|
Picha haihusiani na stori hapo chini |
SIKU chache baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
kuwakamata askari 16 wakituhumiwa kujihusisha na biashara ya magendo,
askari wengine wawili wa jeshi hilo wamekamatwa mkoani Kilimanjaro
wakiwa na shehena kubwa ya bangi wakiisafrisha kwenda nchini Kenya.
Askari hao walikamatwa Mei 19 mwaka huu saa nne usiku eneo la
Kilemapofu, Wilaya ya Moshi Vijijini wakiwa na magunia 18 ya bangi
ambayo walikuwa wameyapakia kwenye gari la Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU) mkoani Arusha aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba PT
2025.
Akithibitisha kukamatwa kwa askari hao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kilimanjaro, Robert Boaz alisema askari hao walikuwa wakipeleka bangi
hiyo Wilaya ya Rombo kwa mfanyabiashra mmoja ambaye hakutaka kumtaja
jina lake.
Kamanda Boaz aliwataja askari waliokamatwa na wanashikiliwa kwenye kituo
kikuu cha polisi katika mji mdogo wa Himo kuwa ni F.1734 Koplo Edward
(dereva) wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) mkoani Arusha na G.2434
Konstebo George wa kituo cha polisi Ngarenanyuki Wilaya ya Arumeru.
Alibainisha kuwa kukamatwa kwa askari hao kunatokana na operesheni ya
kukabiliana na dawa za kulevya inayofanywa na polisi katika mikoa ya
Arusha na Kilimanjaro.
Alisema operesheni hiyo imefanyika kikamilifu katika Mkoa wa Arusha
uliokuwa ukitumika kupitishia bidhaa hiyo, na sasa wahusika wameamua
kuutumia Mkoa wa Kilimanjaro.
“Baada ya kuwahoji askari wale, walidai kuwa walikodishwa na
mfanyabiashara huyo kuipeleka bangi hiyo wilayani Rombo tayari kwa
kusafirishwa kwenda nchini Kenya ambako inaaminika kuna soko kubwa,”
alisema.
Kamanda Boaz alisema hivi sasa polisi wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na
wenzao wa Arusha wanafanya uchunguzi kubaini mtandao wa askari hao
unaojihusisha na vitendo haramu.
Aliongeza kuwa hatua inayofuata kwa askari hao ni kufunguliwa mashtaka
ya kijeshi na iwapo watakutwa na hatia watafukuzwa kazi kisha
watafikishwa katika mahakama za kiraia.
Kamanda Boaz alibainisha kuwa kwa kawaida askari wanapotoka mkoa mmoja
kwenda mwingine hupatiwa kibali maalumu cha kusafiria (Movement Order).
Alisema kibali hicho husaini kila mkoa ambao askari husika hupita, lakini waliokamatwa na bangi hawakuwa nacho.
Kamanda Boaz alibanisha kuwa kwa hali ilivyo askari hao waliondoka na
gari la mkuu wa FFU bila kumpa taarifa wala kupata kibali chake.
Tanzania Daima limedokezwa kuwa askari hao wamekuwa wakisafirisha bangi
hiyo mara kwa mara kupitia mji huo wa Himo bila kukamatwa kutokana na
gari lao kuwa na namba za kijeshi, hivyo kuwa vigumu kwa askari wenzao
kuwatilia shaka.
Taarifa zaidi zimedai kuwa kukamatwa kwa askari hao kulitokana na gari
lao kupata hitilafu katika eneo hilo la Kilemapofu, na ndipo askari wa
doria walipofika kwa lengo la kutoa msaada kwa wenzao, lakini ghafla
walisikia harufu ya bangi.
Mtoa taarifa aliyezungumza kwa sharti la kutotaka jina lake litajwe,
alisema baada ya askari hao kusikia harufu ya bangi waliwaarifu viongozi
wao waliowaamrisha walifanyie upekuzi gari hilo sambamba na kuwaweka
chini ya ulinzi askari wote waliokuwamo.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa katika upekuzi huo walibaini uwepo wa magunia 18 ya bangi yaliyolengwa kupelekwa nchini Kenya.
Kilibainisha kuwa baada askari hao kukamatwa, mmoja wao alisikika akiongea na mtu aliyemuita bosi kumuarifu kukamatwa kwao.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa bosi aliyearifiwa tukio hilo alihoji imekuwaje wakakamatwa kizembe namna hiyo.
Kilidokeza kuwa bosi huyo alimhoji aliyempigia simu kuwa wamebaki na shilingi ngapi ili wawape rushwa polisi waliowakamata.
“Bosi aliambiwa kuna laki tano, naye akawaambia wawape fedha hizo zote,
lakini kwa bahati mbaya hawakufanikiwa,” kilisema chanzo chetu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, hakukiri wala kukanusha kuwapo kwa taarifa za kukamatwa kwa askari wake.
Tanzania Daima lilitaka kujua Jeshi la Polisi mkoani Arusha limechukua
hatua gani dhidi ya askari hao ambapo kamanda Sabas alisema hayupo
katika nafasi nzuri ya kulizungumzia jambo hilo kwa kuwa yupo
hospitalini.
Credit:Tanzania Daima