STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, July 18, 2013

Ajali tena! Basi la Princess Muro lawaka moto abiria chupuchupu


Abiria zaidi ya 50 wilayani Nzega mkoani Tabora wamenusurika kupoteza maisha baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuungua moto kutokana na hitilafu ya kiufundi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Peter Ouma alisema moto huo ulioteketeza mizigo yote ya abiria, ulitokea juzi saa 4 usiku katika kijiji cha Nata kwenye basi la Princess Muro.

Alisema gari hilo aina ya Scania lenye namba za usajili T 6766 CEH, lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza likiwa linaendeshwa na dereva Boniface Francis.

Alisema likiwa na mwendo wa kawaida, lilianza kuwaka moto ndipo kondakta pamoja na dereva waligundua na kulisimamisha.

Abiria walifanikiwa kushuka wakiwa salama isipokuwa mizigo yao iliteketea kwa moto. Jitihada za kuuzima zilishindikana kutokana na eneo ilikotokea ajali hiyo kukosa kikosi cha zima moto na uokozi.
Kwa mujibu wa kamanda, kulitokea hitilafu kwenye injini ya gari hilo hali iliyosababisha moto. Hakuna mtu alijeruhiwa.

Kamanda amewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri hususani vya kusafirisha abiria, kufanya ukaguzi na kuvikarabati kwa nyakati tofauti kuepusha ajali.

Inauma! Bi Harusi mtarajiwa ateketezwa na moto

 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ernest Mangu,
FAMILIA moja ya watu wanne, akiwemo bi harusi mtarajiwa, Bushrati Bushiri (23) aliyetarajia kufunga ndoa Julai 13, mwaka huu, wamepoteza maisha baada ya nyumba walimokuwa wamelala kuteketea kwa moto.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa 6:00 usiku wa  Julai 10, mwaka huu eneo la Lumala, Kata ya Pasiansi, Manispaa ya Ilemela, jijini hapa ikiwa ni siku mbili tu kabla ya ndoa ya Bushrati.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ernest Mangu, nyumba iliyoteketea kwa moto ni ya Nuru Fadhili (46) mkazi wa Lumala, Pasiansi.

Mbali na Bushrati, Kamanda Mangu aliwataja marehemu wengine waliotokana na moto huo uliotokea usiku kuwa ni Amina Musa (75), Mariam Musa (72) na mtoto Janetha Abdul ambaye umri wake haukujulikana mara moja.

Alisema mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kiseke, Doto Twaha (17) alinusurika katika ajali hiyo kwa kupata majeraha mwilini na amelazwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC) akipata matibabu.

Kamanda Mangu alisema chanzo cha moto huo ni jiko la mkaa ambalo lilikuwa sebuleni kwa ajili ya kupasha chakula cha mwezi mtukufu (daku) usiku.

Alisema kwamba mkaa ulidondokea kwenye zulia kisha kushika masofa na pikipiki iliyokuwa imeegeshwa sebuleni na kusambaa nyumba nzima huku marehemu wakiwa usingizini.

GPL

Mzee Mandela atimiza miaka 95 hospitalini

RAIS wa zamani wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela leo ametimiza miaka 95, lakini tofauti na mwaka uliopita alipotimiza miaka 94 safari hii ameshindwa kuisherekea kwa vile yupo mahututi hospitalini.
Siku ya Mandela huadhimishwa kuenzi kazi za kiongozi huyo alizozifanya kwa miaka 67 akiutumikia umma wa wananchi wa Afrika Kusini, zikiwamo vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye kuwa Rais wa kwanza mzalendo kwa miaka mitano, kisha kustaafu.


 “Happy birthday Mzee Madiba.” Rais wa kwanza na mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, leo anatimiza umri wa miaka 95, pia anatimiza siku ya 40 tangu alipolazwa katika Hospitali ya Medclinic, Pretoria kwa ajili ya matibabu.

Nelson Rolihlahla Mandela, alizaliwa Julai 18, 1918 katika Kijiji cha Mvezo, eneo la Mthatha, Transkei Mkoa wa Eastern Cape na ametumia zaidi ya asilimia 70 ya maisha yake akipigania haki na usawa wa wananchi wa Afrika Kusini.


Maadhimisho ya miaka 95 tangu kuzaliwa kwa Mandela yanabeba uzito mkubwa kuliko maadhimisho mengine yaliyotangulia kwani kwa siku 40, wananchi wa Afrika Kusini wamekuwa katika wasiwasi mkubwa hasa kutokana na kuzorota kwa afya ya kiongozi huyo.
Mandela alilazwa katika hospitali hiyo Juni 8, mwaka huu akiugua magonjwa ya figo na afya yake imeelezwa kuwa ni mbaya.

UCHAWI TAZARA: NJIA ATUA NA BARUA YA VITISHO MBEYA

Njiwa akiwa na ujumbe wa barua kama inavyo onekana 


 Njiwa akiwa amedhoofu kwa Baridi akiwa katika choo cha wanaume 
 Hii ni sehemu alipokutwa Njiwa huyo 
 Majengo nje ya Ofisi ya Afisa Mwajiri 
 Baadhi ya wafanyakazi wakielekea eneo la  tukio 
 Afisa Mwajiri (Mwenye shati ya bluu) Na baadhi ya wafanyakazi wakishuhudia tukio 
 Mashuhuda wakitoka eneo la tukio 

 Barua iliyoletwa na Njiwa maeneo ya Ofisi ya Mwajiri upande wa mbele na nyuma 
 Jengo la Ofisi ya Afisa Mwajiri 
Stesheni ya TAZARA kituo  cha Mbeya 


MAKUBWA YAIBUKA TAZARA MBEYA : NJIWA ATUA NA BARUA YA VITISHO .

Njiwa akiwa na ujumbe wa barua kama inavyo onekana 


 Njiwa akiwa amedhoofu kwa Baridi akiwa katika choo cha wanaume 
 Hii ni sehemu alipokutwa Njiwa huyo 
 Majengo nje ya Ofisi ya Afisa Mwajiri 
 Baadhi ya wafanyakazi wakielekea eneo la  tukio 
 Afisa Mwajiri (Mwenye shati ya bluu) Na baadhi ya wafanyakazi wakishuhudia tukio 
 Mashuhuda wakitoka eneo la tukio 

 Barua iliyoletwa na Njiwa maeneo ya Ofisi ya Mwajiri upande wa mbele na nyuma 
 Jengo la Ofisi ya Afisa Mwajiri 
Stesheni ya TAZARA kituo  cha Mbeya 


*******************************************************
WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Reli, kati ya Tanzania na Zambia(TAZARA) jana walijikuta katika wakati mgumu na baadhi yao kulazimika kuzikimbia ofisi zao, baada ya ndege aina ya njiwa kukutuwa katika moja ya choo cha ofisi hiyo akiwa amefungwa hirizi shingoni, huku akiwa na barua yenye ujumbe wa onyo kali.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea mapema leo   saa mbili asubuhi katika ofisi za mamlaka hiyo zilizopo eneo la Iyunga Mkoani hapa, hali ambayo mbali na baadhi ya wafanyakazi wake kuzikimbia ofisi, ilisababisha kuibuka kwa mjadala mkubwa dhidi ya tukio hilo.
Mtandao huu ulifanikiwa  kushudia njiwa huyo  mweusi akiwa nyuma ya choo cha kiume katika eneo hilo la ofisi ya mwajiri, huku akiwa amefungwa hirizi shingoni iliyozungushiwa shanga mchanganyiko wa rangi tatu, ambazo ni Nyekundu, Njano  na Nyeupe.
Mbali ya kuwa na hirizi hiyo, pia njiwa huyo alikuwa amebeba barua inayodaiwa kuwa ni ya mmoja wa wafanyakazi wa Mamlaka hiyo (jina limehifadhiwa kwa sababu maalumu) ambaye anadaiwa hivi karibuni kufukuzwa kazi kwa makosa ya ubadhirifu.
Barua hiyo ilikuwa na maandishi mekundu yenye ujumbe ulioandikwa kwa lugha mbili za Kiswahili na kiarabu, ambapo katika maandishi ya Kiswahili yalisomeka “ Naomba majibu haraka kama mtarudisha binti huyu kazini” ilisema sehemu ya ujumbe huo, huku ikiwa na orodha ya majina matatu ya viongozi wa shirika hilo.
Mbali na ujumbe huo ukiwa umeandikwa kwa maandishi ya mkono yaliyokolezwa kwa wino mwekundu upande wa nyuma, lakini upande wa mbele kulikuwa na maandishi yakiwa ni barua ya kutaarifiwa kufukuzwa kazi kwa mfanyakazi huyo.
Akizungumzia tukio hilo, Mwajiri wa mamlaka hiyo kanda ya Mbeya, aliyejitambulisha kwa jina la Mchaba Mgweno, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba waliobaini ni wahudumu wa usafi.
Aliongeza kuwa baada ya kupokea taarifa hiyo aliwaarifu na wafanyakazi wenzake ambao walikusanyika na kumshuhudia Njiwa huyo mweusi akiwa amedhoofika huku akiwa na barua hiyo yenye vitisho.
Alisema baada ya kushuhudia hali hiyo waliamua kutoa taarifa kituo cha polisi kilichopo ndani ya shirika hilo, ambapo waliichukua barua hiyo na baadhi ya wafanyakazi hao wakienda kutoa maelezo kituoni hapo.
“Kwa kweli hali hii si ya kawaida, ila kwa sasa siwezizungumzia chochote kwa kuwa hata mimi tukio hili limeniweka katika wakati mgumu na nimeshindwa kuendelea na majukumu yangu ” alisema Mgweno.
Hata hivyo kuliibuka malumbano makali kati ya wafanyakazi wa shirika hilo walioshuhudia tukio hilo, ambapo baadhi yao wakidai kuwa tukio hilo ni la kutengenezwa kwa lengo la kuchafuana.
“Hebu angalia hiyo barua yenyewe mbona ni kivuli (Photocopy), kama ingekuwa ni ya ….wanamtaja mfanyakazi aliyefukuzwa jina limehifadhiwa ingekuwa ni nakala halisi….haiwezekani mambo haya ni kutaka kuchafuana tu” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Lakini baadhi yao wakiamini kweli kuwa barua hiyo ilitumwa ili itoe vitisho kwa viongozi wa shirika hilo.
Baadhi ya askari polisi wa kituo cha Tazara walikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli wake.
“Ndugu zangu nyie mnajua taratibu za utoaji wa taarifa kwa jeshi hili, maana wapo wahusika, lakini kwa kifupi sisi tulipokea taarifa na tunaendelea kuzifanyia kazi” alisema mmoja wa askari hao.
Hata hivyo, hadi tunapoondoka eneo la tukio majira ya saa sita mchana Njiwa huyo alikuwa bado yupo eneo la tukio. ANGALIZO: UNAPOTUMIA HABARI HIZI USIPOTOSHE UKWELI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0787-490 752 Au 0654-221465

PICHA ZOTE NA MBEYA YETU 


Watano wajeruhiwa, mmoja vibaya katika ajali Tanga

Picha haihusiani na taarifa hiyo hapo juu
HABARI zilizotufikia muda huu zinasema kuwa watu watano wamejeruhiwa mmoja vibaya baada ya kutrokea ajali eneo la Usagara, mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari ni  kwamba watu hao walijeruhiwa baada ya gari dogo lililokuwa likiendeshwa na mtu ambaye siye dereva kuwagonga.
"Mtu ambaye siye dereva alijaribu kuendesha gari na kwa bahati mbaya akawavamia na kuwajeruhi watu watano, mmoja akiwa katika hali mbaya na wote wamekimbizwa hospitali ya Bombo kwa matibabu.
MICHARAZO inaendelea kufuatilia ikiwemo kujua kama kuna madhara zaidi ya taarifa hiyo, kadhalika inawaombea kila la heri majeruhi hao ili wapone haraka.

Cheka aidindia TPBO, adai atacheza mechi zake mbili iwe isiwe


Bondia Francis Cheka (kulia)
BONDIA Francis Cheka 'SMG' ametaka mzizi wa fitina kwa kusema wazi kuwa yupo tayari kupanda ulingoni kupigana katika mapambano yake mawili aliyopangiwa kuyacheza ndani ya mwezi ujao.
Msimamo huo wa Cheka unatofautiana na mkwara uliotolewa na Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited) iliyomtaka asidhubutu kucheza mechi yake isiyo na ubingwa dhidi la Mmalawi Chiotcha Chimwemwe.
TPBO kupitia Rais wake, Yasin Abdallah 'Ustaadh' ilionya kuwa Cheka hapaswi kupigana ndani ya siku 30 kabla ya pambano lake na Mmarekani Findley Derrick litakalokuwa la kuwania ubingwa wa WBF, litakalochezwa Agosti 30 jijini Dar.
Kabla ya pambano hilo Cheka alishasaini pigano jingine dhidi ya Mmalawi Chiotcha Chimwemwe litakalofanyika Agosti 10 kwenye uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro katika shamrashamra za sikukuu ya Idd el Fitri.
Hata hivyo akizungumza na MICHARAZO kwa njia ya simu jana toka kambini kwake mjini Morogoro, Cheka alisema hawezi kukacha kupigana na Mmalawi kwa madai ni sehemu ya maandalizi ya pambano lake dhidi ya Mmarekani.
Cheka alisema alishasaini mikataba na waratibu wa michezo hiyo na hivyo ni vigumu kusitisha pigano lake la Chimwemwe hata kama silo la ubingwa wowote.
"Mimi nitacheza mapambano yote, lile la Mmalawi ni kama sehemu ya maandalizi ya pigano lake dhidi ya Derrick, pia waratibu wa pambano la pili wenyewe ndiyo waliochelewa kumalizana nami na kujikuta nasaini mechi ya Chimwemwe," alisema Cheka.
Aliongeza haoni ubaya wa yeye kupigana na Mmalawi kabla ya kuvaana na Derrick, licha ya kukiri anapaswa kuwa makini ili asijeruhiwe kama ilivyotokea walipoumana na bondia huyo mjini Arusha na kutetea taji la IBF Afrika.
"Chimwemwe ni bondia nzuri na hatari ulingoni, hivyo nitacheza pambano langu la Idd Pili kwa umakini ili nisishindwe kupigana na Mmarekani, pia muda wa kujiandaa na pigano la pili unatosha kabisa sioni sababu ya kuibuka kwa malumbano wakati huu," alisema Cheka.
Hata hivyo TPBO-Limited kupitia rais wake, imeendelea kusisitiza kuwa Cheka anapaswa kuzingatia ushauri wake ili asije akavuruga pambano hilo la kimataifa la WBF ambalo litazidi kumjengea jina kuliko mechi ya 'ndondo' isiyo na tija.
Pia amesema taarifa walizonazo ni kwamba Chimwemwe ana pambano atakalopigana na Mkenya Agosti 10 na siyo Cheka na kudai huenda ni mbinu zinafanyika kulivuruga pambano hilo la Cheka na Mmarekani.

Mtibwa Javu haendi kokote, bado ni mali yetu- Mtibwa Sugar

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhdEulqye6NB2gXsPi5nX52ruKNuZkwLExeKIBZx9YhfvRv9i-1GRUvXwcGWe-uVRRKZzgwsiMkZgmzbo80RFdgxlHnANAjRcCAnSAEfyBFFwRCrJPMxsv_FBRuFjUHKP11ERryy3d8XlE/s640/Javu.jpg
Husseni Javu
KLABU ya soka ya Mtibwa Sugar imevunja ukimya na kusema wazi kuwa, mshambuliaji wao nyota Hussein Javu bado ni mchezaji wao kwa vile Yanga iliyokuwa ikimhitaji kushindwa kwenda kumalizana nao ili ajiunge Jangwani.
Javu amekuwa akitajwa kuwa ameshasaini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Yanga kwa msimu ujao, lakini uongozi wa Mtibwa Sugar umesema taarifa hizo siyo za kweli kwa sababu hakuna maafikiano yoyote yaliyofanyika.
Mkurugenzi wa klabu hiyo, Jamal Bayser aliiambia MICHARAZO kuwa, ni kweli Yanga waliwafuata wakionyesha nia ya kumsajili mfungaji wao huyo hodari, lakini baada ya kuwapa masharti yao hawakurejea tena kwao.
Bayser alisema kutokana na ukimya huo wa mabingwa hao wa soka nchini, ni wazi huenda wameachana na wazo la kumsajili mchezaji huyo ambaye bado wana mkataba naye wa kuichezea klabu hiyo mpaka mwakani.
"Javu bali ni mali yetu tuna mkataba naye, pia tangu Yanga walipokuwa kwa mara ya kwanza wakionyesha nia ya kutaka kumsajili hawajarudi tena, na kunashangaa kwamba mchezaji huyo akielezwa kasajiliwa Jangwani," anasema.
Anasema anadhani taarifa za Javu kutua Jangwani ni za kuuzia magazeti tu kwa vile hakuna makubaliano yoyote na wenzao wa Yanga, akiamini pia nyota huyo aliyeanza kuichezea Mtibwa kupitia timu ya vijana tangu mwaka 2007 atasalia Manungu kwa msimu ujao.
Javu mwenyewe aliliambia MICHARAZO kwamba bado anajitambua ni mchezaji wa Mtibwa Sugar, licha ya kukiri kuwahi kufuatwa na viongozi wa Simba na Yanga kwa nia ya kumshawishi kujiunga na klabu zao.
"Walinifuata kwa nyakati tofauti ili kunishawishi nitue katika klabu zao, ila niliwaeleza mimi bado nina mkataba na Mtibwa hivyo wakazungumze na mabosi wangu wakiafikiana sintakuwa na tatizo, ila mpaka sasa sijui kinachoendelea," alisema Javu aliyepo pia kwenye kikosi cha pili ya taifa 'Young Taifa Stars.

Mwisho

Kiungo Simba akiri Kibadeni zaidi ya Liewig

Abdallah 'Dullah' Seseme (kushoto) akiwajibika uwanjani
KIUNGO mkabaji chipukizi wa Simba, Abdallah Seseme, amemwagia sifa kocha mkuu mpya wa klabu hiyo, Abdallah Kibadeni 'King' akisema ni bonge la kocha na ana imani ataipa mafanikio klabu hiyo katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Seseme alisema kuondoka kwa makocha Milovan Cirkovic na 'Babu' Patrick Liewig kulimpa hofu kwamba huenda Simba ingeyumba, lakini kwa kipindi kifupi alichokaa na kocha wake wa sasa amemstaajabisha kwa umahiri huku akisema ni zaidi ya waliomtangulia.
Mchezaji huyo alisema kwa staili anazofundisha kocha Kibadeni na wasaidizi wake anaimani kubwa ya Simba kurejesha heshima yake baada ya kuyumba msimu uliopita kiasi cha kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya tatu.
"Simsifii labda kwa kujipendekeza, ila ukweli sijawahi kuona kocha bomba kama Kibadeni. Kwa mtazamo wangu huenda ni zaidi ya watangulizi wake na kama Simba itamng'ang'ania itafika mbali na kurejesha heshima yake kitaifa na kimataifa," alisema Seseme.
Seseme anayemudu nafasi nyingine za mbele na aliyekuwa mmoja wa mhimili walioisaidia Simba kushika nafasi ya tatu msimu uliopita, alisema kwa kuangalia maandalizi ya timu zitakazoshiriki ligi ijayo anadhani msimu ujao kutakuwa na ligi ngumu sana.
"Nadhani msimu ujao kutakuwa na ligi ngumu pengine kuliko iliyopita japo ninaipa nafasi kubwa ya Simba kurejesha heshima yake, pia unaweza kuwa msimu wa kuwika kwa vijana wazawa tofauti na msimu uliopita wageni kuonyesha viwango vya juu," alisema.
Katika msimu uliopita wachezaji wa kigeni waling'ara hasa kwa nafasi ya ushambuliaji na haikuwa ajabu Kipre Tchetche wa Azam kunyakua kiatu cha dhahabu akifuatiwa na Mrundi, Didier Kavumbagu wa Yanga.

Wawakilishi wa WB, TSCP wakagua mradi wa mifereji Mwanza

Wawakilishi wa Benki ya Dunia na Timu ya Mradi wa Kuendeleza Miji Tanzania (TSCP) ulio chini ya OWM-TAMISEMI, wakikagua ujenzi wa Mifereji jijini Mwanza wakati walipokuwa na ziara ya kutembelea miradi hio na kuona maendeleo yake.
 
Standi mpya ya Mabasi ya Dala dala iliyopo katikati ya mji wa Kigoma, Ni moja kati ya matunda ya Mradi wa Kuendeleza Miji hapa nchini  (TSCP) chini ya OWM-TAMISEMI. 
 

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (wa pili kulia), Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Hawa Ghasia (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Benki ya Dunia – Tanzania, Philippe Dongier (kulia), pamoja na Mkurugenzi wa Uendelezaji wa Miji (OWM-TAMISEMI), Anna Mtani (kushoto) katika tukio la Uzinduzi wa mradi wa kuboresha Miji wa ULGSP, mradi uliozaliwa na mradi Mkakati wa Undelezaji Miji (TSCP) chini ya OWM-TAMISEMI kwa mkopo wa Banki ya Dunia

Ujenzi wa Dampo Jijini Arusha, wa TSCP, mradi chini ya OWM-TAMISEMI, ukikaguliwa na wawakilishi wa Banki ya Dunia na timu ya TSCP.

Rais Kikwete ateta na Rais wa Sudan kuhusu vifo wa wanajeshi wa JW


                                THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Sudan Mheshimiwa Omar Bashir kufuatia kuuawa na kujeruhiwa kwa askari wa Tanzania, walioko katika ulinzi wa kimataifa wa amani katika jimbo la Darfur na kumtaka Rais Bashir kuchukua hatua za haraka kuwasaka na kuwakamata waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha mbele ya sheria haraka iwezekanavyo
Katika mazungumzo yao, Rais Omar Bashir amekubaliana na Rais Kikwete na kumuahidi kuwasaka  hadi kuwakamata wale wote waliohusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Rais Bashir amemueleza Rais Kikwete kuwa binafsi anaamini kuwa waliohusika ni wahalifu na hivyo kuahidi kuwa lazima watasakwa hadi kukamatwa kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
Rais Bashir amempa pole Rais Kikwete kwa tukio hilo la kusikitisha ambapo wanajeshi wa Tanzania wameenda nchini Sudan kulinda Amani na Usalama wa wananchi wa Sudan.
Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN) Bw. Ban Ki Moon alimpigia Rais Kikwete na kumpa pole kwa mkasa huo mkubwa na wa kusikitisha ambao umewatokea wa Tanzania hao wakati wakiwa katika kutekeleza jukumu lao la kulinda amani nchini Sudan.
Hadi sasa hakuna kikundi chochote ambacho kimekiri kuhusika na shambulio hilo ingawaje kumekua na  kutupiana lawama baina ya vikundi vya kiserikali na  vya waasi katika jimbo la Darfur.
Mapigano baina ya vikundi vya kikabila na koo mbalimbali zimesababisha mapigano na uvunjifu mkubwa wa amani na usalama katika jimbo la Darfur kwa muda wa miaka 10 sasa, na mara nyingi mapigano  na tofauti zao hizo zimesababisha vifo na uvunjifu wa amani kwa wananchi wa Sudan na wageni pia.
Mwishoni mwa mwaka jana  Wanajeshi wanne kutoka Nigeria waliuawa karibu na El Geneina , Magharibi mwa Darfur ambapo pia inaelezwa na Umoja wa Mataifa kuwa wanajeshi wapatao 50 wameuawa tangu kikosi hiki cha Umoja wa Afrika kinachoundwa kwa  pamoja chini ya Umoja wa Mataifa (UNAMID) kianze operesheni yake mwishoni mwa mwaka 2007.
Taarifa za Umoja wa Mataifa pia zinaeleza kuwa kabla ya mashambulizi yaliyofanyika dhidi ya kikosi cha Tanzania jumamosi iliyopita, wanajeshi 6 wanaolinda Amani wameuawa tangu oktoba mwaka huu ambapo pia inasadikiwa kuwa watu wapatao 300,000 wameyakimbia makazi yao.
Hata hivyo kiini cha mgogoro huo unaosadikiwa kuwa ni ugomvi wa ardhi na rasilimali zilizoko katika jimbo hilo nchini Sudan.
Miili ya maaskari hao saba wa Tanzania inatarajiwa kuwasili nchini ijumaa tarehe 19, Julai kwa ajili ya maziko.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu
Dar-Es-Salaam, Tanzania
16 Julai, 2013