STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, November 1, 2013

Azam, Mbeya City kuendeleza rekodi zao Bara kesho

Azam


Mbeya City
MECHI za raundi ya 12 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinatarajiwa kuendelea tena kesho kwenye viwanja vinne tofauti, huku mashabiki wa soka wakitaka kujua kama Azam na Mbeya City ambazo ndizo pekee hazijapoteza mchezo mpaka sasa zitavuna nini?
Mbali na kuendeleza rekodi pia iwapo timu hizo zitashinda mechi zake hizo zitaiengua Yanga kileleni na kuiporomosha hadi nafasi ya tatu na zenyewe kurejea kwenye uongozi huo wakisubiri mechi za kufungia dimba la duru la pili katikati ya wiki ijayo.
Azam waliokuwa wakiongoza msimamo wa ligi hiyo mpaka jioni hii kabla ya Yanga kuwashusha yenyewe itaikaribisha Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Chamazi, huku wapinzani wao, Mbeya City nao watakuwa dimba la nyumbani Sokoine kuialika Ashanti United.
Michezo hiyo ni migumu kwa timu zote nne, lakini kwa kasi ya Azam na Mbeya City ni wazi Ashanti na Ruvu watakuwa na kibarua kizito cha kuweza kudhibitisha kuwa wao nao ni kiboko iwapo watazisimamisha timu hiyo katika viwanja hivyo.
Afisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire aliiambia MICHARAZO kwamba kesho wanataka kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza msimu huu 'kuwatengua udhu' Azam kwenye uwanja wa Chamazi, kwa madai wamejiandaa vya kutosha kupata ushindi.
Bwire alisema kikosi chao kipo imara japo itaendelea kumkosa kiungo mkabaji wao, Juma Seif Kijiko ambaye alionyeshwa kadi nyekundu katika pambano baina ya timu yao na Ashanti United lililoisha kwa sare.
Ruvu imesema wakali wao kama Elias Maguri, Cosmas Ader, Stephen Mwasyika, Said Dilunga na wengine wapo tayari kuwazima Azam ambao wenyewe wamenukuliwa kupiotia meneja wao Jemedari Said kwamba wanataka kumaliza mechi za duru la kwanza wakiwa kileleni mwa msimamo ili kutimiza ndoto za kuja kuwa mabingwa wapya nchini.
Mechi nyingine za kesho ni kati ya Mgambo JKT itakayoumana na 'majirani' zao Coastal Union katika pambano linalosubiriwa kwa hamu litakalochezwa kwenye uwanja wa  Mkwakwani, Tanga huku Mtibwa Sugar ya Morogoro itaialika Rhino Rangers ya Tabora katika dimba la Manungu, Morogoro.
Siku ya Jumapili kutakuwa na mechi moja tu itakayowakutanisha 'Wajelajela' Prisons ya Mbeya itakayoikaribisha timu ya Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Katika mechi zao mwisho, Prisons ililala mabao 2-0 mbele ya Mbeya City wakati Oljoro ililazimishwa suluhu na Ashanti United.
Mechi za kufungia duru la kwanza zitaanza kuchezwa Novemba 6 kwa pambano kati ya Jkt Ruvu dhidi ya Coastal Union, Ashanti United dhidi ya Simba, Kagera Sugar kuwa wenyeji wa Mgambo JKT na Ruvu Shooting kuumana na Mtibwa Sugar.
Siku inayofuata yaani Novemba 7, Azam itacheza na Mbeya City uwanja wa Chamazi, huku mabingwa watetezi Yanga itaikaribisha Oljoro JKT na Rhino Rangers itakuwa dimba la nyumbani kuikaribisha Prisons ya Mbeya.

Simba, Kagera Sugar zavuna Mil 32 Taifa

Na Boniface Wambura
MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Kagera iliyochezwa jana (Oktoba 31 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 32,726,000.

Washabiki waliohudhuria mechi hiyo namba 81 iliyomalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 walikuwa 5,541 ambapo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Mgawo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 4,992,101.69, gharama za kuchapa tiketi sh. 3,183,890 wakati kila klabu ilipata sh. 7,242,252.45.

Wamiliki wa uwanja walipata sh. 3,682,501.25, gharama za mchezo sh. 2,209,500.75, Bodi ya Ligi sh. 2,209,500.75, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,104,750.37, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 859,250.29.

Yanga 'yachinja' tena maafande Taifa, Ngassa dah!


 Mfungaji wa mabao mawili ya timu ya Yanga dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Mrisho Ngasa akishangilia bao lake la kwanza katika mchezo uliofanyika leo kwenye Uwanjawa Taifa jijini Dar es Salaam.
 Mshambulijia wa Yanga, Hamis Kiiza akiwa katika harakati za kufunga.
Wachezaji wa Yanga wakishangilia.
Beki wa JKT Ruvu akiokoa moja ya hatari langoni mwake.
Kiungo wa JKT Ruvu, Nashon Naftal akimtoka Mrisho Ngasa.
Simon Msuva akichuana na Kessy Mapande wa JKT Ruvu.
Mashabiki wa Yanga wakishangilia timu yao.
Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao la tatu lililofungwa na Oscar Joshua. (Picha zote: Francis Dande)
JANGWANI wanacheka! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga kuendelea kutoa dozi kwa timu za majeshi baada ya jioni hii kuivurumusha JKT Ruvu kwa mabao 4-0 na kukalia kiti cha uongozi wa ligi hiyo.
Mabao mawili ya mapema ya Mrisho Ngassa 'Uncle' na mengine ya kipindi cha pili yaliyofungwa na beki wa kushoto, Oscar Joshua na jingine la Jerry Tegete yameifanya Yanga kufikisha pointi 25 kutokana na kucheza mechi 12, huku Ngassa akifikisha jumla ya mabao matano katika orodha ya wafungaji na Tegete kufikisha manne.
Ushindi huo wa Yanga ni wa tatu mfululizo kwa maafande wa Jeshi baada ya awali kuitafuna Mgambo mabao 3-0 kisha kuisulubu Rhino Rangers kwa idadi kaka hiyo kabla ya leo kuisasambua JKT Ruvu.
Mabingwa hao watetezi watamaliza mechi zao za duru la kwanza kwa kuvaana tena na maafande wengine Oljoro JKT pambano lityakalochezwa Alhamis ijayo kwenye uwanja wa Taifa.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena wikiendi hii katika viwanja viwanja vitano kuamliza mechi za raundi ya 12 kabla ya Jumatano na Alhamis kuhitimishwa kwa ligi hiyo ambayo msimu huu imekuwa na msisimko na ushindani mkubwa.


Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2013-2014                                         P    W   D   L    F    A   GD  PTS
01. Yanga                   12    7    4    1   28  11   17    25
02. Azam                    11    6    5    0   17   7    10    23
03. Mbeya City           11    6    5    0   15   7     8     23
04. Simba                   12    5    6    1   22  11    11    21
05. Kagera Sugar        12    4    5    3   12    9    3     17
06. Ruvu Shooting       11    4    4    3   13   10   3     16
07. Mtibwa Sugar        11    4    4    3   16  15    1     16
08. Coastal Union        11    3    6     2   10   6    4     15
09. JKT Ruvu              12    4    0    8    9   16  -7     12
10.Rhino Rangers         11    2    4    5    9   15  -6     10
11.Ashanti                    11    2    4    5    10  19 -9     10
12.Prisons                    11    1    5    5     5   14 -9      8
13.Oljoro                     11    1    4    6     8    16 -8     7
14.Mgambo                 11    1    2    8     3    21 -18   5

Wafungaji:
9- Tambwe Amisi (Simba)
8- Hamis Kiiza (Yanga)
7- Elias Maguri (Ruvu Shooting), Juma Luizio (Mtibwa Sugar)
6- Kipre Tchetche (Azam)
5- Tumba Sued (Ashanti Utd), Themi Felix (Kagera), Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa (Yanga)
4-Peter Michael (Prisons), Jerry Santo (Coastal Union), Jerry Tegete (Yanga)
3- Haruna Chanongo, Jonas Mkude (Simba), Bakar Kondo (JKT Ruvu), Themi Felix (Kagera), Paul Nonga (Mbeya City), Salum Machaku (JKT Ruvu), Jerry Santo (Coastal Union),
2- Haruna Moshi, Crispian Odulla (Coastal Union), Saady Kipanga (Rhino Rangers), Mwagani Yeya, Jeremiah John, Peter Mapunda,(Mbeya City), Godfrey Wambura (Kagera Sugar), Shaibu Nayopa, Amir Omary (JKT Oljoro), Khamis Mcha (Azam), Shaaban Nditti (Mtibwa Sugar), Betram Mombeki, Ramadhani Singano (Simba), Said Dilunga (Ruvu Shooting)
1- Abdi Banda, Danny Lyanga (Coastal Union), Henry Joseph, Joseph Owino, Gilbert Kazze (Simba), Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, Simon Msuva, Frank Dumayo, Mbuyi Twitte, Oscar Joshua (Yanga), Iman Joel, Salum Majid, Mwalimu Musuku, Kamana Salum, Hussein Abdallah, Abbas Mohammed (Rhino Rangers), Gaudence Mwaikimba, Seif Abdallah,  Aggrey Morris,  John Bocco, Joseph Kimwaga, Faridi Maliki, Hamphrey Mieno, Salum Abubakar, Erasto Nyoni (Azam), Steven Mazanda, Richard Peter, Deo Deus  (Mbeya City), Laurian Mpalile (Prisons-OG), Shaaban Susan, Jerome Lembeli, Cosmas Ader  (Ruvu Shooting), Masoud Ally, Shaaban Kisiga (Mtibwa Sugar), Shaaban Juma, Anthony Matangalu, Paul Maono(OG), John Matei, Mwinyi Ally (Ashanti Utd), Abdallah Bunu, Emmanuel Switta, Amos Mgisa (JKT Ruvu), Fully Maganga, Hamis Msafiri (Mgambo JKT), Seleman Kibuta, Daud Jumanne, Maregesi Marwa, Clement Douglas, Salum Kanoni (Kagera Sugar), Paul Malipesa, Expedito Kidulo, Nurdin Mohammed, Fikiri Mohammed (Oljoro JKT)

Yanga kurejea kileleni kwa mgongo wa JKT Ruvu?

Yanga wataendelea kushangilia leo kama hivi
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga leo ina nafasi kubwa ya kurejea kileleni iwapo itapata ushindi mbele ya JKT Ruvu katika mfululizo wa mechi za raundi ya 12 itakayochezwa uwanja wa Taifa.
Yanga yenye pointi 22 kutokana na kucshuka dimbani mara 11, iwapo itaiangusha JKT ambayo imepoteza yale makali yake iliyopanza nayo ligi ilipoanza miezi mitatu iliyopita, itafikisha jumla ya pointi 25 na kuziengua Azam na Mbeya City waliotangulia kileleni ambao wana piinti 23.
Hata hivyo Yanga, haipaswi kuwadharau JKT Ruvu inayonolewa na kocha mahiri, Mbwana Makatta kwani huenda isikubali kugeuzwa ngazi na mabingwa hao kwenye uwanja wa Taifa.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro, alisema kikosi chao kipo imara kwa ajili ya pambano hilo japo kuna baadhi ya majeruhi na kiungo wao nyota, Haruna Niyonzima aliyeenda kwao Rwanda kwa matatizo ya kifamilia watakosekana kwenye pambano hilo la leo.
Wachezaji watakaoungana na Niyonzima kulikosa pambano hilo kutokana na kuwa majeruhi ni beki wa kushoto, David Luhende na kiungo mshambuliaji Nizar Khalfan'.
Minziro alisema pamoja na kuwakosa wachezaji hao, lakini wamejiandaa kuendeleza wimbi la ushindi kwa sababu wachezaji waliosalia bado ni imara na wana ari kubwa ya kuipa ushindi Yanga iliyopo nafasi ya tatu kwa sasa ikitangulia watani zao Simba ambao jana walilazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar.
Upande wa JKT Ruvu, kocha wake Mbwana Makatta alinukuliwa na kituo cha redio kwamba wanahisi uchovu wa safari waliokuwa nao ukawagharimu baada ya gari lao kuharibika njiani juzi wakirejea jijini toka mjini Tabora walipoenda kucheza na Rhino Rangers na kunyukwa bao 1-0.
Mbwana alisema hata hivyo watapigana kiume kuhakikisha hawapotezi pambano hilo, japo maafande hao kwa siku za karibuni wamekuwa mdebwedo kwa kufungwa mfululizo baada ya awali kushinda mechi tatu mfululizo.
Vijana hao wa JKT kwa sasa wana pointi 12 tu baada ya kucheza mechi 11, wakishinda nne na kufungwa saba na kuleta hisia kilichoikumba msimu uliopita iliponusurika kushuka daraja huenda ikarejea tena msimu huu japo ni mapema wakati duru la kwanza likiisha wiki ijayo.