STRIKA
USILIKOSE
Monday, June 4, 2012
Kitale: 'Teja' la kwenye runinga lisiloujua 'unga'
KWA jinsi anavyoigiza na muonekano wake kama 'teja' katika baadhi ya kazi zake za filamu za kawaida na vichekesho, ni vigumu kuamini kuwa msanii Mussa Yusuph 'Kitale Rais wa Mateja' sio mtumiaji wa dawa za kulevya.
Mwenyewe anadai hatumii kilevi cha aina yoyote zaidi ya kuigiza tu kama muathirika wa dawa hizo haramu za kulevya.
Msanii huyo aliyewahi kutamba na makundi ya Kaole Sanaa na Fukuro Arts Professional, alisema watu wachache wanaoamini kama kweli hatumii kilevi.
"Situmii kilevi chochote, sio pombe wala bangi, naigiza tu we mwenyewe unaniona bonge la HB au vipi?" Kitale alisema kwa utani alipohojiawa.
Kitale alidokeza chanzo cha yeye kupenda kuigiza kama 'teja' aliyeathiriwa na 'unga' kiasi cha kuwa kibaka ni uzoefu alioupata kwa kuishi karibu na 'mateja'.
Kitale, alisema jirani na kwao na sehemu kubwa ya Mwananyamala wapo vijana walioathiriwa na dawa hizo za kulevya, hivyo alikuwa akiwachunguza jinsi wanavyoongea, kutembea na maisha yao kwa ujumla na kujifunza mengi.
"We unajua Mwananyamala na maeneo mengi ya uswazi kuna mateja wengi na bahati nzuri karibu na home kuna maskani yao ndio walionisaidia kunifanya niigize kama teja la kutupwa," alisema.
Alisema mbali na uigizaji huo kuwa kama 'nembo' yake, lengo lake ni kuishtua jamii jinsi ya kuthibiti tatizo la dawa za kulevya, linaloteketeza kizazi na nguvu kazi ya taifa.
"Naigiza hivyo, ili kuizindua jamii na kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, dawa hizi zimekuwa zikiharibu na kupoteza nguvu kazi kwa jinsi zinavyoathiri na kuwa na madhara makubwa kwa taifa letu," alisema.
Alisema japo wanaibuka wasanii wanaoigiza kama yeye (Kitale), msanii huyo alidai hana hofu kwa kutambua ataendelea kubaki kuwa Kitale na kamwe hajishughulishi na wasanii hao wanaoiga 'nembo' yake.
"Kwa kweli wapo baadhi ya wasanii wameanza kuiga uigizaji wangu, ila sina hofu na wala muda wa kuwajadili, mie naendelea kupiga kazi kwani naamini nitaendelea kubaki kuwa Kitale aliye mmoja tu yaani Rais wa Mateja," alisema.
Kitale, aliyeanzia sanaa tangu akiwa kinda wakati akisoma Shule ya Msingi, alisema licha ya umaarufu mkubwa alioupata kwa namna ya uigizaji huo wa kama 'teja' hasa alipong'ara katika tamthilia ya 'Jumba la Dhahabu', alidai wakati mwingine hupata usumbufu.
"Ukiacha watu kunishangaa, wapo wengine hudhani uigizaji wangu ni uhalisia wa maisha yangu hivyo huniogopa wakidhani ni teja na kibaka, ingawa huwa naamini ujumbe nilioukusidia umefika kwa jamii," alisema.
VIPAJI KIBAO
Kitale, mchumba wa Fatuma Salum na baba wa mtoto mwenye umri wa miaka karibu miwili aitwae Ahmed, licha ya kuigiza pia ni mahiri kwa utunzi na utayarishaji wa filamu sambamba na akiimba muziki wa kizazi kipya.
Kwa sasa mkali huyo anatamba na wimbo uitwao 'Hili Dude Noma' alioimba na kaka yake Mide Zo na Corner, kikiwa ni kibao cha pili kwake baada ya 'Chuma cha Reli' alichokitoa mwaka jana akiimba na mchekeshaji wenzake, Gondo Msambaa.
Msanii huyo alisema kwa sasa anaendelea kumalizia kazi yake ya mwisho kabla ya kuhitimisha albamu itakayokuwa na nyimbo nane akizitaja zilizokamilisha kuwa ni 'Anajifanya Msela' alioimba na Juma Nature, 'Hili Toto' ft. Sharo Milionea na Mide Zo, 'Tulianzishe' na 'Kinaunau'.
"Nimebakisha wimbo mmoja tu ambao nimeshautunga na kuufanyia mazoezi ila nasubiri kuafikiana na mmoja wa wasanii nyota nchini ili niurekodi," alisema.
Hata hivyo Kitale alikiri kuwa, licha ya umaarufu mkubwa aliopata katika uigizaji, bado haridhiki na masilhai anayopata katika fani hiyo akidai hailipi kama ilivyo kwa muziki.
Alisema, uigizaji haulipi kama muziki, lakini bado hana mpango wa kuachana na fani hiyo.
"Kwenye uigizaji tunaambulia sifa tu, ila masilahi ni madogo mno tofauti na muziki, hata hivyo siwezi kuachana na fani hii kwani nimeshaizoea, na kwa sasa najiandaa kutoa kazi mpya nikishirikiana na Sharo Milionea," alisema.
Alizitaja kazi hizo mpya ni; 'Sharo Madimpoz', 'Sharo Crazy', 'Sharo Taxi Driver' na 'Drug Dealer' wanazoziandaa na msanii mwenzake.
Kitale alisema hizo ni baadhi ya filamu walizopanga kuzitoa ndani ya mwaka huu, sambamba na kuendelea na masuala ya muziki akidai kila mmoja imekuwa ikimpa mafanikio makubwa.
FILAMU
Kitale aliyezaliwa miaka kadhaa iliyopita mjini Morogoro ni shabiki mkubwa wa soka, mchezo aliowahi kucheza utotoni kabla ya kutumbukia kwenye uigizaji, akizitaka timu anazoshabikia kuwa ni Yanga na Manchester City.
"Aisee katika soka huniambii kitu, licha ya kulicheza pia ni mnazi mkubwa wa Yanga na naipenda mno Manchester City," alisema.
Kitale anayependa kula ugali kwa dagaa na kunywa vinywaji laini, alisema mbali na kucheza 'Jumba la Dhahabu' iliyompa umaarufu mkubwa, ameigiza pia filamu kama 30 na kushiriki kipindi cha vichekesho cha 'Vituko Show'.
Alizitaja baadhi ya kazi hizo kuwa ni 'Back from Prisons', 'Mtoto wa Mama', 'Alosto', Mbwembwe', 'More than Lion' aliomshirikisha msanii wa muziki wa kizazi kipya wa kundi la Tip Top Connection, Abdulaziz Chende 'Dogo Janja'.
Kitale, anayemzimia King Majuto aliyeigiza naye baadhi ya kazi, alisema fani ya sanaa nchini imepiga hatua kubwa, isipokuwa inakwamishwa na wajanja wachache wanaowanyonya wasanii na kuwafanya wasinufaike na fani hiyo.
Alisema ni vema juhudi za kupambana na maharamia ikaongezwa, ili wasanii wa Bongo wanufaike na jasho lao na kuishi kama wasanii wa mataifa mengine ambao ni matajiri kuliko hata watu wa kada zingine.
Kitale, anayefurahishwa na tukio la kuzaliwa kwa mwanae, akihuzunishwa na kifo cha mjomba wake aliyekufa kwa ajali ya gari, alisema matarajio yake ni kumuomba Mungu ampe umri mrefu na afya njema afike mbali kisanii.
Alisema angependa kujikita zaidi katika muziki na kutoa kazi zake binafsi za filamu ili kunufaika na jasho lake baada ya kutumikia watu wengine bila kunufaika zaidi ya kuambulia sifa tu.
Drogba aimwagia sifa Taifa Stars, achekelea kuwatungua
NAHODHA wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba, ameisifu timu ya Tanzania kwamba iliwapa wakati mgumu sana katika mechi yao ya raundi ya awali ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2014 kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny mjini Abidjan Jumamosi.
"Ilikuwa ni mechi ngumu sana, lakini jambo la muhimu ni kwamba tumepata pointi tatu," alisema Drogba baada ya mechi hiyo ambayo wenyeji walishinda 2-0.
"Kocha alikuwa na siku tatu za kuwa pamoja nasi, lakini tumeshinda mechi hivyo ni kazi nzuri kwake. Sasa tuna muda wa kufanya kazi pamoja naye na kujaribu kuboresha tulichofanya. Tutajiandaa na mechi ijayo dhidi ya Morocco kisha tuone nini kitatokea."
Ivory Coast ilimfukuza kocha wake, Francois Zahoui na kumpa nafasi hiyo nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Sabri Lamouchi, siku tatu kabla ya mechi dhidi ya Stars.
Ushindi unaifanya Ivory Coast kuongoza Kundi C la kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za Brazil 2014 ikiwa na pointi tatu baada ya Gambia na Morocco kutoka sare ya 1-1 katika mechi nyingine ya kundi hilo na kuzifanya kuwa na pointi moja kila moja baada ya mechi hiyo moja. Tanzania imeanza kwa kushika mkia ikiwa haina pointi.
Baada ya kuanza vibaya, Stars imedhamiria kumalizia hasira zao kwa ushindi katika mechi yao ya pili dhidi ya Gambia Jumapili 10 jijini Dar es Salaam.
Stars haijaonekana kurudishwa nyuma na kipigo kutoka kwa miamba hao wa Afrika na badala yake kikosi kilianza mazoezi jana asubuhi kwenye uwanja wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ivory Coast (FIF) ambao uko pembezoni mwa jiji la Abidjan.
Timu hiyo ilitarajia pia kutafanya tena mazoezi leo asubuhi asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani saa 1:30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo itawasili Dar es Salaam kesho saa 1:40 asubuhi.
Kocha Kim ambaye amekuja na wachezaji wote hapa ukiondoa wanne ambao ni majeruhi (Thomas Ulimwengu, Nurdin Bakari, Haruna Moshi na Nassoro Masoud Cholo) amesema hivi sasa wameelekeza akili yao kwenye mechi ijayo dhidi ya Gambia.
“Safari ya kujenga timu ndiyo imeanza. Mechi dhidi ya Ivory Coast imepita na ninawashukuru wachezaji kwa kucheza kwa mujibu wa maelekezo na kujituma. Mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa yaliyosababisha tuwape Ivory Coast mabao mepesi," alisema kocha wa Stars, Kim Poulsen.
“Lakini kama nilivyosema mechi hiyo imepita, hivi sasa tunaangalia mechi ijayo dhidi ya Gambia. Hatuna muda mwingine wa kujipanga na ndio maana niliamua kuja na wachezaji wote Abidjan,” amesema Kim.
Mechi dhidi ya Gambia itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Gambia ilitoka sare ya bao 1-1 na Morocco katika mechi iliyochezwa juzi jijini Banjul.
Stars itamkosa nahodha msaidizi Aggrey Morris ambaye alitolewa kwa kadi ya pili ya njano dakika ya 65 baada ya baada ya kumkwatua mchezaji wa Ivory Coast, Gosso Gosso. Morris alipewa njano ya kwanza katika dakika ya 12 baada ya kumkwatua Didier Drogba.
Vikosi katika mechi hiyo vilikuwa; Ivory Coast: Boubacary Barry, Kolo Toure, Siaka Tiene, I. Lolo, Emmanuel Eboue, Cheik Tiote/Ya Konan, K. Coulibaly, Jean Gosso Gosso, Didier Drogba, Salomon Kalou/Max Gardel na Gervinho/Kader Keita.
Tanzania; Juma Kaseja, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Mrisho Ngassa, Shaban Nditi, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar/ John Bocco, Mbwana Samatta na Frank Domayo.
CHANZO:NIPASHE
Wazee wa Ngwasuma kutumbuiza Miss Kigamboni
BENDI ya muziki wa dansi ya FM Academia maarufu kama 'Wazee wa Ngwasuma' na msanii wa vichekesho, Mpoki, wataburudisha wakati wa shindano la kumsaka mrembo kitongoji cha Kigamboni City 2012 litakalofanyika Juni 15 katika ukumbi wa Navy Beach, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa shindano hilo, Somoe Ng'itu alisema kutakuwa na ushindani mkubwa katika shindano hilo kutokana na vimwana wakali waliopo kambini na bendi ya FM inafahamika kwa kutoa burudani nzuri kwa mashabiki wa muziki wa dansi nchini.
Somoe alisema kuwa burudani nyingine kali itatoka kwa Mpoki ambaye mbali ya kuwa ni mkazi wa Kigamboni, lakini ukubwa wa kazi yake unafahamika na kwamba mashabiki watapaswa kuandaa mbavu za ziada kutokana na vichekesho vyake.
Mratibu huyo kutoka kampuni ya K& L, alisema kuwa jumla ya warembo 15 wanaendelea kujifua katika kambi ya mazoezi chini ya mwalimu wao Miss Temeke, Hawa Ismail, ambaye anashirikiana na mshiriki wa Miss Tanzania mwaka jana Blessing Ngowi.
Aliwataja warembo hao kuwa ni pamoja na Carolyne Dandu, Fatina Francis, Edda Slyvester, Aisha Mussa, Rosemary Peter, Doreen Kweka, Caroline Peter, Agnes Goodluck, Sophia Martine, Rosemary Deogratius, Beatrice Boniface, Julieth Philip na Khadija Kombo.
"Kigamboni ni zaidi ya kitongoji, tunaamini shindano letu litakuwa na mvuto na hadhi ya kipekee kama eneo lake lilivyo," aliongeza.
Somoe alisema kuwa warembo watakaofanya vizuri watapata nafasi ya kuwakilisha kitongoji hicho katika mashindano ya kanda ambayo yatafanyika baadaye mwaka huu.
Aliwataja wadhamini ambao tayari wamethibitisha kuwezesha shindano hilo kuwa ni pamoja na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd's, Dodoma Wine na NSSF, Hope Country Motel, Norbro’s Collections, Screen Masters, Global Publishers.
Salha Israel kutoka Kanda ya Ilala ndiye mrembo anayeshikilia taji la taifa ambapo mwaka huu ratiba ya mashindano hayo imebadilika.
CHANZO:NIPASHE
Warembo watakaochuana kwenye shindano la Miss Kigamboni 2012
Masai Nyota Mbofu aachia Rungu na Mukuki
MCHEKESHAJI maarufu nchini, Gilliad Severine 'Masai Nyota Mbofu', ameachia wimbo mpya uitwao 'Rungu na Mukuki' sambamba na video yake akishirikiana na wasanii wa kundi la Vichwa la Zambia, Simple K na G4.
Tayari wimbo na video hiyo imeshaanza kurushwa hewani wakati mwenyewe akijiandaa kupakua kazi nyingine mpya.
Akizungumza na MICHARAZO, Masai Nyota Mbofu, alisema wimbo huo ameurekodia nchini Zambia katika studio za Hez Sound chini ya Prodyuza, Acknex na video yake amefyatulia nchini humo na kuja kuimalizia Tanzania.
Msanii huyo, alisema kazi hiyo mpya ni salamu kwa mashabiki wake waliomzoea kumuona katika filamu na komedi tu, kwamba kwenye muziki naye yumo.
Masai Nyota Mbofu, alisema wakati wimbo na video hiyo ikiendelea kutamba ameanza kuandaa wimbo mipango ya kutoa kazi nyingine kwa lengo la kuja kufyatua albamu hapo baadae.
"Wakati Rungu na Mukuki, ikiendelea kukimbiza kwa fideo na radio, tayari nimenza kuandaa kazi nyingine nataka onyesha mashabiki angu kwamba mi nawesa," alisema Masai kwa kiswahili kibovu cha kikomedi.
Mkali huyo aliyeanza kutamba kwenye michezo ya runinga akiwa na kikundi cha Jakaya Theatre kabla ya kuibukia kwenye filamu chini ya kampuni ya Al Riyamy Production.
Baadhi ya kazi zilizowahi kumpa ujiko msanii huyo ni Iny'e Plus, 'Iny'e Gwedegwede', 'Vumba Vimejaa', 'Pedeshee' na sasa anatamba na kipindi cha Vituko Show.
Mosha awachomolea wazee Yanga, fomu zachangamkiwa
HUKU zoezi la uchukuaji fomu za kuwania uongozi kwa ajili ya Uchaguzi wa klabu ya Yanga ukizidi kupambamoto, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Davis Mosha amewachomolea wazee wa Yanga waliomtaka awanie tena uongozi akidai hana mpango huo.
Aidha, kamati ya uchaguzi imekanusha taarifa kwamba Mfadhili Mkuu wa klabu huyo, Yusuf Manji amejityosa kuchukua fomu za kuwania Uenyekiti, ingawa kamati hiyo imesema milango i wazi kwake kama ana dhamira hiyo ya kuwania uongozi Yanga katika uchaguzi utakaofanyika Julai 15.
Mosha, aliyefuatwa na wazee hadi nyumbani kwake Mikocheni juzi jijini Dar es Salaam, akijibu maombi ya baraza wazee lililomuomba kugombea moja ya nafasi katika uchaguzi huo na kusema hana mpango wa kuwania uongozi.
Alisema kwa sasa hayuko tayari kugombea uongozi katika klabu lakini yupo tayari kusaidia kitu chochote kinachohitajika kwa maendeleo ya klabu.
“NAwashukuru wazee kwa kuja kuniaona na kunipa pole, pia nashukuru kwa kuona umuhimu wa mimi kuwepo Yanga, ila napenda niwaeleze sintoweza kuwania uongozi kwa sasa, bali nipo tayari kuisaidia Yanga kwa lolote litakalokuwa ndani ya uwezo wangu,”alisema.
“Mimi ni mpiganaji kweli, naiopenda Yanga na napenda iwe na maendeleo…nitashirikiana na viongozi watakaochaguliwa lakini mimi siwezi kuongoza Yanga kwa sasa nina mambo mengi ya kufganya,”alisema
Mosha ambaye alijitoa madarakani miezi michache kabla iongeza kuwa wanachama wa Yanga hawana budi kuchagua viongozi ambao wapo tayari kuisaidia klabu hiyo na si kupata chochote.
“Napenda kuwahadharisha wanachama wenzangu nkwamba tusikurupuke, tutafute watu wenye mapenzi ya kweli na si maslahi kwani Yanga ni kwa ajili ya kutumika si kuvuna,”alisema.
Awali Katibu wa baraza hilo Ibrahim Akilimali ‘Abramovich’ kwa niaba ya wazee wengine wa Yanga ambao walikwenda nyumbani kwa Mosha kwa ajili ya kumpa pole kutokana na kufiwa na Mkwewe, aliwasilisha ombi la kumtaka Mosha kurejea kundini.
Mzee Akilimali alisema kuwa wameamua kumuomba Mosha arejee kuongoza Yanga kutokana na umahiri mkubwa aliouonesha kipindi alichoongoza ambapo alikuwa mstari wa mbele kuisaidia timu hiyo na hatimaye kwa kipindi kifupi iliweza kupata mafanikio.
“Mwanetu sisi wazee wako tumekuja kukupa pole lakini pamoja na hilo tunakuomba urejee kuongoza kwani bado tunakumbuka ushupavu wako katika kuongoza…kuna kombe la Kagame linakuja ambalo wewe ulichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana, sasa uje ulibakize tena kombe hilo,”alisema Mzee Akilimali.
Aidha , Mzee Akilimali aliongeza kuwa wanataka Yanga iingie kwenye mashindano na kushiriki hivyo mchango wa Mosha katika hilo ni muhimu sana.
Uuchaguzi huo utajaza nafasi za viongozi waliojiuzulu na ile ya mjumbe mmoja aliyefariki dunia, ambapo viongozi watakaochaguliwa watakaa madarakani kwa muda uliosalia kama katiba inavyoelekeza na kwa mantiki hiyo viongozi hao watamaliza muda wao wa miaka minne mwaka 2014.
Uchaguzi huo unafuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti Lloyd Nchunga baada ya kushinikizwa na baadhi ya wanachama wakiongozwa na baraza la wazee wa klabu hiyo kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio klabu hiyo chini ya uongozi wake.
Pia nafasi ya Makamu mwenyekiti iliyokuwa inashikiliwa na Davis Mosha ambaye alijitoa miezi michache baada ya kuchaguliwa kutokana na kutoelewana na Nchunga, huku mjumbe Theonest Rutashoborwa akitangulia mbele ya haki.
Uchaguzi huo pia utajaza nafasi za Wajumbe walioachia ngazi ambao ni pamoja na Mzee Yusuf, Charles Mgondo na Ally Mayay.
Kwa sasa Yanga imebaki na wajumbe wanne, Mohammed Bhinda, Sarah Ramadhan, Tito Osoro na Salum Rupia ambao baada ya uchaguzi wataungana na viongozi wapya na kuteua wajumbe wengine watatu kwa mujibu wa katiba, hiyo inatokana na wajumbe hao wa kuteuliwa Seif Ahmed, Mbaraka Igangula na Pascal Kihanga kujiuzulu.
Katika hatua nyingine, wagombea watatu walijitokeza kuchukua fomu za kuwanmia nafasi ya ujumbe katika, wanachama hao ni pamoja na Jumanne Mwamamwenye na Salehe Hassan na Ayoub Nyenzi anayewania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.
Huku kamati ya uchaguzi ikikanusha taarifa kwamba Manji naye amejitosa kuchukua fomu kuwania Uenyekiti wa klabu hiyo, ingawa umesema milango i wazi kwake na kwa yeyote mwenye sifa kabla ya zoezi la kuchukua na kurudisha fomu kufungwa rasmi Jumatano jioni.
Simba noma, yabebe mzigo wa matibabu ya akina Boban
UONGOZI wa klabu ya Simba umesema kuwa umechukua jukumu la kuwatibu wachezaji wake Haruna Moshi 'Boban' na Nasoro Masoud 'Cholo' walioumia wakiwa na kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' baada ya kukatishwa tamaa na kusuasua kwa shirikisho la soka (TFF) kubeba gharama hizo.
Akizungumza jijini Dar, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema kuwa klabu yake haina muda wa kusubiri matibabu ya TFF kwa wachezaji hao kwasababu ya kuzongwa na kalenda ya mashindano.
Simba imeanza maandalizi kwa ajili ya mashindano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati hivyo haiwezi kusubiri mpaka TFF liwatibie 'Boban' na 'Cholo'.
Kauli hiyo ya Mtawala imekuja siku moja baada ya katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah, kusema bila kutaja tareeh rasmi kuwa shirikisho litafanya jitihada za kuwatibu wachezaji hao walioumia wakiwa ndani ya kikosi cha Stars.
"Sisi ndio tunawalipa mshahara wachezaji hawa, na mtu akigundulika ameumia anatakiwa kutibiwa haraka na hakuna kusubiri," alisema.
"Tumeanza kuwatibu ili kocha wetu atakaporudi awakute wachezaji katika hali nzuri na kuendelea na programu zake za mazoezi."
Kocha wa timu hiyo Mserbia Milovan Cirkovic atarejea nchini Juni 15, alisema.
Kocha huyo ametuma programu ya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Kagame ambayo kwa sasa yanasimamiwa na kocha wa makipa wa timu hiyo James Kisaka.
"Timu imeanza maandalizi chini ya Kisaka (James) kwa sababu kocha msaidizi naye ameenda mapumzikoni nchini kwao," alisema zaidi Mtawala.
Alisema kocha msaidizi Richard Amatre ataungana na timu Alhamisi baada ya kuwasili nchini Jumatano.
Mtawala alisema klabu hiyo imeweka malengo ya kutwaa ubingwa wa Kagame ambao unashikiliwa na watani zao Yanga walioutwaa kwenye mashindano ya mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Simba goli 1-0.
Noela ndiye Miss Tabata 2012
MREMBO Noela Michael, 19, usiku wa kuamkia juzi alifanikiwa kutwaa taji la Tabata 'Miss Tabata 2012' katika shindano lililofanyika kwenye ukumbi wa Da’ West Park jijini Dar es Salaam.
Noela ambaye awali alibwagwa katika kuwania taji la talent aliweza kuwafunika warembo wengine 18 waliokuwa wanawania taji hilo lililokuwa linashikiwa na Faiza Ally.
Noela alizawadiwa shilingi 500,000 na king’amuzi iliyolipiwa miezi sita iliyotolewa na Multichoice.
Nafasi ya pili katika shindano hilo ilishikwa na Diana Simon, 20, aliyeshinda Sh 500,000 watatu ni Wilhemina Mvungi, 21, (Sh 350,000), wanne ni Phillos Lemi, 19, na Suzzane Deodatus, 20, alishika nafasi ya tano. Wote wawili walizawadiwa Sh 200,000 kila moja.
Warembo hao watano watakiwakilisha Tabata katika mashindano ya Kanda ya Ilala yatakayofanyika baadaye mwaka huu.
Warembo wengine waliofanikiwa kuingia hatua ya 10 walikuwa ni Angel Kisanga, Khadija Nurdin, Haika Joseph, Queen Issa na Neema Saleh. Wote walizawadiwa Sh 100,000 kila moja.
Queen Issa alifanikiwa kutwaa taji la mrembo mwenye kipaji cha kucheza huku Mercy Mlay akiteuliwa kuwa mrembo aliyekuwa na nidhamu ya juu tangu kuanza kwa shindano hilo. Queen na Mercy kila moja alizawadiwa Sh 100,000.
Warembo waliosalia walipata kifuta jasho cha Sh 50,000 kila moja.
Shindano hilo lilipambwa na burudani kutoka kwa bendi ya Mashujaa, Mashauzi Classic iliyoko chini ya Isha Ramadhani Mfalme na Costa Sibuka.
PICHA Tofauti za matukio ya Miss Tabata 2012, ambapo Noela Michael aliibuka kidedea.
Subscribe to:
Posts (Atom)