STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, November 7, 2013

Kocha Azam abwaga manyanga, kisa...!

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
KOCHA Muingereza, Stewart John Hall ameamua kujiuzulu kufundisha klabu ya Azam FC baada ya kukubaliana na wamiliki wa timu hiyo na leo hii amewaaga wachezaji wa timu hiyo.
Stewart aliwaaga wachezaji na benchi la Ufundi mara tu baada ya mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya timu hiyo na Mbeya City ulioisha kwa sare ya kufungana mabao 3-3 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Amebwaga manyanga; Stewart Hall amewaaga wachezaji na benchi la Ufundi baada ya sare ya 3-3 na Mbeya City leo Camazi

“Ni kweli nimewaaga wachezaji na wenzangu katika benchi la Ufundi, nimewaambia imebidi niondoke kwa sababu nimepata kazi sehemu nyingine. Lakini pia wamiliki wa timu wameridhia niondoke na ninaondoka vizuri, nawatakia kila heri,”alisema Stewart alipozungumza na BIN ZUBEIRY jioni hii.
Hii inakuwa mara ya pili, Stewart kuondoka Azam, baada ya awali Agosti mwaka jana kuondolewa kiasi cha mwaka mmoja tu tangu aajiriwe akitoka kufundisha timu ya taifa ya Zanzibar.
Stewart alifukuzwa baada ya kuiwezesha Azam kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu na Kombe la Kagame, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati pamoja na kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi na nafasi yake ikachukuliwa na Mserbia, Boris Bunjak.
Hata hivyo, baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita, Stewart aliyehamia Sofapaka ya Kenya, alirejeshwa Azam kufuatia kutimuliwa kwa Mserbia, Bunjak.
Stewart akarudia kuipa nafasi ya pili Azam katika Ligi Kuu na kuipa Kombe la Mapinduzi pamoja na kuiwezesha kutwaa taji la Ngao ya Hisani, michuano iliyofanyika mjini Kinshasa, DRC, Desemba mwaka jana. 
Bado haijajulikana sasa Azam itaangukia mikononi mwa kocha gani, ikiwa sasa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu umemalizika na wachezaji wanakwenda mapumzikoni.
Stewart ni kocha wanne kuondolewa Azam tangu ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2007/2008 baada ya Wabrazil Neider dos Santos na Itamar Amorin na Mserbia Bunjak.
Azam imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi zake 27 sawa na Mbeya City, nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 28.

Yanga yarejea kileleni, Azam, Mbeya City zawekwa rekodi zikitoka sare ya 3-3,Mwagane Yeya apiga hat trick

Azam wakishangilia moja ya mabao yao msimu huu

Mbeya City wakiomba dua kuwasaidia wafanye vyema katika mechi zao
MSHAMBULIAJI Mwagane Yeya ameingia kwenye rekodi ya wafungaji wa hat trick msimu huu baada ya jioni ya leo kutupia mabao matatu wavuni wakati timu yake ya Mbeya City ikilazimisha sare ya mabao 3-3 na Azam.
Mchezaji huyo anakuwa wa tatu kufunga mabao matatu katika mechi moja na mzawa wa pili baada ya Abdallah Juma wa Mtibwa Sugar kuvunja rekodi iliyokuwa imedumu kwa misimu miwili tangu iwekwe na Juma Semsue wa Polisi Dodoma mwaka 2010-2011.
Yeya alifunga mabao hayo katika pambano la funga nikufunge baina ya timu yake na Azam lililochezwa kwenye uwanja wa Chamazi na kuzifanya timu hizo kugawa pointi na kuipisha Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi.
Mabao yake aliyafunga katika dakika ya 30, 50 na 73 na kuwafanya washambuliaji wa Azam kuwa na kazi ya kuyarejesha ambapo John Bocco 'Adebayor' alifunga bao la kusawazisha la pili kabla ya Mcha Khamis Vialli kuchomoa bao la tatu dakika ya 83 na kuzifanya timu hizo zigawane pointi na kuweka rekodi ya kutofungika duru zima la kwanza.
Timu hizo ndizo pekee hazijafungwa katika ligi mpaka sasa na zikiwa zimemaliza mechi zake zikiwa na ponti 27 kila mmoja wakizidiwa na Yanga waliorejea kileleni wakiwa na pointi 28 baada ya kuinyuka Oljoro JKT mabao 3-0 kwenye uwanja wa Taifa.
Bao la tatu la Azam lilifungwa na Humphrey Mieno aliyetangulia kufunga dakika ya 13 tu ya mchezo kwa kichwa kabla ya Yeya kusawazisha na kwenda mapumziko wakiwa nguvu sawa ya bao 1-1.
Katika uwanja wa Taifa Yanga ilipata mabao yake kupitia Simon Msuva aliyefunga katika dk ya 23 kabla ya Mrisho Ngassa kufunga bao la pili dakika ya 30 na Jerry tegete kuongeza bao jingine dakika ya 54 na kuhitimisha ushindi wa mechi nne mfululizo wote ukiwa kwa timu za maafande na kurejea kileleni hadi mwakani.
Katika mechi nyingine ya mjini Tabora matokeo ni kwamba timu ya Rhino Rangers ikiwa nyumbani imeshindwa kufurukuta kwa kulazimishwa suluhu na Prisons ya Mbeya.

Kiiza kumkamata Tambwe lna kutimiza ahadi yake leo Taifa?

Hamis Kiiza wa Yanga

Amissi Tambwe wa Simba

Kipre Tchetche wa Azam
MSHAMBULIAJI wa kiganda, Hamis Kiiza 'Diego' hivi karibuni alinukuliwa kwamba angependa kumaliza mechi za duru la kwanza kwa kufunga jumla ya mabao 10, na kabla ya pambano la leo la timu yake ya Yanga dhidi ya Oljoro JKT, tayari anayo mabao nane.
Mabao hayo ni pungufu ya mabao mawili na aliyonayo mkali wa Msimbazi, Mrundi Amissi Tambwe anayeongoza orodha ya wafungaji bora kwa sasa katika Ligi Kuu akiwa na mabao 10, nusu ya mabao aliyoahidi kuyafunga katika msimu wake wa kwanza akiwa na Wekundu wa Msimbazi.
Kiiza, ili kutimiza ahadi yake ya kufunga mabao 10 anapaswa leo kutumbukiza wavuni mabao mawili ambapo mbali na kumkamata mpinzani wake, pia itamfanya kuuaga mwaka 2013 akiwa na furaha na kusubiri kuona mwaka ujao wa 2014 utakuwa wa aina gani kwake na wote wanaokifukizia kiatu cha dhahabu.
Mganda huyo mbali na kutaka kumkamata Tambwe, pia atalazimika kufunga mabao zaidi ikiwezekana ili kumpita Elias Maguri anayeshika nafasi ya pili akiwa na mabao 9 na pia kuwaacha mbali Kipre Tchetche wa Azam mwenye mabao 7 na Juma Luizio wa Mtibwa aliyefunga mabao nane na kulingana naye.
Iwapo atatoka kapa, basi ile ahadi yake ya kufikisha mabao 10 itaambulia patupu na pia kuwaacha wapinzani wake wakimcheka kwa mbaaali kwani itambidi asubiri hadi mwakani panapo majaliwa kuwakimbiza tena.
Wakati Mganda akiwaza hivyo, Kipre Tchetche leo atakuwa na wasaa nzuri wa kuthibitisha kuwa hakubahatika kuwa Mfungaji Bora kwa msimu uliopita wakati atakapovaana na Mbeya City.
Tchetche mwenye mabao saba kwa sasa akishika nafasi ya nne ya wafuingaji inayoongozwa na Tambwe na kufuatiwa na Maguri kisha Kiiza na Luizio, ana kazi nghumu mbele ya Mbeya City ambayo kama ilivyo kwa Azam haijapoteza mechi yoyote msimu huu.
Mashabiki wa soka wangependa kuona 'vita' ya mapro hao ikinoga kama Tchetche atatupia mabao kambani kadfhalika kwa Kiiza na kukimbizana na Tambwe, japo wazawa Muguri na Luizio hawana chao kwa sasa mpaka mwakani kwa vile shughuli yao waliimaliza jana walipozifungia timu zao mabao.
Mbali na mechi za Azam na Mbeya City na ile ya Yanga na Oljoro, leo pia kuna mechi nyingine kati ya Rhino Rangers ya Tabora dhidi ya Prisons Mbeya mechi inayochezwa uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambayo matokeo yake yataweza kuvuruga tu msimamo wa timu zilizopo chini tofauti na mechi hizo mbili za awali ambazo zinaweza kubadilisha taswira ya msimamo wa Tatu Bora wakati ligi ikienda mapumzikoni.
Azam wanaoongoza msimamo ikiwa na pointi 26 sawa na Mbeya City wakizidiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa na watetezi Yanga wapo nafasi ya tatu na pointi zao 25 na mechi yao na Oljoro inaonekana kama nyepesi, japo katika soka hakuna kitu kama hicho.

Arsenal, Chelsea zaua, Barca yaichinja Milan, Atletico Madrid dah!

Samuel Eto'o aliyeifungia Chelsea mabao mawili

Ramsey akishangilia bao lake na Mesut Ozil

KOCHA Arsene Wenger huenda sasa anapumua na kuondokana na presha juu ya uwezo wa kikosi chake baada ya usiku wa kuamkia leo kuwatungua Borussia Dotmund ya Ujreumani ikiwa kwao kwa bao 1-0 na kujiweka pazuri kwenye kundi lake katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Bao pekee lililowekwa na kiungo Aaron Ramsey katika dk ya 62, lilitosha kuzima ngebe wa wanafainali hao wa msimu uliopita na kuipa Arsenal ushindi huo na kuifanya ilingane pointi na Napoli walioinyuka Olympique Maseille mabao 3-2 zote zikiwa na pointi 9 na kutofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika mechi nyingine zilizochezwa jana  Barcelona ikiwa nyumbani iliisulubu AC Milan kwa mabao 3-1, huku nyota wa Argentina,  Lionel Messi akifunga mawili na jingine likizamishwa na Busquets, huku Gerrard Pique akijifunga na kuizawadia wageni bao la kufutia machozi.
Chelsea ilifuata nyayo za Arsenal kwa kuizabua Schalke 04 ya Ujerumani mabao 3-0 kayika pambano lililoshuhudia Samuel Et'oo na mbadala wakem Demba Ba wakifunga mabao hayo yote na kuwapa ushindi muhimu vijana wa Jose Mourinho.
Eto'o alifunga mabao mawili na alipotoka na kuingizwa Ba naye alitupia moja na kufanya Chelsea kutakata ikiwa nyumbani, huku Atletico Madrid ikiwa nyumbani ikiidadavua Viena kwa mabao 4-0, Ajax ikiizima Celtic kwa bao 1-0  na timu za Basel vs Steau Bucharest na Porto na Zenit zikishindwa kutambia katika michezo yao kwa kutoka sare ya baoa 1-1.