STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, November 26, 2013

Uhai Cup yahami Chamazi, Usajili wafafanuliwa

Michuano ya Kombe la Uhai imeingia hatua ya robo fainali ambapo sasa mechi zinachezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Uamuzi wa kuhamisha mechi hizo kutoka viwanja vya Karume na DUCE ni kuziwezesha zote kuoneshwa moja kwa moja (live) na Azam Tv.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunaomba radhi kwa washabiki ambao watakuwa wameathirika kutokana na uamuzi huo.
USAJILI DIRISHA DOGO KUFUNGWA DESEMBA 15
Wakati dirisha dogo la usajili linafungwa Desemba 15 mwaka huu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tunazikumbusha klabu zote kuheshimu kanuni na kuzingatia muda uliowekwa.
Pia tunakumbusha kuwa kupeleka mchezaji kwa mkopo katika klabu nyingine hakutoi nafasi ya kusajili mchezaji mpya. Kama klabu ilisaji wachezaji 30 maana yake ni kuwa haina nafasi ya kuongeza wachezaji.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni (foreign players), tunakumbusha kuwa kuanzia msimu ujao 2014/2015 watakuwa watatu tu badala ya watano wa sasa.
Kuhusu usajili wa wachezaji kutoka nje mpaka sasa hakuna hata klabu moja imeshaingia kwenye TMS kuomba uhamisho. Itakapofika Desemba 15, system ya TMS itafunga.
RAMBIRAMBI MSIMBA WA ANDREW KILOYI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mwamuzi wa zamani wa FIFA, Andrew Kiloyi kilichotokea mjini Iringa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mahano, Kiloyi alifariki dunia juzi (Novemba 24 mwaka huu) kutoka na ugonjwa wa fangasi ya ubongo, na marehemu amesafirishwa kwenda kwao Kigoma ambapo atazikwa.
Kiloyi alizaliwa Mei 5, 1968. Alijiunga na uamuzi wa mpira wa miguu mwaka 1988 ambapo alipata beji ya FIFA mwaka 2001 akiwa mwamuzi msaidizi. Alistaafu uamuzi mwaka 2009, na hadi anafariki akiwa mjumbe wa Kamati ya Waamuzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IREFA).
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pole kwa familia ya marehemu, IREFA, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na msiba huo na kuwataka kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hicho cha majonzi. Mungu aiweka mahali pema roho ya marehemu Kiloyi.

Wanne washinda Uchaguzi CECAFA

Tanzania FA President Leodegar Tenga: I do not intend to run for re-election on February 24
Rais wa CECAFA, Leodger Tenga
BARAZA la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limepata wajumbe wapya wa wanne wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi uliofanya leo (Novemba 26 mwaka huu) hoteli ya Hillpark jijini Nairobi.
Uchaguzi huo ulifuatiwa na Mkutano Mkuu wa CECAFA ulioongozwa na Mwenyekiti wake Leodegar Tenga na kuhudhuriwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kalusha Bwalya na ofisa wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Emmanuel Maradas.
Rais wa zamani wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa ndiye aliyeongoza katika uchaguzi huo ambapo wasimamizi walikuwa Bwalya na Maradas.
Mulindwa alipata kura zote 12 na kufuatiwa na Tariq Atta wa Sudan (10), Abdigaani Saeb Arab wa Somalia (9) na Raoul Gisanura wa Rwanda (8). Atta, Arab na Gisanura walikuwa wakitetea nafasi zao.
Walioshindwa ni Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Sudan Kusini (SSFA), Alei Chabor aliyepata kura tano na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya aliyepata kura nne.

Kili Stars yatua salama Nai, Znz Heroes kuanza kibarua kesho

Timu ya Kilimajaro Stars

TIMU ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) imewasili salama Nairobi, Kenya tayari kwa mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoanza kesho (Novemba 27 mwaka huu) katika Uwanja wa Nyayo.
Kilimanjaro Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliwasili saa 3 usiku kwa ndege ya RwandAir, na imefikia katika hoteli ya Sandton iliyoko katikati ya Jiji la Nairobi.
Kwa mujibu wa programu ya Kocha Mkuu Kim Poulsen, Kilimanjaro Stars leo (Novemba 26 mwaka huu) ni mapumziko ambapo kesho itafanya mazoezi kujiandaa kwa mechi yake ya kwanza dhidi ya Zambia itakayochezwa Novemba 28 mwaka huu Uwanja wa Machakos.

Mechi ya Tanzanite sasa kuchezwa Dar

Mashujaa wa Tanzania, Tanzanite
MECHI ya kwanza ya raundi ya michuano ya Kombe la Dunia, Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Tanzanite) na Afrika Kusini iliyokuwa ichezwe Mwanza sasa itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya ukaguzi uliofanywa na maofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imebainika uwanja huo unatakiwa ufanyiwe marekebisho ambayo hayawezi kuwahi Desemba 7 mwaka huu, siku ambayo ndiyo mechi hiyo inatakiwa kuchezwa.
Vyumba vya wachezaji vya uwanja huo ndilo eneo ambalo linatakiwa  kufanyiwa marekebisho makubwa.

Zitto Kabwe, Dk Kitila wana mashtaka 11 ya kujibu CHADEMA

Zitto Kabwe
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo kimesema kimewaandikia barua aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zitto Kabwe na Mjumbe wa kamati Kuu Dk Kitila Mkumbo ambazo wanapaswa kujieleza kwa siku kumi na moja, kisha watapata fursa kujieleza mbele ya kamati kuu maalumu kwanini wasifukuzwe Chama.
Akizungumza katika makao makuu ya chama hicho, Mkurugenzi wa habari na Uenezi John Mnyika, alisema barua hizo zipo tayari na wahusika watapatiwa wakati wowote kuanzia leo Novemba 26.

Mnyika alikuwa akitoa taarifa ya kikao cha Utekelezaji cha sekretarieti ya chama hicho iliyoketi baada ya mkutano wa kamati kuu iliyoketi tarehe 20 – 22 Novemba mwaka huu.

Ni katika Mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho, Tundu Lissu alisema kuwa mkutano uliofanywa na Zitto na Dk Kitila mbele ya waandishi hawajazungumzia tuhuma zinazowakabili, badala yake walichofanya ni  kujitungia tuhuma ambazo kimsingi sizo zilizo wavua nafasi zao.

Lissu alisema, Zitto na Dk Kitila hawakusimamishwa nyadhifa zao kwa masuala ya PAC, Uchaguzi wa mwaka 2010, wala kutoshiriki kwenye operesheni za chama au sababu zingine, na walitaja  hizo sababu ili kupotosha tuhuma zinazowakabili kwa jamii.

“Walichokifanya kina Zitto na Kitilla ni "Diversion" (kubadili mwelekeo) wa  mashtaka yao yanatokana na waraka wa kihaini wa mabadiliko ambao ni kinyume na katiba, kanuni na maadili na itifaki ya Chama.  anawaambia waandishi, "wamevuliwa nafasi zao na kamati kuu kwa sababu ya waraka wenye nia ovu" alisema Lissu.

Aliongeza kuwa Chadema kina mwongozo wa uchaguzi uliopitishwa na kamati kuu, Zitto na Kitila wanaufahamu ingawa haijulikani ni kwanini wao walienda kinyume na mambo yanayojadiliwa katika kamati kuuu

Aidha Lissu alieleza kuwa Dk Kitilla anapotosha umma na wanachaka kwa kauli yake kuwa kamati kuu haina mamlaka ya kumvua yeye nafasi yake ya ujumbe wa kamati kuu maana amechaguliwa na baraza kuu, alimtaka Kitila na Zitto waangalie vema katiba ya chama hasa majukumu ya kamati kuu, pale yanaporuhusu Mwanachama yeyote kusimamishwa au kufutiwa uanachama haraka kama kamati kuu itaona kuna umuhimu wa kufanya vile.

Kigaila alisema, Kamati kuu iliyoketi Novemba 20-22/2013 ilipitisha ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama kama ifuatavyo.

22/11/2013-14/12/2013 ni kukamilisha zoezi la usajili wa  wanachama, 15 Desemba hadi 15 Januari uchaguzi ngazi za vitongoji, 16 januari 30 Januari 2014 Rufaa naukaguzi, ambapo tarehe 01 Februari hadi 15 Februari ni uchaguzi wa matawi.

Chadema pia ilisema 16 Februari hadi 29 mwezi huo huo ni kusikiliza rufaa na ukaguzi, ambapo uchaguzi wa majimbo utaanza rasmi 1 Aprili hadi Aprili 10, huku uchaguzi ngazi ya Wilaya ukitarajiwa kufanyika 25 Aprili hadi mei 5 mwaka 2014, na ngazi ya Mikoa ni 20 Mei hadi 25 Mei.

Huku uchaguzi wa kanda ukitarajiwa kufanyika Julai 9, na haada ya hapo Julai 23 hadi Julai 30 utakuwa ndio muda wa uchaguzi ngazi ya Taifa, utakaoanza na baraza la Wazee, Baraza la Vijana, Baraza la Wanawake kisha uchaguzi wa ndaniya chama.

Bw' Misosi sasa avuta raha

Joseph Rushahu 'Bwana Misosi
NYOTA wa zamani wa muziki wa kizazi kipya nchini, Joseph Rushahu a.k.a 'Bwana Misosi', ameamua kuvunja ukimya kwa kupakua wimbo mpya uitwao 'Vuta Raha'.
Akizungumza na MICHARAZO, Misosi alisema wimbo huo ameurekodia katika studio za Plexity Records chini ya maprodyuza Zest ba Fide Touch.
Misosi alisema tayari wimbo huo ameuachia mwishoni mwa wiki na tayari umeanza kurushwa hewani kupitia vituo vya redio, mitandao ya kijamii na kupigwa katika kumbi za disko.
Msanii huyo aliyewahi kutamba nchini kwa vibao vikali kama 'Nitoke Vipi', 'Mabinti wa Kitanga' na 'Mungu Yupo Bize', alisema wimbo huo mpya ni kati ya kazi zake mpya alizopanga kuzitoa kabla ya kufungia mwaka 2013.
Misosi ambaye mapema mwaka huu alijitosa kwenye masuala ya filamu, alisema kwa sasa anajipanga ili kutengeneza video ya wimbo huo kabla ya kuachia kazi nyingine za kufungia mwaka na kuukaribisha mwaka mpya.
"Baada ya kimya kirefu nimeachia wimbo mpya uitwao 'Vuta Raha' nilioimba na mwanadada aitwaye Namcy na tayari umeshaanza kuwa gumzo katika vituo vya redio na kumbi za disko, nafurahi ulivyopokelewa," alisema Misosi.

Kijogoo wa Jakaya agtaka wasanii wenzake kubadilika wathaminike


MUIGIZAJI anayetamba na kundi la kundi la Jakaya Arts, Boniface Gilliard 'Kijogoo', amewataka wasanii wenzake kutambua nafasi zao ndani ya jamii na kuepuka kujihusisha na mambo ya hovyo kwa madai yanachangia hata kuwanyima tenda za matangazo ya biashara.
Kijogoo anayefahamika pia kama 'Kikoti', alisema kujihisha na skendo mara kwa mara mbali na kuonyesha ujinga walionao baadhi ya wasanii, lakini pia inawanyima nafasi ya kulamba 'tenda' za matangazo ya biashara kama wanavyoneemeka wasanii wenzao wa kimataifa.
"Wasanii lazima wabadilike, watambue nafasi zao mbele ya jamii. Skendo zimekuwa zikichafua sifa ya tasnia na wasanii kwa ujumla na hii inatufanya tuendelee kudharauliwa na kupuuzwa kwa sababu ya wachache wasiojitambua na wanaoendekeza ujinga," alisema Kijogoo.
Kijogoo alijipatia umaarufu mkubwa kwa uigizaji wake kupitia michezo kama 'Riziki', 'Barafu la Moyo', 'Mapito', 'Donda la Kichwa', 'Ulimbo' na 'Chekecheo', alisema ni lazima wasanii wajue wao ni kioo cha jamii hivyo wanapaswa kuwa mfano bora katika maneno na matendo yao.
Alisema ni jambo gumu jamii kuwaelewa wasanii katika kile wanachokifikisha kwao kupitia kazi zao iwapo wenyewe wanafanya mambo ya ovyo na yasiyo ya mfano bora ambayo pia huharibu baada ya vijana na watoto wakiwa miongoni mwa mashabiki wao wanaowafuatilia kwa karibu.
Msanii huyo anayeshiriki pia filamu kadhaa kama 'Mahaba Niue', ' Like Father Like Son', 'XXL' na Best Palyer', alisema wasanii wanapaswa kuthamini fani hiyo kwa vile ni ajira yao na tegemeo la kuwainua kiuchumi kama watajikita kwenye kazi kuliko skendo chafu.

K-Guitar wa Bana Marquis wala hajutii


Kelvin Nyoni 'K Guitar' kaika pozi
MUIMBAJI wa bendi ya muziki wa dansi ya Bana Marquiz, Kelvin Nyoni 'K Guitar', amefyatua wimbo wake binafsi uitwao 'Sintojutia' uliopo katika miondoko ya Zouk.
Tayari wimbo huo umeanza kurushwa hewani na baadhi ya vituo vya redio nchini na kwa sasa anajipanga kwa ajili ya kufyatua video yake ili mashabiki wapoate uhondo kamili.
Akizungumza na MICHARAZO, mwanamuziki huyo anayecharaza pia gitaa la rythm alisema wimbo huo ameurekodia katika studio za Swadt Records chini ya prodyuza T-Tach kwa msaada mkubwa wa mameneja wake watatu  akiwamo mchora katuni wa gazeti hili, Abdul King'O.
Kelvin alisema wimbo huo ni mwanzo wa safari ndefu ya kuwapa burudani mashabiki wa muziki kupitia albamu yake binafsi itakayokuwa na nyimbo zaidi ya sita katikka miondoko tofauti za Zouk, Bongofleva na Rhumba.
"Baada ya kukamilisha kutoa video ndipo nitaanza kurekodi nyimbo nyingine ambapo mpaka sasa tayari ninazo kama tatu zilizokamilisha mashairi yake," alisema Kelvin.
Kelvin kabla ya kuingia kwenye muziki wa dansi akijiunga na bendi ya Bana Marquiz inayoongozwa na mwanamuziki nyota wa kimataifa, Tshimanga Assosa Kalala 'Mtoto Mzuri', alishawahi kutoa wimbo wa Bongofleva wa 'Mapenzi Siyo Pesa' kabla ya kuurudia tena katika bendi hiyo.

Hapatoshi Ligi ya Mabingwa Ulaya

Arsenal watakaokuwa nyumbani Ligi ya Mabingwa Ulaya
KIVUMBI cha Ligi ya Mabingwa Ulaya kinatrajiwa kuendelea tena leo, huku kivumbi kikiwa katika pambano kati ya Borussia Dortmund itakapoikaribisha Napoli ya Italia, hiyo ikiwa ni nafasi pekee kwao kujua kama itakuwa na nafasi ya kusonga hatua ya mtoano ama la.
Kwanza inakabiliwa na majeruhi kutokana na kipigo cha 3-0 ilichokipata Jumamosi kwenye Bundesliga dhidi ya wapinzani wao wakubwa Bayern Munich, timu hiyo ya Kocha Juergen Klopp inahitaji kushinda mechi zake mbili za mwisho katika Kundi F, dhidi ya Napoli na Olympique Marseille ili kutinga hatua ya mtoano.
Matokeo yoyote kinyume na ushindi, yatamaanisha timu hiyo ambayo ilitinga fainali msimu uliopita, itakuwa imeshindwa kufikia malengo hayo.
"Tunakosa umakini na malengo," alisema kipa wa Dortmund, Roman Weidenfeller. "Tunachukua muda mrefu kumalizia gonga zetu. Tunapasiana badala ya kwenda moja kwa moja langoni."
"Bado hakuna lolote ambalo limefanyika, iwe kwenye ligi ya nyumbani ama Ulaya. Lakini mechi ya Jumanne (leo) ni muhimu sana kuliko hii dhidi ya Bayern. Tunahitaji kushinda mechi hii ya nyumbani na tunahitaji kutumia nafasi zetu kwa sababu mchezo ni kushinda kwa kufunga mabao."
Dortmund inashika nafasi ya tatu katika kundi lao ikiwa na pointi sita, tatu nyuma ya kinara Arsenal na  Napoli ambazo zina pointi tisa zikitofautiana kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa. Marseille haina pointi yoyote baada ya kupoteza mecho zote. Napoli iliichapa timu hiyo ya Ujerumani kwa mabao 2-1 katika mechi ya kwanza iliyopigwa Septemba mwaka huu.
"Niliiambia timu yangu baada ya mechi ya Bayern kuwa ina dakika tano za kusahau machungu na kisha kujipanga upya," alisema Klopp, ambaye timu yake ipo pointi saba nyuma ya vinara Bayern katika Bundesliga.
"Tunapaswa kufikiri kuhusu mechi ijayo, kutoa maamuzi sahihi na kuwa na utayari kimichezo. Tunahitaji kujua mustakabali wa yote katika mechi na Marseille (katika mechi yetu ya mwisho)."

Majeruhi
Klopp atahitaji kufanya mabadiliko katika safu yake ya ulinzi kwa mara nyingine tena baada ya Manuel Friedrich kuwa mbadala pekee wiki iliyopita kutokana na Mats Hummels, Neven Subotic na Marcel Schmelzer, kuwa majeruhi na kuenguliwa katika michuano hiyo ya Ulaya.
Hata hivyo, kuna habari njema kutokana na beki wa kulia Lukasz Piszczek Jumamosi kurejea uwanjani baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakimkabili majira ya joto.

Napoli nayo yashikwa
Napoli nayo kimatokeo haikufanya vizuri baada ya kupoteza mechi zao mbili zilizopita za Serie A tena bila kufunga, awali ilikubali kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Juventus wiki mbili zilizopita na kisha Jumamosi ikanyukwa nyumbani bao 1-0 dhidi ya Parma.
Kocha Rafael Benitez alibadili kikosi chake dhidi ya Parma, sera ambazo zilizua maswali mengi katika vyombo vya habari, hivyo kushuhudia timu yake ikilala kwa bao la usiku la Antonio Cassano.
Hofu kubwa ni mshambuliaji Marek Hamsik, ambaye aliingia dakika 10 za mwisho na kuumia unyayo, hivyo ataikosa Dortmund leo.
Benitez alilalamikia mapumziko ya mechi za kimataifa. "Tumefanya makosa mengi, lakini ni vigumu kufanya vizuri kwa muda mfupi kama huo," alisema.
"Tunapoteza mipira kirahisi, tunaruhusu nafasi nyingi za kuchezewa mashambulizi ya kushtukiza na kupoteza nafasi chache za kusonga mbele kwa  Gonzalo Higuain na Goran Pandev.
"Sishangai kwa Borussia kufungwa na Bayern. Ninayaangalia zaidi matokeo yetu kuliko Borussia. Tayari tunaelekeza akili zetu katika mechi inayofuata."

Cazorla aionya Arsenal kwa Marseille
Licha ya Arsenal leo kuwa nyumbani kwenye dimba lao la Emirates ikicheza dhidi ya vibonde Olympique Marseille, haitahitaji kulala kwenye mchezo huo.
Miamba hiyo inayoongoza Kundi F ikiwa juu ya Napoli kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa huku ikiizidi Borussia Dortmund kwa pointi sita, kama itafanikiwa kuifunga Marseille na Wajerumani hao wakashindwa kuifunga Napoli, kikosi hicho cha Arsene Wenger kitakuwa kimejihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya mtoano.
Kiungo Santi Cazorla ameonya kutobweteka katika mechi hiyo wakati huu wakiwa bado wana safari ya kwenda Napoli, kuhitimisha safari yao ya hatua ya makundi.
"Tatizo kubwa ni kwamba, kila mmoja anafikiri itakuwa mechi rahisi kwetu kushinda," Mhispania huyo aliiambia tovuti ya Arsenal (www.arsenal.com) baada ya ushindi wa 2-0 walioupata Jumamosi dhidi ya Southampton, uliowafanya kuendelea kukaa kileleni mwa Ligi Kuu England.
"Hakuna wanalolitarajia Marseille kwa sababu hawana pointi yoyote, lakini watafanya mambo kuwa magumu kwetu. Itakuwa mechi ngumu na kama hatutakuwa makini tutashindwa kupata nafasi ya kusonga mbele.
"Tunapaswa kutambua kwamba ni mechi muhimu," alisema Cazorla. "Kama hatutapata matokeo mazuri, yatafanya mambo kuwa magumu kwetu kwani tutakapokwenda Napoli tutalazimika kushinda."
Marseille ililazimisha suluhu dhidi ya Arsenal zilipokutana Emirates miaka miwili iliyopita, lakini Klabu hiyo ya Ufaransa ina rekodi mbaya ikiwa England.
Ushindi pekee iliyopata katika mechi 11 za mashindano ilizocheza England, ulikuwa wa bao 1-0 dhidi ya Liverpool msimu wa 2007-08 katika mechi ya Ligi ya Mabingwam Ulaya hatua ya makundi na imepoteza mara sita.
Hata hivyo, Marseille itamtegemea Andre-Pierre Gignac baada ya mshambuliaji Dimitri Payet kuwa majeruhi wa goti. Mabingwa hao wa Ulaya wa 1993, pia watamkosa mshambuliaji Mghana Andre Ayew anayesumbuliwa na goti.

Basel v Chelsea, Barca na Ajax
Katika mechi nyingine itakayopigwa leo, Kundi E, Basel  itakuwa mwenyeji wa Chelsea wakati huo Steaua Bucharest ikiialika Schalke 04. Kundi G, Zenit St Petersburg itaialika Atletico Madrid  huku
FC Porto ikiwa nyumbani kuisubiri Austria Vienna.
Kundi H, Ajax Amsterdam itaisubiri  Barcelona wakati  Celtic ikiwa mwenyeji wa  AC Milan.

NIPASHE