Dometria Alphonce 'DD' katika pozi |
MUIGIZAJI wa filamu ambaye ni pacha wa nyota wa fani hiyo na muziki, Husna Posh 'Dotnata', Dometria Alphonce 'DD', amepakua filamu mpya iitwayo 'Kua Uyaone' ambayo inasimulia mkasa wa kweli uliowahi kumpata katika maisha yake ya ndoa.
DD, aliiambia MICHARAZO juzi kuwa filamu hiyo imeshakamilika na wakati wowote itaachiwa hadharani, ikiwa imemshirikisha yeye mwenyewe na wasanii wengine waliopo katika kikundi chake cha sanaa cha DD Films kilichopo Ukonga.
Msanii huyo ambaye pia anajihusisha na nyimbo za Injili akishirikiana na pacha wake wakiandaa albamu kwa sasa, alisema hiyo itakuwa filamu yake ya kwanza kuitunga na kuiandaa mwenyewe baada ya kushirikishwa kazi kadhaa siku za nyuma.
'Nimekamilisha filamu yangu mpya iliyojikita kwenye simulizi la kweli ambao limewahi kunitokea katika maisha yangu ya ndoa, nimecheza na wasanii mbalimbali baadhi wakiwa ni askari waliopo katika kikundi changu cha sanaa cha DD Films," alisema.
Alisema filamu hiyo ni maalum kwa wanawake wote waliowahi kukutwa na misukosuko katika maisha ya ndoa zao, kwani mbali na mikasa ya kusisimua, lakini pia inatoa suluhu ya nini kifanyike mtu anapokumbwa na misukosuko kama hiyo.
Msanii huyo ambaye kama pacha wake naye ni mjasiriamali, alisema filamu hiyo ni yenye kuwatia nguvu na ujasiri wanawake wote wanaoteseka katika ndoa zao.
Aliongeza kuwa, wakati filamu hiyo ikiwa katika harakati ya kutolewa hadharani pia tayari anaendelea kuandaa kazi nyingine ambayo hakupenda kuitaja, ingawa alidai imeshaanza kufanyiwa 'shutingi'.
Mwisho