STRIKA
USILIKOSE
Thursday, June 7, 2012
Mchumiatumbo atamba hana mpinzani Bongo
BONDIA wa ngumi za kulipwa wa uzito wa juu, Alphonce Joseph 'Mchumiatumbo' ametamba kuwa, haoni bondia wa kupigana nae nchini kutokana na karibu mabondia wote wa uzito wake kuwachapa na wengine kuingia mitini kukacha kupigana nae.
Aidha, amewaomba mapromota na wafadhili wa ngumi nchini kumsaidia kumtafutia mapambano ya kimataifa na mabondia wa nje ili awe kutimiza ndoto za kutwaa na kulitangaza jina lake katika anga hizo.
Akizungumza na MICHARAZO
kwenye mahojiano maalum, Mchumiatumbo alisema kutokana na kuwapiga karibu mabondia wote wa uzani wake na wengine kumkacha ulingoni anahisi hana bondia wa kupigana nchini hivyo kuwataka mabondia wa nje.
Bondia huyo aliyepigana mapambano sita na kushinda matano, manne kati ya haayo kwa KO na kupata sare moja dhidi ya Ashraf Suleiman, alisema bondia aliyekuwa akidhani angeweza kumpa upinzani Amur Zungu alishaawahi kumkacha ulingoni.
"Kwa kweli kama kila bondia ninayepigana nae naamshinda na wengine kunikacha ulingoni, sidhani kama kuna wa kupigana nami kwa sasa, hivyo nilikuwa naomba nitafutiwe michezo ya kimataifa kujitangaza zaidi na kuwania mikanda," alisema.
Bingwa huyo wa zamani wa Mkoa wa Dar es Salaam wa ngumi za ridhaa, alisema mabondia wengi wa Tanzania wanaishia kutamba nchini tu kwa vile mapromota na waandaaji wa michezo ya ngumi hawawatafutii michezo ya kimataifa kama nchi nyingine.
Mara ya mwisho Mchumiatumbo kupata ushindi ni wiki mbili zilizopita alipomtwanga kwa KO Bahati Mwafyale katika pambano lililofanyika kwenye ukumbi wa DDC Keko.
Madega awaonya Yanga kuhusu uchaguzi
WANACHAMA wa klabu ya soka ya Yanga wameonywa na kutakiwa kuwa makini katika uchaguzi wao mdogo utakaofanyika Julai 15, kwa kuhakikisha wanachagua viongozi wenye uchungu na nia ya dhati ya kuipeleka mbele klabu hiyo.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Imani Madega ambapo alisema uchaguzi huo unapaswa kutumiwa vema na wanachama wa Yanga kuhakikisha wanachagua viongozi wenye sifa na wataoikwamua klabu yao.
Madega, alisema pupa yoyote watakayofanya wanachama hao kwa kuchagua viongozi wasiokuwa makini maana yake ni kuiweka pabaya Yanga na huenda watu wakaanza kunyoosheana vidole kama ilivyotokea katika uongozi uliopita.
Mwenyekiti huyo wa zamani aliyeondoka madarakani kwa heshima kubwa ikiwemo kuiachia klabu hiyo akaunti iliyokuwa na fedha za kutosha, alisema ingawa katika kipindi kama hiki wanachama hunufaika, lakini waikumbuke klabu yao.
"Ni vema wanayanga wakawa makini katika uchaguzi huu kwa kuhakikisha wanachangua watu wa mpira, wenye upeo na uwezo wa kuiongoza Yanga ili itoke mahali ilipo na kuweza kuwa klabu yenye hadhi kimtaifa," alisema.
Kauli ya Madega imekuja wakati mchakato wa uchaguzi huo wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na waliokuwa viongozi wa Yanga, ambapo wagombea 28 kati ya 33 walirudisha fomu za kuwania uongozi katika kinyang'anyiro hicho.
Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Uchaguzi wa Yanga, Francis Kaswahili waliojitokeza kuwania nafasi ya Uenyekiti ni wagombea wanne ambao ni pamoja na Sarah Ramadhan, Edger Chibura na John Jambele.
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti pia ina wagombea wanne ambao ni meneja wa zamani wa klabu hiyo, Ayoub Nyenzi, Ali Mayay, Yono Kevela na Clement Sanga huku kwenye Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ina wagombea 20.
Wagombea hao ni nyota wa zamani wa timu hiyo akiwemo aliyekuwa nahodha Shaaban Katwila, Aaron Nyanda, Edger Fongo na Ramadhan Kampira.
Wengine wanaowania nafasi nne za ujumbe huo wa kamati ya utendaji ni Lameck Nyambaya, Mohammed Mbaraka, Ramadhani Saidi, Beda Tindwa, Ahmed Gao, Mussa Katabalo, George Manyama, Omary Ndula na Jumanne Mwamwenya.
Wagombea wengine ni Abdallah 'Binkleb' Mbaraka, Peter Haule, Justine Baruti, Abdallah Sheria, Jamal Kisongo, Gaudecius Ishengoma na Yona Kevela.
Bingwa wa karate aililia serikali
BINGWA wa mchezo wa Karate kwa nchi za Afrika Mashariki ngazi ya klabu, Sensei Mikidadi Kilindo, ameiomba serikali iutupie macho mchezo huo na kuupa sapoti kama ilivyo kwa michezo mingine ili kuuhamasisha nchini.
Aidha, Kilindo amedai kuwa kutopewa kipaumbele kwa mchezo huo ndio kilichomfanya mara zote awe anaenda na kurudi na medali bila hata kutangazwa au kufahamika kwa wananchi kitu kinachomsikitisha.
Akizungumza na MICHARAZO
, Sensei Kilindo alisema licha ya mchezo huo kuwa na manufaa makubwa kwa taifa na jamii kwa ujumla umekuwa haupewi kipaumbele kama michezo mingine.
Alisema kutokana na hali hiyo ni vema serikali na wadau wa michezo kuutupia macho na kuusaidia ili utangazike na kutumiwa kuiletea sifa Tanzania baada ya michezo mingine kushindwa kufanya hivyo.
Bingwa huyo wa miaka minne mfululizo wa Afrika Mashariki tangu 2008 alisema, kutopewa kipaumbele kwa karate ndiko kunakofanya hata wachezaji wanaoenda kuitangaza nchi wasifahamike warudipo na ushindi.
"Mimi nimerudi hivi karibuni na medali ya dhahabu baada ya kuwa mshindi wa kwanza Afrika Mashariki, hii ni mara ya nne mfululizo, ila hakuna anayejua wala kiongozi aliyewahi kunipokea na kunipongeza inauma sana," alisema.
Pia Kilindo alisema ukimya unaofanywa na viongozi wa Chama cha Karate nchini, TASHOKA katika kuutangaza mchezo huo ni tatizo linalofanya usisikike licha ya mafanikio yake kwa ngazi ya klabu.
Alisema ni vema TASHOKA ikafanya utaratibu wa kuandaa michuano ya taifa angalau mara mbili kwa mwaka itakayoshirikisha klabu mbalimbali nchini kwa lengo la kuuhamasisha na kuutangaza mchezo huo.
Zuri Chuchu Anapenda Kuishi bwana!
MUIMBAJI wa zamani wa bendi za Bambino Sound na Double M Sound, Zuri Chuchu ambaye kwa sasa anaimba muziki wa Injili, yupo mbioni kuingiza sokoni albamu yake ya kwanza iitwayo 'Napenda Kuishi', huku akianza kuipika nyingine mpya.
Zuri, ambaye majina yake kamili ni Esther Charles Mugabo, alisema albamu hiyo yenye nyimbo 12 ilishakamilika mujda mrefu kiasi baadhi ya nyimbo zake kuchezwa redioni, ila aliichelewa kuingiza sokoni kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake.
Alisema hata hivyo anashukuru kwa sasa mipango yake ya kuitoa hadharani albamu hiyo inaelekea vema na wakati wowote ataingiza sokoni.
Zuri, ambaye alitangaza kuishi na VVU akiendesha kampeni mbalimbali kwa sasa kutoa elimu dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, alisema wakati albamu hiyo ya kwanza ikiandaliwa kutoka, tayari ameanza maandalizi ya albamu yake nyingine ya pili.
Alisema mpaka sasa amesharekodi nyimbo sita katika studio za Katra Production iliyompa ofa ya kufyatua albamu hiyo bure kama kuunga mkono juhudi zake za kuendesha neno la Mungu na kutoa elimu ya Ukimwi kwa jamii.
"Nashukuru kwa nafasi niliyopewa na Katra Studio kutoa albamu yangu ya pili ambapo mpaka sasa nimesharekodi nyimbo sita, wakati nikitaka kuingiza sokoni kwanza albamu yangu ya kwanza iitwayo Napenda Kuishi yenye nyimnbo 12," alisema.
Muimbaji huyo, alisema ameamua kutumia muziki kuhubiri na kutoa elimu ya Ukimwi kutokana na ukweli wanaoathirika na ugonjwa huo ni wengi, licha ya kwamba mambo hayawekwi hadharani hivyo anataka maambukizi mapya yasiendelee kuwepo kwa jamii.
Yanga, Simba 'jino kwa jino' kisa Kelvin Yondani
KLABU za soka za Simba na Yanga zimeingia katika vita mpya kufuatia beki wa kati wa kimataifa nchini, Kelvin Yondani kudaiwa kusaini kwa mpigo ndani ya klabu hizo kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Wakati Simba ikiendelea kushikilia msimamo kwamba Yondani ni mali yao baada ya kusaini mkataba mpya, Yanga wenyewe wamesisitiza kuwa beki huyo wameshamilazana nao na kuinyoa Simba iache kutupia vitisho katika suala la mchezaji huyo.
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu amesema wameshamalizana na Yondani kwa kumsainisha mkataba wa miaka miwili na kwamba kinachofanywa na watani zao kutaka kuwayumbisha mashabiki na kusisitiza watakula nao sahani moja hadi kieleweke ili kubaini nani mkweli katika hilo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Simba Ismail Rage, amesema Yanga inajidanganywa kwa Yondani na huenda ikala kwao kwa hasara waliyoingia juu ya beki huyo wa kimataifa ambaye pia anaichezea timu ya taifa, Taifa Stars.
Subscribe to:
Posts (Atom)