|
Kikosi cha Azam |
MABINGWA wa
Kombe la Mapinduzi, Azam Fc wanatarajiwa kurejea leo usiku Dar es Salaam,
wakitokea Nairobi, Kenya walipokwenda kwa ziara ya wiki moja hya michezo ya
kujipima nguvu kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
AZAM FC yenye
maskani yake Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ilihitimisha vema
ziara yake hiyo jana, baada ya kuifunga timu ya Benki ya Biashara Kenya, KCB
bao 1-0 kwenye Uwanja wa City, Nairobi jioni hii.
Bao pekee la
ushindi la Azam jioni ya jana lilifungwa na kiungo Ibrahim Mwaipopo kwa shuti
la mpira wa adhabu katika dakika ya pili ya muda wa nyongeza, baada ya kutimu
kwa dakika 45 za kawaida za kipindi cha kwanza.
Hata hivyo,
Azam ingeweza kuondoka na ushindi mnene zaidi jana, kama si kiungo wake
mwingine Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ kukosa penalti dakika ya 83 baada ya shuti
lake la kudakwa na kipa wa KCB.
Huo unakuwa
ushindi wa pili katika mechi zake tatu za kujipima nguvu nchini humo, kwani
awali bao pekee la Gaudence Exavery Mwaikimba kwa penalti dakika ya 58 liliipa
Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Sofapaka ya Kenya kwenye Uwanja wa Nyayo,
Nairobi, Kenya.
Katika
mchezo wake wa kwanza, mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi walifungwa mabao 2-1
na AFC Leopard kwenye Uwanja huo huo wa Nyayo.
Pamoja na
kufungwa na Leopard, Azam watajilaumu wenyewe, kwani walipoteza penalti mbili
kupitia kwa Joackins Atudo na Khamis Mcha ‘Vialli’.
Mabao ya
Leopard katika mchezo huo, yalifungwa na Paul Were na Mike Barasa, wakati la
Azam lilifungwa na Sammih Hajji Nuhu kwa penalti.
Azam
ilimaliza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi
zake 24, nyuma ya vinara Yanga waliomaliza na pointi 29, wakati Simba
walimaliza nafasi ya tatu kwa pointi zao 23.
Pamoja na
Ligi Kuu, Azam pia itacheza Kombe la Shirikisho la Soka Afrika na itaanza na Al
Nasir Juba ya Sudan Kusini mjini Dar es Salaam kati ya Februari 15 na 17 mwaka
huu.
Mechi hiyo
itachezeshwa na marefa wa Kenya, katikati Davies Omweno na atakayesaidiwa na
mwamuzi msaidizi namba moja Peter Keireini, mwamuzi msaidizi namba mbili
Gilbert Cheruiyot wakati mwamuzi wa mezani Anthony Ogwayo.
Kamisaa wa
mechi hiyo atakuwa Hassan Mohamed Mohamud kutoka Somalia, wakati marefa wa
mechi ya marudiano itakayochezwa mjini Juba wiki mbili baada ya mechi ya kwanza
watatoka Rwanda, wakiongozwa na Gervais Munyanziza.
CHANZO:BIN ZUBEIRY