STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 19, 2013

Van Persie, Suarez, Bale kuwania tuzo ya PFA

Robin Van Persie akiwa na tuzo ya PFA ya mwaka jana

KIUNGO nyota wa Tottenham Hotspurs, Gareth Bale, Luis Suarez wa Liverpool na Mholanzi Robin van Persie wa Manchester United wanatarajia kuonyesha kazi katika kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka (PFA) iliyotangaza kwa msimu wa mwaka 2012-2013
Orodha iliyotangaza leo Ijumaa imetaja majina ya wachezaji sita wakiwemo hao watatu ambao wamekuwa moto msimu huu katika Ligi Kuu ya England.

Orodha hiyo imewajumuisha pia wakali wengine watatu ambao ni pamoja na Michael Carrick wa Manchester United, Eden Hazard na Juan Mata wa Chelsea.
Hata hivyo mshambuliaji wa Swansea City, Michu mwenye mabao 17 katika Ligi Kuu ya England yeye hayupo katika orodha hiyo kama ilivyo kwa nyota yeyote wa Manchester United..
Bale aliyeshinda tuzo hiyo mwaka 2011, ameteuliwa kutokana na mafanikio makubwa aliyoipa timu yake, ila anatarajiwa kupata upinzani toka kwa Suarez aliyeifungia Liverpool mabao 22 mpaka sasa katika Ligi Kuu.
Mshindi wa tuzo hiyo wa mwaka jana, Van Persie anayechuana na Suarez katika ufungaji wa mabao msimu huu akizidiwa kwa bao moja yeye na Carrick wanakaribia kuipa timu yao taji ya 20 la Ligi Kuu.

Hazard na Mata wapo katika orodha hiyo kutokana na kuisaidia timu yao katika msimu huu baada ya awali kuregarega.
Katika orodha wa Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi ya Mwaka wapo Romelu Lukaku anayekipiga kwa mkopo West Brom na mshambuliaji wa Aston Villa, Christian Benteke.
Wachezaji wengine wanaokamilisha orodha hiyo ni wachezaji wa kimataifa wa England Danny Welbeck na  Jack Wilshere.
Washindi wa tuzo hizo watatangazwa Aprili 28 mwaka huu.
 

Orodha ya washindi waliopita 2011-12: Robin van Persie (Arsenal)
2010-11: Gareth Bale (Tottenham)
2009-10: Wayne Rooney (Man Utd)
2008-09: Ryan Giggs (Man Utd)
2007-08: C Ronaldo (Man Utd)

Kila la Heri Azam kufa ama kupona kesho, TFF yaitakia la heri

Kikosi cha Azam kinachotegemewa na watanzania kutoa raha kesho Taifa

Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam FC katika mechi yake ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco itakayochezwa kesho (Aprili 20 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Azam FC ina fursa nzuri ya kufanya vizuri kwenye mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Emile Fred kutoka Shelisheli kutokana na maandalizi iliyofanya, lakini vilevile tunatoa mwito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kuiunga mkono.

Makocha wasaidizi wa timu zote mbili, Kalimangonga Ongala wa Azam na Lahcen Ouadani wa AS FAR Rabat wamezungumza na waandishi wa habari kuhusu mechi hiyo, kuwa wamejiandaa kuibuka na ushindi.

Kocha Ongala amesema wamepata DVD za mechi tatu za mwisho za AS FAR Rabat, moja ikiwa dhidi ya timu ya Al Nasir ya Libya ambayo waliitoa katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho na nyingine mbili za ligi ya Morocco ambazo wanazifanyia kazi kuhakikisha wanashinda kesho.

Naye Ouadani amesema hawaifahamu vizuri Azam, lakini wanaujua mpira wa Tanzania baada ya kuangalia mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas) iliyochezwa jijini Dar es Salaam Machi 24 mwaka huu na Stars kushinda mabao 3-1.

Baadhi ya wachezaji ambao Azam inatarajia kuwatumia kwenye mechi ya kesho ni pamoja na Aishi Manula, Mwadini Ally, Khamis Mcha, John Bocco na Salum Abubakar ambao pia wamo kwenye kikosi cha sasa cha Taifa Stars kilicho chini ya kocha Kim Poulsen.

AS FAR Rabat ina wachezaji sita kwenye timu ya Taifa ya Morocco. Wachezaji hao ni mabeki Younes Bellakhdar, Abderrahim Achchakir, Younnes Hammal, na viungo Salaheddine Said, Salaheddine Aqqal na Youssef Kaddioui.

Golden Bush wazee kwa vijana kuonyeshana kazi kesho

Golden Bush Veterani

Golden Bush Fc

BAADA ya kutoka Morogoro wakiwa wameacha kumbukumbu ya kutoa kipigo uwanja wa Jamhuri, wakali wa soka la maveterani jijini Dar es Salaam, Golden Bush Veterani kesho asubuhi wanatarajiwa kuvaana na vijana wao wanaotisha kwenye Ligi Daraja la Nne Wilaya ya Kinondoni, Golden Bush Fc.
Pambano hilo la kirafiki la kujipima nguvu kuziweka vyema timu hizo katika michuano inayoshiriki, utachezwa majira ya saa 1 asubuhi kesho kwenye viwanja vya Chuo Kikuu (UDSM).
Msemaji wa timu hiyo, Onesmo Waziri 'Ticotico' alisema kuwa pambano hilo kwao ni maalum kwa ajili ya kujianda na mchezo wao dhidi ya mahasimu wao, Wahenga Fc watakaoumana nao siku ya Muungano.
Ticotico ambaye ni mmoja wa washambuliaji wa timu hiyo alisema kuwa wanaamini pambano lao litakuwa tamu ikizingatiwa vijana wao wanafanya vyema kwenye ligi hiyo ya TFF ikiongoza msimamo wa kundi lake ikiwa na pointi 12 kutokana na kushinda mechi zake zote nne ilizocheza mpaka sasa huku ikiwa na hazina kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa idadi ndogo ya mabao.
Timu hizi kwa hivi karibuni zilishakutana na mara ya kwanza wazee walichezea kichapo kabla ya kurudiana nao na kuwanyuka vijana hao mabao 2-1.
Ticotixo alisema wazee watakishusha kikosi chao chote kikali ili kuwatia adabu vijana wao ambao wameanza kuchonga kwa mafanikio yao ya kwenye ligi.

Mzambia kuwahukumu Cheka, Mashali PTA

Mashali (kushoto) na Cheka wakitunushiana misuli


SHIRIKISHO la Ngumi la Kimataifa (IBF) limeteua refarii na majaji wa pambano la kutetea ubingwa wa Afrika kati ya anayeushukilia ubingwa huo Francis Cheka wa Tanzania na mpinzani wake Thomas Mashali ambaye ni bingwa wa uzito wa Middle ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati (ECAPBA)

Refarii wa mpambano huo wa kukata na shoka atakuwa ni John Shipanuka kutoka nchini Zambia mbaye alilisimamia pambano kati ya Francis Chaka na Mada Maugo mwaka jana kwa ustadi mkubwa. Shipanuka ni Afisa Ugavi katika jeshi la Jamhuri ya Watu wa Zambia na ana ujuzi mkubwa wa kusimamia mapambano ya ngumi ya kimataifa.
Francis Cheka (kushoto) na Thomas Mashali (kulia) wakiwa wameushika mkanda wa ubingwa

Aidha, majaji wa mpambano huo ni Daudi Chikwanje kutoka Malawi ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Chama Cha Ngumi Cha Malawi na ambaye anakuwa jaji namba moja. Steve Okumu wa Kenya ambaye anakuwa jaji namba mbili na Ismail Sekisambu wa Uganda ambaye anakuwa jaji namba tatu. Msimamizi mkuu wa mpambano huo ni Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtanzania Onesmo Ngowi.

Hata hivyo Ngowi amemwagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Viwango  na Ushindi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC) Boniface Wambura amshikie nafasi hiyo ili Ngowi apate nafasi nzuri ya kusimamia mapambano matatu ( moja la ubingwa wa dunia kwa vijana,, lingine la ubingwa wa mabara kwa wanawake na lingine ubingwa wa Afrika) yatakayofanyika nchini Ghana tarehe 3 mwezi Mei.

Nayo Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini TPBC imeshateua maofisa watakaosimamia mapambano ya awali pamoja na kutoa kibali kwa kampuni ya Mumask Investment and Gebby ili iendeshe mpambano huo!

Hii ni mara ya pili kwa bondia Francis Cheka kutetea ubingwa wake tangu amsambaratishe kwa TKO bondia machachari Mada Maugo katika mpambano uliofanyika mwaka jana mwezi wa Aprili katika ukumbi wa PTA jijini Dar Es Salaam.

Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kuanza Mei 12



Na Boniface Wambura
LIGI ya Mabingwa wa Mikoa kutafuta timu tatu zitakazopanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itaanza Mei 12 mwaka huu.

Mwisho wa mikoa kuwasilisha majina ya mabingwa wao ni Mei 1 mwaka huu wakati ratiba ya ligi hiyo itapangwa mbele ya waandishi wa habari Mei 3 mwaka huu kwenye ofisi za TFF.

Uwasilishaji wa jina la bingwa wa mkoa unatakiwa kufanyika pamoja na ulipaji ada ya ushiriki ambayo ni sh. 100,000. Mfumo wa ligi hiyo ni bingwa wa mkoa X kucheza na bingwa wa mkoa Y nyumbani na ugenini ambapo mshindi ndiye anayesonga mbele katika hatua inayofuata.

Usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika hatua ya mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.

Azam wamtengea Shomari Kapombe kiasi cha Sh Mil.90/-


Shomari Kapombe

Na Somoe Ng'itu
KATIKA kuhakikisha mwakani inakuwa na ukuta imara, klabu ya Azam imeanza mikakati ya kumnasa beki tegemeo wa Simba na timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Shomary Kapombe na tayari imetenga kiasi cha Sh. milioni 60.
Mbali na kiasi hicho cha fedha pia Azam imepanga kumpatia beki huyo kiraka gari jipya la thamani ya Sh. milioni 30.
Azam inataka kutumia udhaifu wa Simba kushindwa kumpatia mkataba mpya beki huyo ambaye mkataba wake wa sasa unamalizika Desemba, jambo linalomaanisha anaweza kuondoka bure iwapo atakataa kusaini mkataba mpya Msimbazi na pesa zote kutoka katika klabu itakayomsajili zitaingia mifukoni mwake.
Hata hivyo, beki huyo amemweleza rafiki yake wa karibu kwamba kiasi hicho ni kidogo kwa kiwango alichonacho hivi sasa.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam, uongozi wa Azam, timu pekee nchini ambayo kwa sasa inashiriki mashindano ya kimataifa, imetenga kiasi cha Sh. milioni tatu kama mshahara wa kila mwezi wa beki huyo aliyesajiliwa na Simba akitokea timu ya Polisi Morogoro.
Chanzo kililiambia gazeti hili kuwa Azam wakifanikiwa kumpata Kapombe, mikakati yao itakuwa ni kwa chipukizi Haruna Chanongo na Ndembla Ibrahim.
"Wameanza maandalizi ya kumshawishi asisaini mkataba mwingine wa Simba na wao watamsainisha ifikapo mwezi Agosti mwaka huu," kilisema chanzo hicho.
Kapombe alishindwa kusema lolote kuhusiana na kuwapo kwa mazungumzo dhidi ya Azam na kuongeza kwamba yeye kwa sasa ni mchezaji wa Simba hivyo anajipanga kuisaidia timu yake ifanye vizuri katika mechi zilizosalia.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, Kapombe ni mmoja wa wachezaji mihimili wa klabu hiyo na hawatakuwa tayari kuona wanasajiliwa na klabu nyingine.
Mtawala alisema kwamba Kapombe ni mchezaji muelewa na kamwe hataweza kukurupuka na kukubali kuiacha Simba iliyomchukua hali ya kuwa klabu yake imeshuka daraja.
"Anafahamu ana kiwango cha kucheza soka Ulaya na Simba ni sehemu pekee inayoweza kutimiza ndoto zake, tutakaa naye na kumpa mkataba mnono ndani ya muda muafaka," alisema katibu huyo mwenye taaluma ya sheria.
Viongozi wa Azam, katibu mkuu Nassor Idrissa na meneja Patrick Kahemele, hawakupatikana jana katika simu zao za mikononi kuzungumzia mipango hiyo ya kumnasa Kapombe.
Hata hivyo, Azam imekuwa na kawaida ya kufanya usajili wake kimya kimya na hutangaza mchezaji mpya baada ya kukamilisha taratibu zote zinazotakiwa iwe kwa mchezaji wa ndani au nje ya nchi.

Chanzo:NIPASHE

Niyonzima ‘abomoka’ pua


Haruna Niyonzima dimbani

Na Sanula Athanas, Tanga
WACHEZAJI watatu wa Yanga akiwamo kiungo wao wa kimataifa Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, waliumia vibaya katika mechi yao ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya ‘maafande’ wa Mgambo JKT iliyomalizika kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa juzi, imefahamika.
Akizungumza na NIPASHE wakati wa mazoezi ya Yanga kwenye uwanja huo jana asubuhi, Daktari wa timu hiyo, Nassoro Matuzya alisema kuwa Niyonzima aliumia vibaya pua yake alipogongana na beki 'kisiki' wa Mgambo, Bashiru Chanacha dakika 12 kabla ya mechi hiyo kumalizika.
Matuzya, ambaye pia aliwahi kuwa daktari wa timu ya taifa ya vijana (Serengeti Boys), alisema kuwa kugongana kwa wawili hao kulisababisha kupasuka kwa jipu dogo alilokuwa nalo nyota huyo puani kwake.
Mwandishi alishuhudia pua ya Niyonzima aliyekuwa amekaa kwenye benchi wakati wachezaji wengine wa Yanga wakiendelea na mazoezi jana, ikiwa ‘imebomoka’ sehemu ya juu na baadhi ya nyama zikining’inia kwa chini ndani ya matundu ya pua.
Hata hivyo, maofisa wa Yanga waliokuwa uwanjani waliwakataza waandishi kumpiga picha kwa sababu jeraha alilokuwa nalo lilikuwa linatisha.
Akizungumza kwa tabu, Niyonzima aliliambia gazeti hili kuwa alikuwa akijisikia maumivu makali usiku wa kuamkia jana, lakini anaamini kidonda hicho kitapona haraka ili arejee uwanjani kupambana kuwania ubingwa wa 23 wa ‘Wanajangwani’.
“Kwa kweli mechi ya jana (juzi) ilikuwa ngumu. Wapinzani (Mgambo) walikuwa wameikamia, walikuwa wanacheza rafu za kutisha. Angalia pua yangu ilivyo. Usiku nimehangaika sana kupata usingizi. Kinachouma zaidi marefa hawakutoa adhabu yoyote licha ya kufanyiwa faulo mbaya kama hii,” alisema Niyonzima huku akishika pua yake.
“Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kupata pointi moja kwa sababu tulicheza katika uwanja usiokuwa na hadhi na waamuzi hawakutenda haki kwetu kwa kiasi kikubwa,” aliongeza mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya maafande wa APR ya Rwanda.
Mbali na Niyonzima, ambaye mkataba wake na Yanga unamalizika mwishoni mwa msimu huu, kiungo Frank Domayo na mshambuliaji Mganda Hamis Kiiza pia wanasumbuliwa na majeraha baada ya kuumia katika mechi ya juzi.
Kwa mujibu wa daktari wa Yanga (Mtuzya), Kiiza ambaye alishindwa kufanya mazoezi ya jana, aliumia kifundo cha mguu wa kulia dakika moja kabla ya mapumziko ya mechi yao ya juzi na nafasi yake kuchukuliwa na mfungaji bora wa Kombe la Kagame mwaka jana, Said Bahanunzi.
“Kiiza ameshindwa kufanya mazoezi kwa sababu jana (juzi) aliumia kifundo cha mguu. Domayo nililazimika kumshona nyuzi mbili usoni baada ya kupasuka,” alisema Matuzya.
Yanga waliondoka jijini hapa jana saa 5:24 asubuhi kurejea Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi yao ya 24 ya ligi msimu huu dhidi ya JKT Ruvu itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini humo.
Kabla ya kuondoka jijini hapa jana, meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh alisema kuwa baada ya kutua Dar es Salaam, wachezaji watapewa mapumziko ya saa 12 kabla ya kuingia tena kambini jijini humo kujiandaa kwa mechi dhidi ya JKT Ruvu.
Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati Yanga wanaongoza msimamo wa ligi ya Bara wakiwa na pointi 53, sita juu ya mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam wanaokamata nafasi ya pili. Yanga wanahitaji pointi nne tu kutawazwa mabingwa pasipo kujali matokeo ya Azam katika mechi tatu zilizobaki.

CHANZO:NIPASHE

Azam wajipanga kuwalipua Wamorocco kesho Taifa

Kocha wa Azam John Stewart Hall

Kikosi cha Azam kitakachowakabili As FAR -Rabat ya Morocco kesho

KOCHA wa klabu ya Azam ya jijini Dar es Salaam, Stewart Hall, alisema kuwa tayari amewaambia wachezaji wake kutocheza kwa hofu katika mechi yao ya kesho dhidi ya AS FAR ya Morocco itakayokuwa ya kwanza katika hatua ya pili ya mashindano ya Kombe la Shirikisho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wapinzani hao wa Azam walianza kuwasili nchini juzi kujiandaa kwa mechi hiyo itakayofanyika kuanzia saa 10:00 jioni.
Hall alisema kuwa hadi jana mchana, kikosi chake hakikuwa na majeruhi hivyo anaamini kuwa watafanya vyema na kujiandalia mazingira mazuri ya kusonga mbele.
Akizungumza jana, Hall alisema kuwa anafahamu mechi hiyo itakuwa na ushindani mkali kwa sababu kila upande unataka matokeo mazuri.
"Najua wao wamekuja kusaka matokeo mazuri ugenini ili iwe kazi rahisi nyumbani kwao na sisi tumejipanga kuanza vyema ili tusipate tabu katika mchezo wa marudiano... ni mechi itakayokuwa na ushindani mkali," alisema kocha huyo raia wa England.
Hall aliongeza kwamba wao wanatambua kuwa hatua waliyofika ni ngumu na yenye changamoto huku akisema pia wanakutana na timu yenye uzoefu wa muda mrefu wa kushiriki mashindano ya kimataifa.
"Tunahitaji kuwa makini na kutumia vizuri nafasi tutakazotengeneza ili kupata matokeo bora... nimeshaona baadhi ya mechi zao katika DVD na hivyo tunajua mbinu zao uwanjani," alisema kocha huyo.
Alisema pia hatua waliyoifikia ni nzuri na endapo watasonga mbele, watajiwekea historia kwani klabu hiyo inashiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Afrika inayosimamiwa na kuandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Azam walisonga mbele katika mashindano hayo baada ya kuzitoa Al Nasri ya Sudan Kusini na Barrack Young Controllers ya Angola.
Hall na kocha mwenzake wa timu ya As FAR Rabat wanatarajiwa kuzungumza na wanahabari asubuhi ya leo kuelezea maandalizi ya kuelekea pambano lao la kesho, wakiwa sambamba na manahodha wa timu hizo.

Twanga Pepeta kusindikiza Utamaduni wa Msukuma Kirumba

 
BENDI ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta' ni miongoni mwa makundi yatakayotoa burudani katika tamasha kihistoria la 'Utamaduni wa Msukuma' litakalofanyika Mei 27 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mraribu wa tamasha hilo kutoka kampuni ya May Way Entertainment, Rose Mwita, alisema kuwa mbali na Twanga Pepeta ambayo itatumbuiza pia kwenye mwendelezo wa tamasha hilo mjini Nansio, Ukerewe siku ya Mei 28, pia kutakuwa na wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya wakiwamo wanaotoka jijini Dar es Salaam.
“Tamasha hili linalenga kuhamasisha jamii ya Wasukuma, Wakerewe na makabila mengine kuenzi mila na tamaduni zetu. Vilevile, jamii na familia zilizopo ndani na nje ya mikoa  zikumbuke nyumbani na kutembelea wazee mara kwa mara,” alisema Rose.
Aliongeza kuwa wakati wa tamasha hilo, pia watakaohudhuria watapata nafasi ya kusikia historia ya Wasukuma na Wakerewe kwa kina kutoka kwa wazee wanaotoka maeneo mbalimbali, hasa kwenye familia za watemi wa Kisukuma na Kikerewe.
Maonesho mengine yatakayokuwapo wakati wa tamasha ni pamoja na maonyesho ya zana za kale za jadi zilizotumiwa na makabila hayo, kucheza ngoma za asili za Wasukuma na Wakerewe pamoja na vikundi tofauti vya ngoma za asili na sanaa za makabila mengine.
"Pia kutakuwa na vyakula vya aina mbalimbali vyenye asili ya Usukumani na Ukerewe... na pia vinywaji vya asili ya Msukuma na Mkerewe," alisema Rose.