Chipolopolo katika pozi |
MUIMBAJI wa zamani wa kundi la King's Modern Taarab, Mwanahawa Ally 'Mwanahawa Chipolopolo', ameanza kulisuka kundi lake la miondoko hiyo aliloliunda hivi karibuni baada ya kupata mfadhili aliyempa vyombo vya muziki.
Pia msanii huyo amekanusha kumnyakua wasanii waliodaiwa kujiengua katika kundi lake la zamani wa King's Modern, kwa kile alichodai hataki ugomvi na 'bosi' wake wa zamani wala kutaka wasanii wenye majina makubwa.
Akizungumza na MICHARAZO jana, alisema kundi lake linaloendelea kujifua kabla ya kutoa burudani, linaundwa na wasanii kadhaa wasio na majina makubwa lakini wenye vipaji vya hali ya juu katika muziki.
Msanii huyo aliwataja baadhi ya wasanii wanaounda kundi lake hilo lenye maskani yake Keko kuwa ni Haruna Hassani 'Bonge la Bwana', Kuruthumu Akida, Mwajuma Abdalla na Rehema 'Mtu Mzima Dawa ambao ni waimbaji.
Msanii huyo aliongeza hata taarifa kwamba wamewanyakua baadhi ya wasanii wenzake wa zamani wa Kings Modern waliodaiwa kulihama kundi hilo, sio za kweli kwa sababu hana mpango wa kunyakua msanii yeyote mwenye jina kubwa.
"Hakuna msanii hata mmoja mwenye jina aliyetua kwangu, wala sijamnyakua msanii aliyetoka Kings Modern au kokote kule kunakotajwa kuna wasanii wakali," alisema.