Ghana |
Libya |
BAO pekee lililofungwa na Kwabena Adusei katika dakika ya 77 limeisaidia kuivusha Ghana hadi hatua ya robo fainali ya michuano ya CHAN baada ya kuinyuka Ethiopia, huku Kongo ikiduwazwa na Libya baada ya kuchomoa kipigo dakika za jioni na kupata sare ya 2-2.
Abdelrahman Fetori aliifungia Libya bao wakati Kongo wakiamini wamepata ushindi wao wa pili katika michuano hiyo kutoka kundi C na kujihakikishia tiketi ya kucheza robo fainali.
Fetori alifunga bao hilo dakika ya pili ya nyongeza baada ya dakika 90 kukamilika na kufanya matokeo kuwa 2-2- na hivyo Libya kuungana na Ghana iliyoongoza kundi hilo kufuzu mtoano.
Kongo ilitangulia kupata mabao mawili na kuonekana kuikamata vilivyo libya katika pambano lililochezwa kwenye uwanja wa Peter Mokaba, Polokwane (Pietersburg), wakati Ghana iliichapa Ethiopia uwanja wa Free State, mjini Bloemfontein.
Mabao ya Kongo katika mchezo huyo yalifungwa na Nkounkou dakika ya 36 na Binguila dakika ya 54, kabla ya Abdulsalam Omar kufunga bao la kwanza katika dakika ya 75.
Kwa matokeo hayo Ghana imemaliza mechi zake tatu kwa kukusanya pointi saba na kuongoza na kufuatiwa na Libya yenye pointi tano na Kongo imesaliwa na pointi tatu, huku Ethiopia ikitoka patupu na kuweka rekodi ya kutofunga bao hata moja wala kupata pointi katika michuano hiyo tofauti na wengi walivyoitegemea.
Timu hizo mbili zimeungana na zimeungana na Nigeria, Mali kutoka kundi A na Morocco na Zimbabwe za kundi B kucheza hatua ya mtoano na timu za mwisho zitapatikana kesho katika mechi za mwisho za makundi wakati kundi D litakalofunga dimba usiku.
Burundi inayoongoza kundi hilo itapepetana na majirani zao DR Congo na Mauritania itaumana na Gabon.