|
Bale na Ronaldo |
WAKATI kocha hasimu wa Bayern Munich, Jurgen Klopp wa Borussia Dortmund akiwapa nafasi kubwa mabingwa watetezi hao kutinga fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya, miamba wa soka wa Hispania, Real Madrid timu yenye mafanikio zaidi katika historia ya michuani hiyo wakitwaa taji hilo mara tisa wamepania safari hii kuondokana na mzimu wa kulikosa kila mara kwa miaka 12 sasa.
Madrid imeangukia katika hatua ya nusu fainali katika michuano yote mitatu iliyopita, mara mbili ikitolewa dhidi ya timu za Ujerumani.
Borussia Dortmund waliwafunga jumla ya magoli 4-3 katika nusu fainali ya mwaka jana wakati Bayern waliwatoa kwa 'matuta' katika nusu fainali ya msimu wa 2011-12 lakini wanaingia katika mechi ya leo ya marudiano kwenye Uwanja wa Allianz Arena kwa ushindi wa 1-0, kufuatia kiwango cha juu walichoonyesha katika mechi yao ya awali mjini Madrid.
Karim Benzema alifunga goli pekee la mechi hiyo, kuipa timu ya kocha Carlo Ancelotti uongozi, lakini, licha ya hilo, watatakiwa kuwachunga Bayern ambao wamekuwa na mafanikio chini ya kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola.
Mabingwa hao wa Bundesliga wanafukuzia kutwaa makombe matano chini Guardiola baada ya kutwaa Uefa Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu, huku pia wakiwasubiri Borussia Dortmund katika fainali ya Kombe la 'FA' la Ujerumani la DFB-Pokal.
Bayern wamepoteza mechi nne tu nyumbani tangu mwanzo wa msimu huu, huku Manchester City na Arsenal zikiwa ni timu pekee za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya zilizoonja mafanikio kwenye Uwanja wa Allianz Arena katika kipindi hicho, lakini Ancelotti amesisitiza timu yake itakwenda kwenye mechi hiyo ikijiamini wakati wakidhamiria kutwaa makombe matatu katika msimu wa kwanza chini ya kocha huyo Muitalia.
"Nina imani na wachezaji na nadhani kila mmoja anapaswa kuwa hivyo pia," aliuambia mkutano na waandishi wa habari wa Hispania. "Mpango wetu mjini Munich ni kufunga, kuliko kujilinda."
Ancelotti alibainisha kuwa washambuliaji watatu wa Madrid, Benzema, Cristiano Ronaldo na Gareth Bale, wote wataanza mjini Munich.
Alvaro Arbeloa, Jese Rodriguez na Sami Khedira (wote goti) ndiyo wachezaji pekee watakaokosa Real.
Beki Rafinha amerejea kwa Bayern baada ya kutumikia adhabu ya kadi katika mechi ya ligi wikiendi lakini, wakati Thiago amerejea mazoezini, Holger Badstuber (goti), Xherdan Shaqiri (paja) na Tom Starke (kiwiko) wote bado wako nje ya uwanja.
Bayern wamekuwa wakitajwa kama timu inayopewa nafasi kubwa zaidi ya kutwaa taji hilo kwa muda wote wa michuano na Guardiola anaamini kwamba mabingwa hara tano wa Ulaya wanaweza kupindua matokeo ya mechi yao ya awali.
"Ninaiamini kwa asilimia 100 timu yangu," Mcatalunya huyo aliiambia tovuti rasmi ya klabu hiyo ya mjini Munich. "Tunaweza kama tutafanya kazi pamoja."
Mshambuliaji wa Bayern, Mario Mandzukic na nyota wa Madrid, Sergio Ramos, Xabi Alonso na Asier Illarramendi watakosa fainali kama watapigwa kadi za njano katika mechi hiyo ya leo.
Licha ya kuwa bado na nafasi ya kutwaa taji hilo, staili ya uchezaji inayofundishwa na Guardiola imezidi kupoteza umaarufu na haiwavutii wakosoaji wa Bayern.
"Kumiliki mpira hakuna maana yoyote pale mpinzani wako anapotengeneza nafasi bora zaidi yako. Tuna bahati walifunga goli moja tu," alisema rais wa heshima wa Bayern, Franz Beckenbauer katika ukosoaji wake mpya alioutoa karibuni dhidi ya staili ya kucheza ya Guadiola ya tiki-taka la Kijerumani.
Katika hatua nyingine meneja wa klabu ya Borussia Dortmund, Jurgen Klopp ameipa nafasi Bayern Munich kugeuza matokeo ya kufungwa bao 1-0 na Real Madrid katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bao la Karim Benzema lilitenganisha timu hizo mbili katika mchezo huo uliofanyika wiki iliyopita katika Uwanja wa Santiago Bernabeu baada ya Madrid kucheza mchezo wa tahadhari kubwa.
Hata hivyo, Klopp ambaye timu yake ilienguliwa na Madrid katika mzunguko wa mwisho anaamini mahasimu wao Bayern watashinda mchezo huo.
Klopp amesema bado anashawishika kuamini kuwa Bayern wanaweza kushinda hususani kwa mchezo maridadi waliouonyesha mara ya kwanza pamoja na kufungwa. Bayern na Madrid zinatarajiwa kukwaana kesho katika mchezo wa marudiano kutafuta nafasi ya kucheza fainali ya michuano hiyo itakayofanyika jijini Lisbon, Ureno.