|
Wema Sepetu |
TAMASHA la Usiku wa Matumaini la mwaka 2014 linatarajiwa kufanyika
Agosti 8 na litapambwa na wasanii mbalimbali nyota nchini pamoja na
mwanadada mkali toka Nigeria Yemi Alade anayetamba na wimbo wa 'Johnny'
Kawaida ya tamasha hilo hufanyika Julai 7, lakini kutokana na mwaka huu tarehe hiyo kuangukia kwenye mfungo wa mwezi wa Ramadhani, waandaaji wake wameamua kupeleka hadi Nanenane kwa heshima ya waumini wa Kiislam.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo, Abdallah Mrisho alisema kuwa 'Usiku wa Matumaini' safari hii umeboreshwa kwa upande wa burudani ambapo Mnigeria Yami Alade anatarajia kutua kutumbuiza.
Mrisho alisema kwa upande wa wasanii wa nyumbani 'ujazo'umeongezwa kwa kuwakusanya wakali watupu kuanzia waigizaji, wasanii wa muziki wa kizazi kipya hadi wanamiochezo.
Wasanii wanaoatarajiwa kupanda jukwaani siku hiyo ni pamoja na Ali Kiba, Roma Mkatoliki, Madee, Juma Nature na wengineo kibao akiwamo Wema Sepetu atakayeimba na kucheza nyimbo za 'baby' wake, Diamond Platnumz.
"Upande wa masumbwi kutakuwa na pambano kati ya Mada Maugo na Thiomas Mashali, huku Khaleed Chokoraa aliyehamia kwenye ngumi atazipiga siku hiyo na Saim Memba, " alisema Mrisho kutoka kampuni ya Global Publishers ambao ndiyo waandaaji wa tamasha hilo la kila mwaka.
Aliongeza kuwa, Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge, Mwingulu Nchemba atapanda ulingoni kuzipiga na Dk Hamis Kigwangala, huku wana Bongo Movie JB atazipiga na Cloud 112 na Irene Uwoya atappetana na Jackyline Wiolper.
"Pia kutakuwa na pambano la soka la Bongo Movie dhidi ya wapinzani wao Bongofleva na mechi ya wabunge wa Simba na Yanga ambao safari hii watakuwa na nyota wapya, Yanga wana Ridhiwani Kikwete na Simba wanaye Godfrey Mgimwa," alisema Mrisho.
Mwaka jana pambano la wabunge lilianzishwa na Rais Jakaya Kikwete kabla ya kupokewa na mwamuzi wa zamani wa kimataifa nchini, Othman Kazi 'Collina'.