STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, March 5, 2013

ZFA yaridhia Aman Makungu kujiuzulu Urais

Aman Ibrahim Makungu; Si rais tena ZFA

Na Ally Mohamed, Zanzibar
HATIMAYE Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), imekubali ombi la Rais wake, Aman Ibrahim Makungu kujiuzulu nafasi hiyo.
Katika Barua iliyoandikwa na ZFA Machi 4, mwaka huu, yaani jana, ikisainiwa na Makamu wa Rais Kisiwani Unguja, ambaye pia ni Kaimu Rais wa ZFA kikatiba, Alhaj Haji Ameir, ikiwa na Kumbukumbu namba. ZFA/PRESIDENT/VOL.11/05, ombi hilo limekubaliwa.
Barua hiyo imesema Kamati ya Utendaji ya ZFA Taifa, imekaa na kujadili kwa kina ombi la kujiuzulu kwa Makungu, na kutafakari kwa makini na hatimaye kufikia uamuzi wa kulikubali ombi hilo.
Aidha katika barua hiyo, ZFA Taifa wamemshukuru Aman Makungu kwa msaada wake alioutoa huku wakimuomba aendelee kuwa na chama hicho wakati wowote atakapohitajika.
Nakala za barua hiyo zimetumwa kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo la Zanzibar pamoja na Msaidizi Katibu ZFA Kisiwani Pemba.
Kwa mujibu wa Katiba ya ZFA, sasa ni wazi kuwa kunalazimika kufanyika uchaguzi mwingine ndani ya siku 90.
Itakumbukwa kuwa miezi miwili iliyopita, Rais wa ZFA, Aman Ibrahim Makungu aliandika barua ya kuomba kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile kilichoelezwa katika barua hiyo kuwa ni kuchoshwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho wasiotaka mabadiliko huku wakionekana kuwagawa baadhi ya wajumbe wa ZFA kwa kisingizio cha U-Unguja na U-Upemba, ambapo Kamati ya Utendaji ya ZFA Taifa walilikataa ombi hilo kwa madai kuwa litachangia kurejesha nyuma soka la Zanzibar.


Imehamishwa:Bin Zubeiry


TFF yawasilisha barua ya kutaka kuonana na Waziri




NA BONIFACE WAMBURA
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewasilisha rasmi maombi ya kuonana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara ili kuzungumzia uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya 2012.
Maombi hayo yaliwasilishwa rasmi Wizarani jana (Machi 4 mwaka huu) ambapo TFF imependekeza kikao hicho kifanyike keshokutwa (Machi 7 mwaka huu) au Machi 13 mwaka huu.
Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Machi 2 mwaka huu kujadili tamko ya Waziri kutengua matumizi ya Katiba ya 2012 ndiyo iliyopendekeza kikao hicho kwa lengo la kusikiliza upande wa TFF katika suala hilo.
TFF imeamua kuchukua hatua hiyo kufuatia tamko la serikali kutangaza kuifuta katiba mpya ya shirikisho hilo iliyorekebishwa kwa njia ya waraka na iliyotumika kuwaengua baadhi ya wagombea kwenye uchaguzi wake uliokuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu.
Hatua ya serikali imekuwa ikielezwa na wadau kama tisho la Tanzania kuadhibiwa na Shirikisho la Soka Duniani, FIFA linalopinga serikali kuingilia vyama wanachama wake.

Hatma ya Lyon kesho Chamazi, Ligi Kuu ikiendelea




NA BONIFACE WAMBURA
HATMA ya African Lyon kuendelea kushika mkia au la kwenye Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inajulikana kesho wakati itakapokuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Lyon yenye pointi 13 kutokana na mechi 19 inabidi iifunge Ruvu Shooting kama inataka kuirejesha mkiani Toto African yenye pointi 14. Kama kweli inazitaka pointi zote tatu itabidi ifanye kazi mbele ya Ruvu Shooting inayotiwa makali na Kocha Charles Boniface Mkwasa.
Hiyo itakuwa mechi ya 18 kwa Ruvu Shooting inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 26 ikitanguliwa na vinara wa ligi hiyo Yanga, Azam, Simba, Coastal Union, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar yenye pointi 28 ikinolewa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime.
Mechi hiyo namba 139 itachezeshwa na mwamuzi Amon Paul kutoka Musoma wakati wasaidizi ni Anold Bugado wa Singida na Milambo Tshikungu kutoka Mbeya. Mwamuzi wa mezani atakuwa Shafii Mohamed wa Dar es Salaam.
Nayo Tanzania Prisons ya Jumanne Chale itakuwa mgeni wa Oljoro JKT katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha wakati Mgambo Shooting itaoneshana kazi na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Keshokutwa (Machi 7 mwaka huu) Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya JKT Ruvu ya Kocha Charles Kilinda na Kagera Sugar.
Ligi hiyo itaendelea tena Jumamosi ya Machi 9 mwaka huu kwa mechi mbili; Yanga vs Toto Africans (Uwanja wa Taifa), na Azam vs Polisi Morogoro (Azam Complex, Chamazi).

 

Simba kurejea kinyonge nyumbani leo usiku

Na Ezekiel Kamwaga, Kwanza Sul, Angola
TIMU ya Smba inarejea nchini Tanzania kesho usiku ikitokea Angola ambako jana ilitolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Libolo ya hapa.
Wachezaji wa Simba leo asubuhi wamefanya mazoezi katika Uwanja wa Libolo uliopo hapa ambako mechi hiyo ilichezwa na mchana itasafiri kwenda mji mkuu wa Angola, Luanda, itakapolala kusubiri safari ya kesho.
Hali katika kambi ya Simba iliyopo katika Hoteli ya Ritz, ilikuwa ya huzuni kutokana na kipigo hicho kikubwa zaidi cha ugenini ambacho Simba imewahi kukipata katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Mara ya mwisho Simba kupata kipigo kikubwa ilikuwa mwaka 2009 ilipofungwa mabao 5-1 na Harass Al Hadoud ya Misri katika michuano kama hii kwenye mechi iliyopigwa jijini Alexandria, Misri.
Kwa ujumla, Simba ilicheza vizuri katika mchezo huo isipokuwa katika dakika 10 za mwisho ambazo iliruhusu mabao matatu kati ya manne iliyofungwa.
Hata hivyo, matokeo hayo ya 4-0 hayatoi tathmini halisi ya mechi hiyo kwa vile katika sehemu kubwa ya mchezo huo, Simba na Libolo zilikuwa zimetoshana nguvu.
Libolo walikuwa na faida ya kuwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa kama vile kiungo Ruben aliyekuwa nyota wa mchezo huo ambaye pamoja na kufunga bao la tatu, ndiye aliyekuwa akiichezesha timu hiyo.
Ruben ametoka kuichezea klabu ya Braga ya Ureno iliyokuwa ikishiriki katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na tofauti za wachezaji kama hao na wale wa Simba ilionekana katika namna ambavyo wenyeji walitumia nafasi zao.
Saa moja kabla ya mechi kuanza, mvua kubwa ilinyesha katika mji wa Calulo na kuathiri hali ya uwanja jambo lililosabisha mpira kuchezwa katika mazingira magumu.
 

TFF YAIPONGEZA AZAM KUSONGA MBELE AFRIKA


NA BONIFACE WAMBURA
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa timu ya Azam ya Tanzania Bara kwa kufanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Ushindi wa jumla ya mabao 8-1 ambao Azam imeupata dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini si fahari kwa timu hiyo tu, bali Tanzania kwa ujumla, na unaonyesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kiushindani katika michuano hiyo ya Afrika.
Hata hivyo, ni vizuri Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wakautazama ushindi huo kama changamoto kwao kuhakikisha wanajipanga vizuri zaidi kwa raundi inayofuata.
Timu ya Azam inayofundishwa na Mwingereza John Stewart Hall ilishinda nyumbani mechi ya kwanza mabao 3-1, na juzi kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 ugenini jijini Juba.
Kwa kufanikiwa kuing’oa Al Nasir Juba, Azam sasa watacheza raundi ya kwanza (raundi ya 16 bora) ya michuano dhidi ya Barrack Y.C.II ya Liberia ambayo katika raundi ya awali iliitoa Johansens ya Sierra Leone. Barrack ilishinda bao 1-0 nyumbani katika mechi ya kwanza na kulazimisha suluhu katika mechi ya marudiano jijini Freetown.
 
Azam itaanzia mechi hiyo ugenini kati ya Machi 15,16 na 17 mwaka huu wakati mechi ya marudiano itachezwa Tanzania kati ya Aprili 5,6 na 7 mwaka huu.