FAINALI za mashindano ya soka katika Jimbo la Bagamoyo maarufu 'Kombe la Kawambwa' zitaanza rasmi kesho kwenye viwanja vinne vya Mwanakalenge, Vigwaza, Karege na Magereza - Kigongoni mjini humo.
Timu 16 zimetinga hatua hiyo ya fainali kati ya 72 zilizoshiriki mashindano hayo ngazi ya kata huku Majengo Stars wakitwaa ubingwa wa Ngao ya Hisani baada ya kuwafunga kwa matuta mabingwa watetezi, Beach Boys FC katika mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mwanakalenge mjini Bagamoyo juzi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mashandano hayo makubwa mjini humo, ambayo mwaka huu yanafanyika kwa mara ya nane tangu yaanzishwe 2006, Mkuu wa Wilaya hiyo, Ahmed Kipozi alisema mashindano hayo yatarejesha heshima ya soka katika wilaya hiyo na Mkoa wa Pwani kwa ujumla kwa vile yatazalisha vijana wengi wenye vipaji.
Mjumbe wa Kamati ya Mashindano hayo, Masau Bwire alisema Dk. Shukuru Kawambwa, ambaye ni Mbunge wa jimbo hilo (CCM) na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi tayari ameshagawa jezi seti moja, mipira na fedha za usafiri wakati wa mashindano kwa kila timu inayoshiriki fainali hizo mwaka huu.
Bwire, ambaye pia ni msemaji wa kamati hiyo, alizitaja baadhi ya timu zilizoingia katika hatua hiyo kuwa ni pamoja na Majengo Stars, Bongororo FC na Maji Coast za kata ya Magomeni.
Kata ya Dunda itawakilishwa na Beach Boys FC na Mwambao FC wakati Muungano FC na Buyuni FC zitaiwakilisha Kata ya Vigwaza huku Vijana Stars na Balack Rhino FC zikitoka Kata ya Zinga.
Timu nyingine na kata zinakotoka kwenywe mabano ni Tungutungu FC, Kegere United FC na Udindivu FC (Kegere), Kongo FC na Yombo FC (Yombo).