Kazi Ukushoto) akiwa na Man Bizo |
Katika pozi zake |
Kazi (kulia) akiwa na Tabitha |
KUVUTIWA kwake kisanii na mchekeshaji Amri Athuman 'King Majuto' tangu utotoni, ndiko kulikomfanya msanii Kazi Suleiman 'Kazi' kuamua kuacha kazi ya ukondakta wa daladala awe muigizaji.
Aliingia rasmi katika fani hiyo mwaka 1993 kupitia kundi la Mzimuni Arts kabla ya baadae kuibukia kundi la Africando, ambapo baada ya kuona hajapata kile anachokipata alihamia Al Riyamy Production.
Filamu ya kwanza kumtangaza katika ulimwengu wa sanaa ni 'Olopong' kabla ya kufuatiwa na nyingine zipatazo 20 kwa sasa.
Baadhi ya kazi zake nyingine za mchekeshaji huyo mwenye umbile fupi na anayechekelea kuigiza na wasanii wenye majina makubwa nchini kama Mzee Majuto, Sharo Milionea, Kitale, Senga, Pembe, Man Bizo na wengine ni 'Harusi ya Mwanangu', 'Pedeshee', 'Choo cha Kike' na vichekesho vya 'Vituko Show' vinavyorushwa kwenye runinga.
Kazi ambaye bado hajaoa ingawa anaye mtoto mmoja, anasema sanaa kwa kiasi fulani imemsaidia kwa mengi ikiwemo kufahamika na kujipatia kipato cha kila siku, licha ya kwamba bado hajaridhika.
Matarajio ya mkali huyo aliyezaliwa mwaka 1980 Kawe jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa nne kati ya sita wa familia yake ni kufika mbali kisanii na kuja kumiliki miradi yake binafsi ya kibiashara.
Msanii huyo anayependa kula ugali kwa nyama na mchicha na kunywa Pepsi, anasema sanaa Bongo inalipa ingawa bado wasanii wanashindwa kunufaika na jasho lao kutokana na kukithiri kwa uharamia.
Akaiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia wasanii, sambamba na kuiwekea mipango mizuri fani hiyo ili kuwainua wadau wake sawia na nchi kuvuna pato kubwa linaloendelea kupotea kwa sasa.
Shabiki huyo wa Yanga na Manchester United, naasema hakuna tukio la furaha kwake kama kukubalika kwa mashabiki na anahuzunishwa na vitendo vinavyofanywa na wasanii wenzake hasa suala la skendo.
Anawataka wasanii wenzake kupendana, kushikimana na kujiepusha na yote yanayowachafua wao na familia zao pamoja na fani nzima ya sanaa mbele ya jamii.
Kazi anadai ukiacha Mungu aliyemuumba na kumjalia kipaji cha uigizaji shukrani zake nyingine zinaenda kwa wazazi wake, Mzee Majuto,mkurugenzi wake wa Al Riyamy Production na wasanii wenzake.