KWA niaba ya uongozi wa Coastal Union, tunatangaza msiba wa mchezaji wa
zamani wa timu hii Bakari Jeki, pichani, aliefariki usiku wa kuamkia jana katika
hospitali ya rufaa Bombo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kaka wa marehemu ndugu Ally Jeki, ndugu yetu aliugua kwa muda mfupi ambapo alilazwa katika hospitali ya Bombo wiki iliyopita mpaka mauti yalipomfika siku tatu baada ya kuanza kuugua.
Mwandisi wetu
alizungumza na mchezaji wa zamani wa Coastal Union, ambae alipata bahati
kumuona Bakari Jeki akiitumikia Coastal Union, Razak Yusuf ‘Careca’
ambae alibainisha kuwa marehemu alikuwa na mchango mkubwa katika timu. Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kaka wa marehemu ndugu Ally Jeki, ndugu yetu aliugua kwa muda mfupi ambapo alilazwa katika hospitali ya Bombo wiki iliyopita mpaka mauti yalipomfika siku tatu baada ya kuanza kuugua.
“Coastal Union imekosa mtu muhimu katika soka ambae alikuwa msaada mkubwa akitoa mawazo, vilevile alikuwa hakosi katika mechi na mazoezi ya timu,” Careca.
Aidha beki namba tano wa zamani Coastal Union, Mzee Salim Amir ambae alicheza na marehemu katika michuano ya UFUMA, iliyoandaliwa na Chama Cha Soka nchini (FAT), ambao ulikuwa ni ushauri wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere.
Nyerere alitoa ushauri huo ili kuisaidia FAT iliyokuwa chini ya Said El Maamry, kuondokana na madeni. Michuano hiyo ikapewa jina la Operesheni Futa Madeni (OFUMA).
Ilishirikisha timu nne ambazo ni Simba (Dar es Salaam), Nyota (Mtwara), Coastal Union (Tanga) na Nyota Afrika (Morogoro), Coastal Union waliibuka mabingwa marehemu Bakari Jeki akiwa beki mbili na langoni alikuwa mdogo wake Said Jeki ambae pia alikuwa golikipa wa Taifa Stars.
Baadhi ya wachezaji waliokuwa katika kikosi kilichotwaa kombe la OFUMA, ambalo lilichezwa mara moja tu na kutoendelea tena ni Zacharia Kinanda, Mohammed Makunda, Bakari Rashid, Kuzu Mbwana, Salim Amir, Mohammed Salim, Zaharan Makame, Said Jeki na Mguruko.
“Alikuwa ni beki mzuri, Coastal Union ilinufaika na uchezaji wake kwani alicheza kwa moyo wote beki mbili ambayo ilipanda na kushuka bila kuchoka. Mbali na hayo aliishi vizuri na wenzake hakuwa mtu wa matatizo muda mwingi alipenda utani.
“Alinikuta mwaka1976 nikitokea Misri na timu ya Taifa, tukashiriki kombe la OFUMA tukiwa pamoja katika safu ya ulinzi lakini baadae nilistaafu baada ya kuumia, yeye aliendelea mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1980 ndipo akaachana na soka, lakini hakuacha kuwa karibu na Coastal Union, muda mwingi alijitokeza kutoa ushauri na kila alipohitajika hakusita kuitikia mwito, huyo ndie Bakari Jeki ninaemfahamu,” alisema Salim Amiri.
Marehemu, alianza kucheza Coastal Union mwaka 1976 akitokea timu ya Magunia Moshi, alipotua Coastal Union alicheza kwa moyo wake wote mpaka alipostaafu soka, mpaka mauti yanamfika alikuwa kocha wa timu za mchangani mjini tanga na mshauri mkubwa wa benchi la ufundi Coastal Union.
Vilevile marehemu alitoka katika familia yenye vipaji vya soka kwani walikuwa ndugu watatu wa baba mmoja na mama mmoja ambapo Said Jeki alikuwa golikipa wa Coastal Union na timu ya Taifa, mwingine ni Hassan Jeki ambae alikuwa akichezea Reli Morogoro, lakini kwa sasa wote watatu ni marehemu.
Mwili wa Marehemu utatolewa Hospitali ya Rufaa Bombo mjini Tanga kuelekea nyumbani kwa kaka yake Ally Jeki maeneo ya Majengo, ifikapo saa tisa alasiri mwili wa marehemu utasaliwa katika msikiti wa Majengo kabla ya kupelekwa kijijini kwa Masuguru Wilayani Muheza Mkoani Tanga saa kumi alasiri.
Kaka wa marehemu hakuweka wazi kuhusu familia ya marehemu hasa upande wa mke ama watoto lakini alibainisha kuwa marehemu alizaliwa mwaka 1953 wilayani Muheza, Tanga.
KWETU HANDENI