Tayari Yanga imekubaliana na kuingia mkataba wa miaka miwili na Kocha Mholanzi, Johannes Franciscus ‘Hans’ van der Pluijm.
Kazi hiyo ilipangwa kumalizika leo asubuhi na kocha huyo ana mambo mengi sana ya kuburudisha.
Pamoja na kuwa na miaka 64, lakini ni mchapakazi na amekuwa gumzo alipokuwa na kikosi cha Berekum Chelsea ya Ghana.
Akiwa na timu hiyo msimu wa 2012-13, alizitoa jasho na kuzipa wakati mgumu pia timu vigogo kama Al Ahly, TP Mazembe na Zamalek.
Sasa ndiyo wakati wake na Yanga
wamempa kazi ya kuhakikisha kikosi chao kinafanya kazi ya uhakika katika
Ligi ya Mabingwa na mtihani mkubwa ni watakapokutana na Al Ahly kama
watavuka kizingiti laini cha Wacomoro.
Gazeti la Championi lilikuwa chombo cha kwanza nchini cha
habari kuandika kuhusu uamuzi wa Yanga kujitupia kwa van der Pluijm.
Sasa tayari yuko na leo alikuwa apelekwe Zanzibar, lakini huenda akapumzika kujiandaa na safari ya Uturuki.
Pamoja na mambo mengi lakini kocha huyo ana mambo mengi ya kujifunza kutoka kwake.
Utulivu:
Yanga imeamua kufanya kwa utulivu suala la kocha,
awali lilikuwa likipelekwa mbio na kambi ya Uturuki, ikitaka kocha awahi kambi
hiyo.
Lakini sasa uongozi wake umekubali hata kama kocha
mpya hatakwenda Uturuki, lakini inataka ipate ‘mtu’ wa uhakika wa kuziba nafasi
ya Brandts na ambaye atakuwa na uwezo kweli.
Mvuto:
Mvuto wa van der Pluijm kwa Yanga umetokana na
mafanikio yake kwa Berekum Chelsea ambayo ilifanya vizuri katika Ligi ya
Mabingwa msimu uliopita.
Ilikuwa Kundi B na timu za Al Ahly, TP Mazembe na
Zamalek ambao ni vigogo waliowahi kuchukua ubingwa Afrika zaidi ya mara moja,
lakini Berekum Chelsea ikaonyesha inaweza.
Hicho ndiyo kitu cha kwanza kilichoivutia Yanga kwa
kuwa inahitaji kocha wa kuifikisha mbali kwenye Ligi ya Mabingwa ikizingatiwa
katika mechi ya pili tu (kama itawang’oa Wacomoro), itakutana na Al Ahly ambao
ndiyo mabingwa.
Kingine kinachoonyesha kuwavuta Yanga ni umri wa
kocha huyo, miaka 64 ni sawa na mzazi hasa, lakini makocha wengi wenye umri huo
wamekuwa wakali, wanajali zaidi kazi na wasiokuwa na mzaha hata kidogo.
Mazingira:
Kwa mazingira ya nchi za Kiafrika, van Pluijm
hawezi kuwa na hofu hata kidogo kwa kuwa ameishi katika bara hili kwa zaidi ya
miaka 10.
Miaka yote hiyo ameishi nchini Ghana ambako ameoa
mrembo wa Kiafrika wa nchi hiyo.
Uwanja:
Mholanzi huyo ni mtu wa misimamo sana, amewahi
kususia mazoezi kutokana na ubovu wa uwanja. Kama Yanga itaingia mkataba naye,
basi ina wakati mgumu kuhakikisha inamaliza tatizo hilo.
Kabla ya kuondoka kwa Brandts, kilio chake kilikuwa
uwanja usiokuwa na kiwango na magoli madogo, maana yake van Pluijm lazima
atalizungumzia, kama halitatekelezwa kama ilivyokuwa kwa Brandts, basi kuna
tatizo linaweza kutokea.
Misimamo:
Van der Pluijm ni mtu mwenye misimamo kweli, kama
akikubaliana na Yanga na kuanza kazi, maana yake wachezaji wajiandae.
Anatoa ushirikiano mkubwa kwa wachezaji, lakini ni
mkali na asiyehofia jina la staa yeyote.
Vyombo vya habari vya Ghana vilimbandika jina la Kiboko
ya Vigogo kwa sababu mbili, kwanza kuzipa wakati mgumu timu kongwe za Ghana
kama Asante Kotoko lakini kuwaweka benchi wachezaji nyota walioonekana kuvimba
vichwa na timu ya Berekum Chelsea ikaendelea ‘kukamua’.
Wachezaji wageni:
Amekuwa na msimamo wa kutaka wachezaji wa kigeni
wanaoonyesha uwezo mkubwa kuthibitisha tofauti yao na wenyeji.
Hivyo, Emmanuel Okwi, Mbuyu Twite, Hamisi Kiiza na
Didier Kavumbagu wanalazimika kufanya kazi kweli na si kubahatisha, la sivyo
kibarua kitakuwa kigumu ikizingatiwa msimu ujao ni wachezaji watatu tu.
Mfumo:
Uchezaji wa timu anazozifundisha ni kasi sana, anataka
washambulie pamoja na kurudi pamoja, lakini amekuwa akisisitiza kikosi chenye
walinzi warefu au wenye uwezo mkubwa wa kupiga vichwa.
Mchezaji akiwa mvivu, huenda akawa na wakati mgumu
wa kupata namba katika kikosi chake.
Ndiyo maana mazoezi yake ya mwanzo wa msimu kama
timu ataanza nayo, yanakuwa makali sana kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa
fiti kweli.
Van Nistelrooy:
Alimuibua mshambuliaji nyota wa
Uholanzi, Ruud van Nistelrooy akiwa na umri wa miaka 17 tu na kumpa nafasi ya
kucheza katika kikosi cha FC Den Bosch cha nchini kwao Uholanzi.
Van Pluijm aliitumikia FC Den Bosch kwa
miaka 28 akiwa mchezaji na baadaye kocha. Akiwa kipa alicheza mechi 338 kwa
misimu 18 kabla ya maumivu ya goti kumlazimisha kupumzika soka.
Aprili 1995, aliingia mkataba wa miaka
miwili kuinoa SBV Excelsior hadi Desemba kabla ya kumuachia nafasi hiyo
msaidizi wake John Metgod.
Mwaka 1999 alitua nchini Ghana na
kujiunga na Ashanti Gold SC na kusaini mkataba wa mwaka, baadaye alitua nchini
Ethiopia na kuanza kuinoa Saint George.
Sasa amekuwa akifanya kazi ya kuinoa
timu ya vijana ya Feyenoord Ghana inayopata msaada kutoka katika klabu ya
Feyenoord ya Rotterdam nchini Uholanzi.
Ngumi mkononi:
Oktoba, mwaka jana, akiwa
na kikosi cha mabingwa wa Ghana wakati huo cha Medeama Sporting Club, van Der
Pluijm alisaini mkataba wa miaka miwili, lakini hakudumu hata robo ya mkataba
huo.
Kwani siku chache baada
ya Makamu wa Rais wa Madeama, Albert Commey, kumtangaza kuwa kocha mkuu, akiwa
ameiongoza timu hiyo katika mechi saba tu, van Der Pluijm alitangaza kuachia
ngazi.
Uongozi wa Madeama ulikubali na kuficha, lakini
ukweli baadaye uligundulika kuwa kocha huyo Mholanzi alizozana na msaidizi wake
akavurumisha ngumi.
Katika mahojiano yake na mtandao wa Caf na vyombo
vingine vya habari, Mholanzi huyo amekuwa akisisitiza kutotaka kulizungumzia
suala hilo kwa madai ni sawa na kuongeza maadui bila sababu za msingi.
Kutokana na hali hiyo, alionyesha kuchukizwa na
mwenendo wa mambo kwa kuwa kila alichokuwa akieleza kibadilishwe hakikufanyika,
pia msaidizi wake pamoja na kwamba alipendekeza kuchukuliwa kwa Mholanzi huyo
kama bosi wake, alikuwa mbeya sana.
Pamoja na hivyo, kikosi chake cha Madeama
hakikufanya vizuri kabisa, kwani alianza na mechi ya Kombe la Super Cup dhidi
ya Asante Kotoko na kuchapwa bao 3-0.
Aliiongoza timu kwa jumla ya mechi saba, badala ya kubeba jumla ya pointi 21,
timu yake ilipata pointi nane tu!
Katika mechi hizo saba, kikosi chake kilishinda mechi moja tu, sare
tano na kupoteza mechi moja.
Wakati anaondoka alikiacha kikiwa katika nafasi ya tisa kwenye ligi
hiyo kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya vinara wakati huo, Asante Kotoko.
Credit:SALEH ALLY BLOG