STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 12, 2013

Said Ndemla: Kinda la Simba lililoifunika Yanga Okt 20

 
YANGA ilipokuwa ikiongoza kwa mabao 3-0 katika kipindi cha kwanza cha pambano lao dhidi ya watani zao, Simba lililochezwa Oktoba 20 mwaka huu hakuna aliyekuwa akiamini kama mabao hayo yangerudishwa na Simba.
Hii ni kwa sababu Yanga ilitawala mchezo huo na kuifunika kabisa Simba na hasa 'dimba' la kati na kuifanya Simba ya King Abdallah KIbadeni kuonekana siyo lolote wala chochote mbele ya vijana wa Jangwani wa Ernie Brandts.
Hata hivyo badiliko lililofanywa na Kibadeni kwa kumtoa Abdulhalim Humud 'Gaucho' na Haruna Chanongo na kuwaingiza William Lucian 'Gallas' na Said Ndemla, lilileta maajabu ya aina yake kwenye uwanja wa Taifa.
Simba iliwafunika Yanga na kurejesha mabao yote matatu na lau kama dakika zingeongeshwa zaidi katika pambano hilo ni dhahiri Simba ingeibuka na ushindi kwa vile ilionekana kupata uhai na kuwakimbiza Yanga watakavyo.

Unajua kwa nini?
Moja ya 'mashine' zilizoingizwa, iliwafunika nyota wote wa Yanga waliotawala awali  dimba la kati, akikaba vilivyo na kusukuma mashambulizi ya Simba langoni mwa wapinzani wao kiasi mabeki ya Yanga kutamani mpira uishe.
Said Khamis Ndemla ndiye aliyekuwa akifanya kazi hiyo na kuwafanya wale wote walioikatia tamaa Simba kupata uhai na hasa Simba ilipoanza kurudisha bao moja baada ya jingine na hatimaye kusawazisha bao na kuwa mabao 3-3.
Ndemla, chupukizi ambaye hilo lilikuwa pambano lake la kwanza kubwa kwa wapinzani wa jadi Simba na Yanga, alifanya kazi ambayo ilithibitisha kuwa Tanzania imejaliwa hazina kubwa ya vipaji vya soka iwapo vikitumiwa vyema.
Hata mwenyewe anakiri itamchukua muda mrefu kulisahau pambano hilo kwa namna alivyocheza kwa jihad na kusaidiana na wenzake kulazimisha sare ya mabao 3-3 wakati tayari Simba ilionekana imekubali kuelekea 'Kibla'.


"Siwezi kulisahau pambano la Simba na Yanga kwa sababu lilikuwa pambano langu la kwanza kubwa na gumu lenye ushindani na la kwanza kwangu kati ya Simba na Yanga na bahati nzuri niling'ara," anasema.
Ndemla, anayevutiwa na soka la kiungo wa Ujerumani anayeichezea klabu ya Bayern Munich, Bastian Schweinsteiger anasema anaamini kujiamini na kipaji alichojaliwa kilimbeba na kumfanya awe anafanya mambo makubwa dimbani.
Mkali huyo ambaye licha ya kumudu nafasi ya kiungo pia anamudu kucheza kama winga wa kulia na mshambuliaji namba 10, anasema anashukuru Mungu kwa kipaji alichonacho na kuota kuja kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.
"Licha ya kufurahia kuichezea Simba, lakini ndoto zangu ni kuja kucheza nje ya nchi na hasa bara la Ulaya, naamini ninao uwezo mkubwa," anasema.
 

DALILI NJEMA
Ndemla aliyezaliwa Machi 11, 1994 jijini Dar es Salaam akiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto wanne wa familia ya Mzee Khamis Ndemla, anasema licha ya kucheza kitambo kifupi, lakini soka limempa mafanikio ya kujivunia.
Anasema ukiacha mambo binafsi ambayo hakupenda kuyaanika gazetini, lakini tayari ameshanyakua mataji na medali kadhaa katika mchezo huo.
"Kwa kipindi kifupi tu nimeshanyakua vikombe vitatu na medali nikiwa na Simba B. Nimetwaa nao ubingwa wa Uhai, Kinesi na ule wa ABC Super8," anasema.
Anasema mafanikio hayo ni dalili njema kwake katika usakataji wake wa soka huku akisisitiza kuwa hajaridhika wala kuvimba kichwa na badala yake atazidisha juhudi ili aweze kufika mbali zaidi.
Kabla ya Simba kumuona, Ndemla aling'ara katika soka akisoma Shule ya Msingi Uzuri na Makongo, huku chandimu alicheza Soccer Rangers iliyokuza kipaji chake kabla ya kunyakuliwa na Messina Linea na baadaye Red Coast.
"Nikiwa naichezea Red Coast kwenye michuano ya Kinesi, ndipo Simba B waliponiona na kunishawishi kujiunga nayo nikianzia katika kikosi hicho kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa," anasema.
Ndemla, anasema Simba ilivutiwa naye hasa baada ya kuifungia timu yake ya Red Coast mabao 2-0 dhidi yao na kumsajili kikosi chake cha vijana alichoichezea msimu miwili kabla ya mwaka huu kupandishwa timu kubwa.
Mchezaji huyo anayekiri kama siyo soka anmgependa kuwa mfanyabiashara anasema hakuna tukio la furaha kwake kama siku Simba iliponyakua ubingwa wa Super8 na kulizwa na kifo cha baba yake mzazi.
"Kwa kweli huzuni yangu ni kumpoteza baba yangu mzazi na furaha ni siku nilipotwaa ubingwa wa Super8 kwa kuwanyuka Mtibwa Sugar," anasema.

VIJANA
Ndemla anayependa kula kunywa ugali kwa samaki na mboga za majani na kunywa juisi ya matunda, anasema soka la Tanzania linazidi kupanda juu na kutaka vijana wapewe zaidi nafasi akiamini watalikomboa taifa kimataifa.
Anasema vijana wakipewa nafasi itawasaidia kujiamini na kupigana kwa mafanikio ya taifa kama mataifa mengine yaliyosonga mbele na kutamba katika soka la kimataifa kwa kutegemea nguvu ya vijana wenye vipaji.
Shabiki huyo wa Chelsea, hata hivyo anawakumbusha wachezaji wenzake kuzingatia nidhamu, kujituma na kuwasikiliza makocha wao iwapo wanataka kufika mbali na kulingana na nyota wanaowashabikia wanaotamba duniani.
"Bila nidhamu, kujituma na kuwaizngatia makocha ni vigumu kufikia kwenye malengo, pia ikumbukwe soka la sasa ni ajira," anasema.
Ndemla anayependa kutumia muda wake wa ziada kupumzika nyumbani na kusikiliza muziki akimzimia Diamond, anasema hakuna mchezaji yeyote nchini anayemnyima raha awapo dimbani kwa vile anajiamini.
Kiungo anayefurahia tukio la kwenda kujifunza soka nchini Ujerumani akiwa na kituo cha TSS cha Mwanza anasema anawashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono katika kucheza kwake soka na hasa mama yake.
Pia anawamwagia sifa na pongezi makocha wake wote waliomsaidia katika kukuza soka lake tangu utotoni mpaka sasa hasa Ramadhani Kipira, Max, Suleiman Matola, Ngongo na Abdul Mashine.

Young Stars, Taifa Stars kumenyana kesho Karume



TIMU za Taifa za Future Taifa Stars na Taifa Stars zinacheza kesho (Novemba 13 mwaka huu). Mechi hiyo ya kirafiki itafanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mechi hiyo ni maalumu kwa Benchi la Ufundi la Taifa Stars linaloongozwa na Kim Poulsen kuangalia wachezaji kumi kutoka Future Taifa Stars watakaoongezwa katika Taifa Stars tayari kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa Novemba 19 mwaka huu jijini Arusha.

Watazamaji 300 tu wataruhusiwa kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 5,000.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeingia kambini leo (Novemba 12 mwaka huu). Miongoni mwa wachezaji wanaotarajia kuripoti ni kipa Ivo Mapunda wa Gor Mahia.

Bodi ya Ligi yafungia viwanja 7 yaadhibu wachezaji, klabu



BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) imefungia viwanja saba vilivyokuwa vikitumiwa na timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) hadi vitakapofanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji ya mechi za mpira wa miguu.
Uamuzi huo umefikiwa na TPL Board katika kikao chake cha kwanza kilichofanyika juzi (Novemba 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine kilipitia ripoti za mechi za VPL na FDL katika mzunguko wa kwanza.
Viwanja vilivyofungiwa na marekebisho yanayotakiwa kufanyika kwanza ili viruhusiwe kutumika tena ni Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba (majukwaa yake yamechakaa, hivyo kuhatarisha usalama wa watazamaji), na Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga (vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo (dressing rooms) havina hadhi).

Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya (sehemu ya kuchezea- pitch ni mbovu), Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha (pitch ni mbovu), Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi (vyumba vya kubadilishia kutumika kwa ajili ya shule ya awali), Uwanja wa Majimaji mjini Songea (pitch ni mbovu) na Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro (pitch ni mbovu).
Klabu ambazo timu zake zinatumia viwanja hivyo zimeshaarifiwa rasmi juu ya uamuzi huo ambapo ama vinatakiwa kuwasiliana na wamiliki wa viwanja hivyo ili wafanye marekebisho au kutafuta viwanja vingine vya kuchezea mechi zao.
Kwa upande wa ripoti za mechi za VPL; Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 na kupewa onyo kali kwa timu yake ya U20 kutocheza mechi ya utangulizi walipocheza na Yanga. Pia wanatakiwa kulipa gharama za uharibifu baada ya washabiki wao kuvunja kioo cha basi la Yanga baada ya gharama hizo kuthibitishwa na Bodi ya Ligi.
Pia Mbeya City imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa washabiki wake kushambulia basi la wachezaji wa Tanzania Prisons baada ya mechi dhidi yao, na kulipa gharama za uharibifu baada ya kuthibitisha na Bodi ya Ligi.
Coastal Union imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake ilipocheza na Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambapo mwamuzi msaidizi Hassan Zani alishambuliwa kwa mawe na kujeruhiwa mkononi na kichwa, tukio lililosababisha mchezo kusimama kwa dakika tatu.
Beki wa Coastal Union, Hamad Khamis wa Coastal Union amepigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga kichwa kwa makusudi Kipre Tchetche wa Azam. Kitendo hicho kilisababisha refa amtoe nje kwa kadi nyekundu, hivyo atakosa mechi tatu zinazofuata za timu yake.
Mchezaji Cosmas Lewis wa Ruvu Shooting alifanya kitendo cha utovu wa nidhamu kwa kupiga kelele wakati mgeni rasmi akisalimia timu na kukataa kupeana mkono na kamishna kwenye mechi dhidi ya Rhino Rangers, hivyo amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000.
Mtunza vifaa (Kit Man) wa JKT Ruvu, Selemani Oga aliondolewa kwenye benchi la ufundi wakati wa mechi yao dhidi ya Mbeya City kwa kosa la kutoa lugha chafu kwa refa, hivyo suala lake litapelekwa katika Kamati ya Maadili.
Kocha Msaidizi wa Oljoro JKT, Fikiri Elias amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa kumshambulia kwa matusi refa wakati wa mechi yao dhidi ya Ashanti United. Naye mtunza vifaa wa timu hiyo Elas Justin amepelekwa Kamati ya Maadili kwa kumshambulia refa kwa matusi ya nguoni.
Simba wamepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar.
Katika FDL, mchezaji Ally Mtoni wa Villa Squad amepigwa faini y ash. 200,000 na kufungiwa mechi tano. Kosa lake ni kujisaidia haja ndogo golini wakti wa mechi dhidi ya Ndanda FC iliyochezwa mjini Mtwara.
Kamishna Paul Opiyo wa mechi ya FDL kati ya Villa Squad na Transit Camp kwa kutokuwa makini. Katika ripoti yake ameeleza kuwa Transit Camp ilichelewa kufika uwanjani, lakini hakusema ilichelewa kwa muda gani.
Kocha wa Polisi Dar es Salaam, Ngelo Nyanjabha na Meneja wa timu hiyo Mrimi Masi wamepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi tatu kila mmoja kwa kuongoza kundi la washabiki kumvamia refa wa mechi yao dhidi ya Villa Squad iliyochezwa Dar es Salaam.
Pia Bodi ya Ligi imeagiza Polisi waandikiwe barua ya onyo kwa vile wakati waamuzi wanapigwa walikuwepo lakini hawakutoa msaada kwa wakati.
Kocha wa Friends Rangers, Kheri Mzozo amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kosa la kumtukana refa na kutishia kuhamamisha washabiki waingie uwanjani kufanya fujo kwenye mechi dhidi ya Villa Squad.
Naye Kocha msaidizi wa timu ya Transit Camp, Haji Amiri amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi sita kwa kutoa lugha ya matusi kwa mwamuzi wa akida wakati wa mechi dhidi ya Friends Rangers.
Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa kanuni. Pia Bodi ya Ligi imeahirisha kufanya uamuzi wa mechi kati ya Stand United na Kanembwa JKT iliyochezwa Uwanja wa Kambarage ili kukusanya taarifa zaidi. Mechi hiyo haikumalizika. Bodi ya Ligi itakutana tena Jumapili (Novemba 17 mwaka huu).

TANZIA! MASKINI DK MVUNGI HATUNAYE

Dk Mvungi enzi za uhai wake
Dk Mvungi alipokuwa akiipigania roho yake baada ya kujeruhiwa na majambazi
ALIYEKUWA Mjumbe wa Tume ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi amefariki dunia mchana wa leo.
Taarifa zilizotufikia kutoka Milpark Hospitali, zinasema kuwa Dk Mvungi alifariki majira ya saa 9 Alasiri alipokuwa akitibiwa baada ya kupigwa mapanga na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi waliomvamia nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Kinondoni.
Kabla ya kupelekwa Afrika Kusini, Dk Mvungi alikuwa akitibiwa katika hospitali ya Moi Muhimbili kabla ya kukimbizwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi.
Taarifa za kifo chake zimethibitishwa na Mwenyekiti Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Dk Mvungi ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alijeruhiwa  Novemba  3, mwaka huu.
MICHARAZO inaungana na familia, ndugu na jamaa wa marehemu Dk Mvungi katikamkipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito na kuwataka wawe na subira kwa kutambua kuwa 'KILA NAFSI ITAONJA MAUTI' Dk Mvungi katangulia sisi tuy nyuma yake. Mungu aiweke mahali pema roho ya marehemu.

Ivo Mapunda, Waziri Salum watemwa Stars, Dida aula

Ivo Mapunda
WACHEZAJI watatu wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars), akiwamo kipa wa Gor Mahia, Ivo Mapunda, hawajaripoti katika kambi ya timu hiyo inayojiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa inayotarajiwa kufanyika Novemba 19 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Kutokana na Mapunda kutofika kwenye kambi hiyo kama ilivyopangwa, tayari kipa wa Yanga, Deogratius Munishi 'Dida', ameitwa kujaza nafasi hiyo.
Meneja wa Taifa Stars, Tasso Mukebezi, alisema mpaka jana mchana hakuwa na taarifa zozote kuhusu Mapunda na kuwataja wachezaji wengine ambao hawajajiunga na kambi hiyo kuwa ni Wazir Salum kutoka Azam na Miraji Athumani wa Simba.
Mukebezi alisema kikosi hicho kinakabiliwa na majeruhi wawili ambao ni David Luhende anayeichezea Yanga na Khamis Mcha wa Azam.
"Wachezaji wengine walioitwa katika timu hiyo maarufu kama Future Young Taifa Stars, wako salama na kesho (leo) tutawapokea wale wengine wa Taifa Stars kwa ajili ya kujiandaa na mechi iliyoko kwenye Kalenda ya Fifa," aliongeza meneja huyo.
Alisema kesho kutakuwa na mechi ya kirafiki kati ya timu ya Yosso dhidi ya Taifa Stars ambayo itasaidia kupata kikosi kamili kuelekea kwenye michuano ya Kombe la Chalenji itakayofanyika Nairobi, Kenya kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12, mwaka huu.
Wachezaji wa Stars wanaotarajiwa kuingia kambini leo ni Mwadini Ally, Ally Mustapha 'Barthez', Aggrey Moris, Shomary Kapombe, Nadir Haroub 'Cannavaro', Erasto Nyoni, Vicent Barnabas, Salum Aboubakar 'Sure Boy', Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Athumani Iddi 'Chuji', Mrisho Ngasa, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na John Bocco.