STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 4, 2012

Drogba aimwagia sifa Taifa Stars, achekelea kuwatungua

NAHODHA wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba, ameisifu timu ya Tanzania kwamba iliwapa wakati mgumu sana katika mechi yao ya raundi ya awali ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2014 kwenye Uwanja wa Felix Houphouet Boigny mjini Abidjan Jumamosi. "Ilikuwa ni mechi ngumu sana, lakini jambo la muhimu ni kwamba tumepata pointi tatu," alisema Drogba baada ya mechi hiyo ambayo wenyeji walishinda 2-0. "Kocha alikuwa na siku tatu za kuwa pamoja nasi, lakini tumeshinda mechi hivyo ni kazi nzuri kwake. Sasa tuna muda wa kufanya kazi pamoja naye na kujaribu kuboresha tulichofanya. Tutajiandaa na mechi ijayo dhidi ya Morocco kisha tuone nini kitatokea." Ivory Coast ilimfukuza kocha wake, Francois Zahoui na kumpa nafasi hiyo nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Sabri Lamouchi, siku tatu kabla ya mechi dhidi ya Stars. Ushindi unaifanya Ivory Coast kuongoza Kundi C la kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za Brazil 2014 ikiwa na pointi tatu baada ya Gambia na Morocco kutoka sare ya 1-1 katika mechi nyingine ya kundi hilo na kuzifanya kuwa na pointi moja kila moja baada ya mechi hiyo moja. Tanzania imeanza kwa kushika mkia ikiwa haina pointi. Baada ya kuanza vibaya, Stars imedhamiria kumalizia hasira zao kwa ushindi katika mechi yao ya pili dhidi ya Gambia Jumapili 10 jijini Dar es Salaam. Stars haijaonekana kurudishwa nyuma na kipigo kutoka kwa miamba hao wa Afrika na badala yake kikosi kilianza mazoezi jana asubuhi kwenye uwanja wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ivory Coast (FIF) ambao uko pembezoni mwa jiji la Abidjan. Timu hiyo ilitarajia pia kutafanya tena mazoezi leo asubuhi asubuhi kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani saa 1:30 usiku kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo itawasili Dar es Salaam kesho saa 1:40 asubuhi. Kocha Kim ambaye amekuja na wachezaji wote hapa ukiondoa wanne ambao ni majeruhi (Thomas Ulimwengu, Nurdin Bakari, Haruna Moshi na Nassoro Masoud Cholo) amesema hivi sasa wameelekeza akili yao kwenye mechi ijayo dhidi ya Gambia. “Safari ya kujenga timu ndiyo imeanza. Mechi dhidi ya Ivory Coast imepita na ninawashukuru wachezaji kwa kucheza kwa mujibu wa maelekezo na kujituma. Mpira ni mchezo wa makosa, tumefanya makosa yaliyosababisha tuwape Ivory Coast mabao mepesi," alisema kocha wa Stars, Kim Poulsen. “Lakini kama nilivyosema mechi hiyo imepita, hivi sasa tunaangalia mechi ijayo dhidi ya Gambia. Hatuna muda mwingine wa kujipanga na ndio maana niliamua kuja na wachezaji wote Abidjan,” amesema Kim. Mechi dhidi ya Gambia itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Gambia ilitoka sare ya bao 1-1 na Morocco katika mechi iliyochezwa juzi jijini Banjul. Stars itamkosa nahodha msaidizi Aggrey Morris ambaye alitolewa kwa kadi ya pili ya njano dakika ya 65 baada ya baada ya kumkwatua mchezaji wa Ivory Coast, Gosso Gosso. Morris alipewa njano ya kwanza katika dakika ya 12 baada ya kumkwatua Didier Drogba. Vikosi katika mechi hiyo vilikuwa; Ivory Coast: Boubacary Barry, Kolo Toure, Siaka Tiene, I. Lolo, Emmanuel Eboue, Cheik Tiote/Ya Konan, K. Coulibaly, Jean Gosso Gosso, Didier Drogba, Salomon Kalou/Max Gardel na Gervinho/Kader Keita. Tanzania; Juma Kaseja, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Mrisho Ngassa, Shaban Nditi, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar/ John Bocco, Mbwana Samatta na Frank Domayo. CHANZO:NIPASHE

No comments:

Post a Comment