RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho ameamuru majambazi
na wahamiaji haramu wote katika mikoa mitatu nchini kujisalimisha katika muda
wa siku 14 kuanzia leo, Ijumaa, Julai 26, 2013 kabla ya kuanza kwa operesheni
kubwa kuliko zote katika historia ya Tanzania nyenye lengo la kukomesha
ujambazi katika mikoa hiyo na kukamata wahamiaji haramu.
Rais
Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu amesema kuwa leo ametoa amri kwa vyombo
vyote vya ulinzi na usalama nchini kuanza maandalizii ya operesheni hiyo na
hatimaye kuiendesha katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.
“Majambazi
wanateka magari, wanaua watu wetu, wanapora mali zao. Watanzania hawawezi kuendelea kuishi kwa hofu, woga na taabu katika nchi yao
wenyewe. Tutawasaka majambazi misituni, tutawasaka majumbani, tutachimbua
ardhini kutafuta hata silaha zilizofukiwa chini,” amesema Rais Kikwete.
Rais
Kikwete ametoa amri hiyo mchana wa leo, Ijumaa, Julai 26, 2013 wakati
alipohutubia wananchi wa mjini Biharamulo, Mkoani Kagera, kabla ya kuweka jiwe
la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kagoma, Wilaya ya Muleba
kwenda Lusahuga, Biharamulo.
Rais
Kikwete ametoa amri hiyo kufuatia matukio ya mara kwa mara na yasiyokuwa na
mwisho ya majambazi kuteka mabasi, kuua watu na kupora mali zadi katika mikoa
hiyo, hali ambayo imesababisha malalamiko ya wakazi wa mikoa hiyo.
Rais
Kikwete ameaambia wananchi: “Tumeamua kukomesha upuuzi huu katika mikoa
ya Kagera, Kigoma Geita. Leo nimetoa maagizo kwa vyombo vyetu vya ulinzi na
usalama – Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Usalama wa Taifa
kuandaa operesheni maalum, operesheni kubwa kuliko zote tokea tupate uhuru.
Upuuzi huu hauwezi kuendelea.”
Ameongeza
Rais Kikwete na kuwaambia wananchi: “Nawaamuru majambazi wote, wenye kumiliki
silaha kinyume cha sheria na wahamiaji haramu wote wajisalimishe katika wiki
mbili kuanzia leo. Wajisalimishe wao pamoja na silaha zao. Baada ya hapo,
tunaanzisha operesheni ambayo haijapata kuonekana katika historia ya nchi
yetu.”
Amesisitiza
Rais Kikwete: “Sitanii, sina mzaha na hili. Nimechoka. Nalisema hili mchana, macho
makavu. Nawaambia majambazi watafute kazi nyingine, kazi hii hailipi tena. Kwa
wale majambazi na wahamiaji haramu kutoka nchi za jirani, waanze safari ya
kurejea kwao.”
Rais
Kikwete ameonya: “Na hata wale wanaoishi na kulea majambazi na wahamiaji haramu nao
wajisalimishe. Na ole wao majambazi watakaojaribu kuwapiga risasi askari wetu.
Watakiona cha mtema kuni.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano
ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.