Vita ya Ivory Coast na Guinea ilikuwa hivi |
Seydou Keita wa Mali akichuana na mchezaji wa Cameroon |
VIGOGO vya soka barani Afrika, Ivory Coast na Cameroon zimeanza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, Afcon 2015 kwa kuponea chupuchupu vipigo toka kwa wapinzani wao katika mechi zao tofauti za Kundi D, zilizochezwa kwenye uwanja wa Malabo, mjini Malabo.
Ivory Coast walicheza mapema na Guinea katika mechi ya Kundi D, walinusurika kipigo toka kwa Guinea wakiwa pungufu baada ya nyota wake, Gervinho kulimwa kadi nyekundu katika kipindi cha pili kwa kuchomoa bao dakika 18 kabla ya pambano lao kumalizika.
Guinea walionyesha kandanda safi wakiwabana nyota wa Ivory Coast walioongozwa na nahodha wake, Yaya Toure, Mchezaji Bora wa Afrika kwa mwaka wa nne mfululizo, walitangulia kupata bao dakika ya 36 kupitia kwa Mohammed Yattara.
Hata hivyo Ivory Coast ilipambana na kurejesha bao hilo dakika ya 72 kupitia mtokea benchi Seydou Doumbia na kuipa pointi moja muhimu kigogo hicho kilichokuwa kikipewa nafasi kubwa kushinda pambano hilo na miongoni mwa zinazopewa nafasi ya kubwa bingwa.
Katika pambano jingine lililofuata Cameroon ililazimika kusubiri hadi dakika ya 84 kuchomoa bao mbele ya wapinzani wao Mali waliokuwa wakiumana nao kwenye uwanja wa Malabo.
Shujaa wa Cameroon alikuwa ni beki Ambroise Oyongo aliyefunga bao la kusawazisha baada ya Mali kutangulia kupata bao katika dakika ya 71 kupitia kwa Sambou Yatabare.
Katika mfululizo wa michuano ya fainali hizo za 30, timu za kundi A leo zitashuka dimbani kuumana ambapo wenyeji Guinea ya Ikweta itakuwa dimbani kujiuliza na Burkina Faso, huku Gabon wakipepetana na Kongo wakati kesho kutakuwa na mechi za kukata na shoka kwa timu za Kundi B, Zambia kupepetana na Tunisia kabla ya Cape Verde kupepetana na DR Congo katika mechi zitakazochezwa kwenye uwanja wa Ebebiyin, mjini Ebebiyin.
Katika mechi za kwanza kwa timu za kundi hilo kila moja iliambulia sare ya bao 1-1, Zambia ikitoshana nguvu na DR Congo na Tunisia na Cape Verde zilishindwa kutambiana.
Ijumaa kutakuwa na mechi za kundi C ambapo Ghana itashuka tena dimbani mjini Mongomo kuumana na Algeria baada ya kutoka kupokea kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Senegal ambayo itashuka dimbani kucheza na Afrika Kusini.