|
Michael Wambura |
|
Mwenyekiti wa Simba, Evance Aveva |
ALIYEKUWA mgombea wa nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Soka ya Simba uliofanyika mwezi Juni mwaka huu, Michael Wambura, pamoja na wanachama wengine 70 jana walifutwa rasmi uanachama wa klabu hiyo kutokana na hatua ya kufungua kesi kwenye mahakama za kawaida jambo ambalo ni kinyume na katiba.
Maamuzi ya kumfuta uanachama Wambura pamoja na wanachama wengine yalifikiwa kwa pamoja jana katika Mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Wanachama 860 waliokutana jana hawakutaka agenda hiyo ya 12 ijadiliwe na badala yake wakisema kwa sauti kwamba wanachama hao wafutwe mara moja.
Agenda hiyo ya kuwajadili wanachama hao ambao awali walisimamishwa na Kamati ya Utendaji ilianza kujadiliwa saa 6:33 mchana na ilipofika saa 6:49 mchana Aveva alitangaza kwamba wanachama hao 71 wamefutwa uanachama wao kutokana na kwenda kinyume na ibara ya 55 ya Katiba ya Simba.
Kabla ya kutoa maamuzi hayo, Aveva alisema alipokea maoni mbalimbali kutoka kwa wanachama na aliamua kumtumia mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo, Ramesh Patel, ili akutane na wanachama hao kwa ajili ya kupata suluhu.
Aveva alisema wanachama hao walielezwa na Patel kwamba wanatakiwa kwanza wafute kesi waliyoifungua Juni 23, mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam na kwamba walikataa na hakuna kati yao ambaye alijitokeza kukanusha kuhusika na uvunjwaji huo wa katiba.
"Natangaza rasmi watu wote 71 sio wanachama wa Simba Sports Club kuanzia leo (jana)", alisema Aveva na kumaliza agenda hiyo iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na wanachama waliohudhuria mkutano huo.
Rais huyo alisema kwamba wanachama walikosea kwa kupinga bila kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya Simba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Fifa.
NIPASHE lilipomtafuta Wambura jana ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa FAT sasa TFF, kuelezea maamuzi hayo yaliyochukuliwa na mkutano mkuu wa wanachama, alisema "siwezi kuzungumza lolote kwa sasa hadi nitakapopewa barua ya kufahamishwa kufutwa uanachama."
MABADILIKO YA KATIBA
Wanachama wa klabu hiyo pia walifanya mabadiliko kadhaa katika baadhi ya vipengele vya katiba ikiwamo ibara ya 5 inayoainisha aina ya wanachama kwa kuteua wanachama wa heshima ambao waliitumikia Simba kwa muda mrefu na kutoa mchango mkubwa.
Ibara ya 18 sasa inasomeka kuwa wadhamini wa klabu watakuwa wanne na ndiyo wamiliki na wadhibiti wa mali zote za klabu zinazohamishika na zisizohamishika. Pia mkutano mkuu ndiyo utakuwa na mamlaka ya kumuondoa mdhamini kutoka kwenye wadhifa huo baada ya kupata taarifa kutoka katika Kamati ya Utendaji.
Kipengele kingine kilichofanyiwa marekebisho ni cha ibara ya 22 ambacho kinaelezea Mkutano Mkuu wa dharura sasa kinasema kuwa wanachama wasiopungua 1000 waliojiorodhesha ndiyo wanaweza kuomba mkutano huo kwa maandishi na Kamati ya Utendaji itatakiwa kuitisha mkutano ndani ya siku 30 baada ya kuwasilisha ombi.
Ibara ya 25 (8) (111) inayompa nguvu rais wa klabu kuteua wajumbe wengine watano wa Kamati ya Utendaji ambao anaweza kuwabadilisha kwa kadri anavyoona inafaa ilipitishwa lakini baadhi ya wanachama walikuwa wakiipinga kwa madai kwamba itafanya kiongozi huyo wa juu kuwa dikteta.
Wanachama hao pi walitoa ridhaa ya kuundwa kwa Kamati ya Maadili (ibara ya 40) huku ibara ya 42 ikieleza kwamba kutaundwa Kamati ya Nidhamu ya Simba ambayo Mwenyekiti na Makamu wake lazima wawe na taaluma ya sheria.
Mkutano huo uliamua kwamba kila tawi litaendelea kuwa na wanachama kuanzia 50 na wasiozidi 250 na kukataa idadi ya tawi moja kuundwa na wanachama 500 kwa kuhofia 'mapinduzi'.
SITTA, MO WAULA SIMBA
Rais huyo aliyechaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Juni 29, mwaka huu pia aliwatangaza wadhamini wapya wa klabu hiyo kuwa ni pamoja na Samwel Sitta, Patel, Hassan Dalali na Adam Mgoyi.
Aveva pia aliwatangaza wanachama wengine wanne ambao watakuwa ni walezi wa Simba kuwa ni aliyekuwa mfadhili wa klabu hiyo, Mohammed Dewji 'Mo', Naibu Waziri Wizara ya Maji, Amos Makalla , Jaji, Thomas Mihayo na Zacharia Hanspoppe.
Wadhamini na walezi hao walithibitishwa na mkutano huo na watatambuliwa kwa muda wa miaka minne.
NIPASHE