Aman Ibrahim Makungu; Si rais tena ZFA |
Na Ally Mohamed, Zanzibar
HATIMAYE Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), imekubali ombi la Rais wake, Aman Ibrahim Makungu kujiuzulu nafasi hiyo.
Katika Barua iliyoandikwa na ZFA Machi 4, mwaka huu, yaani jana, ikisainiwa na Makamu wa Rais Kisiwani Unguja, ambaye pia ni Kaimu Rais wa ZFA kikatiba, Alhaj Haji Ameir, ikiwa na Kumbukumbu namba. ZFA/PRESIDENT/VOL.11/05, ombi hilo limekubaliwa.
Barua hiyo imesema Kamati ya Utendaji ya ZFA Taifa, imekaa na kujadili kwa kina ombi la kujiuzulu kwa Makungu, na kutafakari kwa makini na hatimaye kufikia uamuzi wa kulikubali ombi hilo.
Aidha katika barua hiyo, ZFA Taifa wamemshukuru Aman Makungu kwa msaada wake alioutoa huku wakimuomba aendelee kuwa na chama hicho wakati wowote atakapohitajika.
Nakala za barua hiyo zimetumwa kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo la Zanzibar pamoja na Msaidizi Katibu ZFA Kisiwani Pemba.
Kwa mujibu wa Katiba ya ZFA, sasa ni wazi kuwa kunalazimika kufanyika uchaguzi mwingine ndani ya siku 90.
Itakumbukwa kuwa miezi miwili iliyopita, Rais wa ZFA, Aman Ibrahim Makungu aliandika barua ya kuomba kujiuzulu nafasi hiyo kwa kile kilichoelezwa katika barua hiyo kuwa ni kuchoshwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho wasiotaka mabadiliko huku wakionekana kuwagawa baadhi ya wajumbe wa ZFA kwa kisingizio cha U-Unguja na U-Upemba, ambapo Kamati ya Utendaji ya ZFA Taifa walilikataa ombi hilo kwa madai kuwa litachangia kurejesha nyuma soka la Zanzibar.
Imehamishwa:Bin Zubeiry
No comments:
Post a Comment