STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 18, 2010

Baba Diana a.k.a Lukasa kuzikwa kesho mjini Tanga

MWANAMUZIKI Mkongwe wa muziki wa dansi, Abuu Semhando 'Baba Diana', 57, aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajili ya barabarani anatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda wilayani Muheza, Tanga kuzikwa.
Kwa mujibu Meneja Masoko wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' aliyokuwa akiifanyia kazi marehemu huyo,Martin Sospeter ni kwamba Semhando aliyefahamika pia kama Lukasa enzi akiwa Super Matimila, atazikwa kesho nyumbani kwao Tanga, ingawa msiba upo Mwananyamala Kisiwani alipokuwa akiishi enzi za uhai wake.
Sospeter, alisema mwili wa marehemu kwa sasa upo Muhimbili na wanafanya mipango ya kuusafirisha kwenda kuzikwa kwao Tanga kesho alasiri.
"Marehemu anatarajiwa kusafirishwa kwao Tanga kwa ajili ya mazishi, ingawa kwa sasa msiba upo nyumbani kwake, Mwananyamala Kisiwani na mwili wake umeshapelekwa hospitali ya Muhimbili," alisema Sospter.
Meneja huyo alisema kuwa marehemu aliyezaliwa Oktoba 24, 1953 na kuanza muziki mwaka 1974 katika bendi ya Sola Tv kabla ya kupita bendi mbalimbali Twanga Pepeta aliyoiongoza kama Katibu wake, amewaachia pengo kubwa lisilozibika aslan.
"Ni pigo kwetu na tumeshtushwa na kuhuzunishwa na kifo chake cha ghafla," alisema Sospeter.
Kifo cha mkongwe huyo aliuyewahi kuzipigia bendi za Super matimila, Orchestra Toma Toma, Tango Musica, Diamond Sound 'Wana Kibinda Nkoy', Beta Musica kabla ya kuasisi Twanga Pepeta, kimekuja masaa machache tangu fani ya muziki kumpoteza Ramadhan MToro Ongalla aliyefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Dk Remmy alifariki Jumatatu na kuzikwa Alhamis, huku Semhando na wanamuziki wenzake wakishiriki mwanzo mwisho katika msiba huo.

Mwisho

Buriani Baba Diana utakumbukwa daima





KIFO kimeumbwa kwa usiri mkubwa hata hujaji wake, pia huwa ni siri mno, kiasi ni vigumu kwa kiumbe chochote duniani kubaini lini atakumbana nacho.
Lau kisingekuwa na usiri katika suala la kifo, kwamtu kufahamu kitakufikia lini, wapi na kwa njia gani, sidhani kama kuna ambaye angekuwa akitoka nje siku ya ahadi yake kwa kuhofia kukutana nacho.
Ila kwa kuwa Mungu ana hekima na maana kubwa ya kukifanya kuendelea kuwa ni siri yake pekee yake duniani na ahera, kifo kinaendelea kuogopwa.
Ndio maana hata mwanamuziki gwiji wa muziki wa dansi, marehemu Marijani Rajabu 'Jabari la Muziki' enzi za uhai wake alitunga wimbo ulioelezea hamu yake ya kutaka kuwepo rufaa ya kifo ili mradi kuwarudisha wapendwa wetu wanaondoka ghafla bila kutarajiwa.
Abuu Semhando maarufu kama 'Baba Diana' au 'Lukasa' ambaye kwa siku zote nne za msiba wa mwanamuziki mwenzake, Ramadhani Ongolla 'Dk Remmy' alishiriki mwanzo mwisho hadi alipopumzishwa makaburini Sinza, Dar es Salaam, naye amefariki dunia.
Semhando, aliyekuwa mpiga dramu na Katibu wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' alifariki usiku wa kuamkia jana, ikiwa ni masaa machache tangu amzike mwenzake baada ya kupatwa na ajali mbaya ya barabarani.
Marehemu huyo alikumbwa na mauti hayo maeneo ya Mbezi Beach, akitokea kazini kwake baada ya kugongwa na gari akiwa anaendesha pikipiki na kujeruhiwa vibaya kichwani kabla ya kufa papo hapo.
Mwili wa mkongwe huyo aliyefanyia kazi bendi mbalimbali hapa nchini tangu miaka ya 1970 na aliyekuwa mpiganiaji wa haki za wanamuziki wenzake kama baadhi ya waliowahi kufanya nae kazi wanavyomueleza, uliohifadhiwa katika hospitali ya Muhimbili, utasafirishwa leo kwenda kuzikwa Muheza jiji Tanga.
Baadhi ya wanamuziki wa dansi nchini wamedai kushtushwa na kifo hicho cha ghafla cha Semhando, wakirejea kwamba walikuwa naye katika safari ya kumsindikiza Remmy aliyefariki Jumatatu na kuzikwa Alhamis, masaa machache kabla naye hajapatwa na mauti hayo.
Tshimanga Kalala Assosa, mtunzi na muimbaji aliyezipigia bendi mbalimbali kama Lipualipua, Le Kamalee, Fuka Fuka na Orchestra Marquis, alisema kama sio kuogopa kufuru, angeweza kusema Mungu ni kama amewaonea wanamuziki wa Tanzania wiki hii kwa vifo hivyo mfululizo.
"Naogopa kumkufuru Mungu, lakini misiba hii na hasa huu wa Semhando niliofahamishwa usiku wa manane kwa kupigiwa simu umeniuma kupindukia, ila sina jinsi kwa kuwa kazi ya Mungu haina makosa," alisema Assosa.
Assosa, alisema kuondoka kwa wakongwe hao ni kama uzindushi kwa waliosalia juu ya umuhimu wa kushikamana na kumcha Mungu, pamoja na kufanya maandalizi ya kusaka warithi wa nafasi zao katika muziki kwa sababu bila ya hivyo fani yao itatereka.
Ally Choki 'Mzee wa Farasi', aliyewahi kufanya kazi na Semhando wakati akiwa mwanamuziki na kiongozi wa Twanga Pepeta, alisema kifo cha Semhando ni pigo kwa familia ya marehemu, wadau wa muziki na hususani bendi yake ya Africana Stars kwa kuwa alikuwa nguzo.
"Sio siri ni msiba mkubwa na pengo kubwa katika muziki wa dansi na hasa Twanga Pepeta kwa vile nafahamu jinsi gani marehemu alivyokuwa 'roho' ya bendi hiyo, licha ya kwamba wapo waliokuwa wakimuona kama 'mnoko' fulani, namlilia milele Semhando," alisema Choki.
Choki alisema uzoefu wake katika fani ya muziki, ilimfanya marehemu kuwa mhimili wa bendi hiyo na muziki wa dansi kwa ujumla, akipigania masilahi ya wanamuziki wenzake na kusema hajui nani wa kuliziba pengo lake.
"Muhimu ni kumuombea kwa Mungu na pia kuiombea familia yake iwe na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi," alisema Choki.
Meneja wa Masoko wa bendi hiyo, Martin Sospeter, alisema kifo cha kiongozi mwenzao na mwanamuziki wao, ni pigo kubwa kutokana na kutokea kwake ghafla, lakini wanamuachia Mungu kwa kuwa alimpenda zaidi kuliko walivyompenda na kumthamini wao.
"Ni pigo kwetu na fani nzima ya muziki, tunajipanga kufanya maandalizi ya kumplekea mwenzetu katika makazi yake ya milele, ambapo atazikwa kesho (leo) nyumbani kwao mjini Tanga," alisema.
Marehemu Semhando ambaye majina yake kamili ni Abubakar Semhando, alizaliwa Oktoba 24, mwaka 1953 huko Muheza Tanga na kupata elimu ya msingi huko huko kwao, kabla ya kutumbukiza kwenye muziki miaka ya mwanzoni ya 1970.
Bendi yake ya kwanza kuifanyia kazi ni Sola TV ya jijini Dar mnamo mwaka 1974 kabla ya kutua Tanga International na kukaa nao hadi miaka ya 1980 alipohamia Super Matimila iliyokuwa chini ya Dk Remmy.
Aliihama Matimila na kutua Tomatoma Jazz akiwa na marehemu Adam Bakar 'Sauti ya Zege', kabla ya kuhamia Orchestra Safari Sound 'OSS' na kukaa nao hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 alipohamia Tango Musica, kisha kujiunga Vijana Jazz.
Baadae alitua Diamond Sound 'Wana Kibinda Nkoy' mwaka 1996 na kutunga kibao cha Neema kilichoipaisha bendi hiyo, miaka miwili baadae alihamia Beta Musica na kukaa nao kwa muda mfupi kabla ya kuhamia African Stars akiwa mmoja wa waasisi wake.
Amekuwa na bendi hiyo ya Twanga Pepeta tangu wakati huo hadi mauti yalipomkuta juzi akiwa ameshiriki kupiga dramu karibu nyimbo zote za albamu 10 za bendi hiyo kuanzia ile ya Kisa cha Mpenda hadi Mwana Dar es Salaam iliyozinduliwa mwaka huu.

Mwisho

BREAKING NEWS-ABUU SEMHANDO 'BABA DIANA' IS NO MORE





MWANAMUZIKI Mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Abuu Semhando 'Baba Diana' amefariki Dunia usiku wa kuamkia leo kwa ajali ya gari baada ya kugongwa akiwa kwenye pikipiki eneo la Africana, Mbezi jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mapema zinasema kifo hicho kilitokea majira ya saa 9 usiku baada ya kugongwa na gari aina ya Benz lililomjeruhi vibaya sehemu ya kichwani.
Abuu aliyetamba miaka ya 1970 akiwa na bendi ya Vijana Jazz, amepatwa na mauti hayo ikiwa ni siku moja tu tangu ashiriki kumziba mkongwe mwenzake, Ramadhani Mtoro Ongalla 'Dk Remmy' aliyefariki Jumatatu na kuzikwa Alhamis.
Kwa hakika ni pigo kwa wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki na wadau wa muziki wa dansi kwa ujumla, ingawa Kazi ya Mola Haina Makosa kwa sababu alishatuambia mapema kwamba KILA NAFSI ITAONJA MAUTI, wametangulia sisi tu nyuma yao tuwadhaike na vifo vyao kwa vile hatujui saa au siku ambayo Malaikat Maut, Izraili atatupitia kuchukua AMANA.
INNALILLAH WAINNA ILAHI RAJIUN!