Omar Matuta 'Wanchope' |
Omar Matuta 'Wanchope' (kati) akishangilia bao lililoipa Mtibwa Ubingwa wa Kombe la Tusker lililofungwa na Rashid Gumbo (kulia), Kushoto yao ni Uhuru Seleman alipokuwa wakiichezea Mtibwa Sugar |
UMAHIRI wake wa kuwasumbua mabeki na kuwatungua makipa hodari uwanjani, ilimfanya Omar Matuta abatizwe jina la 'Wanchope' akifananishwa na nyota wa zamani wa Costa Rica aliyetamba timu za West Ham na Manchester City, Paulo Wanchope.
Kwa wanaomkumbuka Wanchope aliyezichezea pia Derby County na Malaga alikuwa na kipaji kikubwa cha ufungaji kilichomfanya ashikilie nafasi ya pili ya wafungaji bora wa timu yake ya taifa akiifungia mabao 45 katika mechi 73 alizoichezea.
Kama ilivyokuwa kwa Wanchope, ndivyo ilivyokuwa kwa Matuta, ambaye katika timu zote alizozichezea kuanzia zile za Ligi daraja la nne mpaka za Ligi Kuu Tanzania amekuwa akifungia mabao muhimu na kuwa tegemeo.
Nyota huyo aliyewahi kutamba na timu za Ndanda Republic, Vijana Ilala, AFC Arusha kabla ya kudakwa na Mtibwa Sugar tangu mwaka 2004 anakumbukwa na mashabiki nchini kwa mabao yake mawili yaliyoipa nafasi timu ya vijana 'Serengeti Boys' tiketi ya kucheza Fainali za Vijana Afrika za mwaka 2005.
Matuta alifunga katika ushindi wa 3-1 dhidi ya vijana wa Zimbabwe yaliyoifanya ifuzu kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kwenda kushinda 1-0 Harare kwa bao la Nizar Khalfan, hata hivyo waliondolewa fainali na kufungiwa na CAF kwa udanganyifu.
Bao lake la pili katika mechi hiyo, Matuta analitaja kama bao bora kwake kwa namna alivyolifunga, ingawa mechi isiyofutika kichwani mwake ilikuwa ni dhidi ya Ethiopia mwaka 2005 kwa namna walivyofanyiwa vimbwanga na kufungwa kwa hila.
Matuta, ameamua kupumzika soka msimu huu baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Mtibwa klabu anayoitaja kuwa bora kwake na anayeishabikia.
"Nimeamua kupumzika ili nifanye mambo yangu binafsi, ila nikiwahi kumaliza huenda nikarejea tena dimbani kwenye duru la pili la ligi kuu, ingawa sijui itakuwa timu ipi."
Mkali huyo anayefurahia soka kumpa mafanikio kimaisha ikiwamo kujenga nyumba Kigamboni na kumiliki miradi kadhaa ya biashara, anasema hajawahi kuona klabu iliyo makini na inayojali wachezaji wake kama Mtibwa Sugar.
Anasema kama mfumo wa klabu hiyo wa kujali na kuwathamini wachezaji wake ndio unaomfanya aiheshimu Mtibwa iliyomuuguza goti lake kwa miaka miwili kitu alichodai kwa klabu nyingine nchini ni vigumu kufanya jambo hilo hata kama umeisaidia vipi.
OWINO
Matuta asiyekumbuka idadi ya mabao aliyoyafunga kwa kutoweka kumbukumbu, anasema licha ya umahiri wake dimbani, kwa beki wa kimataifa wa Azam, Mganda Joseph Owino ndiye ananayemnyima raha kwa uwezo wake mkubwa kisoka.
"Ni bonge la beki, anacheza kwa akili na ndiye anayenisumbua dimbani tangu nianze kukutana nae katika mechi za kimataifa na zile za Ligi Kuu Tanzania Bara."
Matuta anayependa kula ugali kwa samaki au nyama choma na kunywa vinywaji laini, anasema uwezo wake uwanjani na mwili na nguvu alizojaliwa huwa hapati shida kwa mabeki wenye papara na wanaotumia nguvu, tofauti akutanapo na Owino.
Matuta, ambaye hajaoa ila ana mtoto mmoja aitwae Zuma, anayesoma darasa la tatu katika Shule ya msingi Bunge, anasema soka la Tanzania licha ya kusifiwa kukua ukweli limedumaa kwa muda mrefu kutokana na sababu kadhaa.
Anadai moja ya sababu hizo ni u-Simba na u-Yanga uliowaathiri karibu wadau wote wa soka, kufutwa kwa mfumo wa ligi ya madaraja kama ilivyokuwa zamani na kupewa kisogo kwa michezo ya Yosso.
"Usimba na uyanga na kubadilishwa kwa mfumo wa ligi ya madaraja kama ilivyokuwa zamani ni sababu ya kukwama kwetu sawa na kupuuzwa kwa soka la vijana wenzetu wamekuwa wakilitegemea kupatia mafanikio yao," anasema.
Anasema ni muda wa wadau wa soka kubadilika japo anakiri huenda ikawa ngumu kwa namna ushabiki huo ulivyowathiri watu, pia akiwaomba viongozi wa FA na klabu kuwekeza nguvu kwa vijana sawia na kuwaruhusu kucheza soka nje ya nchi.
MIKWAJU
Matuta, mwenye ndoto za kufika mbali kisoka na kuwa mfanyabiashara mkubwa hapo baadae, anasema wakati akiibukia kwenye soka alipata wakati mgumu kwa baba yake ambaye ni marehemu kwa sasa aliyekuwa hapendi acheze soka badala yake asome.
Anadai baba'ke alilazimika wakati mwingine kumcharaza bakora ili kumzuia kucheza soka na kukazinia masomo, lakini haikusaidia kitu kwani alijikuta akikacha hata masomo ya sekondari ili ajikite kwenye soka.
"Nilikacha masomo ya sekondari pale JItegemee kwa ajili ya soka, wakati mwingine huwa najuta, lakini nafarijika kwa mafanikio niliyonayo," anasema.
Matuta aliyemudu pia nafasi za kiungo, anawashukuru makocha Mussa Stopper, Mzee Panju na Abdallah Kibadeni waliogundua na kukikiendeleza kipaji chake, pia akiwataja wazazi wake na uongozi mzima wa Mtibwa kumsaidia kufika hapo alipo.
Mkali huyo, aliyezaliwa mwaka 1988, akiwa mtoto wa nne kati ya watano wa Mzee Othman Matuta, anadai alivutiwa kisoka na nyota wa zamani wa RTC Kagera, Msabah Salum, licha ya kukiri kukunwa na soka la Ronaldo de Lima na Romario wa Brazil.
Matuta alianza safari yake kisoka tangu akisoma Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, akiichezea timu ya yosso ya Vijana Ilala na baadae kupandishwa timu B na baadae kutua Ndanda kuichezea Ligi Daraja la Nne wilayani Ilala kabla ya kurudishwa Vijana Ilala alioisaidia kuipandisha Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2002.
Bao pekee aliloifungia Vijana dhidi ya Pallsons ya Arusha ndilo lililoipandisha daraja timu hiyo jambo ambalo anadai anajivunia mpaka sasa kabla ya kuichezea AFC Arusha katika michuano ya Nane Bora ya Ligi Kuu na mwaka 2004 kutua Mtibwa aliyoichezea mpaka msimu uliopita akiisaidia kuiwezesha kushika nafasi ya nne katika Ligi Kuu.
Akiwa Mtibwa, Matuta anayechizishwa na rangi zote isipokuwa zenye mng'ao mkali,
alitwaa nao ubingwa wa Kombe la Tusker- 2008, akiwa mmoja wa walioifungia mabao akishirikiana na Uhuru Seleman, Monja Liseki na Rashid Gumbo.
Kuhusu timu ya taifa aliyoichezea kuanzia timu za vijana tangu mwaka 2004, anasema inaweza kufuzu fainali za kimataifa iwapo TFF na wadau wote wataipa maandalizi ya kutosha.
Anasema chini ya kocha Kim Poulsen anamatumaini makubwa licha ya kutaka wadau kumpa nafasi kocha huyo na kuepukwa kubadilishwa kila mara kwa kikosi cha timu hiyo ili kuwafanya wachezaji wazoeane.
Pia anataka timu za taifa za vijana zipewe kipaumbele zikitafutiwa wadhamini wake ili kuwa na maandalizi mazuri, huku akiitaka TFF irejeshe mfumo wa ligi ya madaraja na kuwa wakali kwa wavunjaji wa kanuni za sheria za soka.
Omar Matuta 'Wanchope' akiwa ameshikilia kombe la Tusker la mwaka 2008 alilotwaa na Mtibwa Sugar |
No comments:
Post a Comment