|
Dihile (chini) |
KIPA mkongwe na nyota wa zamani wa Taifa Stars, Shaaban Dihile
anayeidakia JKT Ruvu ameweka bayana kwamba hana mpango wa kustaafu soka
kwa sasa kama alivyotangaza nahodha wake, Husseni Bunu waliojiunga wote
katika timu hiyo mwaka 2005.
Akizungumza na MICHARAZO, Dihile alisema bado yupo sana dimbani
katika kuendelea kucheza soka akiamini uwezo na umri unamruhusu kufanya
hivyo kwa muda mrefu.
Dihile, alisema kwa nafasi ya kipa kadiri umri unavyosonga mbele ndivyo
uimara wa makipa unavyoimarika na kwamba hadhani kama atatundika 'glovu'
zake mapema katika misimu ya karibuni.
"Sijafikiria kustaafu kwa sasa, bado najiona nina uwezo na umri wa
kuendelea kucheza kwa muda mrefu, japo kustaafu kunategemea mambo mengi
ukiacha suala la umri," alisema.
Alisema kupata majeraha makubwa ni sababu inayowaondoa wachezaji
uwanjani na kwa bahati nzuri yeye hajawahi kupatwa na kitu hicho hivyo
haoni sababu ya kutundika glovu zake kwa sasa, labda kama ataamua
mwenyewe kwa masuala mengine ikiwamo kutaka kuzisimamia miradi yake ya
biashara anayoiendesha kwa sasa.
"Ya Mungu mengi, naweza kufanya maamuzi hayo labda kutaka kusimamia
biashara zangu, lakini kwa sasa zinaendelea vyema ndiyo maana sina
mpango wa kustaafu kwani najiona bado sana kisoka," alisema Dihile
aliyewahi kuichezea Pan Africans ya jijini Dar.
Nahodha wa JKT Ruvu, Hussein Bunu alinukuliwa na MICHARAZO katika
mahojiano yake maalumu wiki iliyopita akidai huu ni msimu wake wa mwisho
kucheza kwa vile atatundika 'daluga' zake na kujikita kwenye ukocha
aliouanza kwa sasa.