IKIWA safarini mkoani Mbeya kwa ajili ya pambano lao lijalo dhidi ya wenyeji wao, Prisons ya Mbeya, uongozi wa timu ya Ruvu Shooting umeliomba Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kuwa makini na Kamati ya Ushindi za klabu mbalimbali zilizoundwa wakati Ligi Kuu Tanzania Bara ikielekea ukingoni.
Uongozi huo wa Ruvu umedai kuwa, kamati hizo huenda zikatumika vibaya katika upangaji na hulazimishaji wa matokeo viwanjani kutokana na ukweli kamati hizo mara nyingi huusisha viongozi wa FA mkoa na hata ofisi za wakuu wa mikoa husika wanaoweza kutumia vibaya nafasi zao kuzibeba timu zao hasa zikiwa kwao.
Akizungumza na MICHARAZO hivi punde, Msemaji wa klabu hiyo, Masau Bwire alisema kamati ya kusaka ushindi kwa timu za ligi kuu, siyo tatizo ila hofu yao namna zinavyoundwa wakati huu ligi ikielekea ukingoni na baadhi yao ni zile timu ambazo zipo katika hali mbaya kwenye ligi hiyo.
Bwire alisema, ingekuw vyema wakafuatilia kwa ukaribu mechi za mwisho za ligi hiyo ili kuepusha hujuma kwa timu nyingine, ili ligi imalizike salama kama ilivyoanza.
"Hatupingi kuundwa kwa hizi kamati kwa baadhi ya timu, lakini zinatutia hofu kwa namna zinavyoundwa kila mara timu zikiwa katika nafasi mbaya na hasa ligi ikielekea ukingoni, mbaya zaidio hujumuisha watu wenye nyadhifa ambazo wanaweza kutumika kuwatisha au kuwalazimisha waamuzi kutengeneza matokeo ya kuzibeba timu hizo," alisema Bwire.
Alisema kwa vile vyama vya mikoa (FA) ni wanachama wa TFF na majukumu yao ni kuhakikisha utekelezwaji wa sheria 17 za soka zinatumika uwanjani, hadhani ni sahihi nao kuingizwa kwenye kamati hizo kwani wanaweza kulaumiwa inapotokea dosari kwenye mechi ndani ya mikoa yao.
Aliongeza kuwa ni vyema kamati hizo zingekuwa zikiundwa mapema na kufanya kazi kuzisaidia timu zao kuliko sasa ambako imekuwa kama fasheni na kuleta hisia mbaya hasa wakati huu watanzania wakiwa na hisia kali juu ya vitendoi vya rushwa michezoni.
Juu ya pambano lao lijalo Bwire alisema kikosi chao kipo safarini lakini wakiwa na morali wa kupata ushindi mjini Mbeya, cha muhimu akiiomba TFF kuhakikisha wanausimamia kwa ukamilifu mchzeo huo ili kusiwepo na matukio kama waliyokutana nao jana kwenye pambano lao na Polisi Moro lililoisha kwa suluhu ya 0-0.