|
Ngassa (17) akishangilia na wenzake moja ya mabao yake wakati wakiichakaza Komorozine ya Comoro kwa mabao 70-0 uwanja wa Taifa katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2014 |
|
Siku ya mechi hiyo dhidi ya Komorozine, Ngassa alikuwa akinyanyasa kama anavyoonekana pichani akimtokea beki wa timu hiyo ya Comoro waliong'olewa kwa jumla ya mabao 12-2 |
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Yanga Mrisho Ngassa ameweka historia baranui Afrika baada ya kuwa miongoni mwa wachezaji wanne walioibuka 'Wafungaji Bora' wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyomaliza mwishoni mwa wiki kwa timu ya Es Setif ya Algeria kutwaa ubingwa.
ES Setif ilinyakua taji hilo ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1988 baada ya faida ya goli la ugenini kuwabeba kutokana na kufungana jumla ya mabao 3-3 baada ya kufunga 2-2 mjini Kinshasa kabla ya Jumamosi kufunga tena 1-1 Algeria.
Ngassa anayeichezea pia timu ya taifa, Taifa Stars ambaye timu yake ya Yanga ilitolewa katika raundi ya pili amefungana na wachezaji wenzake watatu wakiwa na mabao sita kila mmoja.
Wachezaji wengine waliofungana na Ngassa ni El Hedi Belameiri wa ES Setif ambaye ana nafasi kubwa ya kunyakua Kiatu cha Dhahabu kutokana na kuweza kuifikisha timu yake fainali na kutoa pasi ya mwisho iliyowapa sare nyumbani dhidi ya Vita.
Nyota wengine waliomaliza wakiwa na idadi hiyo ya mabao mbali na
Ngassa na Belameiri, ni Ndombe Mubele wa As Vita ya DR Congo na Haythem
Jouini wa Esperance ya Tunisia.
Ngassa alifunga mabao hayo sita yaliyomfanya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kumaliza Mfungaji Bora Afrika wakati wakiingamiza Komorozine ya Comoro kwa jumla ya mabao 12-2, yeye akifunga 'hat trick' mbili, moja katika kila mechi nyumbani na ya ugenini kabla ya Yanga kutupwa nje na Al Ahly ya Misri.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam ambapo Yanga ilishinda mabao 7-0, Ngassa alifunga mabao yake dhidi ya Komorozine katika dakika za 14, 65, 68, huku mengine yakifungwa na Nadir Haroub Cannavaro (Dk 20) Didier Kavumbagu (Dk 57 na 80) na Hamis Kiiza (Dk 60)
Walipowafuata wapinzani wao nchini Comoro ambapo Yanga waliigagadua Komorozine mabao 5-2, Ngassa alifunga tena 'hat trick' ya pili kwa mabao ya DK 22, 87 na 90, huku magoli mengine yalifungwa na Hamis Kiiza katika dakika ya 13 na Simon Msuva aliyefunga dakika ya 37 na mabao ya wenyeji yakiwekwa kimiani na Anli na Ismail katika dakika ya 41 na 77.
Yanga ilikutana na waliokuwa mabingwa watetezi, Al Ahly ya Misri na kuwalaza bao 1-0 nyumbani katika mechi ya raundi ya pili, goli likifungwa na Cannavaro kabla ya kwenda Misri na kulala 1-0 na kulazimisha mechi hiyo kumalizwa kwa mikwaju ya penati na Yanga kutolewa kwa mikwaju 4-3.
Licha ya Al Ahly kuitoa Yanga ilienda kukwama kwa Al Ahly Benghazi ya Libya na kuhamia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambapo Wamisri hao wamefanikiwa kufika fainali na watavaana na Sewe Sports ya Ivory Coast kuwania taji hilo katika mechi mbili zitakazochezwa Novemba 29 na Desemba 6 mwaka huu.