STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, February 24, 2013

BREAKING NEWS:RAGE KUACHIA NGAZI SIMBA

Mwenyekiti wa Simba ismail Aden Rage


HABARI zilizotufikia hivi punde kutoka ndani ya klabu ya soka ya Simba zinasema kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage anatarajiwa kujiuzulu nafasi yake kutokana na kipigo ilichopewa timu yake jioni ya leo na Mtibwa Sugar.
Taarifa hizo zimedokeza kuwa, Rage atatangaza msimamo huo wa kuachia ngazi Msimbazi kesho atakapokutana na waandishi wa habari.
MICHARAZO imekuwa ikimsaka Rage mwenyewe kusikia kauli yake, lakini simu yake imekuwa haipatikani, hivyo juhudi zinaendelea ili kuthibitisha taarifa hizo na tutawajuvya mara tukibahatika kumpata.

CHELSEA HOI KWA MAN CITY, NEWCASTLE YATAKATA



Lampard (8) akikosa penati iliyopanguliwa na kipa Joe Hart


WAKATI Newcastle United ikitakata nyumbani kwake kwa kuigagadua Southampton kwa mabao 4-2, vijana wa Rafa Benitez wamejikuta wakiangukia pua ugenini kwa kunyukwa na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City mabao 2-0 katika pambano kali lililochezwa jioni hii.
Chelsea walionyesha kuhimili vishindo vya wenyeji wao na kulazimisha kwenda mapumziko wakiwa nguvu sawa kwa kutofunga bao lolote.
Hata katika kipindi cha pili, Chelsea walionyesha uhai kwa kuwakimbiza wapinzani wao na kufanikiwa kupata penati iliyoshindwa kufungwa na mkongwe Frank Lampard kabla ya Yaya Toure kuifungia wenyeji bao dakika ya 63.
Dakika tano kabla ya pambano hilo kumalizika shuti kali la kushtukiza la Carlos Tevez liliwanyong'onyesha Chelsea kwani liliwavunja nguvu za kuweza kusawisha bao na kuambulia sare.
Katika pambano jingine lililochezwa leo, Newcastle United wakiwa nyumbani waliishindilia wageni wao Southampton kwa mabao 4-2.
Wageni waliwashtua wenyeji wao wa kuandika bao la kuongoza dakika tatu tu ya mchezo kupitiaMorgan Schneiderlin kabla ya Mousa Sissoko kusawazisha dakika ya 33 na na nyota wa Senegal, Papiss Demba Cisse kuongeza la pili dakika ya 42 naa kufanya hadi mapumziko Newcastle kuongeza bao 2-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa wageni kusawazisha bao kupitia Rickie Lambert  kabla ya Yohan Cabaye kufunga bao la tatu la Newcastle dakika ya 67 na dakika ya 79 beki wa Southampton, Jos Hooiveld kujifunga na kuihakikishia wenyeji ushindi huo mnon0.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kwa mchezo mmoja tu, West Ham United kuikaribisha Tottenham Hotspur ambayo itakuwa inafukuzia kukalia nafasi ya tatu baada ya leo Chelsea kudorora mbele ya Manchester City.

SIMBA YAVUTWA SHARUBU, YALALA TENA NA MTIBWA

KIkosi cha Simba kilicholala leo kwa Mtibwa Sugar


Mtibwa Sugar walioendeleza ubabe kwa Simba leo uwanja wa Taifa (Picha Zote:Francis Dande)

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba jioni ya leo imeendelea kuwa mteja wa Mtibwa Sugar baada ya kufungwa bao 1-0 katika pambano kali lililochezwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mtibwa ilijipatia bao hilo la pekee katika dakika ya 19 ya mchezo kupitia kwa beki wake mahiri, Salvatory Ntebe bao lililoihakikishia timu yake kuvuna pointi zote sita kwa msimu mbele ya Simba.
Kwani katika pambano lao la duru la kwanza Simba ilikubali pia kichapo cha mabao 2-0 na kupelekea kuibuka kwa mtafaruku toka kwa wanachama wa klabu hiyo waliokuwa wakishinikiza nahodha na kipa tegemeo wa timu hiyo Juma Kaseja na baadhi ya viongozi kujiuzulu kwa madai waliifanyia hujuma.
Katika pambano hilo, beki kisiki wa Simba Juma Nyosso alijikuta akitolewa nje na mwamuzi Kidiwa dakikia za lala salama, wakati tayari jahazi la timu yake likielekea kuzama mbele ya Mtibwa ambayo katika mechi yake ya mwisho ilikumbana na kipigo cha mabo 4-1 toka kwa Azam.
Kipigo hicho kimeiacha Simba kuendelea kusalia kwenye nafasi yake ya tatu nyuma ya Azam waliolala bao 1-0 jana kwa vinara wa ligi hiyo Yanga wanaoongoza msimamo kwa sasa wakiwa na pointi 39.
Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu wanatarajiwa kuondoka nchini katikati ya wiki hii kuelekea Angola kwa ajili ya pambano lake la marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao Libolo ambao walishinda meechi ya wali kwa bao 1-0.
Kocha Msaidizi wa Simba alizungumza baada ya pambano hilo akidai wanakubali matokeo kwanu kufungwa ni sehemu ya matokeo matatu ya soka, huku akiahidi kujipanga kwa ajili ya mechi zao nyinginee za ligi mara watakaporejea toka Angola.

Sheikh auwawa Zenji, ni muendelezo wa mauaji wa viongozi wa kidini


IGP Said Mwema wakati wa mkutano na waandishi wa habari kufuatia tukio la kuuwawa kwa Padri wa Kikatoliki
SIKU chache baada ya kutokea kifo cha Padri Evarist Gabriel Mushi kupigwa risasi na watu wasiojulikana kichwani eneo la Beit el Raas, Jana Imamu wa Msikiti wa Mwakaje ameuawa baada ya kupigwa mapanga hadi kufa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ahmada Khamis amethibitisha kutokea kwa tukio hilo hapo jana mchana majira ya saa 8 na kumtaja aliyefariki kuwa ni Sheikh Ali Khamis ambaye ameuawa na watu wasiojulikana.
Kamanda Ahmada alisema Sheikh Khamis mbali ya kuwa ni Imamu wa Msikiti lakini pia ni mkulima na ameuliwa wakati akiwa katika mazingira ya kazi zake ndani ya shamba lake huko Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akielezea mazingira ya tukio hilo Kamanda Ahmada alisema tukio hilo limetokea baada ya Sheikh Khamis kwenda shambani kwake katika shmba la minazi Kidoti ambapo wakati akiwa shambani hapo ndipo walipotokea watu kadhaa na kumpiga mapanga sehemu za shingoni mwake na kusababisha kifo chake muda mfupi baada ya kipigo hicho.
Alisema baada ya tukio hilo, watu walimchukua na kumkimbiza hospitali lakini kutokana na kupoteza damu nyingi alifariki dunia wakati akiwa njiani na hivyo harakati za mazishi zinafanyika baada ya kuchukuliwa vipimo na wataalamu wa afya.
Kamanda Ahmada ametoa wito kwa wananchi kutopuuzia taarifa za watu ambao wanawashuku na wenye kuleta maafa yakiwemo mauaji hapa nchini, kwani kuwaficha wahalifu ni kuendeleza utamaduni usiofaa katika jamii ambayo imeanza kuharibika kutokana na mauaji hayo yanayoendelea kila kukicha.
Hili ni tukio la nne kwa viongozi wa dini kuhujumiwa ambapo tukio la kwanza Sheikh Fadhil Suleiman Soraga kumwagiwa tindi kali na watu wasiojulikana na kujeruhiwa vibaya wakati akifanya mazoezi nyakati za asubuhi karibu na nyumbani kwake Magomeni, tukio la pili ni lile la Padri Ambrose Mkenda aliyepigwa mapanga shingoni na kurejuhiwa vibaya na watu wasiojulikana wakati akitaka kuingia nyumbani kwake huko Tomondo Mjini Unguja. matukio hayo mawili yalitokea mwaka jana.
Katika mwaka huu nako kumetokea matukio mawili kwa kuuawa kwa Pardi Evarist Mushi huko Beit El Raas wakati akitaka kuingia Kanisani na pia kuuawa kwa Sheikh Ali Khamis huko Kidoti shambani kwake Mkoa wa Kaskanizini Unguja.  Inna lillahi wainna ilayhi rajiiun.

MECHI YA YANGA, AZAM YAINGIZA MIL 240

Mshambuliaji wa Azam Kipre Tchetche akichuana na beki wa Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' katika mechi yao iliyochezwa jana na Yanga kuibuka mshindi wa bao 1-0
Na Boniface Wambura
MECHI namba 120 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa jana (Februari 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Yanga kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam imeingiza sh. 239,686,000.

Watazamaji 39,315 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 58,794,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 36,562,271.19.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 33,315 na kuingiza sh. 165,655,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 485 na kuingiza sh. 9,700,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 29,895,725.82, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 17,937,435.49, Kamati ya Ligi sh. 17,937,435.49, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 8,968,717.75 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 6,975,669.36.