Bastia yamtema kocha wao Claude Makelele
KLABU ya Bastia inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) imethibitisha kuachana na aliyekuwa kocha wao, kiungo wa zamani wa kimataifa wa The Blues, Claude Makelele.
Taarifa ya klabu hiyo inayokamata nafasi ya pili toka mkiani, imesema Makelele ameondoka katika klabu hiyo leo Jumagtatu kutokana na mwenendo mbaya wa timu yao ikiwa imeshinda mechi mbili kati ya 12 za ligi.
Makelele aliyetamba na klabu mbalimbali zikiwamo Real Madrid na Chelsea, alipewa mikoba ya kuinoa timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita akitokea PSG.
Miezi sita tangu awe na kikosi hicho, Bastia imeweka bayana kuwa inasaka kocha mpya baada ya kuwa na Makelele kutemwa.
"Kamati ya Wakurugenzi ya SCB inapenda kuwataarifu wote wanaoiunga mkono klabu yetu kuwa kuanzia leo Claude Makelele siyo tena kocha mkuu wa SC Bastia," taarifa hiyo ya klabu imesomeka hivyo.
"Mazoezi kwa sasa yatakuwa mikononi mwa Ghislain Printant na Herve Sekli mpaka atakapoteuliwa kocha mkuu mpya," taarifa ya klabu hiyo iliongeza.
Makelele alikiongoza mara ya mwisho kikosi cha timu hiyo siku ya Jumamosi wakati waliponyukwa bao 1-0 na Guingamp kwa goli lililofungwa na Sambou Yatabare.
No comments:
Post a Comment