipa Tunisia alama za kutosha kuipiku Cape Verde kutoka kileleni mwa kundi B ikiwa na alama 14 .Cape Verde ni ya pili na alama 14.
Shirikisho la soka la Cape Verde lilimetozwa faini ya dola $ 6400 Sadfa ni kuwa Cape Verde ilinufaika na alama za bwerere mapema mwakani Equatorial Guinea ilipoadhibiwa kwa kumshirikisha mchezaji kinyume na sheria za FIFA za uraiya wa wachezaji.
The Blue Sharks ya Visiwa vya Cape Verde walikuwa wamelazwa mabao 3-4 na Equatorial Guinea lakini FIFA ikabadilisha matokeo hayo kwani Emilio Nsue Lopez hakutimiza kanuni za uraiya wa taifa hilo .
Sasa Tunisia ndiyo itakayosonga mbele katika raundi ya mwisho itakayochezwa katika droo itakayofanyika Jumatatu tarehe 16.
Msimamo Mpya baada ya maamuzi ya FIFA
Kundi B
Tunisia - 14
Cape Verde - 9
Sierra Leone - 8
Eq Guinea - 2

BBC

DAR FILAMU FESTIVAL INAMTAMBULISHA LULU KWENU


TAMASHA Kubwa la Filamu litakaloandika historia ya tasnia ya filamu Tanzania la Dar Filamu Festival (DFF 2013) linamtambulisha Elizabeth Michael kama Official Actress for DFF 2013/14 katika muonekano mpya akiwa kama balozi wetu wa kwanza kutambulishwa kutoka DFF, alafu utapata muonekano wa Official Director/ Producer DFF 2013/2014 Vincent Kigosi ‘Ray the Greatest’.
Dar Filamu Festival 2013 awali ilitambulishwa kwa wadau na wanahabari wiki iliyopita na sasa tupo katika hatua nyingine ya kuwatangaza na kuwapa majukumu mabalozi wetu ambao ni Ray na Lulu katika kuhakikisha kampeni ya kupenda filamu za Kiswahili na kuzipa thamani zinafanikiwa na kuwa ni soko lenye nguvu zaidi katika tasnia ya filamu Ulimwenguni.
Tamasha la Dar Filamu Festival (DFF 2013) litafanyika katika viwanja vya CoICT- UDSM- Kijitonyama kuanzia tarehe 24 hadi 26 Septemba 2013, filamu za Kitanzania kama ufunguzi wa tamasha hilo zitaonyeshwa kwa kiingilio cha Bure kabisa  kiingilio chako ni kufika katika viwanja vya Posta pale Kijitonyama na kushuhudia filamu kutoka kwa wakali wa filamu Bongo Movie.
Sasa ni zamu yako kukutana na Lulu kisha kuongea naye kuhusu filamu na soko jipya la Filamu,  kupitia Projector kubwa  na kuona filamu kwa uzuri zaidi huku ukiburudika kwa kazi nzuri kutoka nyumbani.

Ilala yaifuata Mjini Magharib Fainali za Copa


TIMU ya Ilala imepata tiketi ya kucheza fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 upande wa wavulana baada ya kuivua ubingwa Morogoro katika mechi iliyoamriwa kwa mikwaju ya penalti.

Hadi muda wa kawaida wa mchezo huo uliochezwa leo (Septemba 13 mwaka huu) jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.

Paul Ngowi ndiye aliyeanza kuifungia Ilala dakika ya 30, lakini Morogoro wakasawazisha dakika ya 50 kupitia kwa Omari Sultan. Katika changamoto ya mikwaju ya penalti, Ilala ilipata tatu dhidi ya mbili za Morogoro.

Ilala sasa itacheza fainali na Mjini Magharibi itakayofanyika kesho (Septemba 14 mwaka huu) kuanzia saa 9 alasiri.

Fainali hiyo ya wavulana itatanguliwa na ile ya wasichana kati ya Mwanza na Ilala itakayoanza saa 7 mchana. Mwanza imepata tiketi ya kucheza fainali baada ya leo kushinda nusu fainali ya pili dhidi ya Mbeya kwa mabao 3-0.

Mabao hayo katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume yamefungwa na Flora Fulgence dakika ya 47, Emiliana Akuti dakika ya 56 na Yulitha Masamu dakika ya 57.

Ngeta kuwakabidhi bendera Airtel Rising Stars

 
Na Boniface Wambura
TIMU ya Airtel Rising Stars ya Tanzania kwa wavulana na wasichana itakabidhiwa bendera kesho (Septemba 14 mwaka huu) tayari kwa safari ya Nigeria itakayofanyika keshokutwa alfajiri.

Hafla hiyo ya kukabidhi bendera kwa timu hiyo yenye kikosi cha wachezaji 32 itafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah ndiye atakayekabidhi bendera kwa kikosi hicho.

Sambazeni ujuzi wenu,Tenga awaambia wahitimu Grassroots

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodgar Tenga amewataka wahitimu wa kozi ya ukocha wa grassroots kusambaza ujuzi walioupata nje ya shule zao ili mradi huo uwe na manufaa nchi nzima.

Akifunga kozi hiyo iliyoshirikisha makocha 30 kutoka Tanzania Bara na Visiwani kwenye ukumbi wa TFF leo (Septemba 13 mwaka huu), Rais Tenga amewakumbusha kuwa mradi huo umelengwa kuenea nchi nzima katika kipindi cha miaka mitatu.

Mradi wa grassroots unalenga wachezaji mpira wa miguu (wasichana na wavulana) wenye umri kuanzia miaka 6-12, na kozi hiyo ilikuwa chini ya Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Govinder Thandoo kutoka Mauritius.

Washiriki waliohitimu kozi hiyo na kukabidhiwa vyeti ni Abdulkheir Khamis Mohamed (Kaskazini A), Ali Hamad Mohamed (Wete), Ali Khamis Ali (Wete), Amin Amran Yunus (Micheweni), Amina Mhando (Kibaha), Benito Mwakipesile (Kibaha), Deogratius Yesaya (Kibaha), Editha Katabago (Bagamoyo), Habiba Mulungula (Bagamoyo) na Irene Semng’indo (Kibaha).

Juma Omar Abdallah (Kaskazini A), Kassim Ibrahim Mussa (Mkoani), Khamis Haji Ali (Kusini Unguja), Khamis Hamad Rajab (Chakechake), Mahfoudh Abdulla Said (Wete), Marianus Nyalale (Bagamoyo), Maryam Suleiman Ali (Mjini Magharibi), Maryasa Juma Ali (Mjini Magharibi), Mohamed Ali Abdullah (Mjini Magharibi) na Mohamed Salim Omar (Micheweni).

Mohamed Seif Abeid (Mkoani), Ramadhan Kejeli (Bagamoyo), Rhobi Kibacho (Kibaha), Salim Suleiman Juma (Chakechake), Shaaban Naim Suleiman (Kusini Unguja), Shabani Rashid Masimbi (Bagamoyo), Talib Ali Rajab (Chakechake), Thabit Juma Makungu (Kusini Unguja), Yusuf Ali Issa (Mjini Magharibi), Zakia Choum Makame (Mjini Magharibi).

Hiyo ni kozi ya pili ya grassroots kufanyika nchini ambapo ya kwanza ilifanyika Desemba mwaka juzi.

Simba kamili gado 'kuiua' Mtibwa kesho, Owino, Dhaira watua

Joseph Owino
KLABU ya soka ya Simba imekamilika tayari kulipa kisasi kwa Mtibwa Sugar kesho katika pambano lao la Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya nyota wao wa kimataifa kutoka Uganda, Abel Dhaira na beki Joseph Owino kuwasili kikosini.

Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliliambia MICHARAZO kuwa, kikosi chao kipo 'kamili gado' kambini na kesho kitashuka dimba la Taifa, Dar es Salaam kwa nia ya kulipa kisasi kwa Mtibwa waliowanyuka na kuzoa pointi zote sita katika mechi mbili za msimu uliopita.

Kamwaga alisema benchi lao la ufundi limewahakikishia wachezaji wote wapo fiti kukiwa hakuna majeruhi na la furaha zaidi ni kurejea kwa mastaa wao wa Uganda, kipa Dhaira na beki Owino waliokuwa wameenda kwao kwa matatizo ya kifamilia.

"Tunashukuru kambi yetu ipo fiti na kwamba kikosi kimekamilika baada ya nyota wetu kutoka Uganda kutua nchini tayari kwa vita ya kesho, lengo likiwa kulipa kisasi dhidi ya Mtibwa sambamba na kuzoa pointi zitakazotuweka pazuri katika msimamo wa ligi," alisema.

Kamwaga alisema Simba inafahamu mechi ya kesho itakuwa ngumu na yenye upinzani mkali, lakini wamehakikishwa na benchi lao la ufundi pamoja na wachezaji wenye ari kuwa ushindi ni lazima Taifa kabla ya kusubiri mechi yao ijayo ya siku ya Jumatano dhidi ya Mgambo JKT.

Simba iliyoanza ligi hiyo kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Rhino Rangers kisha kuifunga JKT Oljoro, ililala bao 1-0 jijini Dar es Salaam katika mechi yao ya pili dhidi ya mabingwa hao wa Tanzania  wa 1999 na 2000 baada ya awali kufungwa mabao 2-0 mjini Morogoro.

Baadhi ya nyota wa Mtibwa Sugar kama Salum Sued 'Kussi' na Salvatory Ntebe wametamba kuwa wamekuja  Dar kwa nia moja ya kuzoa pointi tatu pamoja na kuendeleza ubabe kwa vijana wa Msimbazi, licha ya kukiri litakuwa pambano la 'kufa mtu'.

Mtibwa kama ilivyo Simba na klabu nyingine tano zinazokamata nafasi ya pili nyuma ya JKT Ruvu ina pointi nne zilizotokana na sare ya 1-1 dhidi ya Azam na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya ndugu zao wa Kagera Sugar ambao kesho wapo Kagera kuumana na Azam.

Mechi nyingine za kesho ni kati ya Mbeya City na Yanga zitakazoumana uwanja wa Sokoine Mbeya, JKT Ruvu itakayokuwa wageni wa Ashanti Utd uwanja wa Chamazi, Coastal Union kuialika Prisons-Mbeya na JKT Oljoro itakayoikaribisha Rhino Rangers ya Tabora.

Tenga aipongeza Kamati ya Ligi

Rais wa TFF, Leodgar Tenga
Na Boniface Wambura
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodgar Tenga ameishukuru Kamati ya Ligi kwa usimamizi mzuri tangu ilipokabidhi Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) katika mzunguko wa pili msimu uliopita.

Amesema TFF iliamua kuanzisha Kamati ya Ligi kwa lengo la kutaka klabu zijisimamie zenyewe ili kuongeza ufanisi, jambo ambalo limeleta mabadiliko kwa vile hivi sasa hakuna matatizo katika kuwalipa marefa na makamisha wanaosimamia VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

“Fedha za udhamini sasa zinakwenda moja kwa moja kwenye Kamati ya Ligi. Ni matarajio yangu kuwa ufanisi utaongezeka, kwani tumeanzisha jambo hili kwa lengo la kuleta tija, maendeleo na utulivu,” amesema Rais Tenga wakati akizungumza na Wahariri wa Michezo kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

Rais Tenga amesema mahali penye utulivu na utawala bora watu wanakuwa na imani hasa katika masuala ya fedha, hivyo ni lazima kwa kampuni kuwekeza kwa vile kunakuwa hakuna vurugu.

Amesema ukiondoa Afrika Kusini na Angola katika ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, Ligi Kuu ya Tanzania ndiyo yenye udhamini mkubwa kupitia mdhamini wa ligi na udhamini wa matangazo ya televisheni.

Pia amesema kuanzia msimu ujao 2014/2015 klabu za Ligi Kuu hazitaruhusiwa kusajili wachezaji hadi zitakapowasilisha TFF ripoti zao za mapato na matumizi zilizokaguliwa (Audited accounts), hivyo klabu husika zijiandae kwa ripoti hizo za Januari hadi Desemba 2013.

Kuhusu tiketi za elektroniki, Rais Tenga amesema bado linafanyiwa kazi na CRDB ambayo ndiyo iliyoshinda tenda hiyo na liko katika hatua nzuri, kwani nia ya TFF na benki hiyo kuona kuwa linaanza haraka iwezekanavyo.

“Tiketi za elektroniki zimechelewa kuanza kwa sababu ambazo haziwezi kuzuilika, lakini CRDB imeshatengeneza miundombinu katika karibu viwanja vyote. Kulitokea uchelewaji katika kuleta printer (mashine za kuchapia), zilizokuja hazikuwa zenyewe. Kwa upande wa Uwanja wa Taifa, system (mfumo) iliyopo inatofautiana na ile ya CRDB. Hivyo sasa tunaangalia uwezekano wa zote mbili zitumike kwa pamoja, kwa sababu Uwanja wa Taifa una system yake tayari. Printer zimeshafika, tunataka ili suala lisitucheleweshe,” amesema.

620 wapitishwa kucheza FDL, wanne Ndanje akwama


Na Boniface Wambura
KAMATI ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imethibitisha usajili wa wachezaji 620 kati ya 624 wa timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza kutimua vumbi kesho (Septemba 14 mwaka huu).

Wachezaji wanne ambao usajili wao umezuiwa mpaka watakapokamilisha taratibu ni Emmanuel Simwanza Namwando wa African Lyon, Godfrey Bonny Namumana (Lipuli FC), na Enyinna Darlington na Chika Keneth Chukwu wote wa Mwadui FC ya Shinyanga.

Darlington na Chukwu ambao wote ni Wanigeria wamezuiwa mpaka watakapowasilisha vibali vya kufanya kazi nchini kutoka Idara ya Uhamiaji wakati Namumana aliyekuwa akicheza nchini Nepal bado hajapata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).

Nayo African Lyon imetakiwa kufikia muafaka na AYOSA Academy ambayo Namwando anatoka juu ya usajili kabla ya kuanza kumtumia mchezaji huyo.

Klabu ambazo zimemaliza nafasi zote 30 usajili katika FDL ni Friends Rangers FC ya Dar es Salaam, na Stand United FC ya Shinyanga wakati iliyosajili wachezaji wachache zaidi ni Burkina Faso FC. Klabu hiyo ya Morogoro imesajili wachezaji 19 tu.

Vilevile Kamati hiyo vilevile imethibitisha usajili wa wachezaji wanane wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) waliosajiliwa katika hatua ya pili ya usajili iliyoanza Agosti 14 hadi 30 mwaka huu.

Wachezaji hao ni Samir Ruhava na Amani Simba (Ashanti United), Robert Machucha na Said Ndutu (Yanga U20), Ayoub Masoud na Abdallah Selemani (Coastal Union U20), Ramadhan Kipalamoto (Simba U20) na Henry Joseph (Simba) ambaye tayari Hati yake Uhamisho wa Kimataifa (ITC) imeshawasili.

Vita vya Ligi Kuu vyaanza tena, Simba, Yanga kuvuna nini?


Yanga watawafunga mdomo Mbeya City kesho jijini Mbeya?

Vijana wa Kibadeni wataizuia Mtibwa jijini Dar?
 Na Boniface Wambura
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya tatu kesho (Septemba 14 mwaka huu) kwa timu zote 14 kushuka viwanjani huku masikio ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar na ile kati ya Mbeya City na Yanga.

Simba inaikaribisha Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma. Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.

Pia Azam TV itautumia mchezo huo kwa ajili ya mazoezi (broadcast training) kwa wafanyakazi wake. Hivyo mechi hiyo haitarekodiwa au kuoneshwa moja kwa moja.

Katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, shughuli itakuwa kati ya mabingwa watetezi Yanga na wenyeji wao Mbeya City SC. Mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna wa mechi hiyo James Mhagama kutoka Songea.

Mechi nyingine za ligi hiyo ni Coastal Union na Tanzania Prisons (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Ruvu Shooting na Mgambo Shooting (Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani), Oljoro JKT na Rhino Rangers (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha), Kagera Sugar na Azam (Uwanja wa Kaitba, Bukoba), na Ashanti United na JKT Ruvu (Uwanja wa Azam Complex,

Mjini Magharib yaifyatua TMK na kutinga fainali za Copa Coca Cola

TIMU ya Mjini Magharibi imepata tiketi ya kucheza fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 upande wa wavulana baada ya kuing’oa Temeke kwenye nusu fainali iliyochezwa leo (Septemba 13 mwaka huu) asubuhi Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam.

Ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa dakika za 30 na 63 kupitia Juma Ali Yusuf ndiyo yaliyoipa Mjini Magharibi tiketi ya kucheza fainali itakayofanyika kesho (Septemba 14 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kuanzia saa 9 alasiri.

Mjini Magharibi itacheza fainali hiyo na mshindi wa nusu fainali ya pili inachezwa leo jioni kwenye uwanja huo huo kati ya mabingwa watetezi Morogoro na Ilala.

Kwa upande wa wasichana Ilala imetinga fainali baada ya kuifunga Kinondoni mabao 2-0 katika nusu fainali ya kwanza. Mabao ya washindi yalifungwa dakika ya 27 na Fatuma Bahau wakati Happiness Lazoni alifunga la pili dakika ya 39.

Nusu fainali ya pili kwa wasichana itakuwa kati ya Mwanza na Mbeya.

30 waitwa kambi ya Twiga Stars

Kikosi cha Twiga Stars
Na Boniface Wambura
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Rogasian Kaijage ameita kambini kikosi cha wachezaji 30, wengi wao wakiwa vijana ikiwa ni mwendelezo wa programu ya kujenga timu hiyo.

Kambi hiyo itakuwa jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 15 hadi 26 mwaka huu. Vijana wengi wamejumuishwa ikiwa ni hatua ya mwanzo ya kuandaa timu itakayocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20.

Kaijage amesema pamoja na malengo hayo kwa timu ya vijana, bado maana kubwa inabaki kuandaa Twiga Stars iliyo imara kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Amesema Twiga Stars haikabiliwi na mashindano yoyote mwaka huu, hivyo lengo ni kuijenga upya ndiyo maana haichezi michezo ya kimataifa ya kirafiki hadi itakapofika wakati wake.

Utaratibu huo ulianza kuanzia kambi ya Machi mwaka huu, na ndio umezaa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ambayo sasa itashiriki mashindano ya Kombe la Dunia.

Wachezaji walioitwa ni Amina Ally (Lord Barden, Pwani), Asha Rashid (Mburahati Queens, Dar es Salaam), Belina Julius (Lord Barden, Pwani), Donisia Daniel (Lord Barden, Pwani), Esther Chabruma (Sayari Queens, Dar es Salaam), Eto Mlenzi (JKT, Dar es Salaam) na Evelyn Sekikubo (Mburahati Queens, Dar es Salaam).

Fatuma Bushiri (Simba Queens, Dar es Salaam), Fatuma Hassan (Mburahati Queens, Dar es Salaam), Fatuma Issa (Evergreen, Dar es Salaam), Fatuma Mustafa (Sayari Queens, Dar es Salaam), Fatuma Omari (Sayari Queens, Dar es Salaam), Flora Kayanda (Tanzanite, Dar es Salaam) na Gerwa Lugomba (Umisseta, Kanda ya Ziwa).

Hamisa Athuman (Marsh Academy, Mwanza), Maimuna Hamisi (Airtel Rising Star, Ilala), Maimuna Said (JKT, Dar es Salaam), Mwanahamisi Omari (Mburahati Queens, Dar es Salaam), Mwapewa Mtumwa (Sayari Queens, Dar es Salaam), Pulkeria Charaji (Sayari Queens, Dar es Salaam) na Rehema Abdul (Lord Barden, Pwani).

Sabahi Hashim (Umisseta, Zanzibar), Semeni Abeid (Tanzanite, Dar es Salaam), Sharida Boniface (Makongo Sekondari, Dar es Salaam), Sofia Mwasikili (Sayari Queens, Dar es Salaam), Tatu Idd (Lord Barden, Pwani), Therese Yona (TSC Academy, Mwanza), Vumilia Maarifa (Evergreen, Dar es Salaam), Yulitha Kimbuya (Marsh Academy, Mwanza) na Zena Khamis (Mburahati Queens, Dar es Salaam). 

Yanga wapewa wiki 2 kuwalipa akina Nsajigwa

Nsajigwa (2) akiwa ameshikwa na Godfrey Taita
Na Boniface Wambura
KLABU ya soka ya Yanga imepewa siku 14 kuanzia leo (Septemba 13 mwaka huu) kuwalipa waliokuwa wachezaji wake msimu uliopita, nahodha Shadrack Nsajigwa na Stephen Mwasika wanaoidai klabu hiyo jumla ya sh. milioni 15.5.

Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Septemba 12 mwaka huu) ambapo pamoja na mambo mengine ilisikiliza madai ya wachezaji hao.

Fedha hizo ni ada ya usajili ambayo klabu hiyo ilikubaliana na wachezaji hao wakati ikiwasainisha mikataba. Yanga imeshawalipa sehemu ya fedha walizokubaliana na kiasi hicho ndicho bado hakijalipwa. Nsajigwa anadai sh. milioni 9 wakati Mwasika ni sh. milioni 6.5.

Baba wa Ozil kuishtaki Real Madrid

Ozil na baba yake
Mesut Ozil

MADRID, Hispania
BABA wa Mesut Ozil, Mustafa, ametishia kuchukua hatua za kisheria kufuatia taarifa za katika vyombo vya habari nchini Hispania kudai kwamba kiungo huyo Mjerumani alikuwa akiathiriwa kipaji chake na matatizo ya nje ya uwanja wakati akiwa Real Madrid.
Mapema wiki hii, gazeti la Hispania liitwalo ABC, ambalo lina mahusiano na rais wa Real, Florentino Perez, liliripoti kuwa rais huyo wa Madrid anaamini kwamba Ozil "hakuwa vizuri kiweledi na alikuwa akichanganywa na wanawake na maisha ya kujirusha usiku".
Lakini baba wa kiungo huyo Mjerumani amejia juu tuhuma hizo akisema Perez anajaribu kumfanya kiungo huyo aliyetua Arsenal kuwa mbuzi wa kafara.
"Kwa sababu tu ana pesa nyingi haimaanishi kwamba yeye ni mtu wa heshima," baba wa Ozil alikaririwa na gazeti la Bild. "Na Perez si mtu wa heshima.
"Mesut anatumiwa kama mbuzi wa kafara sasa lakini baba yake nipo. Nitaingia mchezoni. Tutatetea upande wetu kisheria.
"Kama Mesut alikuwa na maisha yasiyozingatia weledi Madrid, kwanini sasa alikuwa akichezeshwa kila siku? Wanataka kumlaumu sasa kwa vile mashabiki na wachezaji wenzake wamekasirika (kuuzwa kwake)."
Ozil, ambaye alifunga ama kutoa pasi ya magoli 108 katika mechi 159 akiwa na Madrid, alikamilisha uhamisho wa aina yake katika siku ya mwisho na kutua Arsenal kwa ada ya paundi milioni 40, jambo lililowakera wachezaji wenzake wengi akiwamo Cristiano Ronaldo.

'Unga' wachelewesha safari ya Mark Band

Rashid Pembe (kushoto) akiwa na mwanamuziki wenzake wa Mark Band

SAKATA la kubambwa kila uchao kwa Watanzania nje ya nchi kwa tuhuma za kujihusiaha na dawa za kulevya limesababisha safari ya Mark Band kwenda Chile na Peru ichelewe kutokana na ugumu wa kuzipata visa za kuingia katika nchi hizo.
Mark Band iliyojikita na kupiga muziki asilia kwenye mahoteli ya kitalii, ilikuwa itimke nchini wiki iliyopita, lakini zoezi la upatikanaji wa visa za kuingia nchini humo kupitia balozi zilizopo Kenya na Afrika Kusini limeichelewesha safari hiyo kwa wakati.
Mkurugenzi wa bendi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2006, Rashid Pembe 'Profesa' alisema tangu Tanzania ichafuke kutokana na kukamatwa kwa raia wake wakihusisha na dawa za kulevya imekuwa usumbufu kwa watu wengine kiasi cha wao kucheleweshewa safari yao.
"Yaani kwa sasa hakuna Mtanzania anayeaminiwa anapotaka kwenda nje ya nchi au kuingia katika taifa jingine kwa kudhaniwa ni wale wale wanaojihusisha na dawa za kulevya, hata sisi imekuwa tabu kupata visa kwa wakati na kufanya tukwame kuondoka mapema," alisema.
Hata hivyo, alisema zoezi la kupata visa za kuingia katika nchi hizo wanazoenda kutumbuiza kwa mualiko maalum limekamilika na wanamaliza mambo madogo kabla ya wiki ijayo kuondoka nchini.
"Nadhani tutaondoka wiki ijayo kwani karibu kila kitu kimekaa vyema kwa sasa japo ratiba yetu ilishavurugwa kwa kuchelewa kuzipata visa," alisema.
Kwa siku za karibuni Tanzania imekuwa ikichafuka kimataifa kutokana na baadhi ya raia wake wakiwamo wasanii na wanamichezo kuripotiwa kutiwa mbaroni katika mataifa mbalimbali kwa tuhuma za kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya.
Baadhi ya walioripotiwa  kunaswa ni pamoja na video queen na nduguye, Agness Gerald  'Masogange' na Mellisa Erdwad, strika wa zamani wa Simba, Joseph Kaniki na bondia wa ukoo wa Matumla, Mkwinda na Mbwana Matumla mbali na watanzania wengine kadhaa.

Waziri Mulugo aahidi Mil 2 kwa Mbeya City wakiitungua Yanga kesho

http://kifltd.files.wordpress.com/2012/01/01_12_enn75u.jpg
Naibu Waziri Philipo Mulugo

Kikosi cha Mbeya City
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiSJsNsHjk8oZes4gIRZJMglBDLy-cqJ__Id6KV6ouVjbXYivTnjTaWyCOanYX5Ih6OyrwPaHjkzm8Gxz-fLOi_cbctliSDX9r5rqi82IUo5V_Wg7As77JRaNzSAHzEH_bs5dPA0IN52NbE/s1600/IMG_8317.JPG
Kikosi cha Yanga

NAIBU Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo ametanga kutoa dau la Sh Milioni 2 kwa kikosi cha Mbeya City iwapo watafanikiwa kuifunga Yanga katika pambano lao la Ligi Kuu Tanzania Bara linalochezwa kesho kwenye uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Aidha Waziri huyo ameamua kufunga safari kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Mbeya kwa ajili ya kuipa sapoti timu hiyo ya Mbeya City katika mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa kandanda mkoani humo.
Waziri Mulugo alisema amefunga safari hiyo ili kuhakikisha timu hiyo ya Mbeya City inapata ushindi dhidi ya mabingwa watetezi hao, Yanga ambao wameshatangaza vita dhidi ya timu hiyo wakitamba wameenda mkoani humo kuzoa pointi sita zikiwamo tatu za mechi ya leo.
Mechi nyingine ambayo Yanga imetangaza kuipigia hesabu ni ile ya Jumatano dhidi ya Prisons Mbeya iliyoanza ligi hiyo vibaya.
Waziri Mulugo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songwe  mkoani humo, alisema kwa vile anaamini Mbeya City ni timu nzuri na iwapo ikipata sapoti itafanya maajabu katika mechi hiyo ya kesho na nyingine za ligi hiyo iliyokuw amesimama kwa wiki mbili mfululizo.
Alisema kutokana na hilo ndilo maana amefunga safari kwenda Mbeya kuisapoti timu hiyo na kuahidi kuwapa Sjh Mil 2 iwapo watafanikiwa kuifunga Yanga, aliyokiri ni moja ya timu kubwa yenye uzoefu, lakini bado haamini kama inaweza kufua dafu kwa Mbey City katika mechi hiyo.
"Naifahamu Yanga ni timu nzuri yenye wachezaji wazuri, lakini katika mchezo wa Jumamosi naamini kabisa watabugizwa mabao mengi ya Mbeya City, iliyonilazimu kufunga safari kuja kuisapoti ili ishinde na wakifanya hivyo nitawapa Sh. Mil 2 taslim kama zawadi yao," alisema.
Mbeya City inayonolewa na kocha mzoefu, Juma Mwambusi inashiriki ligi hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kupanda daraja ikiwa na timu nyingine mbili za Rhino Rangers ya Tabora na Ashanti United ya Dar es Salaam na mpaka sasa ina pointi nne kutokana na mechi mbili ilizocheza.
Ilianza kwa kutoka sare ya bila kufungana na Kagera Sugar kabla ya kuicharaza Ruvu Shooting kwa mabao 2-1 katika mechi yao ya mwisho zote zilizochezwa uwanja wa Sokoine kabla ya ligi kusimama kupisha pambano la kimataifa la Taifa Stars dhidi ya Gambia.

ROCK CITY MARATHON 2013 KUZINDULIWA SEPT 19

 Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi, akikata utepe kuzindua Mbio za Rock City Marathon 2012, katika hafla iliyofanyika mwaka jana katika Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam.
Wadhamini wa Mbio za Rock City Marathon 2012, pamoja na Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi (wa tatu kulia), wakiwa katika picha ya pamoja katika hafla ya uzinduzi wa mbio hizo mwaka jana uliofanyika katika Hoteli ya New Africa Dar. 

DAR ES SALAAM, Tanzania

UZINDUZI wa msimu wa tano wa mbio za Rock City Marathon 2013 zilizoanza mwaka 2009, zikiwa na lengo la kukuza Utalii wa Ndani kupitia michezo, unatarajia kufanyika Septemba 19, kwenye Hoteli ya New Afrika, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mratibu wa mbio hizo, Mathew Kasonta, alisema kuwa pamoja na mambo mengine, mbio za mwaka huu za Rock City Marathon, zitakuwa kubwa na bora zaidi kulinganisha na miaka minne iliyotangulia.

“Tuko tayari kwa mbio za Rock City Marathon 2013, zitakzofanyika Oktoba 27. Kamati ya Maandalizi imeweka mikakati mizuri ili kuhakikisha mbio za mwaka huu zinakuwa bora na zenye mafanikio kulinganisha na misimu iliyopita,” alisema Kasonta.

Rock City Marathon zinaandaliwa na Kampuni ya Capital Plus International (CPI), kwa ushirikiano na Chama cha Riadha Tanzania (RT), pamoja na Chama cha Riadha mkoa wa Mwanza (MRAA), ambazo zimewavutia washiriki wengi wa ndani na nje ya nchi.

Kasonta aliongeza kwamba, mbio hizo zitakuwa na vipengele vitano kwa msimu huu, ambavyo ni mbio za kilometa 21 (wanawake na wanaume) na zile za kilometa tano kwa wakimbiaji kutoka makampuni mbalimbali.

Kategori nyingine za mbio hizo ni kilometa tatu kwa watu wenye ulemavu, kilometa tatu kwa watu wazima (zaidi ya miaka 55) na kilometa mbili kwa watoto walio kati ya miaka 7 mpaka 10.

Bw. Kasonta alisema kutokana na uzoefu wa mwaka jana kwa wanariadha wengi kujitokeza kushiriki, kamati ya maandalizi imeongeza idadi ya waongozaji watakaosaidia katika kuzifanikisha mbio hizo.

“Tunatarajia watu wengi kujitokeza mwaka huu, kwa kuwa tuna vitu vizuri kwa msimu huu. Tumejifunza kupitia mbio za mwaka jana, hivyo Kamati ya Maandalizi imekuja na mpango madhubuti utakaoboresha mbio zetu kwa mwaka huu,” alisema Kasonta.

Kivumbi cha FDL kuanza kesho, Kawawa Stadium kutumika Kigoma

JKT Kanembwa wakikaguliwa kwenye michuano ya Miaka 50 ya JKT jijini hivi karibuni jijini Dar
PAZIA la Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) linatarajiwa kufunguliwa rasmi kesho katika viwanja tofauti, huku uwanja wa nyumbani wa  Kanembwa JKT ya Kigoma sasa utakuwa Uwanja wa Kawawa badala ya ule wa Lake Tanganyika.

Uamuzi wa kuhamishia mechi hizo Uwanja wa Kawawa ulioko Ujiji umetokana na Uwanja wa Lake Tanganyika kutumiwa na Serikali katika Operesheni Ondoa Wahamiaji Haramu inayoendelea nchini kwa sasa. Uwanja huo hivi sasa unatumika kuhifadhi wahamiaji hao.
 

Kanembwa JKT inaanzia nyumbani kwa kuikaribisha Polisi Tabora. Mechi hiyo itachezwa Jumamosi (Septemba 14 mwaka huu).

Mechi nyingine za kufungua dimba za ligi hiyo kuwania nafasi tatu za kucheza Ligi Kuu msimu wa 2014-2014 ni Burkina Faso na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro, Mkamba Rangers na Lipuli ya Iringa kwenye Uwanja wa CCM Mkamba, Majimaji na Mlale JKT kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea na Kimondo na Kurugenzi kwenye Uwanja wa CCM Vwawa katika mechi za kundi B.
Mechi nyingine kwa kesho ni Tessema na Green Warriors zitaoneshana kazi Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. Siku inayofuata (Septemba 15 mwaka huu) Transit Camp na Polisi Dar (Mabatini mjini Mlandizi) wakati mechi nyingine za kundi hilo la A zitakuwa kati ya Villa Squad na African Lyon (Karume) na Ndanda FC na Friends Rangers (Nangwanda Sijaona, Mtwara).

Kundi C ni Polisi Mara na Polisi Dodoma (Uwanja wa Karume, Musoma), Kanembwa JKT na Polisi Tabora (Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma), Stand United na Mwadui (Kambarage, Shinyanga) wakati Pamba na Toto Africans zitamenyana Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Mzee Gurumo kuagwa rasmi Oktoba 11 Diamond Jubilee

 
 
 
Mwenyekiti wa kamati ya kumuenzi Muhidin Maalim Gurumo, Asha Baraka, akizungumza jambo katika kutambulisha onyesho maalum la Gurumo litakalofanyika Oktoba 11 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.Anayefuata upande wa kushoto wa Asha ni mzee Muhdini Gurumo, Juma Mbizo, na Said Kibiriti.
Asha Baraka na wanakamati katika kutambulisha onyesho maalum la Gurumo litakalofanyika Oktoba 11 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam. Anayefuata upande wa kushoto wa Asha ni mzee Muhdini Gurumo, Juma Mbizo, Cosmas Chidumule na Said Kibiriti. Kulia ni Katibu wa kamati Saidi Mdoe
Juma Mbizo, mratibu wa shoo hiyo, akionyesha mfano wa CD itakayouzwa ikiwa ni juhudi za kumuwekea mazingira mazuri mwanamuziki Muhdini Gurumo, baada ya kutangaza kustaafu muziki. Picha zote na Kambi Mbwana
MWANAMUZIKI mkongwe aliyestaafu muziki akiwa na bendi ya Msondo Ngoma, Muhidini Maalim Gurumo, ameandaliwa shoo mbili za kumuaga, moja wapo ikipangwa kufanyika Oktoba 11, ikiwa ni VIP, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee. 
Shoo nyingine kwa wapenzi wote itafanyika Novemba Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa TCC Sigara Chang’ombe, jijini Dar es Salaam, zote zikiwa na lengo la kumuaga kwa heshima mwanamuziki huyo na kumpa nafasi ya kuyamudu maisha yake baada ya kuachana na muziki. 
 Akizungumza leo na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa shoo hiyo iliyopewa jina la (Gurumo 53), Asha Baraka, alisema kuwa ni heshima kuwa na mwanamuziki kama Gurumo, hivyo wadau wameamua kuandaa shoo hizo za kumtafutia fedha mkali huyo. 

 Alisema wazo hilo limefanyiwa kazi kwa pamoja, akiwa na wadau kadhaa, akiwamo Said Mdoe Katibu wa Kamati hiyo, Richard Sakala mjumbe, Cosmas Chidumule, Waziri Ally, Said Kibiriti na Juma Mbizo, ambaye ndio mratibu wa Kamati hiyo. 

 ”Lengo si kumpa karatasi za kuthamini mchango wake katika tasnia ya muziki wa dansi Tanzania, ila kuhakikisha kuwa anapata mwangaza wa maisha yake baada ya kuachana na muziki. 

 ”Huyu ni mwanamuziki mwenye uwezo wa juu wakati huo, hivyo kwa sasa lazima sisi wadau tuhakikishe anajiweka katika ramani nzuri, ikiwa ni kutambua ataishi vipi nje ya muziki,” alisema.

Naye Gurumo aliwaambia waandishi wa habari kuwa ameamua kuachana na muziki kwa sababu umri na afya yake hairuhusu kufanya kazi hiyo, hivyo asitokee mtu wa kupotosha ukweli wake huo. 

 ”Nasikia watu wanasema naachana na muziki Msondo nikiwa na lengo la kurudi tena Sikinde, jambo ambalo si kweli kwa kuwa sioni nitamuimbia nani wakati nimechoka. 

 ”Naomba kwa sasa kuwapa nafasi watu waliojitolea kunisaidia hasa kwa kuunda kamati hii ambayo nitapanda jukwaani kuimba mara ya mwisho, ukizingatia kuwa kazi yangu inahitaji kuagana na mashabiki wangu jukwaani na si mahali pengine,” alisema. 

 Katika hatua nyingine, mwanamuziki Cosmas Chidumule, alisema kuwa licha ya kuwa ameokoka, ila atapanda jukwaani kuimba na mzee Gurumo kama sehemu ya kutambua mchango wake.

”Nimeokoka lakini si sababu ya kunifanya nishindwe kumheshimu mwanamuziki ambaye nina uhakika mchango wake ulinifanya niwe juu katika muziki wa dansi Tanzania,” alisema.

 Kwa mujibu wa Kamati hiyo ambayo Mdoe ndio Katibu wake, taratibu zote zinaendelea ikiwa ni kuandaa nyimbo alizowahi kuimba na kuziweka katika mfumo wa kibiashara, ikiwamo mpango wa kuuza nyimbo zake katika makampuni ya simu za mikononi.

SGM ruksa kukipiga Ashanti Utd, wawili waombewa ITC

Said Maulid 'SMG'
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa Watanzania wawili kucheza mpira wa miguu nchini Afrika Kusini.

Wachezaji hao; Robert Kobelo na Mohamed Ibrahim wamepewa hati hizo baada ya kuombewa na Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kama wachezaji wa ridhaa ili wajiunge na klabu ya Cacau United ambayo timu yake inacheza Ligi Daraja la Pili katika Wilaya ya Cacau.

Naye mchezaji Said Maulid aliyejiunga na Ashanti United akitokea nchini Angola msimu huu amepata ITC ambayo sasa inamwezesha kuchezea timu hiyo katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoingia mzunguko wake wa tatu keshokutwa (Septemba 14 mwaka huu).

TEMEKE, MJINI MAGHARIBI KUCHEZA NUSU FAINALI COPA COCA COLA LEO

TEMEKE na Mjini Magharibi zinapambana leo (Septemba 13 mwaka huu) katika mechi ya nusu fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 itakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, jijini Dar es Salaam.

Timu hizo zimetinga hatua hiyo baada ya kushinda mechi zao za robo fainali ya michuano hiyo zilizochezwa jana (Septemba 12 mwaka huu) asubuhi kwenye uwanja huo huo.

Wakati Temeke imetinga hatua hiyo baada ya kuilaza bao 1-0 Iringa lililofungwa dakika ya 18 na Ramadhan Mohamed, Mjini Magharibi imeing’oa Mtwara kwa ushindi wa bao 1-0.

Robo fainali nyingine zinachezwa leo (Septemba 12 mwaka huu) jioni kwa Kilimanjaro kuvaana na mabingwa watetezi Morogoro huku Arusha ikioneshana kazi na Ilala.