STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, February 13, 2013

MALINZI AFUNGIWA 'VIOO' TFF BARUA YAKE YADUNDA


Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Tarehe 13 Februari 2013



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linapenda kuwajulisha wapenzi wa mchezo huu kuwa limepokea barua kutoka kwa Ndg. Jamal Malinzi ambayo inaomba kuangaliwa upya kwa maamuzi ya Kamati ya Rufaa za Uchaguzi ya TFF ya kuliondoa jina lake kwenye orodha ya wagombea urais wa Shirikisho.



Barua hiyo ya tarehe 13 Februari 2013 ilielekezwa kwa mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF. Baada ya kuipata barua hiyo, Sekretarieti iliwasiliana na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ambaye alielekeza kuwa Ndg. Malinzi alielekeza barua yake kwenye chombo ambacho hakikufanya uamuzi wa kuliengua jina lake na hivyo hakina mamlaka ya kuangalia upya suala hilo.



Mwenyekiti alishauri kuwa TFF imwandikie Ndg. Malinzi barua ya kumshauri kuwa aelekeze maombi yake kwenye chombo kilichofanya maamuzi kwa kuwa ndicho kinachoweza kuangalia upya maamuzi yake.



Sekretarieti pia imepokea maamuzi rasmi ya Kamati ya Rufaa za Uchaguzi ya TFF na imeshayawasilisha kwenye Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uchaguzi za TFF.



Angetile Osiah

Katibu Mkuu,

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Coastal yaangukia pua Kagera, Mgambo yatakata Tanga

Hamis Shengo (kulia) wa Coastal akijaribu kumtoka Felix Themi ya Kagera Sugar katika pambano la leo. (Picha kwa hisani ya Blog ya Coastal Union)
TIMU ya Coastal Union ya Tanga jioni hii imeangukia pua baada ya kunyukwa bao 1-0 mjini Bukoba na wenyeji wa Kagera Sugar, wakati majirani zao JKT Mgambo ikinawiri nyumbani mjini Tanga kwa kuilaza JKT Oljoro kwa mabao 2-0.
Bao pekee lililowazamisha wagosi wa kaya lilitupiwa kimiani kwa kichwa na Felix Themi akitokea benchi kwenye dakika ya 58 baada ya mabeki wa Coastal kuzembea.
Kipigo hicho kinaifanya Coastal kufuata mkondo wa Mgambo ambao nao walichezea kipigo kama hicho katika mechi yao iliyopita mjini humo.
Hata hivyo Mgambo leo ilizinduka na kuzima wimbi la ushindi la JKT Oljoro kwa kuwanyuka mabao 2-0 katika pambano lililochezwa kwenye uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mechi nyingine katika Ligi Kuu leo imeshuhudiwa Mtibwa ikilazimishwa sare ya 0-0 mbele ya Ruvu Shooting, huku Toto Africans wakiwa nyumbani CCM Kirumba Mwanza walilazimishwa sare ya mabao  2-2 na timu iliyozinduka tangu iwe chini ya nyota wa zamani wa Yanga, Pan na Taifa Stars, Mohammed Rishard 'Adolph' kama kocha wao, Polisi Morogoro.

Tegete azidi kung'ara Yanga ikiizamisha Lyon 4-0



Beki wa Yanga, David Luhende, (Kulia), akijaribu kumzuia mchezaji wa timu ya African Lyon Yusuph Mpili, wakati wa mchezo wa ligi kuu uliofanyika leo katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaa Yanga imepata ushindi wa mabao 4 -0 ikiwa imebaki kileleni



MABAO mawili ya mshambuliaji aliyerejea kwa kasi nchini, Jerry Tegete ya kipindi cha kwanza na mawili mengine ya watokea benchi Didier Kavumbagu na Nizar Khalfan katika kipindi yameipa Yanga ushindi wa mabao 4-0 mbele ya vibonde African Lyon.
Tegete aliyekuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Lyon, alifunga mabao hayo katika pambano lililokosa msisimko kama ilivyotarajiwa lililochezwa jioni hii kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Yanga kuiacha Azam kwa pointi tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Tegete akijiongezea hazina ya mabao akiwafukuzia akina Kipre Tchetche wa Azam na Didier Kavumbangu aliyefikisha bao la tisa baada ya leo kutupia moja la penati.
Yanga imefikisha jumla ya pointi 36 kutokana na michezo 16 sawa na timu nyingine 13 zinazoshiriki ligi hiyo, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 33.
Katika pambano hilo beki wa Lyon, Mpilipili alilimwa kadi nyekudnu kwa kumchezea vibaya kiungo wa Yanga Haruna Niyonzima dakika za lala salama, huku Yanga ikikosa penati kupitia Hamis Kiiza.
Ushindi huo wa Yanga umekuja baada ya kupunguzwa kasi katika mechi iliyopita kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar na kufikisha idadi ya mechi 18 tangu timu hiyo iwe chini ya kocha Ernest Brandts

MALINZI SASA AMTEGEMEA TENGA TFF





Mgombea Urais wa TFF aliyeenguliwa, Jamal Malinzi akizungumza na vyombo vya habari kuhusu sakata zima kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam leo. Picha: Bongostaz.blogspot.com



YAH: KUENGULIWA KWANGU KUGOMBEA URAIS WA TFF 2013

Ndugu zangu,kupitia vyombo vyenu vya habari ninaomba niueleze umma wa watanzania,hususani wadau wa mpira wa miguu,yafuatayo kuhusu kuenguliwa kwangu.

Awali ya yote nieleze kusikitishwa kwangu na maamuzi yaliyotolewa na kamati ya rufaa ya TFF ya kuniengua kugombea urais wa TFF.Sikubaliani na maamuzi haya .

Katika kuniengua kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF imetoa sababu mbili (nanukuu magazeti ya jana tarehe 12/02/2013 maana hadi leo sijakabidhiwa barua ya kuenguliwa).

1. Kukosa uadilifu kwa kupinga waraka uliotolewa na TFF wa kubadili Katiba ya TFF mwezi Desemba 2012.

2. Kukosa uzoefu wa miaka mitano ya uongozi.

Ndugu zangu,kiini cha maamuzi ya Kamati ya rufaa dhidi yangu ni pingamizi lililowekwa na mtu mmoja anayeitwa AGAPE FUE.Bwana Agape Fue aliniwekea pingamizi katika kamati ya uchaguzi akidai mimi nilipinga waraka wa kubadili katiba ya TFF na pia sina uzoefu wa miaka mitano ya uongozi wa mpira.Kinyume na matakwa ya kamati ya uchaguzi kama yalivyotangazwa kuwa mtoa pingamizi aje mwenyewe kutetea pingamizi lake ,Bwana Agape Fue hakutokea mbele ya Kamati ya Bwana Lyatto.Matokeo yake tarehe 31/01/2012 kamati ya uchaguzi ya TFF ilitoa maamuzi ya ya kutupilia mbali pingamizi hili.

Bwana Agape Fue hakuishia hapo kwa mara nyingine tarehe 06/02/2013 alikata rufaa kwenye kamati ya rufaa ya uchaguzi akidai kamati ya uchaguzi haikumtendea haki. Rufaa hii haikuwa na anwani wala namba ya simu ya Bw.Agape Fue.Rufaa ilisikilizwa tarehe 10/02/2013 na maamuzi ya kukata jina langu yakatangazwa jioni ya tarehe 11/02/2013.

Mpaka leo najiuliza hivi huyu Bw. Agape Fue ni mwanaume au ni mwanamke?(hakueleza kama ni Bwana au Bibi Agape Fue). Agape Fue ni nani hasa? Anaishi wapi?Je ni Mtanzania au sio Mtanzania maana kikanuni wasio watanzania hawaruhusiwi kujihusisha na uchaguzi wa TFF (rejea kifungu cha 9 cha kanuni za uchaguzi),pingamizi lake halikuambatana na udhibitisha wa uraia. Kwa nini alichukua maamuzi haya? Sipati jibu. Iweje mtu achukue maamuzi mazito ya kumkatia mtu rufaa kisha uishie kusaini karatasi na kuwaachia wengine wakusemee na usije hata kushuhudia kinachoendelea kama kweli una maslahi na madai yako? Waandishi wa habari mnisaidie kupata majibu.



Ndugu zangu ,mtoa pingamizi alidai haikuwa sahihi kupinga azimio la kubadili katiba ya TFF kwa njia ya waraka.Naomba nisistize mambo matatu:

1. Wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF wanawakilisha matakwa ya vyama vilivyowatuma kwenda kwenye mkutano mkuu wa TFF,na ndio maana chama cha mpira cha mkoa wa Kagera (KRFA) kiliitisha kikao cha kamati ya utendaji ili kamati iweze kutoa mwongozo kwa wajumbe wake kuhusu nini kifanyike kuhusu waraka ulioletwa na TFF, hivyo maamuzi yaliyotolewa ya kuukataa waraka huu yalikuwa ni maamuzi ya chama cha mpira mkoa wa Kagera na wala hayakuwa ni maamuzi ya Jamal Malinzi,iweje malinzi niadhibiwe kwa maamuzi haya,kwa nini usiadhibiwe mkoa mzima na mikoa yote iliyopinga waraka?hii ni haki kweli? Siamini kama kuna mjumbe wa mkutano mkuu aliyekiuka maamuzi ya kamati yake ya utendaji.

2. Katika mchakato wa kubadili katiba kwa njia ya waraka kilichokuwa kinagomba sio maudhui (content) ya mabadiliko ya Katiba bali utaratibu uliotumika kubadili Katiba. Swali la msingi tulilojiuliza wajumbe wa kamati ya utendaji KRFA ni kwamba je kwa mujibu wa Katiba ya TFF kifungu 22 na kifungu 30 wapi katiba inatamka kuwa inaweza kubadilishwa kwa njia ya waraka? Mpaka leo hilo jibu hakuna,labda aliyeniwekea pingamizi atusaidie kupata jibu la swali hili. Katiba ya TFF iko wazi kabisa inatamka kuwa Katiba itabadilishwa kwa njia ya Mkutano Mkuu tu (General Assembly).

3. Ni kweli FIFA iliagiza yafanyike mabadiliko ya Katiba ya kuingiza kipendele cha ‘club licencing’ katika Katiba ,lakini je FIFA katika agizo hilo ilisema Katiba ya TFF ivunjwe ili kutimiza azma hiyo? Ikumbukwe kuwa mwaka 2004 FIFA iliagiza TFF iingize kwenye Katiba kipengele cha Katibu Mkuu awe wa kuajiriwa badala ya kuchaguliwa,agizo hili lilitekelezwa kwa kupitishwa na Mktano Mkuu wa TFF,iweje leo utaratibu huu ukiukwe? Hata majuzi CAF walipotaka kubadili katiba ili Rais wa CAF atokane na wajumbe wa Kamati ya Utendaji jambo hili lilitekelezwa kwa kuitisha mkutano mkuu wa dharura uliofanyika Seychelles majuzi. Katiba ndio msingi mkuu wa uendeshajiwa TFF,nitaipigania siku zote.Huo ndio utaratibu,si CAF si FIFA si Vyama vya mpira vya nchi,hakuna anayebadili Katiba kwa njia ya waraka,kama kuna mwenye ushahidi aulete.



Kuengua jina langu eti kwa kuwa nilipinga waraka wa kubadili Katiba sio uamuzi sahihi.



Kuhusu uzoefu wa miaka mitano katika Uongozi:



Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi mkuu wa TFF mwaka 2008 niligombea na jina langu lilikatwa na kamati ya uchaguzi ya TFF.Nilikata rufaa katika Kamati ya Rufaa ya TFF na kushinda . Hukumu hii ni halali hadi leo.Iweje leo hii miaka minne baadae Kamati hiyo hiyo ya rufaa (kubadili majina ya wajumbe sio kubadili taasisi) inione sina uzoefu?.Si hilo tu ,hata katika kujaza fomu namba moja ya kugombea niliambatanisha vielelezo vyote vya uzoefu wangu ikiwa ni pamoja na kudhibitisha kuwa katika kipindi cha miaka mine iliyopita nimekuwa:

-Mjumbe wa Baraza la michezo mkoa wa Dar es salaam.

-Mwenyekiti wa kamati ya mashindano chama cha mpira mkoa wa Pwani COREFA.

-Mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa wa Kagera

-Mwenyekiti wa chama cha mpira mkoa wa Kagera

Hii ni pamoja na kuongoza Yanga 2002-2005.

Hivi katika nafasi hizi za uongozi ipi ni ya kuongoza ‘bonanza’? Nimedhalilishwa sana.



HITIMISHO

Vyombo vya habari kupitia makala,tahariri na maoni ya wasikilizaji/wasomaji/watazamaji vimesifia sana awamu mbili za uongozi wa Bwana Leodeger Tenga.Bwana Tenga amesifiwa kwa umahiri wake wa kuleta utulivu katika sekta ya mpira wa miguu Tanzania.Amesifiwa kwa kujenga taasisi imara ambayo mhimili wake mkuu ni sekretarieti makini na kamati mbali mbali zilizo imara .Let him rise to the occasion,muda wa kuonyesha uongozi imara ni huu,historia itamhukumu kwa jinsi gani atasimamia suala hili,haki sio lazima itendeke lakini pia inatakiwa ionekane inatendeka.

Kamati ya utendaji ya TFF inayo mamlaka ya kubatilisha maamuzi haya kwa maslahi ya mpira wa Tanzania.Ninamshauri Rais wa TFF aitishe kikao cha dharura cha kamati ya utendaji ili kijadili hali hii na kunirudishia haki yangu ya kugombea urais wa TFF.

Nihitimishe kwa kuwaomba wadau wa mpira wa miguu Tanzania wawe watulivu wakati tukisubiri kupata ufumbuzi wa suala hili.



Mungu ibariki Afrika,

Mungu ibariki Tanzania.

Ahsanteni sana,



Jamal Emil Malinzi

Dar es salaam

13/02/2013


Yanga kuvuna nini leo kwa Lyon?

Kikosi cha Yanga kitakachovaana na African Lyon
VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jioni ya leo wanatarajiwa kuvaana na wanaoburuza mkia katika ligi hiyo, African Lyon katika mfululizo wa mechi za duru la pili pambano litakalofanyika kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tayari kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro ameweka bayana kwamba wanaingia dimbani leo kwa lengo la kushinda mchezo huo ili kuwakimbia Azam na kujiwekea mazingira mazuri ya kutwaa taji la msimu huu.
Yanga iliyolazimishwa sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar katika mechi yake ya mwisho inalingana pointi na Azam waliopo nyuma yake ambao wapo mapumzikoni wakijiandaa na mechi yao ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kikosi cha Yanga kinakutana na Lyon ambayo imekuwa na matokeo mabaya tangu kuanza kwa duru la pili wakiwapokea Polisi Moro katika nafasi ya mkiani.
Hata hivyo Yanga isitarajie wepesi katika mechi hiyo ya leo kutokana na rekodi zilizopo pale timu hizo mbili zinapokutanana ambapo Yanga hupata tabu kuifunga timu hiyo ya Lyon.
Mbali na mechi hiyo pia leo kutakuwa na mechi nyingine kadhaa katika viwanja wa Mkwakwani Tanga, JKT Mgambo itavaana na JKT Oljoro, Coastal Union itakuwa uwanja wa Kaitaba kuumana na Kagera Sugar, huku Toto African itakuwa nyumbani kuwakaribisha Polisi Moro na Mtibwa Sugar kuivaa Ruvu Shooting.

Juve, PSG waua Ulaya, Man U, Madrid vitani leo

Juventus stun Celtic Park thanks to Matri's early strike and temporarily silence one of the most partisan crowds in European football. The goal came following a dreadful defensive error from Efe Ambrose, who helped Nigerian win the Africa Cup of Nations just last Sunday.
Wachezaji wa Juventus wakishangilia moja ya mabao yao
WAKATI mashabiki wasoka dunia wakiwa na hamu  kushuhudia pambano kabambe kati ya Manchester United na Real Madrid, timu za Juventus na PSG usiku wa kuamkia leo wameanza vema mechi zao mtoano Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Juvetus ya Italia ikiwa ugenini nchini Scotland ilipata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Celtic na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.
Bao la mapema la dakika tatu toka kwa Alessandro Matri na mengine ya kipindi cha pili yaliwafanya 'kibibi' hicho cha Turin, kwenda kuisubiri Celtic katiak mechi ya marudiano ikiwa haina presha kubwa.
Mabao mengine ya Juvetus, vinara wa Ligi ya Seria A yalitupiwa kambani na Claudio Marchisio katika dakika ya 77 na Mirko Vucinic dakika saba kabla ya pambano hilo kumalizika.
Katika mechi nyingine iliyochezwa jana usiku, Valencia ya Hispania ilijikuta ikichezea kichao cha mabao 2-1 wakiwa nyumbani kutoka kwa wenyeji wao PSG ya Ufaransa.
PSG, ilijikuta hata hivyo ikimaliza pambano hilo vibaya kwa kumpoteza nyota wake Zlatan Ibrahimovic aliyelimwa kadi nyekundu dakika za lala salama.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea usiku wa leo kwa mechi nyingine mbili, Manchester United ya Uingereza itasafiri mpaka Madrid, Hispania kuivaa Real Madrid katika pambano linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani,
Pambano hilo linasubiriwa kwa hamu kutokana na hali ilizonazo timu hizo mbili ambazo zinanolewa na makocha waliowahi kuwa wapinzani wakubwa katika Ligi Kuu ya Engaland, Jose Mourinho na Sir Alex Ferguson.
Mechi nyingine inayochezwa leo itazikutanisha pia timu za Shakhtar dhidi ya Borrusia Dotmund, itakayokuwa ugenini nchini Ukraine
Utamu wa pambano hilo unachagizwa na 'vita' ya makocha waliowahi kuwa wapinzani baada ya kupewa kadi ya pili ya njano.lijikuta akimaliza mchezo huo vibaya kwa kulipwa kadi nyekundu dakika za lala salamai.